Featured Post

RANGI ZA NYUMBA HUATHIRI MFUMO WA FAHAMU

NYUMBA hata kama itakuwa bora na imara haiwezi kupendeza ikiwa haitakuwa na rangi ya kuvutia.
Siyo siri kwamba, mahali popote rangi huleta mvuto wa pekee, na katika suala la nyumba, uchaguzi wa rangi gani upake kati kuta na hata paa (mabati au vigae) ni suala la msingi kabisa.

Hata hivyo, baadhi ya rangi, hasa zenye mchanganyiko wa madini ya risasi (lead), hazifai kwa sababu huathiri mfumo wa ufahamu.
Shirika linalojishughulisha na Mazingira na Maendeleo (AGENDA) kwa kushirikiana na Mtandao wa Kuondoa Kemikali Zisizooza (POPs) ujulikanao kama IPEN na asasi isiyo ya kiserikali ya Toxics Link ya India, waliwahi kuzindua kampeni ijulikanayo kama ‘Afya ya Watoto Kwanza’ mwaka 2010.
Lengo la kampeni hiyo lilikuwa kuondoa madini ya risasi katika rangi na kuhamasisha matumizi ya rangi mbadala zisizo na madini hayo, kupitia makubaliano ya kimataifa ya kuondoa matumizi ya madini ya risasi katika rangi chini ya mkakati wa kimataifa wa kuelekea Usimamizi Salama wa Kemikali (SAICM).
Sylvan Mung’anya, ofisa mwandamizi wa AGENDA, aliwahi kukaririwa akisema kwamba, utafiti wa kwanza wa rangi wakati huo ulibaini kuwepo kwa madini ya risasi katika rangi kwa asilimia 77.
Na kwa bahati mbaya, madini hayo yapo katika rangi za nyumba nyingi ambazo kwa sasa zipo kwenye soko hali ambayo ni ya hatari kwa watoto ambao wako hatarini kuathirika na sumu hizo.
Utafiti wa rangi zitumikazo katika kupaka nyumba na vifaa vinginevyo zinazouzwa sehemu mbalimbali nchini Tanzania unaonyesha kwamba, rangi hizo zina kiasi kikubwa cha madini ya risasi.
Utafiti huo, kwa mujibu wa Mung’anya, ulihusisha sampuli 26 za rangi na ukaonyesha kwamba sampuli zote 26 sawa na asilimia 100 zilikuwa na madini ya risasi huku rangi zote za mafuta zikionyesha kuwa na kiasi kikubwa cha madini hayo kuzidi kiwango kinachoruhusiwa.
Nchini Marekani, wakati rangi zote za maji zilionekana kuwa na kiwango kidogo cha madini ya risasi chini ya kile kinachoruhusiwa nchini humo (yaani sehemu 90 ya milioni – 90 ppm).
Matokeo halisi yaliyonyesha kwamba utafiti huo yalihusisha sampuli 20 za rangi za mafuta na aina tatu za rangi zilizidi kiwango.
Katika rangi hizo, asilimia 100 ilizidi kiwango cha madini ya risasi kilichoruhusiwa nchini Marekani huku asilimia 95 ikizidi kiwango kinachoruhusiwa nchini Tanzania.
Pia iligundulika kwamba, Tanzania ina rangi zilizokuwa na viwango vya chini ya viwango vya nchini Marekani ambayo ilihusisha sampuli zote za rangi ya maji.
Baadhi ya athari za kuwepo kwa madini ya risasi kwenye mwili wa binadamu ni pamoja na kuharibika kwa mfumo wa fahamu kiasi cha kutoweza kutibika tena na kupungua kwa ufahamu hata kiasi cha madini hayo kikiwa kidogo.
Wataalam wanasema, watoto wadogo ndio huathirika zaidi kwa kuwafanya kuwa wazito au kutoweza kutamka maneno mbalimbali na uelewa katika kulinganisha maandishi tofauti, pamoja na uthabiti katika kufuatilia mafunzo na mawasiliano madogo kati ya macho na mikono katika kufanya kazi kama vile kuandika.
Hali hiyo pia inaweza kuwaletea watoto matokeo mabaya shuleni.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, madini ya risasi kwenye rangi yalikwishawahi kupigwa marufuku katika nchi nyingi zilizoendelea kuanzia mwaka 1920.
Katika kutekeleza hilo, mamlaka inayohusika na uhifadhi wa mazingira nchini Marekani (U.S. EPA) imeyaweka madini ya risasi katika kundi la kemikali zinazoweza kusababisha saratani.
Kwa mujibu wa Mfungamano wa Afya na Mazingira wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO – Healthy Environments for Children Alliance), hakuna kiwango salama cha madini ya risasi katika damu, bali inafahamika kuwa madini hayo yanaongeza athari za kiafya.
Moja kati ya vyanzo vikubwa vya madini ya risasi kwa binadamu ni vumbi litokanalo na rangi zenye madini hayo zinapotumika, kuchakaa au kuoza.
Madini hayo yanaweza kumwingia binadamu na kumwathiri kupitia mdomoni na hasa kutokana na mikono iliyogusa au kuyashika madini hayo.
Mwaka 2002 taarifa ya WHO iliainisha madini ya risasi kama moja ya njia ishirini za hatari zinazoathiri afya na vyanzo vya magonjwa na kueleza kwamba asilimia 40 ya watoto walikuwa na viwango vya madini ya risasi katika damu zao kwa kiwango cha juu (zaidi ya 5ug/gl), na asilimia 97 ya watoto walioathirika wakiwa wanaishi katika nchi zinazoendelea.
Daktari mmoja kutoka Idara ya Afya na Mazingira Kazini wa Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba Muhimbili (MUHAS) alisema kwamba madini ya risasi yanatishia kukua kwa ubongo (ufahamu) na afya kwa ujumla.
Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Simu: +255 656331974.

Comments