Featured Post

FULL VIDEO: SERIKALI YASISITIZA DESEMBA 31 KUWA UKOMO WA UWEKAGI WA VIGINGI (BEACONS) VYA MPAKA HIFADHINI




Na Hamza Temba - Wizara ya Maliasili
..........................................................................
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga amesisitiza agizo la Serikali lililotolewa hivi karibuni na Waziri Mkuu kuhusu kukamilisha zoezi la uwekagi wa vigingi vya mpaka kwenye maeneo ya hifadhi nchini ifikapo Desemba 31 mwaka huu.
Amesema lengo la kukamilisha zoezi hilo ni kuiwezesha Serikali kufanya uamuzi wa mwisho wa kumaliza migogoro ya ardhi iliyodumu kwa muda mrefu baina ya vijiji na maeneo ya hifadhi nchini.

Mhe. Hasunga ametoa kauli hiyo jana wakati wa ziara yake ya kikazi katika hifadhi ya msitu wa Isalalo Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe ambapo aliziagiza taasisi zilizo chini ya Wizara yake kukamilisha zoezi hilo kabla ya tarehe hiyo ili kuiwezesha Serikali kubaini maeneo yenye mapungufu na kuyatolea uamuzi.

“Ifikapo tarehe 31 tuwe tumemaliza kuweka hizo beacon (vigingi) za mipaka, baada ya hapo hatua itakayofuata, Serikali tutakaa na kuangaliza ni vijiji vingapi au maeneo gani yameingia ndani ya hifadhi, tuangalie je tuwaachie hayo maeneo wananchi au tuwahamishe tuwapeleke maeneo mengine, maamuzi hayo yatakuja baada ya kufanya tathmini na kubaini penye mapungufu.

“Sasa ikitokea kwamba imefika tarehe 31 hatujatekeleza hili mimi kama Naibu Waziri nitakuwa sina kazi, maana sijatekeleza agizo la Serikali, kwahiyo lazima tulisimamie, na mimi sasa kabla halijanipasukia nitakupasukia bwana Meneja (Meneja TFS Wilaya ya Mbozi), nitakuja kukagua mipaka, na kabla ya tarehe 31 nitakuja kukagua tena,”alisema Naibu Waziri Hasunga.

Wakati huo huo amekemea vitendo vya baadhi ya wananchi wanaoingiza mifugo kwenye maeneo ya hifadhi nchini na kuwataka kufugia majumbani kwao au maeneo yaliyotengwa kwa ajili hiyo, amewatahadharisha pia juu ya ukali wa sheria za uhifadhi na kwamba endapo mifugo itakamatwa hifadhini sheria zilizopo zinaruhusu utaifishaji.

Aidha aliwataka wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo ya msitu wa Isalalo kuacha vitendo vya uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti hovyo kwa ajili ya mkaa na uanzishaji wa maeneo ya kilimo. Pia alitoa wito kwa wananchi kulinda vyanzo vya maji na kuacha vitendo vya uchomaji moto misitu.

Katika hatua nyingine ameuagiza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Nyanda za Juu Kusini kuwashirikisha wananchi wanaoishi jirani na hifadhi hiyo ya msitu kwenye ulinzi wa hifadhi ikiwa ni pamoja na kuwawezesha miche ya miti ya kutosha kwa ajili ya kupanda  kwenye maeneo yao yanayozunguka hifadhi hiyo.

Aidha ameuagiza uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi kupima maeneo yao na kuweka mpango bora wa matumizi ya ardhi kwa kuanisha maeneo kwa ajili ya kilimo, ufugaji na maeneo ya hifadhi ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima ya wananchi

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Wilaya ya Mbozi, Fred Mgeni alisema katika kuimarisha mpaka wa hifadhi ya msitu huo wa Isalalo ambao una ukubwa wa hekta 11,552, jumla ya vigingi 30 vimewekwa kuzunguka hifadhi hiyo.

Alizitaja baadhi ya  changamoto katika hifadhi hiyo kuwa ni uvamizi wa wakulima na wafugaji, uvunaji haramu wa miti, uchomaji mkaa na moto, na ung'oaji wa vigingi vya mpaka na mabango.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, John Palingo alisema ili kuimarisha uhifadhi wa msitu wa Isalalo ni vema wananchi wakashirikishwa ikiwemo kuanzishwa kwa vikundi vya vijana ambao watawezeshwa bodaboda zitakazowanufaisha kiuchumi na wakati huo huo zikatumika kwenye ulinzi wa hifadhi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kushoto) akioneshwa ramani ya Hifadhi ya Msitu wa Isalalo na Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Wilaya ya Mbozi, Fred Mgeni (kulia) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua hifadhi hiyo kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi mkoani Songwe jana.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, John Palingo wakati wa kukagua Hifadhi ya Msitu wa Isalalo Mkoani Songwe kwenye ziara yake ya kikazi ya kuimarisha uhifadhi mkoani humo jana.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akizungumza na Mkuu wa Wilaya Mbozi, John Palingo (kushoto) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua Hifadhi ya Msitu wa Isalalo uliopo wilaya ya Mbozi mkoani Songwe jana kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi mkoani humo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (wa pili kulia) akimsikiliza Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Wilaya ya Mbozi, Fred Mgeni (kulia) wakati akikagua Hifadhi ya Msitu wa Isalalo uliopo wilaya ya Mbozi mkoani Songwe wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuimarisha uhifadhi mkoani humo jana. Wa tatu kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, John Palingo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Malolo wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuimarisha uhifadhi mkoani humo jana, alikagua Hifadhi ya Msitu wa Isalalo na kuagiza zoezi la uwekaji vigingi vya mpaka likamilike ifikapo Desemba 3l.

Comments