Featured Post

WAFANYAKAZI WA UMMA WAONYWA KUHUSU JANGA LA UKIMWI


Na Khadija Khamis  Maelezo    29/12/2017.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais(OMPR) Mihayo Juma Nunga amewataka wafanyakazi  wa taasisi mbali mbali za serikali kujiepusha na tabia hatarishi ambazo zitapelekea kupata maambukizo ya ukimwi .

Hayo aliyasema leo huko katika Ukumbi wa Wizara ya Habari Utalii Utamaduni na Michezo , Kikwajuni  wakati akifungua warsha ya siku moja juu ya elimu ya ukimwi kwa wafanyakazi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wakijumuisha na wafanyakazi wa Taasissi mbali mbali za serikali .
Alisema wafanyakazi wawe makini katika kupata mafunzo juu ya hali halisi ya VVU na ukimwi ili kupata uwelewa wa kuweza kujiepusha na maambukizi ya ukimwi pamoja na kupata fursa ya uwakilishi kwa kutoa mafunzo  kwa wafanyakazi wengine pamoja na jamii kiujumla.
Aidha alisema serikali imetilia mkazo kuwapa mafunzo  ya maambukizi ya VVU na ukimwi wafanyakazi wake ili kuweza  kupata uwelewa ushauri na maelekezo ya kuweza kuepuka na kujikinga  .
 “Ukumbusho wa kupatiwa elimu unaweza kumsaidia mfanyakazi kupata uwelewa zaidi  wa ushauri na maelekezo jinsi ya kujiepusha na maambukizi na kuweza kubadilisha tabia  hatarishi “alisema Naibu Waziri .
Alieleza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejitahidi kuchukua tahadhari mbali mbali tangu kugundulika ugonjwa wa ukimwi hapa Zanzibar kwa kutoa elimu kwa wananchi wa mjini na vijijini kwa  kuepuka unyanyapaa kwa wale waliopata maambukizi ya ukimwi na  jinsi ya kuishi nao pamoja na  kuepukana maambukizi .
Nae Mkufunzi wa mafunzo juu ya Hali Halisi ya VVU na Ukimwi  Sihaba Saadat alisema kuwa ni wajibu wao kuhakikisha wanatoa elimu kwa wafanyakazi  ili waweze kutoa mafunzo kwa watu wengine.
Alisema kila baada ya miaka mitano utafiti unafanyika kuweza kujua jinsi ya hali halisi ya ongezeko la maambukizi ya VVU na Ukimwi Tanzania tafiti zilizofanyika katika mwaka 2012 hadi 2017 zinaonyesha kuwa ongezeko kubwa la maambukizi ni kwa  mkoa wa Iringa ,Mbea pamoja na Njombe unaongoza kwa Tanzania
Aidha alisema ongezeko la maambukizi hayo  kwa upande wa kisiwa cha Unguja ni asilimia 0.6 na kwa kisiwa cha Pemba ni asilimia 0.3 kulingana na tafiti zilizofanyika katika mwaka 2012 hadi 2017 jambo ambalo linaonyesha ongezeko kubwa kwa upande wa kisiwa cha Unguja kuliko Pemba na wengi wao ni wanawake na vijana kati ya umri wa  miaka 15 hadi 24 .
Pia alieleza kuwa katika takwimu za maambukizo zilizoonekana katika mwaka 2016 kutoka wizara ya afya inaonyesha watoto 17 wamezaliwa na maambukizi ya ukimwi jambo hili linaonyesha kuwa akinamama wajawazito hawazingatii ushauri wa kidaktari .
Alifahamisha kuwa sababu hasa za kuenea kwa maambukizi ni kuwepo kwa makundi maalum ambayo yanachangia  maambukizi kwa kujiingiza katika  tabia hatarishi kwa vijana hasa akinamama kujiuza miili yao ( Madada poa ) kujidunga sindano kwa kutumia madawa ya kulevya,  wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao na kadhalika hawa wana asilimia 100 ya kupata maambukizi ya VVU na ukimwi.
Hata hivyo sadat alisema vichocheo vya maambukizi ya ukimwi kutokana na taarifa sahihi ya maambukizi husababishwa na umaskini kwa asilimia 10  ,utumiaji wa madawa ya kulevya ,tofauti za kijinsia ,unyanyapaa katika jamii ,mila na desturi uhamiaji na uhamaji pamoja na kuwepo na magonjwa ya ngono na kutotibiwa ipasavyo.
Nae Mratibu Dkt Maryam Ali Khamis alitoa mada kuhusiana na mafunzo juu ya magonjwa ya kujamiiana na uhusiano wake na ukimwi alisema magonjwa ya kujamiiana yana ishara na dalili zake yakiwemo kono ,kaswende ,pangusa na mengiineyo.
Aidha alisema chanzo cha maambukizi ya maradhi  ya kujamiiana yanatokana na maji maji ya mwili vimalea vinavyoambukiza magonjwa ya kuambukiza , kuvumba hasua ,kupata maumivu ya tumbo kwa akinamama ,pamoja na kuvimba korodani kwa wanaume
Dkt Maryam alisema chanzo kikuu cha kupata magonjwa ya kujamiiana ni kuwa na mpenzi zaidi ya mmoja , mila potovu  , na mengineyo na inaonyesha kuwa vijana wako hatarini zaidi kwa sababu wanapenda kujaribu na wanawake pia kutokana na maumbile yao ni rahisi kupata michubuko kunakopelekea kupata maambukizi kirahisi  .
Alieleza kuwa katika maambukizi ya maradhi ya kujamiiana inawezekana kupata maambukizo ya maradhi hayo bila ya kujijua  na kusababisha kupata kensa ya kizazi
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Idrisa Muslimu Hija aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kutekeleza yale yote waliopewa na kuweza kuto elimu kwa wengine ambao hawakubahatika kupata mafunzo hayo ili na wao wapate uwelewa wa kujikinga kwa namna moja au nyengine.

Comments