- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Zao la korosho ambalo linachangia uchumi katika mikoa ya Kusini mwa Tanzania.
USHIRIKA ni dhana ya kuleta maendeleo
kwa kushirikiana. Dhana hii imefanikiwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi na
kijamii katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita. Kutokana na changamoto
mbalimbali zilizoikumba sekta hii ya ushirika watu wengi wamekosa imani na
vyama hivi na baadhi ya vyama vimeshindwa kufanya kazi vizuri.
Hata hivyo, kwa sasa imani kwa vyama
vya ushirika imeongezeka na vyama vingi vinaendelea kuundwa hasa vile vya
kuweka na kukopa, yaani SACCOS.
Uanzishwaji wa vyama vingi vya ushirika kwa sasa unatokana na
elimu watu wengi waliyoipata kuhusu Ushirika na watu kuelewa kuwa changamoto
zilizoko ndani ya ushirika zinatatulika.
Ushirika dhamira yake ni nzuri na kama itafanya kazi vizuri ni
njia nzuri ya kuleta mabadiliko kwa watu wengi.
Ushirika ni nini?
Ushirika maana yake ni muungano wa watu ambao wanafanya kazi
pamoja kwa hiari ili kufanikisha mahitaji yao ya kiuchumi, kijamii na
kiutamaduni kupitia shughuli ya biashara inayomilikiwa kwa pamoja na
kudhibitiwa kidemokrasia.
Ushirika unazingatia maadili ya kujisaidia wenyewe, jukumu
binafsi, demokrasia, usawa na mshikamano.
Wanachama wa Ushirika wanaamini katika misingi ya uaminifu,
uwazi, uwajibikaji kwa jamii na kuwajali wengine.
Muundo wa Ushirika kwa ujumla unategemea uimara wa chama cha
msingi cha Ushirika, hivyo kuna umuhimu wa kuhakikisha vyama imara vya msingi
vinaanzishwa.
Kwa kuzingatia hayo, msisitizo usiwekwe kwenye uanzishwaji wa
vyama vikuu vya Ushirika, lakini kuwepo na uwezeshaji wa wanachama katika vyama
vya msingi kwa lengo la kuunda chama imara cha msingi.
Kukiwa na chama imara cha msingi, chama hiki kinaweza kuunda
chama kikuu kilicho imara.
Leo la kuwa na vyama imara vya msingi litatimia kama kutakuwa na
jjuhudi za makusudi kuimarisha vyama vya msingi vilivyopo.
Vyama hivi vinaweza kuimarika kunapokuwa na kuongezeka kwa
wanachama, uwajibikaji wa viongozi na demokrasia katika maamuzi yanayohusu
chama.
Kwa kuzingatia hiyo, Vyama vya Ushirika nchini vitakuwa imara na
faida kwa wanachama.
MIKUTANO YA
UCHAGUZI WA KAMATI YA KUUNDA CHAMA
Watu wanaopenda kuunda chama cha Ushirika kiwe cha msingi, umoja
wa kibiashara au shirika, chama kikuu, muungano wa vyama vikuu au shirikisho,
watakuwa chini ya uenyekiti wa Ofisa Ushirika aliyeteuliwa na Mrajis kwa
madhumuni ya kuchagua kamati ya kuunda chama.
Kamati ya kuunda chama haitakuwa na wajumbe chini ya idadi ya
wanachama wanaotakiwa kuunda chama.
Kila kamati ya kuunda chama itamchagua Mwenyekiti na kuteua
Katibu na itatunza kumbukumbu za shughuli zake.
Kazi za kamati ya
kuunda chama:
- Kufikiria kwa makini aina ya
chama kinachotarajiwa kuundwa na kuweka madhumuni yake.
- Kukadiria idadi ya wanachama
watakaojiunga na ukubwa wa shughuli zitakazofanyika.
- Kwa msaada wa Ofisa Ushirika
na ambapo ni lazima mtu yeyote mwenye ujuzi, kufanya uchambuzi wa uhai wa
kiuchumi wa shughuli zitakazofanywa
na chama kinachotarajiwa kuundwa.
- Kuandaa taarifa ya uwezekano
wa kufanya kazi kwa ajjili ya kuitumia kwa Mrajis.
- Kuandaa orodha ya wanachama
wanaotazamiwa na kiasi cha hisa au michango inayotarajiwa.
- Kuandaa masharti yanayofaa
ya chama kinachotarajiwa wakishauriana na Ofisa Ushirika.
- Kufanya shughuli nyingine
kama itakavyolazimu kwa ajili ya kuomba kuandikishwa kwa chama hicho
kinachotarajiwa.
KUANDIKISHWA KWA
CHAMA
Kila chama kinachoomba
kuandikishwa lazima kikubaliane na kifungu cha 24 cha Sheria na kitapeleka
maombi kwa Mrajis kwa kutumia fomu zilizoagizwa na kanuni.
Kila maombi ya kuandikisha chama cha Ushirika yatatiwa sahihi
ipasavyo kwa niaba yake na watu waliochaguliwa na kamati kuunda chama. Maombi yanatakiwa
kuambatana na:
- Muhtasari wa mkutano
uliothibitishwa wenye azimio la kuunda chama.
- Nakala nne za masharti ya
chama yaliyokubalika.
- Nakala nne za taarifa ya
uwezekano wa kufanya kazi kwa mradi kama ilivyotajwa katika Kifungu cha 6
cha Kanuni.
Mrajis atakaporudisha
maombi atarudisha kwa chama:
- Nakala moja ya masharti
pamoja na maombi ya kuandikisha chama yaliyotiwa muhuri maalumu pamoja na
cheti cha kuandikishwa.
- Nakala moja ya taarifa ya
uwezekano wa kufanya kazi au uchambuzi wa mradi ulioidhinishwa kwa kupiga
muhuri.
- Nakala moja ya bajeti ya
mapato na matumizi ikiwa ni makisio ya kwanza ya chama hicho.
MRAJIS ANAWEZA
KUONGEZA MASHARTI MENGINE KABLA YA KUANDIKISHWA
Ili kuweza kuamua kama chama kinachotarajiwa kuandikishwa kina
uhai wa kiuchumi ama vinginevyo, Mrajis anaweza kuagiza moja au zaidi ya
mahitaji yafuatayo kabla hajakiandikisha chama:
- Kwamba taarifa za ziada
zitolewe kuonyesha kama chama kinachokusudiwa kuundwa kinatimiza mahitaji
ya kiuchumi au kijamii na uwezekano wa kufikia/kutimiza madhumuni yake.
- Kwamba maombi ya
kuandikishwa yanaungwa mkono na wanachama wengi ambao wanatarajia kuwa
wanachama siku za usoni.
- Kwamba mtaji wa kutosha
unatolewa na waombaji waanzilishi kwa ajili ya kuanzisha chama na watu
wengine wanaotarajia kujiunga na chama na kwamba mtaji huo unatosha
kuanzisha shughuli za chama.
- Kwamba mipango inafanyika
kwa ajili ya kuwaelimisha na kushauri hasa kuhusu kanuni na shughuli za
Ushirika na mashumuni ya chama kwa wanachama waanzilishi na watu wengine
wanaotarajiwa kuwa wanachama siku za usoni.
- Kwamba kuna uwezekano mkubwa
wa upatikanaji wa maofisa watakaomudu kuongoza na kuelekeza shughuli za
chama kinachotarajiwa na kutunza kwa usiri kumbukumbu za vitabu vya hesabu
kama ilivyoagzwa na Mrajis chini ya Sheria ya Vyama vya Ushirika na
ikibidi maofisa wapatiwe mafunzo ya ziada kama Mrajis atakavyoona inafaa.
TAARIFA ZA KUKATAA
KUANDIKISHA CHAMA
Endapo Mrajis atakataa kukiandikisha chama atatoa masharti yake,
sababu zake za uamuzi huo kwa maandishi.
HAKI NA WAJIBU WA
WANACHAMA
Wanachama katika chama cha ushirika watakuwa ni:
- Watu waliojiunga wakati wa
kuomba chama kiandikishwe (waannzilishi).
- Watu walioingizwa uanachama kufuatana
na masharti ya chama.
- Watu waliofikia umri wa
miaka 18 na wenye akili timamu na ambao wanafanya biashara au shughuli
zinazohusiana na madhumuni ya chama na wana mahitaji ambayo chama
kinatazamia kukidhi na wana uwezo wa kulipa viingilio na kununua hisa.
- Watu ambao hawajafikia umri
wa miaka 18 lakini wametimiza umri wa miaka 15 wanaojulikana kama watoto
wanaweza kujiunga na chama cha Ushirika kufuatana na kifungu kidogo cha 3
na 4 cha Kifungu cha 15 cha Sheria ya Vyama vvya Ushirika.
HAKI ZA WANACHAMA
Wanachama watakuwa na haki zifuatazo:
- Haki ya kupiga na kupigiwa
kura, kuhudhuria mikutano, kushiriki katika uongozi wa chama na haki ya
kuitisha mikutano kwa mujibu wa masharti ya chama.
- Hakuna mwanachama wa chama
cha Ushirika atakayetumia haki za uanachama mpaka awe amelipa kiingilio,
hisa na madeni mengine chamani.
- Kila chama kitaweka ukomo wa
idadi ya wanachama kufuatana na shughuli zake kwa mujibu wa Kifungu cha 15
na 23 (2) cha Sheria ya Vyama vya Ushirika.
- Hakuna kampuni iliyounganishwa
au iliyoandikishwa chini ya Sheria ya Makampuni na hakuna kampuni ambayo
haikuunganishwa au kikundi cha watu kilichoandikishwa kitakuwa na haki ya
kuwa mwanachama wa chama cha Ushirika kilichoandikishwa isipokuwa kwa
kibali cha maandishi kutoka kwa Mrajis kwa masharti kuwa:
a)
Kampuni hiyo au kikundi hicho kimeonyesha nia ya kutumia huduma
zitolewazo na chama, na Mrajis ameridhika na hatua hiyo.
b)
Uanachama wa kampuni hiyo au kikundi hicho utakubaliana na
sheria, kanuni na masharti ya chama cha Ushirika.
c)
Chaka kitafaidika kutokana na huduma zitolewazo na kampuni hiyo.
HAKI ZA WATOTO
- Mtoto anaweza kuwa
mwanachama ilimradi wazazi au mlezi wa mtoto wana taarifa kuhusu shauku
yake ya kuwa mwanachama na atafungua hesabu ya hisa au kiingilio na
kununua hisa kama itakavyokuwa.
- Ambapo mzazi au mlezi amearifiwa
kuhusu hesabu ya hisa au amana zinazomilikiwa na mtoto na hakuna vikwazo
vyovyote vilivyowekwa na chama katika hesabu hiyo, mtoto huyo anaweza
kuongeza amana hizo na anaweza kupunguza fedha hizo kutoka katika hesabu
hizo au kuzitumia kwa njjia yoyote ile kama itakavyoonekana inafaa bila ya
kibali cha mzazi au mlezi wake.
- Mtoto ambaye anatumia huduma
za chama kufuatana na kifungu kidogo cha (2, 3) na (4) cha Kifungu cha 15 cha
Sheria atakuwa na haki ya uanachama isipokuwa hatakuwa na haki ya kupiga
kura.
- Kwa masharti kwamba
kipengele hiki cha kanuni hakitahusu chama cha Ushirika cha shule.
Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 6 ya 2013, watu 20
wanaweza kuanzisha ushirika wa mazao na 50 wanaweza kuanzisha ushirika wa akiba
na mikopo (SACCOS).
Hata hivyo, kadiri idadi ya watu inavyoongezeka ndivyo chama
kinavyokuwa na fursa kubwa zaidi ya kujenga mtaji, mfuko wa kukopeshana,
kuzalisha mazao kwa wingi na kupanua soko au wateja wanaohudumiwa.
Baada ya wananchi kwa hiari yao wenyewe, kuamua kuanzisha Chama
cha Ushirika watatoa taarifa kwa Ofisa Ushirika wa eneo husika aje kutoa mwongozo
au maelekezo ya uanzishwaji wa chama.
Zifuatazo ni hatua za kuanzisha chama cha Ushirika:
1. Mkutano mkuu wa
uanzilishi.
Kikundi au wananchi huitisha mkutano mkuu wa uanzilishi ambapo
Afisa ushirika ndiye anakuwa mwenyekiti wa mkutano huo. Malengo makuu ya
mkutano huo ni, kutoa ufafanuzi wa maana ya ushirika, faida za ushirika, nia ya
uanzilishi wa chama, mgawanyo wa faida, haki na wajibu wa wanachama.
2. Uchaguzi wa bodi
ya uanzilishi.
Wanachama huteua bodi ya uanzilishi ambayo huundwa na wanachama 5-9,
ambao watakuwa na majukumu yafuatayo:
·
Kushirikiana na afisa ushirika kutayarisha masharti (Katiba) na
Sera mbalimbali za chama cha ushirika.
·
Kutayarisha taarifa ya uwezo wa kiuchumi wa chama (kidadishi
uchumi)
·
Kuandaa mpango biashara
·
Kuandaa makisio ya mapato na matumizi ya chama ya mwaka wa
kwanza
·
Kuhamasisha wananchi wengi zaidi kujiunga, kukusanya viingilio,
kupokea fedha za Hisa, Akiba na Amana.
·
Kutafuata ofisi ya chama na kununua vitendea kazi.
·
Kuajiri mtunza vitabu/karani
·
Kufanya mambo mengine muhimu ya uanzishwaji wa chama.
3. Kuwasilisha maombi ya usajili wa chama kwa Mrajis Msaidizi
kupitia kwa Ofisa Ushirika wa Wilaya.
4. Mkutano mkuu wa kwanza.
4. Mkutano mkuu wa kwanza.
Mkutano mkuu wa chama utaitishwa katika kipindi cha miezi miwili
baada ya kupata usajili kwa madhumuni ya kukabidhiwa hati ya usajili kutoka kwa
OfisaUshirika na mambo mengineyo.
Kwa maelezo zaidi na ushauri kuhusiana na uanzilishi na
uendeshaji wa chama cha ushirika wasiliana na blogu hii kwa simu +255 656
331974 au Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa Shirikisho la Vyama vya
Ushirika Tanzania (TFC) simu namba +255 716 775 334. Au barua-pepe: maendeleovijijini@gmail.com.
Comments
Post a Comment