- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
MPANGO WA MATUMIZI
BORA YA ARDHI YA KIJIJI - 2
Mikutano kama hii ya kijiji ni muhimu kwa wananchi kutolea uamuzi masuala mbalimbali yakiwemo ya matumizi bora ya ardhi ya kijiji.
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini blog
MIGOGORO mingi katika jamii hutokana na wananchi kutokushirikishwa
katika uamuzi hata wa miradi ya maendeleo kuanzia mwanzo.
Kwa kutambua hilo, ndiyo maana NLUPC imeweka utaratibu
kwamba, suala zima la kutekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi ni lazima
iwashirikishe wananchi wenyewe na wao ndio waridhie na kukubaliana kwa pamoja.
MaendeleoVijijini
inafahamu kwamba, timu ya PLUM hutembelea vijiji vilivyochaguliwa ili kuwezesha
Ushirikishwaji katika Tathmini ya Vijiji (PRA) inayolenga matumizi ya ardhi.
PLUM, kwa kushirikiana na taasisi nyingine kama Halmashauri
ya Kijiji, Mkutano wa Kijiji, Vitongoji na kadhalika, huchambua na kutathmini
matatizo na fursa za utatuzi katika matumizi ya ardhi.
Kwa kawaida, MaendeleoVijijini
inatambua kwamba, taasisi hizo zinapaswa kuwepo kijijini na kufanya kazi kwa
mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa Namba 7 ya mwaka 1982.
Tangu mwanzo, timu ya PLUM inapaswa kuhakikisha kuwa taasisi
hizo zipo na zinafanya kazi kwa mujibu wa sheria, vinginevyo zijengwe na
ziendelezwe kufanya hivyo.
Kutokowepo kwa taasisi hizo, uchunguzi wa MaendeleoVijijini
unaonyesha kuwa, huchangia kuwepo kwa migogoro mingi ya ardhi na hata kudumaa
kwa maendeleo.
Mara nyingi ufanisi wa taasisi hizo, hususan mafanikio ya
mikutano halali ndiyo yanayozaa tathmini nzuri inayoeleza matatizo na fursa za
utatuzi.
Vilevile mikutano hiyo katika ngazi za mashamba, vitalu,
vitongoji na kijiji ndiyo hutoa mipango ya matumizi bora ya ardhi inayoeleweka
na kukubalika katika jamii husika.
Kama kuna tathmini shirikishi ya kijiji iliyokwishafanyika
awali na sekta yoyote, hususan ya matumizi ya rasilimali au maendeleo vijijini
inaweza kutumika kurejewa kwenda na wakati badala ya kuanza upya.
Wawezeshaji wanapaswa kuwa makini kuhakikisha kuwa jamii
katika ngazi husika wanachambua matatizo, fursa za utatuzi, na kuweka
vipaumbele kwa kuhusisha tatizo, chanzo chake na athari.
Mfano mzuri ni kwamba, baa la njaa linaweza kutokana na
uzalishaji duni unaotokana na ukame na uharibifu wa ardhi ambao unaweza kuwa ni
matokeo ya ufyekaji miti na usimamizi mbaya wa ardhi.
Hiyo inaweza kuchangiwa pia na kuwepo migogoro ya mipaka na
miliki na kutokuwa na usalama wa miliki.
Uchambuzi wa namna hiyo ni muhimu na unwasaidia wanakijiji
kulinganisha kati ya kushughulikia matatizo ya ufumbuzi wa papo na yale
yanayohitaji upangaji wa muda wa kati au muda mrefu.
Vilevile ni muhimu kwa wanakijiji kuelewa kuwa uwekezaji
unaohitaji kwenye sekta za huduma kama elimu na afya unatoka katika sekta ya
uzalishaji.
Katika uchambuzi wa fursa, shughuli zinazohitaji msaada wa
nje ya kijiji na nje ya majukumu ya timu ya PLUM zinaweza kurejewa kwa taasisi
husika ndani na hata nje ya wilaya.
Mpango wa Utendaji
Jumuiya
MaendeleoVijijini
inatambua kwamba, matokeo ya kazi ya PRA ni kuwa na mpango wa utendaji wa
jumuiya unaolenga kwenye usimamizi wa matumizi bora ya ardhi (CAP).
Mpango kazi huo, ambao siyo mpango wa matumizi ya ardhi,
utaandaliwa kutokana na mpango katika ‘Hatua ya 4’ ya PLUM ambapo utaweka
bayana vipaumbele vya fursa za maendeleo, kazi zilizopendekezwa na mahitaji,
kazi na majukumu ya watu binafsi na vikundi, ratiba ya kazi, uhusishaji wa
miradi ya kijiji, wilaya na taifa, na maeneo yanayohitaji msaada kutoka nje.
Ujenzi na uimarishaji
wa taasisi za vijiji
Ufanisi wa kazi zilizoainishwa unategemea zaidi kuwepo kwa
taasisi imara katika ngazi ya kijiji na vitongoji vyake.
Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
huendesha mafunzo mbalimbali kutokana na program ya maboresho ya Utawala Bora,
kujenga uwezo katika taasisi ngazi ya kijiji, hususan Mkutano wa Kijiji na
Halmashauri ya Kijiji.
MaendeleoVijijini
inafahamu kwamba, kifungu cha 55 cha Sheria ya Serikali za Mitaa kinaweka
utaratibu wa kila kijiji kuwa na Mkutano wa Kijiji ambao ni mkutano wa
wanakijiji wote wenye miaka 18 na kuendelea.
Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya 1999 katika Fungu la 8 Ibara ya
5, inaelekeza Halmashauri ya Kijiji kutogawa ardhi au kutoa hatimiliki ya haki
za kimila za ardhi bila kwanza kupata kibali cha Mkutano wa Kijiji.
Vilevile katika Ibara ya 6, Sheria inaelekeza Halmashauri ya
Kijiji kutoa taarifa katika Mkutano wa Kijiji na kuzingatia maoni ya Mkutano wa
Kijiji kuhusiana na mambo yote ya usimamizi na utawala wa ardhi ya kijiji.
Mkutano wa Kijiji
Kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa Kifungu cha 103
kinaainisha mikutano ifuatayo inayohusu Mkutano wa Kijiji; Mosi, Kutaitishwa
Mkutano wa Kijiji kila inapobidi kufanya uchaguzi na/au kuunda Halmshauri ya
Kijiji na kuchagua wajumbe wake.
Pili, Kutafanyika mkutano wa kawaida wa kijiji angalau mara
moja katika kila miezi mitatu; Tatu, Halmashauri ya Kijiji inaweza, ikiwa
itaona lazima au inafaa kwa sababu yoyote ile kufanya hivyo, kuitisha mkutano
usio wa kwaida wa kijiji, kujadili na kuamua juu ya suala lolote lenye manufaa
kwa umma.
Kwa kawaida, katika usimamizi na utawala wa ardhi ya kijiji,
Mkutano wa Kijiji hutoa uamuzi kwenye masuala ambayo yana umuhimu wa pekee
kwenye jamii.
Hiyo ni pamoja na kuidhinisha mipango ya matumizi bora ya
ardhi ya kijiji, ugawaji wa ardhi, upitishaji wa sheria ndogo za usimamizi wa
matumizi ya ardhi, uundaji wa kamati za kusimamia matumizi ya ardhi,
kuidhinisha Baraza la Ardhi la Kijiji na kamati za mazingira.
Uzoefu unaonyesha kwamba, mikutano ya kijiji ina manufaa
makubwa katika kuiarifu jamii ya kijiji, kutoa maelezo kuhusu usimamizi wa
ardhi, na kupata ridhaa ya wanakijiji kwa ajili ya shughuli mbalimbali za
usimamizi wa ardhi.
Ni wakati wa mikutano hiyo ambapo wanakijiji binafsi, ambao
siyo wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji au Kamati ya Usimamizi wa Ardhi, wanaweza
kushiriki, kuchangia na kushawishi uamuzi kwenye ngazi ya kijiji.
Halmashauri ya Kijiji
Halmashauri ya Kijiji inaundwa kwa mujibu wa kifungu cha 56
cha Sheria ya Serikali za Mitaa ambapo idadi ya wajumbe hutegemea ukubwa wa
kijiji na idadi ya vitongoji katika kijiji husika, lakini ni lazima wasipungue
15 na wasizidi 25.
Kisheria, halmashauri za wilaya zimepewa mamlaka ya kupokea
mapendekezo ya vijiji, na kutoa uamuzi juu ya idadi ya vitongoji na wajumbe wa
Halmashauri ya kila Kijiji.
Wajumbe hao ni pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kijiji
ambaye huchaguliwa na Mkutano Mkuu wa Kijiji, wenyeviti wa vitongoji ndani ya
kijiji, na wajumbe wengine wanaochaguliwa na Mkutano Mkuu wa Kijiji.
Ili kuleta usawa wa jinsia, sheria inaagiza kwamba, ni
lazima idadi ya wanawake katika Halmashauri ya Kijiji isipungue robo ya wajumbe
wote.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji (Village Executive Officer – VEO)
ambaye huajiriwa na Halmashauri ya Wilaya huwa Katibu wa Halmashauri ya Kijiji
na Mkutano wa Kijiji.
Halmashauri ya Kijiji inayo madaraka ya utendaji ya kufanya
uamuzi au mapendekezo ya kila siku ya usimamizi wa kijiji ikiwemo ardhi ya
kijiji.
Katika kusimamia ardhi, Halmashauri ya Kijiji inaweza
kutayarisha mapendekezo ya mipango ya matumizi bora ya ardhi ya kijiji, sheria
ndogo, mikataba ya pamoja ya matumizi ya ardhi, kugawa ardhi, kutoa hatimiliki
za haki za ardhi za kimila, kuunda kamati mbalimbali kuhusiana na matumizi ya
ardhi, na baadaye kuwasilisha kwenye Mkutano wa Kijiji ambao una madaraka ya
kuidhinisha au kukataa mapendekezo ya Halmashauri ya Kijiji.
Mkutano wa Halmashauri
ya Kijiji
Ili mkutano wa Halmashauri ya Kijiji ufanikiwe, hakuna budi
wajumbe waarifiwe mapema, kwa maandishi, kwa kuonyesha dondoo zitakazojadiliwa,
na siyo kutangaza kwa baragumu tena kwa muda mfupi bila kuwaeleza wajumbe nini
kitakachojadiliwa.
Halmashauri ya Kijiji hukutana wakati wowote inapoona
lazima, lakini kama ilivyoelezwa awali, isiwe chini ya mara nne kwa mwaka (kila
baada ya miezi mitatu) ili kuweza kuandaa agenda na mapendekezo ya kujadiliwa
na Mkutano wa Kijiji.
Akidi ni angalau nusu ya wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji
lazima wawepo wakati wote wa mkutano, kinyume chake uamuzi wowote utakaofanywa
wakati wa mkutano huo hautatambuliwa kisheria.
Mkutano huo ni lazima uhudhuriwe na kufunguliwa na
Mwenyekiti (au Kaimu wake) ambaye ndiye anayehusika na agenda na Katibu (Ofisa
Mtendaji wa Kijiji) ambaye anahusika na kumbukumbu za mkutano.
Ni lazima kumbukumbu za mkutano uliotangulia zisomwe na
kuthibitishwa na wajumbe na kutiwa saini na Mwenyekiti na Katibu kabla ya kuendelea
na agenda nyingine.
Vilevile, yatokanayo na mkutano uliotangulia pia ni lazima
yajadiliwe.
Mawazo ya agenda nyingine kama zilivyoonyeshwa kwenye barua
ya mwaliko, pamoja na taarifa kutoka kwenye kamati zilizoundwa na Halmashauri
zijadiliwe, halafu kuna mengineyo na hatimaye Mwenyekiti atafunga mkutano.
Umuhimu wa Mikutano
Ni vyema kusisitiza umuhimu wa kuwepo mikutano, kwani maeneo
mengi yenye migogoro ya ardhi yamechangiwa na kupuuzwa na kutofuata taratibu za
mikutano.
Katika vijiji vingi, uzoefu unaonyesha kwamba, uamuzi
unaopaswa kutolewa na Halmashauri ya Kijiji, umekuwa ukitolewa na mtu mmoja tu
(Mwenyekiti au Katibu) na kuchukuliwa kama ndio uamuzi wa Halmashauri ya
Kijiji.
Baadhi ya watu huona mikutano inapoteza muda au kuchelewesha
uamuzi, lakini mara nyingi kutokuhudhuria kwao kumekuwa na athari kwa sababu
hao hao wasiohudhuria ndio wakati mwingine huanzisha migogoro kwa kuona kwamba
uamuzi uliopitishwa kwenye mikutano husika haukuzingatia baadhi ya mambo ambayo
kama wangehudhuria wangeweza kupendekeza.
Mfano mzuri ni katika Kijiji cha Sero huko Loliondo wilayani
Ngorongoro ambako Mkutano wa Kijiji wa kugawa ardhi ulisainiwa na majina ya
watu ambao baadhi ya wanakijiji walidai hawawajui kijijini mwao, hali
iliyosababisha mgogoro mkubwa.
Aidha, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mzula wilayani Dodoma
aliwahi kuwasilisha kwenye mkutano wa kijiji, kwa niaba ya Halmashauri ya
Kijiji, majina ya watu wa kuunda Kamati ya Usimamizi wa Ardhi ya Kijiji, lakini
wanakijiji wakachachamaa kuwa majina yote ni marafiki wa karibu au jamaa wa
Mwenyekiti.
Ilibainika pia kwamba, Halmashauri ya Kijiji haikuwahi
kukutana na kupendekeza majina hayo.
Hiyo ni baadhi tu ya mifano michache ambayo inapaswa kutoa
tahadhari wakati taasisi za vijiji zinaposhughulikia masuala nyeti yenye maslahi
makubwa ya jamii, kama ardhi.
Watu wachache wasipewe fursa kutumia vibaya mamlaka ambayo
Sheria inatoa kwa taasisi za kijiji kushughulikia ardhi.
Mafanikio ya Mikutano
Ushirikishwaji katika mipango na usimamizi wa ardhi (PLUM)
umejenga mhimili wake katika majadiliano na hatimaye kufikia makubaliano.
Wakati wote wa mkutano katika ngazi mbalimbali – kuanzia
kaya, jamii, kitongoji, kamati, halmashauri, mkutano – wawezeshaji (wataalam
kutoka nje ya kijiji) ni lazima wajiulize:
* Mahudhurio ya watu wa aina mbalimbali za kiuchumi jamii,
walemavu, wazee, vijana, wanaume na wanawake yakoje?
* Kwa kiwango gani aina mbalimbali za kiuchumi-jamii,
wanaume na wanawake wanachangia wakati wa majadiliano?
* Je, masuala yanaeleweka vizuri?
* Je, watu na kila aina ya watumiaji wa ardhi wanawasilisha
vizuri matilaba na mapendekezo yao?
* Je, kuna mjadala na uchambuzi wa pamoja unaopelekea kwenye
mipango ya utendajji na uhamasishaji wa washiriki?
* Je, wanakijiji wanafikia makubaliano ya bayana na mipango
inayoakisi vipaumbele vya jamii (wanaume, wanawake, vijana) katika njia ya
usawa na haki?
* Je, makubaliano na mipango inatarajiwa kuleta mafanikio?
* Je, hadidu za rejea zinaandikwa vizuri, kutayarishwa na
kusambazwa katika muda unaotakiwa?
Wakati mkutano wa usimamizi wa ardhi kijijini unapokuwa
hauna mafanikio mazuri kuliko ilivyotarajiwa, na moja au zaidi ya maswali hayo
hayakujibiwa kwa usahihi, hatua za kurekebisha lazima zichukuliwe ili kuboresha
utendaji katika mikutano inayofuata.
Marekebisho ya mikutano inayofuata yafanywe kwa kushauri
Halmashauri ya Kijiji kurekebisha kasoro za mkutano uliotangulia.
Kesho tutaangalia
namna kushughulikia mipaka ya ardhi ya kijiji.
Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com.
Tupigie: +255 656 331974
Comments
Post a Comment