Featured Post

USHIRIKA WA WACHINJA KUKU KISUTU WENYE MALENGO MAKUBWA YA UWEKEZAJI

Kuku wakiendelea kuandaliwa ndani ya Soko la Kisutu. Picha zote na MaendeleoVijijini.

Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini
SAUTI za kuku zinasikika hata ukiwa nje ya jengo dogo ndani ya Soko la Kisutu jijini Dar es Salaam, lakini ghafla zinakoma na zinasikika nyingine.
Siyo kwamba kuku hao wanahitaji chakula ama wanacheza, bali hapa ni machinjio, na sauti zinapokoma ujue tayari zimekwishapigwa kisu na zinaandaliwa kwa ajili ya kitoweo.
Nje ya jengo hilo unaweza kuwa umekuta akinamama wengi wakiwa wamelundikana huku wakiwa wamekalia ndoo zao.
Hawa nao wanasubiri huduma, wanataka kununua utumbo, miguu pamoja na vipapatio vya kuku hao wanaochinjwa ili wakafanye biashara.
Akinamama hawa wanatoka katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na hapa Kisutu ndiko mahali pekee ambako wanaweza kupata bidhaa hiyo wanayokwenda kuuza mitaani.
Bila shaka baadhi yetu tumekutana ama tumewakuta akinamama wakiuza firigisi na utumbo mitaani, basi amini kwamba asilimia kubwa wanapata bidhaa hiyo katika eneo hili la Kisutu.
Ukiingia ndani ya jengo hilo usishangae ukasalimia usiitikiwe na watu wengi, japokuwa waliomo ni wengi.
Kabla hujajua usimame wapi, utasikia sauti ya mtu akikutaka radhi kwamba anaomba kupita ama anataka kuweka mzigo.
Naam. Kila mtu hapa yuko ‘busy’ na kazi inakwenda mtindo mmoja, na hata kutokukuitikia si kwamba wanafanya kiburi ama hawajakuona, la hasha. Kwa sababu wanataka kuhakikisha kazi wanayoifanya inakuwa katika hali bora hasa ikizingatiwa kwamba hicho ni chakula kwa afya ya binadamu.

Mazingira ya ndani yanaridhisha kutokana na usafi ambao unazingatiwa sana na wahusika licha ya changamoto za hapa na pale.
Hawa ni wanaushirika wa Kisutu Poultry Farm Cooperative Society (KIPOCOSO), ambao wamekuwepo katika soko hilo kwa zaidi ya miaka 28 na ndio waanzilishi wa kuchinja kuku jijini Dar es Salaam.
Japokuwa hivi sasa baadhi ya masoko yana machinjio ya kuku, lakini wengi wanaohusika na uchinjaji wamejifunza ama wamewahi kufanya shughuli hizo katika Soko la Kisutu.
Kuku walionyonyolewa, kuchunwa ngozi au kukatwakatwa wanaweza kukutoa udenda wangali wabichi na wamewekwa mafungu mafungu.
“Kila fungu unaloliona hapo lina mwenyewe, hawachanganyani kabisa,” ndivyo anavyoeleza Bw. Hamisi Malamla, Mwenyekiti wa KIPOCOSO.
Anaongeza: “Kazi yetu hapa ni kuchinja, kuku wote wana wenyewe na kila mmoja hapa ndani anakwenda hapo nje kwenye mabanda wanakonunua kuku na kutafuta oda, akiipata anakuja kuchinja na kuwatengeneza.”
Bw. Malamla anasema kwamba, asilimia kubwa ya kuku wanaoliwa jijini Dar es Salaam wanachinjwa na kuandaliwa katika soko hilo, sehemu ambayo pia ni maarufu kwa wauzaji wa kuku – wa nyama wa kisasa pamoja na wa kienyeji.

Kuku 3,000 kwa siku
Ndani ya jengo hilo lililowekwa terazo, kujengwa masinki bora pamoja na majiko matatu makubwa yanayotumia gesi, takriban kuku 3,000 huchinjwa kila siku.
Licha ya kufanya shughuli zao kwa ufanisi, lakini unapozungumza na wanaushirika hawa utagundua kwamba wana mawazo makubwa ya maendeleo tofauti na unavyoweza kuwadhania.
“Malengo yetu ni kujikita katika uwekezaji wa kilimo na mifugo, tunataka tuanze kufuga wenyewe kuku (wa kisasa na kienyeji), kuuza kuku wenyewe, kutotolesha vifaranga, kutengeneza vyakula vya kuku pamoja na kusambaza madawa,” anasema Bw. Malamla.
Anasema kwamba, ikiwa wataanza uwekezaji wa kufuga kuku itakuwa ni hatua kubwa kwao kwani watakuwa na uhakika wa kuchinja na kuuza, na kwamba oda wanazozipata kwa sasa zitakuwa ni nyongeza tu na ziada.
Malamla anasema, kwa uzoefu walionao, ikiwa watajikita pia katika ufugaji wanaweza kulisha wananchi wengi jijini Dar es Salaam na kwamba hata kuku watakaowafuga wanaweza kuongezeka ubora tofauti na baadhi ya wanaouzwa sokoni hapo ambao mara nyingi huwa hawana uzito mkubwa.
“Tukianza ufugaji ni dhahiri tutaongeza ubora kulingana na mahitaji ya soko na hatuwezi kubahatisha, kwa sababu hapa wakati mwingine kuku wanaadimika na inapotokea hivyo maana yake tunakosa kazi ya kufanya,” anasema.
Anaongeza kwamba, tangu uongozi wake ulipoingia madarakani mwezi Machi 2017 (miezi nane iliyopita) wamefanikiwa kujiwekea akiba ya kutosha ambayo inawapa msukumo wa kuangalia fursa za uwekezaji ili kuongeza kipato pamoja na kupanua wigo wa ajira.

Usajili

Mwenyekiti wa Ushirika wa Wachinja Kuku Soko la Kisutu (KIPOCOSO), Bw. Hamisi Malamla (kushoto) akiwa na Mjumbe wa Kamati ya Uongozi, Mzee Shaaban Hassan Bogoma leo hii walipotembelewa na MaendeleoVijijini.

KIPOCOSO, ambacho ni miongoni mwa vikundi nane vinavyounda Umoja wa Wafanyabiashara Soko la Kisutu (UWASOKI), kilisajiliwa Juni 28, 1989 kama chama cha ushirika na kupewa hatia namba DSR-382.
Kikundi hicho cha ushirika kina jumla ya wanachama 57 na kinaongozwa na Bw. Malamla kama mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti ni Zuberi Luwono, Hassan Ally Sozigwa (Katibu), na wajumbe ni Shaaban Hassan Bogoma, Ally Omari Vullu, Suleiman Kitalambo na Juma Said Mwinyi.
Malamla anasema kwamba, kwa utaratibu waliojiwekea, kila mwanachama kati ya hao 57 lazima kila siku achangie Shs. 4,000 ambapo Shs. 2,000 ni kwa ajili ya gesi na Shs. 2,000 kama ada.
“Utaratibu huu ni kila siku, hivyo kwa kukusanya Shs. 2,000 za ada kila siku tuna uwezo wa kuingiza Shs. 114,000 kila siku na kwa maana hiyo kwa mwezi tunaweza kuingiza wastani wa Shs. 3 milioni.
“Tunao wasaidizi 30 wanaofanya shughuli za kuchinja pia humu ndani, lakini hawa hawahesabiwi kama ilivyo kwa wanachama wenyewe, na mara nyingi wasaidizi hawa huwa ni wale wanaowasaidia wanachama husika,” anaongeza.
Kwa mujibu wa Malamla, hivi sasa wanayo akiba ya kuridhisha ingawa inaweza isitoshe kuanzisha shughuli za ufugaji mkubwa ambazo zinahitaji fedha nyingi zaidi.
“Hatujapiga hesabu, lakini najua shughuli hizi zinahitaji fedha nyingi zaidi, tunaamini kwa dhamira ya dhati tuliyonayo, ipo siku tutafanikiwa tu katika mipango yetu,” anasema.
Mbali ya akiba ya fedha benki, lakini ushirika huo unamiliki viwanja takriban 21 vyenye ‘Offer’ katika eneo la ekari 10 huko Mbutu, Kigamboni jijini Dar es Salaam ambapo miongoni mwa viwanja hivyo ni eneo la ekari moja ambalo wanataka waanzie ufugaji wa kuku na samaki.
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), Bw. Henry Mwatwinza Mwimbe, anasema kwamba, KIPOCOSO ni miongoni mwa vyama vya ushirika vya msingi vilivyoonyesha mafanikio makubwa katika kipindi kifupi.
“Kimeanzishwa muda mrefu, lakini kimepitia katika uongozi mbovu ambao pengine haukuwa na malengo, uongozi wa sasa tangu ulipoingia madarakani mwezi Machi 19, 2017 umeweza kufanya mambo makubwa sana kwa usimamizi wetu na bado tunaendelea kuwasaidia maoni na mambo mbalimbali kuhakikisha kwamba wanapiga hatua,” anasema Mwimbe.
Mwimbe anasema kwamba, kwa hatua waliyofikia, KIPOCOSO wanaweza kabisa kukopesheka kwani licha ya akiba waliyonayo, bado wanayo rasilimali ardhi na wana malengo ya kuwekeza katika kilimo na ufugaji.

Changamoto
Pamoja na mafanikio waliyonayo, lakini wajasiriamali hao wanasema kwamba, wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, hususan masuala ya usafi wa mazingira.
Mzee Shaaban Bogoma anasema kwamba, mifumo ya majitaka iliyowekwa na Halmashauri ya Jiji (mifumo ya DSSD) haikidhi mahitaji na wakati mwingine mitaro hufurika na kuchafua mazingira.
“Majengo ya jirani hapa yameweka mifumo ya nje ya kumwaga maji, sasa mvua ikinyesha maji yote yanaingia kwenye mfumo wetu na kwa vile wakati mwingine unakuwa umeziba, basi maji hufurika na kuleta kero kubwa ndani ya soko,” anasema Mzee Bogoma.
Kwa upande wake, Malamla anasema kwamba, bila DSSD kurekebisha mifumo ya majitaka, hali itaendelea kuwa tete na kuhatarisha afya za wafanyabiashara na walaji.
“Majengo mengine mara nyingi hutiririsha maji machafu kwa muda mrefu bila watendaji wa halmashauri kufuatilia, lakini ikitokea kwamba mfumo wetu, ambao ni mdogo na unazidiwa, ukatiririsha maji yenye damu kutokana na mitaro kuziba, hapa huwa ni mshike mshike,” anasema.
Amezitaka mamlaka husika kuhakikisha zinawajibika kwa nafasi zao ili kuweka mazingira bora katika soko hilo kwa kulinda afya za walaji na wafanyabiashara kwa ujumla, kwani huduma yao ni muhimu kwa afya ya binadamu na usafi ndiyo kipaumbele cha kwanza.
Kuhusu masuala ya utawala, Malamla ameupongeza uongozi wa TFC kwa kutambua shida zao pamoja na kuwapa miongozo ya mara kwa mara ambayo imezidi kuwaimarisha na kupata fikra mpya za uwekezaji.

 Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Simu: +255 656 331974.

Comments