Featured Post

MKURUGENZI KINGA NA ELIMU YA AFYA ZANZIBAR ASISITIZA ELIMU ZAIDI KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA MARADHI YASIYOAMBUKIZA

Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt. Fadhil Abdalla akifungua mkutano wa wadau wa maradhi yasiyoambukiza uliokuwa na lengo la kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu maradhi hayo katika Ukumbi wa Malaria, Mwanakwerekwe Mjini.

Na Ramadhani Ali – Maelezo, Zanzibar
Licha ya mikakati inayoendelea kuchukuliwa na Serikali na Taaisi za kiraia kuelimisha jamii madhara yanayosababushwa  na maradhi yasiyoambukiza, juhudi zaidi inahitajika katika kutoa elimu ya maradhi hayo.

Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt. Fadhil Abdalla alisema kuwa kuna haja kubwa elimu ya maradhi yasiyoambukiza ikaanzia kwa wanafunzi maskulini na katika vikundi na mikutano ya kijamii.
Dkt. Fadhil alitoa ushauri huo Ofisi ya Malaria Mwanakwerekwe katika mkutano wa wadau wa maradhi yasiyoambukiza uliokuwa na lengo la kuongeza uelewa kwa jamii juu ya maradhi hayo.
Aliweka bayana kuwa njia za kujikinga na maradhi yasiyoambukiza na tiba yake zipo na hazina gharama kubwa kitu muhimu ni kwa wananchi kuwa na elimu ya kutosha juu ya maradhi hayo.
“Kujenga tabia ya kufanya mazoezi kila siku, kupunguza uzito, kula matunda na mboga mboga kwa wingi vitu vinavyopatikana muda wote nchini kwetu kunagharama gani,” aliuliza Dkt. Fadhil.
Alikumbusha kuwa asilimia kubwa ya vifo vinavyotokea duniani hivi sasa vinasababishwa na maradhi yasiyoambukiza kinyume na miaka ya nyuma na ndio maana yanazungumzwa kwa kina kwenye mikutano mingi ya kimatafa ya Afya.
Alisema maradhi yasiyoambukiza matibabu yake yanapatikana katika vituo vya afya kinyume nailivyokuwa siku za awali ambapo huduma za maradhi hayo zilikuwa zinapatikana katika hospitali kubwa pekee jambo ambalo lilileta usumbufu kwa wananchi wa vijijini.
Aidha Dkt. Fadhil amesisitiza umuhimu wa wasomi kujikita katika kufanya tafiti za maradhi yasiyoambukiza zitakazosaidia kutoa muelekeo na kujua sababu ya kuongeza kwa kiasi kikubwa maradhi hayo.
Akiwasilisha taarifa ya Lishe na rasilimali watu na utafiti kuhusiana na mtazamo wa watu wanaoishi na maradhi hayo, Meneja wa Kitengo cha maradhi yasiyoambukiza katika Wizara ya Afya Omar Mwalimu alisisitiza umuhimu wa wanachi kula chakula mchanganyiko chenye lishe kamili kujikinga na maradhi hayo.
Alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2011 imeonyesha kuwa wananchi wa Zanzibar wanaotumia matunda na mboga mboga wakati wa kula ni asilimia mbili na hiyo inapelekea kupata maradhi yasiyoambukiza kwa urahisi.
Aliwashauri wananchi kupunguza matumizi makubwa ya mafuta  kwani ni hatari kwa afya zao.
Akiwasilisha mada ya ushirikishwaji wa wadau mbali mbali katika kupambana na maradhi yasiyoambukiza, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maradhi hayo Tanzania Dkt. Tatizo Waane alisema wenye maradhi hayo mara nyingi wanachelewa kujijua kwa sababu hawendi vituo vya afya kupima afya zao.
Alisema hata wale wanaojijua mara nyingi huchelewa kupata huduma stahiki kutokana na umasikini na hatimae hupoteza maisha.
Aliishauri jamii kujenga utamaduni  wa kupima afya zao mara kwa mara na kufanya mazoezi kupunguza uzito ikiwa ni moja ya tiba sahihi ya maradhi yasiyoambukiza.

Comments