Featured Post

WATU MILIONI 126 KUAJIRIWA NA SEKTA YA USAFIRI WA ANGA KUFIKIA 2024


Na Jumia Travel Tanzania
Usafiri wa anga ni miongoni mwa sekta inayochangia ukuaji wa uchumi wa dunia kwa kiasi kikubwa. Ilichangia moja kwa moja kiasi cha dola za Kimarekani trilioni 2.2 ya Pato la Taifa (GDP) la dunia (sawa na 10% ya uchumi wa dunia) mwaka 2015 na kutoa ajira kwa zaidi ya watu milioni 108 duniani kote. Kufikia mwaka 2024, Baraza la Dunia la Utalii na Usafiri linatarajia ajira za moja kwa moja kwenye sekta ya utalii kuwa zaidi ya watu milioni 126 duniani kote.

Ukiachana na mchango wa usafiri wa anga kwenye sekta nyingine pia ina umuhimu mkubwa kwenye utalii. Zaidi ya 54% ya watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani husafiri kwa kutumia usafiri wa anga. Jumia Travel inatambua kwamba utalii ni sekta muhimu kwa nchi nyingi za Afrika, ambapo ni nyanja muhimu katika mikakati ya ukuaji wa uchumi.

Barani Afrika, inakadiriwa kwamba takribani watu milioni 5.8 huajiriwa kwenye maeneo ambayo hupokea wageni wengi kutoka nje ya nchi, hususani wanaoingia kwa kutumia usafiri wa anga, na ilichangia dola za Kimarekani bilioni 46 ya Pato la Taifa katika uchumi wa nchi za Kiafrika kwa mwaka 2014.

Utalii kama sekta nyinginezo za huduma inaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuunga mkono ukuaji wa uchumi endelevu. Ikikuzwa kwenye namna ya uwajibikaji na mikakati mizuri, utalii unaweza kuwa na mchango mkubwa katika kutoa ajira huku ikitunza na kuenzi rasilimali zetu bila ya kuziharibu.

Ingawa, kuna umuhimu mkubwa kwa sekta binafsi na serikali kukaa kwa pamoja na kujadiliana. Lengo ni kuhakikisha mipango ya maendeleo ya sekta hii inafanywa kwa kuzingatia utunzwaji wa mazingira, ustawi wa jamii pamoja na faida za kiuchumi inazoweza kuzileta.

Katika serikali ya awamu ya tano nchini Tanzania ikiwa chini ya uongozi wa Mh. John Pombe Magufuli tumeshuhudia jitihada kubwa katika ukuzaji wa sekta ya usafiri wa anga. Jitihada hizo ni pamoja na manunuzi ya ndege za abiria, upanuzi wa viwanja vya ndege na maboresho kadhaa kwenye wizara husika kwa ujumla.

Hivi karibuni Rais Magufuli akiwa katika ziara yake ya kikazi Kagera alizindua uwanja wa ndege ambao si tu utaongeza fursa za kiuchumi mkoani humo bali pia utaufungua mkoa huo kiutalii. Majengo ya uwanja huo ni ya tatu kwa uzuri baada ya Dar es Salaam na Kilimanjaro.

Katika uzinduzi huo Mheshimiwa Rais alisema kuwa mbali na uwanja huo wa ndege kukuza na kurahisisha shughuli za kibiashara mkoani humo kama vile usafirishaji wa samaki, ndizi na mazao mengine ya biashara, lakini pia utapelekea watalii kufika kwa urahisi na kutalii vivutio mbalimbali kama vile kwenda Burigi na kujionea wanyama na vivutio vingine vilivyopo huko.
Ukiachana na uzinduzi wa uwanja huo, pia mkoani Geita liliwekwa jiwe la msingi la ujenzi wa uwanja wa ndege wa Chato na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mh. Profesa Makame Mbarawa.

Mbali na ujenzi wa uwanja huo Waziri huyo alibainisha kuwa serikali ina mpango wa kuhakikisha kwamba kila mkoa unakuwa na uwanja wa ndege utakaokuwa unahudumia wananchi wasiopungua 100.

Aliongezea kuwa mbali na ujenzi huo pia imeboresha na kuimarisha ujenzi katika viwanja vya ndege vya Lindi, Iringa, Moshi, na Simiyu. Lengo ni kuviwezesha kusaidia shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo na inatarajia katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2017/2018 kutenga fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi kwenye viwanja vya ndege vya Iringa, Musoma na Songea.

Kuna jitihada mbalimbali ambazo serikali inaweza kuzifanya katika kukuza na kuimarisha sekta ya utalii. Mbali na serikali nyingi kutumia gharama kubwa kwenye kuzitangaza nchi zao kama sehemu zinazovutia kutembelea, kuna masuala kadhaa yanaweza kukwamisha zoezi hilo. Kwa mfano, serikali zinaweza kuanza kushughulikia muda wa utolewaji wa viza kwa wageni uwe mfupi zaidi, kutazama tozo mbalimbali zinazotozwa kwa watalii wanaoingia au kutoka, lakini pia kwa kujihusisha na mashirikisho kadhaa ya kimataifa katika sekta hii.

Hivyo basi, Jumia Travel inashauri kwamba serikali iwe inafanya tathmini ya mara kwa mara kwenye miundombinu ya viwanja vyao vya ndege ili kuendana na uhitaji wa soko kwa wakati uliopo. Hii itahakikisha kuwa sekta ya usafiri wa anga itaendelea kuunga mkono maendeleo ya sekta ya utalii na kuleta manufaa makubwa ya kiuchumi.

Comments