- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Baadhi ya wajumbe waliohudhuria mkutano wa kupitisha rasimu ya tatu ya Katiba ya Chama cha Wadau wa Sekta ya Kuku Tanzania (PAT).
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
JUMLA ya
wajumbe 22 kutoka vyama 11 wamepitisha kwa kauli moja rasimu ya tatu na ya
mwisho ya Katiba ya Chama cha Wadau wa Kuku Tanzania (Poultry Association of
Tanzania – PAT) katika kikao kilichofanyika kwenye Hoteli ya New Africa jijini
Dar es Salaam, jana Jumatano, Novemba 29, 2017.
Kupitishwa
kwa Katiba hiyo kumehitimisha mchakato wa takriban miaka 20 wa kuunda umoja huo
wa wafugaji kuku nchini ili kuirasmisha sekta hiyo ambayo imekuwa ikichangia
kwa kiasi kikubwa pato la jamii pamoja na taifa.
Wajumbe
waliopitisha rasimu hiyo wametoka katika vyama vya Arusha Poultry Keepers
Association (APOKA), Tanzania Animal Feeds Manufactures (TAFMA), Tanzania
Poultry Breeders Association (TPBA), Tanzania Commercial Poultry Association
(TCPA), na African Women Agro- Network (Awan Tanzania Chapter).
Vyama
vingine ni Umoja wa Wafugaji Kuku Dar es Salaam (UFUKUDA), Tanzania Veterinary
Para Professionals (TAVEPA), Ushirika wa kufuga Kuku Morogoro (UWAFUKUMO), Tanzania
Layer Farmers Association (TALFA), Tanzania Broiler Farmers Association (TABROFA), na Kisutu
Poultry Co-operative Society (KIPOCOSO).
Ni chama
cha Mwanza Multipurpose Cooperative Society Limited pekee ambacho
hakikuhudhuria mkutano huo ingawa katika taarifa yake kilieleza kuunga mkono
hatua ambazo zingefikiwa.
Mbali ya
kupitisha rasimu ya katiba hiyo, lakini wajumbe wa mkutano huo walichagua
uongozi wa muda utakaokuwa chini ya uenyekiti wa Harko Bhagat, ambao pamoja na
mambo mengine, utashughulikia usajili wa chama pamoja na kuweka mpango mkakati
kwa ajili ya utekelezaji.
Katibu wa
muda wa PAT, Manase Mrindwa, aliwaahidi wajumbe kwamba, marekebisho ya mwisho
yaliyopitishwa na mkutano huo yatafanyiwa kazi na hatua za usajili zitaanza
mara moja.
“Tumeanza
mchakato huu tangu mwaka 1995, tunashukuru kwamba tumefika mahali
tumekikamilisha kitu ambacho tumekuwa tukikililia usiku na mchana,” alisema
Mrindwa.
Mwenyekiti
wa mkutano huo, Sufian Kyarua, aliwapongeza wajumbe wote waliohudhuria na
kufikia makubalino akisema hiyo imeonyesha mshikamano na nia ya dhati
waliyonayo katika kuendeleza sekta ya ufugaji wa kuku nchini Tanzania.
Kyarua
alisema kwamba, PAT ni chama mwamvuli wa vyama mbalimbali vinavyohusika na
tasnia ya kuku Tanzania, na kwamba chenyewe siyo cha kibiashara wala
hakifungamani na itikadi zozote za kisiasa, kidini au kijamii.
“Jukumu
mojawapo la PAT, kama tulivyoona kwenye katiba yetu, ni kuwaunganisha wanachama
wake pamoja na kuwapatia taarifa mbalimbali za masoko,” alisema.
Awali,
wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, mgeni rasmi kutoka Bodi ya Nyama Tanzania
(TMB), Ezekiel Maro, aliwataka wajumbe hao kuunda chama ambacho hakitakuwa cha
kiharakati wala kisiasa, bali kiwaunganishe wadau wa tasnia ya kuku kwa nia ya
kuwaendeleza na siyo vinginevyo.
“Kama
mtaanzisha kwa mtazamo wa kisiasa au kibiashara, huko mbele mtakwama, lakini
mkianzisha kwa kuangalia maslahi ya wanachama wenu bila kuleta harakati
mtafanikiwa,” alisema Maro, Ofisa Mifugo wa TMB ambaye anahusika na Usajili wa
Wadau wa Tasnia ya Nyama Tanzania.
Maro
alisema kwamba, ni vyema wakaweka kumbukumbu za kitakwimu katika shughuli zao
ambazo ndizo zitakazowaongoza katika kujiletea maendeleo.
“Hivi sasa
ni wakati wa soko huria, serikali inajitahidi kulinda bidhaa za ndani pamoja na
wananchi wake kwa kutoruhusu kuingiza kwa wingi bidhaa za nje, lakini hili
litawezekana ikiwa kutakuwa na takwimu sahihi kwa sababu mwisho wa siku takwimu
ndizo zitakazoongea.
“Huwezi
kusema vyakula vya mifugo kutoka nje visiingizwe wakati hatujui takwimu halisi
za mahitaji pamoja na uzalishaji, lakini kama takwimu ziko sawa, basi hata kama
italazimu kuruhusu bidhaa za nje itakuwa ni kwa kujazia pengo lililopo,”
alisema.
Comments
Post a Comment