Featured Post

SERIKALI YASIKIA KILIO CHA WADAU WA SEKTA YA UWINDAJI WA KITALII NCHINI, YAONGEZEA MIAKA MIWILI YA UMILIKI WA LESENI ZA VITALU

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wadau wa sekta ya uwindaji wa kitalii katika mkutano uliondaliwa na Wizara yake mjini Dodoma jana kwa ajili ya kujadili mikakati mbalimbali ya kuimarisha sekta hiyo ikiwemo utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuanzisha utaratibu mpya wa utoaji wa leseni za vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mej. Jen. Gaudence Milanzi na Naibu Katibu Mkuu, Dk. Aloyce Nzuki (kulia).  

Na Hamza Temba, Dodoma
...............................................................
Serikali imesikia kilio cha wadau wa sekta ya uwindaji wa kitalii nchini na kuamua kuongeza muda wa miaka miwili ya umiliki wa leseni za vitalu 95 vya uwindaji wa kitalii ambazo zilikuwa ziishe muda wake tarehe 31 Desemba mwaka huu (2017).

Uamuzi huo umefikiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla wakati wa kikao cha majumuisho na watendaji wa Wizara hiyo muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkuano wa wadau wa sekta hiyo ulioandaliwa na Wizara hiyo mjini Dodoma jana.

Akizungumzia uamuzi huo Dk. Kigwangalla alisema, lengo ni kuwapa muda wawekezaji hao ili waweze kujiandaa na mabadiliko ya mfumo mpya wa utowaji wa leseni za vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada ikiwemo kurudisha baadhi ya gharama za uwekezaji walizoweka katika vitalu hivyo.

Awali akizungumza katika mkutano huo wa wadau Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Uwindaji wa Kitalii nchini, Michael Mantheakis alimuomba Waziri Kigwangalla kuwaongezea muda wa umiliki wa leseni zao kuanzia miaka mitano au mitatu na nusu ili waweze kurudisha gharama za uwekezaji walizowekeza katika vitalu hivyo ikiwemo ujenzi wa miundombinu, makambi na vifaa vyake pamoja na maji.

Hata hivyo, Waziri Kigwangalla aliweka wazi msimamo wa Serikali wa kutimiza azma yake ya kuingia kwenye utaratibu mpya wa utoaji wa leseni za vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada na kusema kuwa kamwe haitorudi nyuma na kwamba utekelezaji wa zoezi hilo hauwezi kusubiri muda mrefu kiasi hicho.

Akizungumzia kuhusu hatua ya utekelezaji wa utaratibu huo, Waziri Kigwangalla alisema kwa sasa taratibu za kuandaa Sheria za usimamizi zinaendelea na zinatarajiwa kukamilika mwezi Februari 2018 pamoja na kanuni zake zinazotarajiwa kukamilika mwezi Aprili 2018.

Aidha, alisema mfumo maalumu wa kielektroniki unaandaliwa ambapo maombi yote ya leseni za umiliki wa vitalu vya uwindaji kwa njia ya mnada yatafanyika kwa uwazi kwa njia ya mtandao.

Alisema baada ya kukamilika kwa taratibu zote na mfumo huo mpya wa utoaji wa leseni za vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada na maombi kuwasilishwa, mnada wa kwanza utaanza tarehe 1 Julai, 2018 kwa kuanza kunadi vitalu 61 ambavyo kwa sasa havina wawekezaji.

Mnada wa pili utafanyika mwaka 2020 baada ya kuisha kwa muda huo wa nyongeza wa miaka miwili ukihusisha vitalu 95 vilivyoongezewa muda wa umiliki wa leseni pamoja na vitalu vingine endapo vitabaki katika mnada huo wa kwanza kwa sababu mbalimbali.

Alisema sheria na kanuni zinazoandaliwa hivi sasa zitazingatia mambo muhimu ikiwemo kuwapa nafasi watanzania wenye mitaji midogo kuweza kuingia kwenye biashara hiyo pamoja na kuweka adhabu kali dhidi ya wafanyabiashara watakaohujumu biashara hiyo kwa makusudi.

Mkutano huo wa siku moja ulihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi, Naibu Katibu Mkuu, Dk. Aloyce Nzuki, wakurugenzi, wakuu wa vitengo na wakuu wa taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo na waandhishi wa habari.

Oktoba 22 mwaka huu (2017) wakati akiongoza kikao cha wadau wa sekta ya Maliasili na Utalii mjini Dodoma, Waziri Kigwangalla alitangaza kufuta leseni za vitalu vya uwindaji wa kitalii zilizokuwa zianze mwezi Januari, 2018 ili kupisha utarartibu mpya wa utoaji wa leseni hizo kwa njia ya mnada ikiwa ni mkakati wa Serikali wa kuimarisha sekta hiyo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wadau wa sekta ya uwindaji wa kitalii katika mkutano uliondaliwa na Wizara yake mjini Dodoma jana kwa ajili ya kujadili mikakati mbalimbali ya kuimarisha sekta hiyo ikiwemo utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuanzisha utaratibu mpya wa utoaji wa leseni za vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Dk. Aloyce Nzuki.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi (kushoto) akizungumza katika mkutano huo. Kulia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Uwindaji wa Kitalii nchini, Michael Mantheakis (kulia) akiwasilisha mapendekezo yake katika mkutano wa wadau wa sekta ya uwindaji wa kitalii katika mkutano uliondaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii mjini Dodoma jana kwa ajili ya kujadili mikakati mbalimbali ya kuimarisha sekta hiyo ikiwemo utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuanzisha utaratibu mpya wa utoaji wa leseni za vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada.
Mdau wa sekta ya uwindaji wa kitalii, Dk. Licky Abdallah akizungumza katika mkutano huo. 
Mdau wa sekta ya uwindaji wa kitalii ambaye pia ni mmilikia wa kampuni ya uwindaji wa kitalii ya Bushman Hunting Safaris, Talal Abood akiwasilisha mapendekezo yake katika mkutano huo. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akisikiliza kwa makini mapendekezo ya wadau wa sekta ya uwindaji wa kitalii katika mkutano uliondaliwa na Wizara yake mjini Dodoma jana. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi.
Baadhi ya wadau wa sekta ya uwindaji wa kitalii wakiwa katika mkutano huo. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wadau wa sekta ya uwindaji wa kitalii katika mkutano uliondaliwa na Wizara yake mjini Dodoma jana kwa ajili ya kujadili mikakati mbalimbali ya kuimarisha sekta hiyo ikiwemo utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuanzisha utaratibu mpya wa utoaji wa leseni za vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada. Kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mej. Jen. Gaudence Milanzi na Naibu Katibu Mkuu, Dk. Aloyce Nzuki (kushoto kwake). 
Baadhi ya watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zake wakiwa katika mkutano huo. 

Comments