Featured Post

RC MBEYA MHE. AMOS MAKALA AFUNGUA MAFUNZO YA MADAKTARI WA KANDA YA NYANDA ZA JUU KUSINI YANAYORATIBIWA NA WCF


Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Amos Makala, akihutubia wakati akifungua rasmi mafunzo ya siku tano kwa madaktari wanaofikia 100 kutoka mikoa saba ya kanda ya nyanda za juu Kusini, kwenye ukumbi wa Benjamin Mkapa, jijini humo Desemba 12, 2017. Mafunzo hayo yanayoratibiwa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), yanalenga kuwajengea uwezo madaktari na watoa huduma za afya kufanya tahmini ya mfanyakazi aliyepata ulemavu au ugonjwa mahali pa kazi.


NA K-VIS BLOG/Khalfan Said, Mbeya

TAKRIBAN madaktari na watoa huduma za afya 100 kutoka mikoa saba ya Kanada ya Nyanda za Juu Kusini, wameanza kupatiwa mafunzo jijini Mbeya yanayoratibiwa na Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi (WCF).

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa mafunzo hayo ya siku tano yaliyofunguliwa rasmi Desemba 12, 2017 (jana) NA Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Amos Makala kwenye ukumbi wa Benjamin Mkapa jijini Mbeya, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Bw.Masha Mshomba, alisema, mafunzo hayo ni muendelezo wa mafunzo kwa madaktari na watoa huduma za afya ili kuwajengea uwezo wa kufanya tathmini ya ulemavu maradhi anayopata mfanyakazi wakati akitekeleza majukumu yake mahala pa kazi ili hatimaye madaktari hao waweze kutoa mapendekezo kuwezesha mfuko kutoa mafao ya fidia stahiki.

Kwa mujibu wa mratibu wa mafunzo hayo, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini wa WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar, mafunzo hayo yamewaleta pamoja madaktari na watoa huduma za afya kutoka mikoa ya Mbeya, Songwe, Katavi, Rukwa, Iringa, Njombe na Ruvuma.

Katika hatua ya kuimarisha Hifadhi ya Jamii, Tanzania, Serikali ilianzisha Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi kwa mujibu wa kifungu namba 5 cha sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi,  kipengele cha 263 kilichofanyiwa marejeo mwaka 2015 ili kuhakikisha kila mfanyakazi Tanzania Bara kutoka sekta ya umma na binafsi anapata fursa ya kuwekewa bima na mwajiri wake ili anapopata majeraha au magonjwa awapo kazini basi aweze kufidiwa kwa mujibu wa sheria, alisema Bw. Mshomba.

“Lengo kuu la kuanzishwa kwa Mfuko huu ni kutoa fidia stahiki kwa mfanyakazi aliyepatwa na majeraha, maradhi kutokana na kutekeleza wajibu wake awapo kazini, lakini pia kuwalipa fidia wategemezi wake anapofariki katika mazingira hayo.” Alifafanua Bw. Mshomba na kuongeza, WCF ilianza kutekeleza majukumu yake Julai Mosi, 2015 na mwaka uliofuata Mfuko ulianza rasmi kupokea madai ya fidia na kulipa mafao kwa waathirika.

Wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Mwaka wa Wadau wa WCF jijini Arusha mwishoni mwa mwezi uliopita, kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama, aliitaka WCF kuendelea kutoa elimu kwa wadau, ili waweze kuelewa vema shughuli za Mfuko na nia njema ya serikali ya kuanzisha mfuko huo ili mfanyakazi wa Tanzania aweze kupata fidia stahiki anapopata madhara sehemu ya kazi.

Bw, Mshomba aliishukuru Serikali na Wizara zake kwa kuunga mkono na kusaidia juhudi za WCF katika kuimarisha mifumo yake ili kutoa huduma bora kwa wadau wake.

“Pia napenda nizishukuru taasisi za Hospitali ya Taifa Muhimbili, MOI, Ocea Road Hospital, MUHAS, na OSHA kwa kuwaruhusu wataalamu wake ili tuwatumie katika kutoa mafunzo haya.” Alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Amos Makala ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mafunzo hayo, alisema, juhudi za ushirikiano wa pamoja miongoni mwa wadau yaani Serikali, Wafanyakazi, Waajiri unahitajika sana kuhakikisha tathmini endelevu ili kuimarisha mfuko.

“Nimeambiwa mafunzo haya yataongeza uelewa katika kufanya tathmini na uchunguzi wa majeraha au maradhi anayoyapata mfanyakazi mahala pa kazi na kutoa mapendekezo stahiki kwa uamuzi wa mwisho.”

Mkuu wa Mkoa pia alipongeza juhudi za WCF kwa kuendesha mafunzo hayo ambayo yatawezesha kupanua wigo wa mtandao wa watoa huduma za afya na hospitali
“Katika mwaka wa fedha wa 2015/2016 naambiwa mlianza kutoa mafunzo kwa madaktari na watoa huduma za afya wapatao 359, katika wailaya zote za Tanzania Bara mafunzo mliyoyaendesha katika kanda nne za Pwani, kanda ya Ziwa, kanda ya Kaskazini, na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na mwaka uliofuata mkatoa mafunzo kwa madaktari wapatao 145 katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza na kufanya idadi ya jumla hadi sasa ya madaktari na watoa huduma za afya ambao mmewapatia mafunzo kufikia 504, napenda kuipongeza Bodi ya Wadhamini na uongozi wa Mfuko kwa kazi nzuri mnayofanya.” Alimaliza Mkuu wa Mkoa Bw. Amos Makala.

 Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), Bw. Masha Mshomba, akitoa hotuba ya ukaribisho kweye ufunguzi rasmi wa mafunzo ya siku tano kwa madaktari wanaofikia 100 kutoka mikoa saba ya kanda ya nyanda za juu Kusini, kwenye ukumbi wa Benjamin Mkapa, jijini humo Desemba 12, 2017. Mafunzo hayo yanayoratibiwa na WCF, yanalenga kuwajengea uwezo madaktari na watoa huduma za afya kufanya tahmini ya mfanyakazi aliyepata ulemavu au ugonjwa mahali pa kazi. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Amos Makala, na Mkurugenzi wa Tiba na Tathmini wa Mfuko huo, Dkt. Abdulsalaam Omar.
 Washiriki wakifuatilia hotuba kwa umakini.
 Washiriki wakifuatilia hotuba kwa umakini.
 Washiriki wakifuatilia hotuba kwa umakini.
 Mshiriki akizungumza kwenye mafunzo hayo.
 Mshiriki akizungumza kwenye mafunzo hayo.
 Dkt. Ali Mtulia(kushoto) kutoka WCF, na wawezeshaji wakifuatilia hotuba hiyo.
  Washiriki wakifuatilia hotuba kwa umakini.
 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano WCF, Bi. Laura Kungenge, akiwa makini kufuatilia hotuba.
 Sekretariat ya WCF ikiwa kwenye majadiliano ili kuhakikisha mafunzo yanakwenda kwa ufasaha. Kutoka kushoto ni Dkt. Pascal Magesa, Bw.Vincent Steven, Bi. Laura Kunenge, na Bi.Innocencia William.
 Afisa Kazi Mkoa wa Mbeya, Bi. Mary Patrick Mwansisya (kulia na maafisa wengine wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa Mkoa.
Bw. Mshomba akimsikiliza kwa makini Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Amos Makala wakati akihutubia madaktari.
Mhe. Makala, akionyesha kitu, akiwa Bw. Mshomba
Picha ya pamoja kundi la kwanza
Picha ya pamoja kundi la kwanza
Picha ya pamoja kundi la kwanza


Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mheshimiwa Amos Makala, (kushoto), akipongezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, (WCF), Bw. Masha Mshomba, (kushoto) mara baada ya kutoa hotuba yake ya ufunguzi rasmi wa mafunzo ya siku tano kwa madaktari wanaofikia 100 kutoka mikoa saba ya kanda ya nyanda za juu Kusini, kwenye ukumbi wa Benjamin Mkapa, jijini humo jana (Desemba 12, 2017). Mafunzo hayo yanayoratibiwa na WCF yanalenga kuwajengea uwezo madaktari na watoa huduma za afya kufanya tahmini ya mfanyakazi aliyepata ulemavu au ugonjwa mahali npa kazi. Mafunzo hayo yanafanyika jijini Mbeya.


Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mheshimiwa Amos Makala, (kulia), akiongozana na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, 9WCF), Bw. Masha Mshomba, baada ya ufunguzi rasmoi wa mafunzo ya siku tano kwa madaktari wanaofikia 100 kutka mikoa saba ya kanda ya nyanda za juu Kusini, kwenye ukumbi wa Benjamin Mkapa, jijini humo. Mafunzo hayo yanayoratibiwa na WCF yanalenga kuwajengea uwezo madaktari na watoa huduma za afya kufanya tahmini ya mfanyakazi aliyepata ulemavu unaotokana na ajali au magonjwa mahala pa kazi
 




Comments