Featured Post

ASASI ZA KIRAIA ZAIOMBA SERIKALI KUBORESHA SHERIA ZA USALAMA BARABARANI ZA MWAKA 1973

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Walemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Felician Mkude (kulia) akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa Kuwakumbuka Wahanga wa Ajali za Barabarani. Kushoto ni Bi. Edda Sanga wa TAMWA (kulia).MTANDAO wa wadau kutoka asasi za kiraia unaotetea marekebisho ya sheria na sera ihusuyo usalama barabarani umeiomba Serikali kuifanyia maboresho sheria ya Usalama barabarabi ya mwaka 1973 ili iweze kukabiliana ipasavyo na suala la ajali za barabarani pamoja na athari zinazotokana na ajali hizo.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Bi. Edda Sanga alipokuwa akisoma tamko la pamoja la asasi hizo katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa Kuwakumbuka Wahanga wa Ajali za Barabarani.

“Pamoja na mambo mengine, katika kuadhimisha siku hii tunaisihi serikali na watunga sheria kuifanyia maboresho sheria ya Usalama barabarabi ya mwaka 1973 ili iweze kukabiliana ipasavyo na suala la ajali za barabarani pamoja na athari zinazotokana na ajali hizo,” alisema Bi. Sanga.

Alisema miongoni mwa maeneo wanaoshauri marekebisho/maboresho ni pamoja na matumizi ya mikanda, ambapo Sheria ya sasa ya Usalama barabarani inasema ni kosa kisheria kwa dereva na abiria anayekaa kiti cha mbele kutokufunga mkanda wakati wa safari lakini sheria haisemi chochote kwa abiria wanaokaa viti vya nyuma. 

Alisema licha ya Kanuni za SUMATRA zinamtaka abiria yeyote kufunga mkanda ila kwa vile sheria mama (Road Traffic Act of 1973) ipo kimya katika eneo hilo utekelezaji wa kanuni hii unakuwa mgumu. 

Alisema eneo linguine ni pamoja na matumizi sahihi ya kofia ngumu, kwani Sheria ya sasa ya usalama barabarani inatambua kosa kwa mwendesha pikipiki kutokuvaa kofia ngumu lakini sheria hiyo haisemi chochote kwa abiria anayepanda katika chombo hicho wala kutaja aina na ubora wa kofia inayofaa.

“Kwa matumizi ya vilevi na uendeshaji vyombo vya usafiri: Sheria ya sasa ya usalama barabarani inasema kuwa itakuwa kosa kwa mtu yoyote kuendesha chombo cha moto akiwa na kiwango cha kilevi katika damu yake kinachozidi asilimia 0.08% katika mfumo wa mwili. 

Kiwango hiki ni kikubwa sana kikilinganishwa na tafiti zilizofanywa na Shirika la afya duniani na kupendekeza kiwango asilimia 0.05% kwa dereva aliyebobea na asilimia 0.02% kwa dereva mchanga. Hivyo basi ni rai yetu kuwa sheria ifanyiwe marekebisho ili iendane na kiwango cha sasa cha kimataifa kilichofanyiwa utafiti,” alisisitiza Bi. Sanga.

Aidha aliongeza kuwa adhabu zinazotolewa kwa sasa hazikidhi wala kuleta hofu kwa maderava wasiotaka kutii sheria na kanuni hivyo kuendelea kufifisha juhudi za kudhibiti tatizo la ajali za barabarani. 

“Mwendokasi umeendelea kuwa sababu kubwa ya ajali zinazogharimu uhai wa watu wengi. Sheria yetu inayo mapungufu kadhaa pamoja na juhudi nyingi za Jeshi la Polisi na wadau wengine kutaka kudhibiti jambo hili lemeendelea kuwa tatizo. 

Mfano Sheria ya usalama barabarani ya 1973 Kifungu cha 51(8) inatambua maeneo machache katika kuzuia mwendokasi, ni muhimu Sheria sasa itamke maeneo yote na si yale ya mjini tu au makazi, itamke wazi kuhusu maeneo ya shule, nyumba za ibada, maeneo ya michezo na mbuga za wanyama,” aliongeza Bi. Sanga katika taarifa hiyo.

Pamoja na mambo mengine, alisema sheria ya sasa ipo kimya juu ya suala la vizuizi vya watoto katika vyombo vya moto hasa kwa magari binafsi na tumeendelea kushuhudia madhara makubwa katika ajali zilizohusisha watoto vikiwemo vifo. 

Hata hivyo mtandao huo umewasihi wananchi kuwa na taadhari pindi watumiapo vyombo vya moto bila kujali mapungufu yaliyopo kwenye sheria za usalama barabarani ili kupunguza matukio ya ajali.

Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) usalama barabarani Mary Kessy, akitoa ufafanuzi kwa wanahabari, alibainisha takwimu zinaonyesha takribani watu milioni 1.25 duniani hufariki kila mwaka; huku nchini Tanzania asilimia 76 ya ajali za barabarani husababishwa na uzembe wa madereva, asilimia 8 ubovu wa barabara na ubovu wa vyombo vya moto kuchangia ajali hizo kwa asilimia 16.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Ifikapo 2020: Kupunguza vifo na ajali za barabarani kwa asilimia 50%”. Mtandao wa Wadau kutoka asasi za kiraia unaotetea marekebisho ya Sheria za Sera zihusuyo usalama barabarani Tanzania unaundwa na asasi zifuatazo;- TAWLA, TAMWA, WLAC, TCRF, TLS, TMF, RSA, AMEND TANZANIA, SHIVYAWATA, TABOA pamoja na SAFE SPEED FOUNDATION.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA), John Seka (katikati) akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa Kuwakumbuka Wahanga wa Ajali za Barabarani.Kushoto ni Isabela Nchimbi kutoka TAWLA na Bi. Edda Sanga wa TAMWA (kulia).
Kushoto ni Mratibu wa Global Road Safety Partnership Tanzania, Bi. Tusa Bernard akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa Kuwakumbuka Wahanga wa Ajali za Barabarani. Kulia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA), John Seka
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Bi. Edda Sanga (kushoto) akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa Kuwakumbuka Wahanga wa Ajali za Barabarani. Kulia ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Walemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Felician Mkude.
Mratibu wa Kituo cha Usuluhishi (CRC) kilichoko ndani ya Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Gladness Munuo (kulia) akitoa maelezo kabla ya kuanza kwa mkutano huo. 
Mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) usalama barabarani Mary Kessy (kulia) akizungumza katika mkutano huo.

Comments