Featured Post

MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA SIKUKUU YA KRISIMASI

Na Jumia Travel Tanzania
Ule msimu wa watu kufurahi na kujumuika umewadia tena!
Haina ubishi kwamba sikukuu na mapumziko ya mwisho wa mwaka ambayo huambatana na sikukuu za Krismasi (Desemba 25) na mwaka mpya ndiyo huwa na shamrashamra nyingi zaidi duniani.


Ni kipindi hiko ndicho familia, ndugu, jamaa na marafiki hukutana kwa pamoja na kufurahia kuumaliza mwaka na kuukaribisha mwaka mpya unaofuatia. Mbali na hilo, kutokana na shughuli za mwaka mzima katika kutafuta kipato na kujenga maisha, hiki ni kipindi ambacho watu hupumzisha mwili na akili kwa kufurahia matunda waliyoyachuma kwenye kipindi cha mwaka mzima lakini hata kutafakari namna watakavyoukabili mwaka mpya ambao huja na majukumu na matarajio mapya.

Katika kipindi hiki cha sikukuu mambo mengi hutokea ambayo kwa namna moja ama nyingine endapo hautokuwa makini yatakuacha kwenye hali mbaya. Jumia Travel ingependa kukumbusha wakati ukiwa kwenye ari ya shamrashamra za msimu huu wa sikukuu kuepuka kuyafanya mambo yafuatayo.


Tumia muda wa kutosha na familia. Itapendeza endapo sikukuu ya Krisimasi na mapumziko ya mwisho wa mwaka ukazitumia kufurahia na familia yako. Ni kipindi ambacho miongoni mwenu mpo likizo, watoto wamefunga shule na ndugu hupata fursa ya kutembeleana. Ni jambo la kawaida kuona watanzania mbalimbali kilo kona ya nchi wakifurika kurudi makwao au wengine wakialikana ili kufurahia kipindi hiki. Kamwe usiipoteze fursa hii ya kujumuika na wale uwapendao kwani hutokea mara moja tu kwa mwaka na ni vema ukaitumia ipasavyo.



Zingatia kiwango na aina ya vyakula unavyokula. Kwa sababu katika kipindi hiki kunakuwa na vyakula vya kila aina, ndiyo ukawa unakula tu bila ya kuwa makini. Ulaji wa vyakula tofauti bila ya mpangilio na kiwango maalumu unaweza kukusababishia madhara kwenye mwili wako na kukusesha raha ya kufurahia sikukuu. Hivyo basi, kama inawezekana basi jaribu kuendana na utaratibu wako uliojiwekea wa kula. Usizidishe kwa sababu siku hii vyakula ni vingi.



Kuwa makini na kiasi cha pombe. Ndiyo ni sikukuu, hauna wajibu siku inayofuatia au mtondogoo. Lakini hii isiwe sababu ya kutokuwa makini na kiwango cha pombe unachokunywa. Unywaji wa pombe kuzidi kiwango unaweza kukusababishia mbali tu na uchovu kwenye mwili wako na kushindwa kufurahia matukio ya muhimu na familia yako bali pia hata madhara kwako na watu wanaokuzunguka. Jaribu kuwa mvumilivu kwa kipindi hiki kifupi, furahia kwa kunywa kiasi na familia pamoja na wapendwa wako. Kwa kuongezea, unywaji wa pombe kupitiliza unaweza kukusababishia ukaingia matatani na vyombo vya sheria, kwa sababu ni kipindi cha mapumziko haimaanishi kwamba sheria na taratibu za nchi zimelala.



Tumia pesa kwa makini. Kipindi hiki pia watu wengi hushuhudia wakitumia kiwango cha pesa bila ya kutarajia. Ni vema ukawa umetenga kiwango fulani cha fedha kwa ajili kutumika kwenye msimu huu wa sikukuu. Kama haukufanikiwa kutenga mapema bajeti ya kutumika kipindi hiki basi hakikisha fedha utakayoitumia haitaathiri matumizi yako ya baadaye. Unaweza kufanya hivyo kwa kubana matumizi kwani sio lazima kuwa na shamrashamra kubwa. Kwa sababu ni kipindi cha mwisho wa mwaka na tunafahamu namna maisha yetu watanzania yalivyo, mwaka mpya huja na majukumu kama vile kodi za nyumba, karo za shule, pango za sehemu za biashara, leseni au vibali vya vyombo vya moto nakadhalika.



Usijibane sana, furahia! Inawezekana mipango haijakaa sawa kwenye msimu huu wa sikukuu hivyo kukunyima fursa ya kufurahia vilivyo. Kumbuka, kipindi hiki hutokea mara moja tu kwa mwaka na hautakiwi kujuta sana kwamba kwa nini haukufanikiwa. Ni mafanikio kuwa mzima mpaka kufanikiwa kuuona msimu huu wa sikukuu kwani wengine hawajafanikiwa. Jumia Travel inaamini kwamba kwa kuumaliza mwaka ukiwa na matumaini kutakupa fursa ya kujipanga vema zaidi na mwaka ujao.

Comments