Featured Post

WAHANGA WA SOKO LA SIDO MBEYA WALIPWA NA BIMA

Mkuu wa mkoa wa Mbeya akimkabidhi Bw. Mohamed Omary Magayu mfanyabiashara wa Soko la SIDO Mbeya mfano wa hundi ya ya fidia aliyolipwa baada ya kukata bima.

Na Oyuke Phostine
Zaidi ya wafanyabiashara themanini waliokata bima wamelipwa fidia yenye thamani ya kiasi cha fedha cha takribani TZS 1,538,653,057.08 kupitia kampuni za bima zilizosajiliwa kisheria kutoa huduma hapa nchini baadaya wafanyabiashara hao kupatwa na janga la bidhaa zao kuungua katika soko la sido Mbeya mwezi Agosti mwaka huu.
Kamishna wa Bima nchini Dr. Baghayo Saqware akitoa elimu ya bima kwa wafanyabiashara wa soko la Sido Mbeya juu ya namna bima linavyosimamiwa na kurekebiwa na Mamlaka ya Bima nchini (TIRA) sambamba na zoezi la kutoa hundi kwa wahanga amewashauri wafanyabiashara nchini kutumia huduma za bima ili kukinga biashara zao dhidi ya majanga yasiyotarajiwa.
“Na kwa bahati nzuri mfano mzuri na halisi wa faida ya kukata bima ili kukinga biashara zenu uko miongoni mwa wenzenu hapa. Janga ni jambo lisilo na hodi wala taarifa hivyo ni vyema na busara kujikinga nalo kupitia mifumo ya bima” alisema Dr. Saqware.
Pia Dr. Saqware aliwataka watanzania kuondokana na dhana hasi pamoja hofu iliyojengeka siku za hivi karibuni kuhusu huduma za bima kwa sababu sekta hii inasimamiwa kikamilifu na Mamkala ya Bima na makampuni yote yanayofanya shughuli hizo yamesajiliwa na (TIRA) na yanawajibika kisheria kutoa huduma zinazokidhi viwango.  
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mh. Amos Makalla, amesema kwa sababu Mamlaka ya bima ni chombo cha ushauri kwa Serikali kuhusu masuala ya soko la bima, ni imani yake kuwa wananchi sasa hawatasita kukata huduma za bima. Na iwapo kutakuwa na msigano kati ya makampuni ya bima na wateja anaamini Mamlaka iko tayari kuutatua kwa faida ya uchumi wa taifa.
“Soko lilipoungua ni zaida ya Tsh. 14 bilioni ziliteketea, hivyo kama wafanyabiashara wote wangekuwa na bima angalau wangeweza kunufaika kwa kupewa fidia” alisema Mh. Mkalla.
Pia Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ameyataka makampuni ya bima nchini kwenda na kasi ya Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za bima nchini kwani imelenga kuwakwamua wananchi dhidi ya umasikini.
Pamoja elimu iliyotolewa Mamlaka ya Bima nchini inayataka makampuni na wataalamu wa bima nchini kuongezeni huduma na elimu kwa wananchi, na pia walipe madai ya bima haraka bila usumbufu ikiambatana na lugha nzuri kwa wateja.
Naye Bw. Erasto Sanga mmoja wa wahanga moto katika soko la sido ametoa wito kwa wafanyabiashara kote nchini kukata bima kwa sababu imekuwa ni mkombozi wa biashara zake kwani mara zote tatu alizounguliwa na bidhaa zake bima imekuwa ikimunufaisha kwa kumrejesha kwenye biashara.
“Mara ya kwanza moto uliunguza bidhaa zangu mwaka 2006 katika soko la Mwanjelwa nilipata hasara kwasababu sikukata bima baada ya hapo nilikata bima na mar azote tatu nilipounguliwa nililipwa fidia na kampuni niliyokata bima kwao” alisema bw. Sanga.
Pia ni muda mwaafaka kwa Serikali za Mkoa nchini kushirikiana kwa pamoja kuwadhibiti wahalifu katika shughuli za bima kwa sababu kuna wahalifu wachache wanauza bima feki hususani za magari. Hili linaweza fanikiwa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na Mahakama katika kuharakisha upatikanaji wa haki za wakata bima.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Amos Makalla akitembelea soko la bima akiwa na Kamishana wa Bima nchini Dr. Baghayo Saqware (Kulia), Mwenyekiti wa soko na Kamana wa mkoa wa Mbeya Mpinga ( Left)
Kamishna wa Bima Nchini Dr. Baghayo Saqware akiongea na wafanyabiashara wa soko la SIDO Mbeya (hawako pichani) kuhusu umuhimu wa Bima kwa biashara zao.
Wafanyabishara wa soko la SIDO Mbeya wakimsikiliza Kamishna wa Bima nchini Dr. Baghayo Saqware alipokuwa akielezea umuhimu wa Bima kwa biashara zao.
Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuliza Bima Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Bi. Consolata Gabone akitoa historia fupi ya soko la SIDO.

Comments