Featured Post

MBEGU YA MAHINDI YA WEMA 2109 NA MIHOGO ILIYOTOLEWA NA COSTECH WILAYANI MBOGWE MKOANI GEITA KUONGEZA CHACHU YA KILIMO

Wakulima wa Kijiji cha Iponya katika Halmshauri ya Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita wakifurahia kupata mbegu bora ya mihogo aina ya Mkombozi waliokabidhiwa na  Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), kwa ajili ya kuanzisha shamba darasa la mbegu hiyo wilayani humo jana.
Mshauri wa Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange (kulia), akimkabidhi mbegu ya mihogo , Mwakilishi wa Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Furaha Chiwile wakati wa uzinduzi wa shamba hilo katika Kijiji cha Iponya. Katikati mwenye shati la kitenge ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Nsika Sizya.


 Watafiti wakiandaa shamba darasa la mahindi katika Kijiji cha Mponda.
 Wananchi wa Kijiji cha Mponda wakisubiri uzinduzi wa shamba darasa la mahindi.
 Ofisa Kilimo wa Wilaya Mbogwe, Stephen Shilemba akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Mponda kabla ya ufunguzi wa shamba darasa.
 Ofisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, David Makabila, akitoa maelezo kwa wakulima wa Kijiji cha Mponda wakati wa uzinduzi wa shamba darasa la mahindi ya WEMA.
 Mtafiti kutoka COSTECH, Dk.Beatrice Lyimo (kulia), akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Mponda.
  Mtafiti kutoka COSTECH, Dk.Beatrice Lyimo, akimkabidhi mbegu ya mahindi ya Wema, Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Mbogwe, Stephen Shilemba. Kulia ni Mshauri wa Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange.
 Mtafiti kutoka COSTECH, Dk.Beatrice Lyimo, akimkabidhi mbolea ya kupandia mahindi aina ya DAP, Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Mbogwe, Stephen Shilemba.
 Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Mbogwe, Stephen Shilemba, akimkabidhi mbegu ya mahindi aina ya WEMA, Ofisa Ugani wa Kata ya Lugunga, Dickson Namlanda.

 Wanawake wa Kijiji cha Lwazeze wakishuhudia uzinduzi huo.
 Mkulima wa Kijiji cha Lwazeze, Charles Kangai akichimba mashimo kwa ajili ya upandaji mbegu ya mahindi ya WEMA.




 Mtafiti wa Mazao ya Mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibula, akielekeza jinsi ya upandaji wa mbegu hiyo ya mihogo aina ya Mkombozi.
 Makamu Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, Nsika Sizya, akipanda mbegu ya mihogo katika shamba darasa katika Kijiji cha Iponya.
Mshauri wa Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange, akipanda mbegu ya mihogo aina ya Mkombozi kwenye shamba darasa katika Kijiji cha Iponya.

Na Dotto Mwaibale, Mbogwe, Geita.

MAKAMU Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, Nsika Sizya amesema mbegu bora ya mahindi ya WEMA 2109 na mihogo aina ya Mkombozi waliyokabidhiwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB) itaongeza chachu ya kilimo wilayani humo.

Sizya aliyasema hayo wilayani humo jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi na kukabidhi mbegu bora za Mahindi ya Wema yanayostahimili ukame na mihogo kwa ajili ya mashamba darasa kwa wakulima wa vijiji vinne vya Mponda kilichopo Kata ya  Luganga, Kijiji cha Ushetu kilichopo Kata ya Ushirika, Kijiji cha Lwazeze kilichopo Kata ya Ngemo na Kijiji cha Iponya kilichopo Kata ya Iponya.


Alisema changamoto kubwa waliyokuwa nayo wakulima katika Halmshauri hiyo ni kukosekana kwa mbegu bora za mihogo na mahindi ambapo alisema kwa kupata mbegu hizo kutaongeza ari na chachu ya kilimo kwa wananchi.

Aliishukuru CSTECH na OFAB kwa kuwapelekea mradi huo katika wilaya hiyo na kuupokea kwa shangwe kwa kuzingatia kuwa mihogo ni zao la biashara na chakula ambapo aliwataka wananchi kubadilika na kufanya kilimo chenye tija kama wataalamu wanavyowaelekeza.


Mtafiti wa Mazao ya Mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibula aliwaambia wakulima hao kuwa hekta moja ya mihogo iwapo watalima kwa kufuata ushauri wa wataalamu wataweza kupata tani 25 hadi 32 kwa zao la mhogo na viazi watapata tani 7 hadi 9 kwa hekta moja.

Alisema matokeo hayo watayapata endapo watafuata kanuni bora za kilimo cha mazao hayo kwa kuzingatia nafasi kati ya mche na mche na mstari kwa mstari na matumizi ya mbolea hivyo wataweza kuongeza uzalishaji zaidi tofauti na sasa ambapo kwenye hekta moja ya mihogo wanapata tani nane hadi kumi wakati kwenye viazi wanapata tani moja hadi 3.

Mtafiti huyo alisisitiza kuwa mbegu hiyo ya Mihogo ya Mkombozi imefanyiwa utafiti na kuonekana kustahimili magonjwa hatari ya mihogo ya batobato kali na michirizi ya kahawia ambayo imekuwa ikiwapatia hasara kubwa wakulima wengi na kupoteza hadi asilimia 90 za mazao.

Mtafiti kutoka COSTECH, Dk. Beatrice Lyimo aliwataka wakulima wa wilaya hiyo kwa kushirikiana na maofisa ugani kuyatunza mashamba hayo na wao kuwa walimu kwa wakulima wenzao.

"Nawaomba nyinyi mliobahatika kupata mashamba darasa haya muwe walimu wa kutoa mbegu bora ambayo mtaisambaza katika vijiji vingine ili kila mkulima aweze kufaidika" alisema Dk.Lyimo.

Ofisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, David Makabila alisema asilimia 75 ya wakulima katika mkoa huo wanategemea kilimo hivyo mafunzo yaliyotolewa kwa maofisa ugani kupitia COSTECH na OFAB yataongeza kasi ya uzalishaji hasa baada ya kupata mbegu hizo bora.

Alisema changamoto kubwa waliyonayo ni wakulima kushindwa kufuata kanuni bora za kilimo ingawa wameanza  kubadilika pole pole baada ya kupata mafunzo.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni upungufu wa maofisa ugani kwani waliopo kwa mkoa mzima ni 189 wakati wanaohitajika ni 512 na kuwa katika maeneo mengine ofisa ugani mmoja anahudumia vijiji tisa tena bila ya kuwa na usafiri wa uhakika.

Hadi jana Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), imeweza kuwafikia wakulima katika vijiji 22 vya wilaya za Mikoa ya Kagera na Geita na kutoa elimu kwa vitendo kwenye matumizi ya Sayansi na Teknolojia za kilimo kwa uzalishaji wenye tija ambapo kuanzia kesho kutwa Jumatatu Novemba 6,2017 watafanya kazi hiyo katika wilaya zote za Mkoa wa Tabora kwa kuanzisha mashamba darasa ya mbegu za mahindi ya WEMA na Mihogo.

Comments