Featured Post

WAFANYABIASHARA WALIOFUNGA MAGHALA YA MBOLEA KUNYANG'ANYWA LESENI

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa (Katikati) akikagua mbegu zilizohifadhiwa ghalani kabla ya kuanza kusambazwa alipotembelea Wakala wa mbegu za kilimo (Agricultural Seeds Agency-ASA) wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani Morogoro, Leo 29 Disemba 2017. Wengine ni Kaimu Mkurugenzi Wakala wa Mbegu Dkt Sophia Kashenge Kilenge (Kulia) na Meneja uzalishaji Wakala wa Mbegu Ndg Charles Levi (Kushoto). Picha Zote Na Mathias Canal .
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akisalimiana na Mkurugenzi Wakala wa Mbegu Dkt Sophia Kashenge Kilenge alipotembelea Wakala wa mbegu za kilimo (Agricultural Seeds Agency-ASA) wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani Morogoro, Leo 29 Disemba 2017.
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akisisitiza jambo baada ya kukagua baadhi ya mashine za mbegu alipotembelea Wakala wa mbegu za kilimo (Agricultural Seeds Agency-ASA) wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani Morogoro, Leo 29 Disemba 2017. 
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akikagua namna mbegu za mazao mbalimbali zilivyohifadhiwa alipotembelea Wakala wa mbegu za kilimo (Agricultural Seeds Agency-ASA) wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani Morogoro, Mwingine ni Kaimu Mkurugenzi Wakala wa Mbegu Dkt Sophia Kashenge Kilenge (Kushoto). Leo 29 Disemba 2017. 

Na Mathias Canal, Morogoro

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa leo Disemba 29, 2017 amewaagiza wafanyabiashara wa mbolea kote nchini walioweka mgomo wa kupeleka mbolea kwa wakulima kufikia 30 Disemba 2017 wawe wamefungua maghala yao kwa ajili ya kuwauzia mbolea wakulima.

Alisema endapo wafanyabiashara hao wasipofanya hivyo serikali itawanyang'anya leseni zao haraka iwezekanavyo ili kuruhusu wafanyabiashara wenye uwezo wa kufanya jukumu hilo pasina kuwaumiza wakulima kutokana na bei ghali ya mbolea.

Mhe Mwanjelwa ametoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani Morogoro alipotembelea Wakala wa mbegu za kilimo (Agricultural Seeds Agency-ASA) Mara Baada ya kubaini kuwa kuna wafanyabiashara ambao wameanza kufunga maghala kwa madai ya kupanda kwa mbolea katika soko la Dunia.

Alisema kuwa kufanya hivyo ni kinyume na sheria na kuijaribu serikali kwani malalamiko yao ya kupanda kwa bei katika soko la Dunia hayana tija kwani mbolea zote zilipo nchini tayari wakishanunua kipindi soko likiwa kwenye unafuu mkubwa.

Alisema kuwa serikali ilitoa bei elekezi katika mbolea ya kukuzia na kupandia ikifahamu fikra kuwa kupitia gharama hiyo wakulima watanufaika lakini pia wafanyabiashara watanufaika kutokana na faida wanayoipata lakini wameamua kubadili utaratibu wa kutaka kupata faida kubwa zaidi pasina kujali wakulima wataumizwa na bei hiyo kwa kiasi gani.

Mhe Mwanjelwa ameitaka kampuni ya Premium ambayo ni moja ya kampuni zilizogoma kufungua maghala na kupeleka mbolea kwa wakulima kwa bei elekezi iliyotolewa na serikali.

Alisema kuwa wafanyabiashara hao kwa makusudi wameamua kufifisha juhudi za Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli ya kuwakomboa wakulima kupitia gharama nafuu ya mbolea hivyo kufikia kesho wasipofungua maghala hayo watanyang'anywa leseni zao ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa sheria.

Comments