Featured Post

MAMBO TISA YA KUFANYA KUITANGAZA BIASHARA YAKO MSIMU HUU WA SIKUKUU


Na Jumia Travel Tanzania

Kipindi cha sikukuu na mapumziko ya mwisho wa mwaka huongoza kwa watu kufanya manunuzi ya aina mbalimbali. Ni kipindi ambacho si watu hujikita zaidi kwenye kufurahia likizo zao bali hata kuwa huru kutumia pesa kwa ajili ya chakula, zawadi na huduma kadha wa kadha.

Kama wewe ni mfanyabiashara iwe ya kubwa au ndogo,  kipindi hiki cha mwaka huambatana na faida lukuki za kujitangaza na kujitafutia masoko zaidi. Yafuatayo ni mambo tisa ambayo Jumia Travel inapendekeza kuwa unaweza kuyatumia kama fursa ili kuwavutia wateja zaidi na kujitangaza katika msimu huu.   

Punguzo la bei. Kwa kawaida kipindi kama hiki cha msimu wa sikukuu wateja wengi hutegemea punguzo la bei kwenye bidhaa na huduma tofauti. Unaweza kuitumia fursa hii kwa kutoa punguzo la bei pia. Mbali na kutoa punguzo kwenye biashara yako lakini pia unaweza kushirikiana na wafanyabiashara wengine. Kwa mfano, kama unauza nguo unaweza kutoa punguzo la bei ambapo wateja wakifanya manunuzi ya kiwango fulani watajipatia fursa ya kupata chakula kwenye mgahawa fulani.

Maazimio ya biashara kwa mwaka ujao. Kama ni mfanyabiashara ambaye una dira na malengo ya kuifikisha biashara yako mahali fulani lazima utakuwa na maazimio. Unaweza kukitumia kipindi hiki kwa kuwajulisha wateja wako maboresho unayotarajia kuyafanya mwaka ujao ili kuwavutia zaidi.

Chakula. Hakuna mtu asiyependa chakula. Zipo njia nyingi za kuwashukuru wateja na wadau mbalimbali waliofanikisha kwa namna moja ama nyingine kufikia hapo ulipo. Unaweza ukaanda chakula cha pamoja na kupata fursa ya kuzungumza na kujadili masuala mbalimbali yanayoweza kusaidia kukua kwa biashara yako.

Kadi za kushukuru. Nguvu ya kushukuru kwa kutendewa jambo fulani ni kubwa tofauti na unavyofikiri. Kwa kuonyesha kwamba unajali na kutambua mchango wa wateja kwenye biashara yako kunaweza kufungua milango mingi zaidi. Unaweza kuandaa kadi zenye ujumbe mzuri wa shukrani na kuwatumia wateja wako njia ya barua pepe au kuwapatia pale wanapotembelea biashara yako.

Mauzo kwa wateja maalumu. Kila biashara inakuwa na wateja ambao ni waaminifu kwa namna moja ama nyingine. Kwa kutambua mchango wao unaweza kuandaa mauzo maalumu kwa ajili yao. Unaweza kulifanikisha hili kwa kuandaa kuponi na kuwapatia kisha kuwajulisha kwamba wanaweza kutembelea kwenye biashara yako na kufanya manunuzi ya kiwango ulichowapatia.
Saidia jamii inayokuzunguka. Miongoni mwa mbinu ya kujenga uhusiano mzuri na jamii inayokuzunguka na ili kukubalika ni pamoja na kutoa msaada kwa masuala mbalimbali. Zipo nyanja mbalimbali unaweza kulifanikisha hili. Fanya utafiti mdogo kujua changamoto zinazoizunguka jamii yako na kisha omba kutoa mchango wako. Inaweza kuwa ni usafi wa mazingira, elimu, watoto yatima nakadhalika.

Andaa shindano dogo kwa wateja. Kama mfanyabiashara unaweza ukaandaa shindano dogo kwa wateja wanaotembelea dukani kwako na kisha kujishindia zawadi mbalimbali. Unaweza ukaweka tangazo nje ya duka lako ambapo unaweza kuwavutia hata wapita njia.    

Andaa burudani kidogo. Haijalishi biashara yako ipo kwenye hali gani lakini unaweza ukaanda chochote kuwaburudisha wateja wako. Zipo namna nyingi za burudani kama vile kuandaa michezo kwa ajili ya watoto au hata burudani ya muziki.

Tumia mitandao ya kijamii kushirikisha matukio yote. Kwa dunia tunayoishi sasa kamwe hauwezi kuidharau nguvu ya mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, Instagram na Youtube. Itumie fursa inayoitoa mitandao hii kuwashirikisha wateja wako na jamii kwa ujumla mambo yanayotukia kwenye biashara yako na utaona mabadiliko.

Zipo njia nyingi ambazo unaweza kujifunza kutoka kwa wafanyabiashara na sehemu tofauti ili kuongeza thamani ya biashara yako. Jumia Travel inakushauri kujaribu kufanya kitu tofauti katika biashara yako kabla ya mwaka kuisha. Ubunifu ni kitu muhimu ili kukua zaidi lakini pia jifunze kutoka kwa wafanyabiashara wengine wanatumia njia zipi kufanikiwa.

Comments