Mheshimiwa Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Hamidu Awesso
akitoa ngao ya ushindi kwa mjumbe wa kamati ya kudhibiti Ukimwi, Jinsia
na Uongozi ya kijiji cha Msaraza wakati wa tamasha hilo.
Mheshimiwa Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Hamidu Awesso
akitoa zawadi kwa kijana bora wa mfano wa kuigwa kwa mwaka 2017 nafasi
ya kwanza ilichukuliwa na kijana Selemani Hamisi kutokea kijiji cha
Kimang'a(Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha)
Mheshimiwa Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Hamidu Awesso
akitoa zawadi kwa mama bora wa mfano kwa mwaka 2017 ambapo nafasi ya
kwanza ilikwenda kwa Mama Hadija Mrisho wa kijiji cha Kwa-Kibuyu
pichani
Hatimae shindano la kutafuta kamati bora za kudhibiti Ukimwi,
Jinsia na Uongozi vijijini lililokuwa linaratibiwa na shirika la
UZIKWASA wilayani Pangani limemaliza kwa kishindo huku kamati ya kijiji
cha Msaraza kikiibuka na ushindi.
Shindano hilo ambalo
lililokuwa linashirikisha vijiji 33 kutokea wiayani humo, limehudhuriwa
na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji ambaye pia ni Mbunge wa jimbo
hilo Mheshimiwa Jumaa Hamidu Awesso ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi.
Awali
akitangaza kamati tatu bora zilizofanya vizuri kwa mwaka huu mbele ya
mgeni rasmi, mkurugenzi msaidizi kutokea shirika la UZIKWASA Bwana
Novatus Urassa alisema, mchakato wa kupata washindi hao ulikuwa mgumu
kwa kuwa mwaka huu kamati zote zilionesha ushindani wa hali ya juu
katika kutekeleza mipango kazi yao waliyojiwekea.
"Mheshimiwa
mgeni rasmi, takribani vijiji vyote 33 vilivyoshiriki shindano hili kwa
mwaka huu vilikuwa moto, kwa maana kila kijiji kilikuwa na mpango kazi
wake, na kwa asilimia kubwa wote wamefanikiwa kutekeleza mipango kazi
hiyo, lakini wapo waliotekeleza vizuri zaidi na tukaona hao ndio
watakuwa mfano mzuri kwa wenzao, hivyo mpaka kupata kumia (10) bora
haikuwa kazi rahisi, hivyo hivyo mpaka kupata hizi tatu (3) bora pia
haikuwa rahisi" alisema Bwana Urassa.
Bwana Urassa alizitaja
kamati hizo zilizofanya vizuri kuwa ni kamati ya kijiji cha Msaraza
ambacho ndicho kiliibuka na ushindi na kukabidhiwa zawadi ya hundi ya
shilingi laki saba, mshindi wa pili ni kijiji cha Mwera ambacho kilipewa
hundi ya shilingi laki sita na mshindi wa tatu ni kijiji cha Mkwajuni
ambapo walikabidhiwa hundi ya shilingi laki tano.
Kamati nyengine
ambazo ziliingia katika hatua ya kumi bora ni pamoja na kamati ya
kudhibiti Ukimwi, Jinsia na Uongozi ya kijiji cha Tungamaa ambacho
kilishika nafasi ya nne, Kijiji cha Mwembeni nafasi ya tano, Kijiji cha
Mbulizaga nafasi ya sita, Kijiji cha Kimang'a nafasi ya saba, Kijiji cha
Mikocheni nafasi ya nane, Kijiji cha Mikinguni nafasi ya tisa, na
Kijiji cha Kwa-Kibuyu kilishika nafasi ya kumi.
Mbali na
ushindani wa kamati hizo, pia tamasha hilo liliwatambua na kuwazawadia
washindi wa shindano la Kijana Bora wa mfano wa kuigwa pamoja na Mama
Bora wa mfano wa kuigwa kwa mwaka 2017 kutokana na kujikita katika
shughuli za kimaendeleo na kupambana na ukatili wa kijinsia.
Upande
wa kijana bora wa mfano wa kuigwa kwa mwaka 2017 nafasi ya kwanza
ilichukuliwa na kijana Hamisi Salemani kutokea kijiji cha Kimang'a,
nafasi ya pili kijana Geofrey Kalala kutokea kijiji cha Boza, nafasi ya
tatu kijana Mohammed Zuberi kutokea kijiji cha Mkwaja, na kwa upande wa
mama bora wa mfano kwa mwaka 2017 nafasi ya kwanza ilikwenda kwa Mama
Hadija Mrisho wa kijiji cha Kwa-Kibuyu, nafasi ya pili Mama Pili Yusufu
wa kijiji cha Mwembeni na nafasi ya tatu ni ilienda kwa Mama Halima
Hamisi wa kijiji cha Mivumoni
Kwa upande wake mgeni rasmi
Mheheshimiwa Jumaa Hamidu Awesso mbali na kulipongeza shirika la
UZIKWASA kwa kuandaa shughuli hiyo, pia aliwapongeza washindi wote wa
mashindano hayo na kuwataka waendelee kuwa chachu ya maendeleo wilayani
Pangani hasa wakati huu ambao jamii imekuwa ikikumbwa na matukio ya
ukatili wa kijinsia.
"Shirika la UZIKWASA linafanya mambo makubwa
sana hapa wilayani Pangani, wananchi walikuwa wanaogopa kupaza sauti
zao, lakini leo wananchi wanabanja, wanaeleza matatizo ya ukatili,
wanajadili masuala ya maendeleo, wanawahoji viongozi wao wa vijiji kama
kuna ubadhilifu, leo wananchi wanafatilia masuala ya elimu kwa watoto
wao, kamati za shule zinafanya kazi, na pia tunaona hapa mpaka kamati za
kudhibiti Ukimwi zimeanzishiwa mashindano ili kuleta ufanisi wa kazi
zao, yote hii ni juhudi za UZIKWASA, na naomba washindi wote mkawe
chachu ya maendeleo katika maeneo yenu" alisema Mheshimiwa Awesso.
Tamasha
hilo lilihudhuriwa na Mkurugenzi wa halmashauri ya Pangani Bwana Sabas
Damian Chambasi, mkuu wa TAKUKURU wilayani Pangani Bwana Joseph Paul,
Ofisi ya manedeleo ya jamii Pangani ikiwakilishwa na Bi Vicky Mfinanga
na Bi Rose Kaskazi pamoja na mkurugenzi mtendaji wa shirika la UZIKWASA
Mama Vera Pieroth.
Pia Tamasha lilipambwa na burudani mbali mbali
za sanii, ambapo kundi la maigizo na ngoma za asili kutokea Pangani
linalofahamika kwa jina la Banja Basi lilikuwa kivutio kikubwa kwa
wageni waalikwa, kadhalika wasanii wa Bongo Flava kutokea Pangani G-Man,
Ram Bize pamoja Mavokali waliacha historia katika tamasha hilo.
Tamasha
la kukabidhi zawadi kwa kamati bora za kudhibiti Ukwimwi, Jinsia na
Uongozi kwa mwaka 2017 limeandaliwa na shirika la UZIKWASA lenye maskani
yake wilayani Pangani huku likibeba kauli mbiu isemayo "Lisilowezekana,
Linawezekana". Mwaka jana mshindi wa kamati bora kilikuwa kijiji cha
Mseko.
Comments
Post a Comment