Featured Post

DOKTA MPANGO AALIKA WAWEKEZAJI KUTOKA NORWAY

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) akizungumza kuhusu umuhimu wa Sekta Binafsi katika maendeleo ya nchi alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Norway nchini Tanzania Bi. Hanne-Marie Kaarstad,  mjini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) akiangalia zawadi ya kitabu kinachohusu masuala ya uchumi na fedha aliyopewa na  Balozi wa Norway nchini Tanzania Bi. Hanne-Marie Kaarstad (kulia),  baada ya kumaliza mazungumzo yao Makao makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, mjini Dodoma.
Balozi wa Norway nchini Tanzania Bi. Hanne-Marie Kaarstad, (kulia) akiwakabidhi zawadi za vitabu kuhusu uchumi, Kamishna wa Bajeti-Bi Mary Maganga (kushoto) na Kamishna wa Fedha za Nje Bw. John Rubuga (wa pili kushoto) wakishuhudiwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kulia) Mjini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano-Wizara ya Fedha na Mipango)

Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Norway hapa nchini Bi. Hanne-Marie Kaarstad na kutoa wito kwa wawekezaji kutoka Norway kuja kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo Nishati, misitu, kilimo, gesi na mafuta.
Dkt. Mpango amemweleza Balozi huyo kwamba Tanzania iko katika hatua mbalimbali za kukuza uchumi wake kupitia sekta ya viwanda na kwamba wawekezaji kutoka Norway watakuwa na mchango mkubwa wa kuiwezesha Tanzania kufikia lengo hilo.
Aliyataja maeneo ya kuongeza thamani ya mazao ya misitu, mifugo, uvuvi, nishati, kilimo na mengine mengi kwamba yataongeza tija katika sekta hiyo na kwamba malighafi za kilimo zitatochea uzalishaji katika viwanda na kuinua kipato cha wananchi.
“Tumeamua kujenga Reli ya Kati kwa viwango vya kimataifa-SGR ambayo inahitaji umeme wa kutosha kwa hiyo bado tunahitaji mchango wa wadau mbalimbali ikiwemo Norway ili kuhakikisha kuwa tunakuwa na nishati ya umeme ya kutosha na ya uhakika ili kufanikisha mradi huo mkubwa” aliongeza Dkt. Mpango
Kuhusu Sekta Binafsi, Dkt. Mpango amesema kuwa Serikali imeendelea na majadiliano na Sekta hiyo ili kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili ikiwemo masuala ya kodi pamoja na kujenga kuaminiana kati ya pande hizo mbili.
Amefafanua kuwa Sekta Binafsi ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa na kwamba vikao hivyo vya mara kwa mara vimeanza kuzaa matunda.
Ameishukuru nchi ya Norway kwa mchango mkubwa wa maendeleo kwa kusaidia kuboresha masuala ya nishati, kilimo, uboreshaji wa mifumo ya kodi kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, kuchangia fedha katika program ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma na kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali kila mwaka.
Kwa upande wake Balozi wa Norway hapa nchini Bi. Hanne-Marie Kaarstad alisema nchi yake imeridhika na namna Serikali ya Awamu ya Tano inavyopiga hatua kubwa katika maendeleo ya watu wake kupitia kuhamasisha uchumi wa viwanda.
Amesema kuwa nchi yake imesaini mikataba mikubwa miwili hivi karibuni ukiwemo mkataba wa msaada wa krona milioni 600 (fedha za Norway) kwa ajili ya mradi wa kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini-REA, hatua anayoamini kuwa itaharakisha maendeleo na uchumi wa kati wa wa nchi  ifikapo mwaka 2025 na kuongeza kuwa nchi yake itaendeleza uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Amesisitiza umuhimu wa Serikali kuishirikisha kikamilifu Sekta Binafsi katika hatua yoyote inayopiga kuelekea maendeleo ya haraka kwa kuwa sekta hiyo ina mchango mkubwa katika kufikia mafanikio tarajiwa.
Aliahidi kuendelea kuhamasisha wawekezaji kutoka nchini mwake kuja kuwekeza Tanzania na kushauri kuwa wakati mambo hayo yakiendelea, Tanzania ihakikishe kuwa sera zake za uchumi zinakuwa imara na hazibadilikibadiliki ili wawekezaji waweze kuamini wako salama.
Alishauri kuwa kila aina ya mabadiliko katika sera za nchi yakiwemo masuala ya kodi yanapaswa kuwa shirikishi ili sekta hiyo iweze kutoa mchango wake kikamilifu baada ya kushirikishwa katika maamuzi mbalimbali na kupongeza hatua ya Serikali ya kukutana na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kujadiliana kuhusu masuala mtambuka.

Comments