Featured Post

MIZAHA KATIKA MIRADI YA MAJI HAITAVUMILIWA MKOANI SINGIDA

Kaimu Katibu Tawala Sehemu ya Maji Mkoa wa Singida Mhandisi Lyidia Joseph akizungumza na timu ya usimamizi wa sekta ya maji ya halmashauri ya Manyoni, wa kwanza kulia kwake ni Diwani wa Kata ya Mkwese na Mwenyekiti wa huduma za Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Robert Kenze.

Ofisi ya Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Singida imedhamiria kusimamia uboreshaji wa huduma za maji mkoani hapa huku mizaha itakayofanywa na mtu yeyote katika miradi ya maji, kutovumiliwa. 

Kaimu Katibu Tawala Sehemu ya Maji Mkoa wa Singida Mhandisi Lyidia Joseph amebainisha hayo leo wakati wa kikao maalumu na Timu ya usimamizi wa sekta ya maji ya halmashauri ya Wilaya  ya Manyoni, kwa ajili ya kufuatilia usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maji.

Mhandisi Lydia amewaeleza wataalamu hao kuwa uongozi wa mkoa hautavumilia endapo kuna mtumishi yeyote atafanya mzaha katika kusimamia miradi ya maji kwakuwa mkoa umekuwa ukitoa ushirikiano wa kutosha hivyo hakuna sababu ya kushindwa kufanya vizuri.

“Sisi katika ngazi ya mkoa hatutavumilia mzaha katika masuala ya maji, tupo tayari kutoa ushirikiano popote mnapoona mnakwama ili tu tufikie malengo yetu ya kutoa huduma bora za maji kwa wananchi, hali ilivyo sasa hairidhishi kabisa, tufanye kazi kwa kasi zaidi”, ameongeza Mhandisi Lydia.

Amesema, halmashauri hiyo inapaswa kuhakikisha inatekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi la kuongeza asilimia ya upatikanaji wa maji katika halmashauri hiyo kutoka 45 hadi 72 ifikapo mwezi Juni, 2018 pamoja na kuandaa takwimu sahihi za upatikanaji wa maji ifikapo Disemba mwaka huu.

Mhandisi Lydia amefafanua kuwa halmashauri hiyo itaweza kuongeza asilimia ya upatikanaji maji na kufikia lengo la asilimia 72 endapo watendaji wote hasa wajumbe wa timu ya usimamizi wa sekkta ya maji, watashirikiana kusimamia ujenzi wa miradi mitano pamoja na ukarabati wa miradi minne iliyopo kwenye bajeti.

“Kila Mjumbe hapa ana kazi ya kufanya katika miradi hii ya Makanda, Nyaranga, Kikombo, Makutopola na Kicheho inayojengwa pamoja na ile ya Sanza, Mkwese, Londoni na Sorya inayokarabatiwa, Kitengo cha ugavi kisimamie taratibu za manunuzi zinafuatwa pamoja na kuhakiki ubora wa mkandarasi, mwanasheria aelekeze taratibu za kisheria, Maendeleo ya jamii ahakikishe wananchi wanaujua mradi vizuri, kila mmoja akitekeleza jukumu lake ipasavyo tutafikia lengo”, ameeleza na kuongeza kuwa,

“Idara ya maji msifanye siri miradi ya maji na kujifungia wenyewe hakikisheni timu hii ya usimamizi wa sekta yenu inafahamu vizuri miradi yote ya maji pamoja na kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo, mkifanya hivyo mtaenda kwa kasi na kazi itafanyika kwa ufanisi, sio kila kitu mfanye wenyewe tu”, ameongeza Mhandisi Lydia.

Aidha Mhandisi Lydia amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Charles Fussi kwa kujitoa kwake katika kusimamia na kutoa fedha za kusaidia miradi ya maji akitoa mfano wa kiasi cha milioni 16 zilizotolewa na mkurugenzi huyo kutoka katika makusanyo ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji.

Naye Mhandisi wa Maji kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Athanas Nziku ameieleza timu hiyo kuwa usimamizi wa jumuiya za watumia maji ni jambo muhimu kwakuwa takwimu zimeonyesha jumuiya hizo zimekuwa zikikusanya pesa nyingi sambamba na matumizi makubwa ya fedha wanazokusanya.

Mhandisi Nziku amewafafanulia kuwa jumuiya hizo za watumia maji zinapokusanya fedha nyingi sambamba na kutumia fedha nyingi ni moja ya kiashiria kuwa miradi hiyo ya maji inaweza kufa hivyo wazitembelee na kuona tatizo liko wapi endapo liko ndani ya uwezo wa halmashauri liweze kutatuliwa mapema.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mkwese na Mwenyekiti wa huduma za Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Robert Kenze amesema, halmashauri hiyo imedhamiria kuboresha huduma za maji ambapo ajenda ya maji imewekwa kipaumbele katika vikao vyote muhimu.

Kenze amesema wakuu wa Idara wa halmashauri hiyo watashirikiana na Idara ya maji wilayani humo huku wanasiasa wakiwa tayari kutoa elimu na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji. 

Comments