Featured Post

WAKUU WA NCHI WANAWAKE BARANI AFRIKA

Samia Suluhu Hassan (kushoto) akiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli (katikati) na Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa.

Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
ULIMWENGU sasa umeanza kutambua umuhimu na nafasi ya wanawake katika jamii na madaraka, hili linathibitishwa kila mahali kutokana na usawa wa kijinsia katika masuala mbalimbali ya kijamii.
Kwa karne kadhaa imedhihirika katika nchi nyingi kwamba wanawake wanaweza kuwa kwenye madaraka na wakaongoza vyema, wakati mwingine kuliko hata wanaume.
Umoja wa Mataifa katika makongamano mengi umepitisha maazimio mengi ya kuzitaka nchi wanachama kutenga nafasi za kutosha kwa wanawake katika vyombo vya uamuzi, jambo ambalo hata Tanzania imeridhia na kutekeleza kwa vitendo.
Ukiacha wakurugenzi wengi wanawake wa taasisi na idara za umma na zile za binafsi, Tanzania ndiyo pekee ambayo imewahi kutoa Spika wa Bunge la Afrika mwanamke (Balozi Getrude Mongela) lakini pia ikatoa Spika wa kwanza mwanamke wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Anne Semamba Makinda).
Ukiacha hilo, wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, mara baada ya kuteuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Pombe Magufuli aliushangaza ulimwengu baada ya kumteua Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza wake, tofauti na matarajio ya wengi.
Na Mama Samia amekuwa makamu wa kwanza mwanamke tangu kuzaliwa kwa Tanzania mwaka 1964.
Katika historia yake, Bara la Afrika limekuwa na marais nane wanawake – waliochaguliwa au wa muda, na limekuwa na makamu wakuu wa nchi wanawake tisa.
Ifuatayo ni orodha ya marais wanawake waliopata kuongoza nchi za Afrika, pamoja na makamu wakuu wanawake.

1) Sylvie Kinigi: 1993-1994 (Kaimu Rais, Burundi)
Alichaguliwa Oktoba 1993, Slyvie Kinigi alikuwa mwanamke wa kwanza barani Afrika kushika madaraka ya juu kabisa ya uongozi wa serikali barani humo.
Akiwa kiongozi wa jumuiya ya wanawake wa chama tawala cha Watutsi nchini Burundi, aliwezesha kubadilishwa kwa sheria, muundo wa uchumi na kijamii kwa upande wa wanawake.
Wakati Melchior Ndadaye akiwa Rais wa Burundi, alimteua Kinigi kama Waziri Mkuu wake.
Baada ya Ndadaye kuuawa katika Vita vya Wenyewe kwa wenyewe, Kinigi alifanikiwa kuwakusanya mawaziri 15 kati ya 22 kwa pamoja na kufanikiwa kuendelea kutawala nchi hiyo ikiwa katika hali ya mgogoro mkubwa, hivyo kuwa Kaimu Mkuu wa Nchi.
Utawala wake ulipata nguvu zaidi wakati Meja Pierre Buyoya na Jean Baptiste Bagaza, marais wa zamani wa serikali za kijeshi, walipomuunga mkono.
Hadi kufikia mwaka 2004, Kinigi alikuwa akifanya kazi na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

2) Ivy Matsepe-Casaburri: 2005 na 2008 (Kaimu Rais, Afrika Kusini)
Mwanasiasa huyo wa Afrika Kusini alikuwa Waziri wa Mawasiliano kuanzia mwaka 1999 hadi mauti yalipomfika.
Hata hivyo, kwa muda alipata kukaimu nafasi ya Rais wa Afrika Kusini mwaka 2005 wakati Thabo Mbeki alipojiuzulu na baadaye mwaka 2008 kabla ya kurithiwa na Kgalema Motlanthe.
Alifariki dunia Aprili 6, 2009.

3) Ellen Johnson Sirleaf:  2006 – hadi sasa (Rais, Liberia)
Kufuatia ushindi mkubwa wa mwaka 2005 dhidi ya mpinzani wake wa karibu mwanasoka mashuhuri George Oppong Weah, Sirleaf alikuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa mkuu wa nchi barani Afrika.
Awali alishindwa uchaguzi mwaka 1997 na Charles Taylor.
Mwaka 2011, Sirleaf alitunukiwa Nishani ya Amani ya Nobel, kwa pamoja na wanawake wengine Leymah Gbowee wa Liberia na Tawakel Karman wa Yemen.
Kutoka kushoto: Tawakkul Karman, Leymah Gbowee, na Ellen Johnson Sirleaf wakionyesha tuzo zao wakati wa sherehe za Tuzo za Amani za Nobel.
Wanawake hao walitambuliwa “kwa jitihada zao za kutetea usalama wa wanawake na haki za wanawake kushiriki moja kwa moja katika ujenzi wa amani.”
Mwaka huo huo akachaguliwa tena katika kipindi cha pili kuwa Rais wa Liberia.
Kwa sasa anashika nafasi ya 70 kati ya wanawake wenye nguvu duniani, kulingana na jarida la Forbes.

4) Rose Francine Rogombé: 2009 (Rais wa Muda, Gabon)
Alikuwa Rais wa Muda wa gabon kuanzia Juni hadi Oktoba 2009 kufuatia kifo cha rais wa muda mrefu, Omar Bongo.
Alipata nafasi hiyo ya kukaimu kutokana na nafasi yake kama Rais wa Bunge la Seneti la nchi hiyo, nafasi ambayo alichaguliwa Februari 2009.
Alikuwa mwanasheria kitaaluma na mwanachama wa Gabonese Democratic Party (PDG).
Baada ya uchaguzi wa Desemba 2014 wa Bunge la Seneti, Lucie Mboussou alimrithi Rogombé kama rais wa Seneti Februari 27, 2015.
Rogombé alifariki dunia Aprili 10, 2015 katika hospitali moja jijini Paris, Ufaransa ambako alikuwa amepelekwa kwa matibabu siku chache nyuma.

5) Agnès Monique Ohsan Bellepeau: 2012 na 2015 (Kaimu Rais, Mauritius)
Mwandishi mashuhuri wa habari alikuwa Makamu wa Rais wa Mauritius hadi mwaka 2010.
Alipata kuwa Kaimu Rais wa Mauritius kuanzia Machi 31 hadi Julai 21, 2012 wakati Sir Anerood Jugnauth alipojiuzulu hadi Kailash Purryag aliposhika madaraka.
Baadaye akakaimu tena nafasi hiyo kuanzia Mei 29 hadi Juni 5, 2015 wakati Kailash Purryag alipojiuzulu hadi Ameenah Gurib aliposhika madaraka.

6) Joyce Hilda Banda: 2012 – 2014 (Rais, Malawi)
Mwalimu na mwanaharakati wa haki za wanawake, alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje kuanzia mwaka 2006 hadi 2009 na baadaye Makamu wa Rais kuanzia Mei 2009 hadi Aprili 2012.
Ndiye muasisi wa Chama cha People’s Party kilichoanzishwa mwaka 2011.
Banda alichukua nafasi ya urais kufuatia kifo cha Rais Bingu wa Mutharika.
Alikuwa rais wa nne wa Malawi na rais wa kwanza wa nchi hiyo tangu kupata uhuru.
Kabla ya kuwa rais, alikuwa ndiye makamu wa rais wa kwanza mwanamke nchini humo.
Mwaka 2014, jarida la Forbes lilimtaja Rais Banda katika nafasi ya 40 kati ya wanawake wenye nguvu ulimwenguni na nafasi ya kwanza kwa wanawake wenye nguvu barani Afrika.

7) Catherine Samba-Panza: 2014 (Kaimu Mkuu wa Nchi, Jamhuri ya Afrika ya Kati)
Alikuwa rais wa muda wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kuanzia mwaka 2014 na mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo nchini humo. Kabla ya kuteuliwa kwenye nafasi hiyo, alikuwa Meya wa Jiji la Bangui kuanzia Mei 2013.
Aliteuliwa kuwa Meya wa Bangui, makao makuu ya nchi hiyo, na Baraza la Mpito la Taifa (National Transitional Council - CNT) Juni 14, 2013 wakati wa mgogoro wa mwaka 2012–13.
Uteuzi wake uliungwa mkono na pande zote za kwenye mgogoro, pamoja na rais wa Ufaransa Francois Hollande.
Kufuatia machafuko chini ya utawala wa Djotodia na hatimaye Rais Michel Djotodia kujiuzulu baada ya mkutano wa CEEAC wa Januari 10, 2014, Alexandre-Ferdinand Nguendet alikaimu nafasi ya urais hadi CNT ilipomteua Samba-Panza kuwa rais wa muda baada ya kupitia orodha ya wateule nane ambao walipaswa kuthibitisha kwamba hawakuwa na uhusiano wowote kwa upande wa Séléka au kundi la Anti-balaka.
Aliiongoza nchi hiyo hadi mwaka 2015 wakati wa uchaguzi mkuu.

8) Ameenah Firdaus Gurib-Fakim: 2015 – hadi sasa (Rais, Mauritius)
Alianza kazi yake kama mhadhiri katika Kitivo cha Kilimo cha Chuo Kikuu cha Mauritius, akawa Mkuu wa Kitivo cha Sayansi na baadaye Makamu Mkuu wa Chuo cha Mauritius kuanzia mwaka 2004 hadi 2010.
Ana shahada ya uzamivu (Ph.D) katika Kemia Asilia (Organic Chemistry) kutoka Chuo Kikuu cha Exeter, cha Uingereza.
Gurib-Fakim ni mwanachama wa Royal Society Chemistry, International Union Pure and Applied Chemistry na Third World Academy Sci.
Mwaka 1989, alitunukiwa tuzo ya C.Chem na taasisi ya Royal Society of Chemistry kwa kutambua stadi zake na mchango wake kwenye tasnia hiyo.
Ameandika na kuhariri vitabu 26, mbali ya makala mbalimbali kwenye sekta ya uhifadhi wa mazingira na viumbehai na maendeleo endelevu.
Amepata kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Centre for Phototherapy and Research na Profesa wa Organic Chemistry pamoja na nafasi ya uenyekiti katika Chuo Kikuu cha Mauritius.
Mei 28, 2015 utawala wa mseto wa Waziri Mkuu Anerood Jugnauth ulimpendekeza kuwa Rais.

MAKAMU WAKUU WA NCHI AFRIKA

1975-76 Makamu Mkuu wa Nchi, Waziri Mkuu ÉLISABETH DOMITIÉN, Jamhuri ya Afrika ya Kati
Aliwahi kukaimu kama Rais wa muda wakati Rais Jean Bedel Bokassa alipokuwa akisafiri nje ya nchi. Alizaliwa mwaka 1926 na kufariki dunia mwaka 1997.

1980-91 Makamu Mkuu wa Nchi, Rais wa Bunge la Taifa ALDA NEVES DA GRAÇA DO ESPIRITO SANTO, Sao Tomé e Principe
Pia anajulikana kama Alda do Espírito Santo au Alda Graça, alipigana katika vita ya uhuru wa visiwa hivyo na alikuwa mshairi mashuhuri.
Mwaka 1975-78 alikuwa Waziri wa Utamaduni na Elimi na mwaka 1978-80 alikuwa Waziri wa Elimu, Masuala ya Jamii na Utamaduni.
Akiwa Rais wa Bunge la taifa (Assembléia Popular Nacional) alikuwa ndiye Makamu Mkuu wa Nchi. Alizaliwa mwaka 1926 na kufariki dunia mwaka 2010.

1992- Makamu Mkuu wa Nchi, KADIDJA ABEBA, Djibouti
Hadi alipoteuliwa kuwa Rais wa Mahakama ya Juridical, alikuwa mshauri wa Mahakama Kuu na kukaimu nafasi ya urais kila ilipobidi. Alichaguliwa kuwa Rais wa Mahakama Kuu kuanzia mwaka 2000.

1994-2003 Makamu wa Rais, DKT. WANDIRA SPECIOZA KAZIBWE, Uganda
Kati ya mwaka 1989-91 alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda, kati ya mwaka 1992-94 alikuwa Waziri wa Utamaduni, Wanawake na Vijana, mwaka 1994-96 alikuwa Waziri wa Jinsi na Maendeleo ya Jamii, na mwaka 1996-99 alikuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Alizaliwa mwaka 1955.

1997- Makamu wa Rais, AISATOU N'JIE SAIDY, Gambia
Waziri wa Ustawi wa Jamii, Afya na Masuala ya Wanawake kuanzia mwaka 1996.

2004-14 Makamu wa Rais, JOYCE MUJURU, Zimbabwe
Alikuwa Jenerali wakati wa vita dhidi ya ukoloni akitumia jina la Teurai-Ropa Nhongo. Pia alikuwa Katibu wa Elimu wa ZANU-Party.
Mwaka 1980 alikuwa Waziri wa Vijana, Michezo na Burudani, mwaka 1980-85 Waziri wa Maendeleo ya Jamii na Masuala ya Wanawake, mwaka 1985-88 Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, mwaka 1988-92 Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Ushirika na Masuala ya Wanawake, mwaka 1992-96 Waziri Mkazi na Gavana wa Jimbo la Mashonaland Central, mwaka 1996-97 Waziri wa Habari, Posta na Mawasiliano, mwaka 1997 Waziri wa Rasilimali Vijijini na Maendeleo ya Maji, na mwaka 2001 Kaimu Waziri wa Ulinzi, na mwaka 2004-14 Makamu Rais wa ZANU-P. Alizaliwa mwaka 1955.
         
2005-08 Makamu wa Rais, PHUMZILE MLAMBO-NGCUKA, Afrika Kusini
Mwaka 1996-99 alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, mwaka 1999-2005 Waziri wa Madini na Nishati, kaimu Waziri wa Sanaa na Utamaduni mwaka 2004 na kuteuliwa Kaimu Rais mwaka 2004 kuanzia Julai 28 – 30, 2004 na baadaye Januari 23, 2005.
Wakati Rais Thabo Mbeki alipoondolewa kwenye uongozi na ANC, naye akaamua kujiuzulu badala ya kuwa Kaimu Rais, nafasi ambayo baadaye ilikuja kushikwa na Ivy Matsepe-Casaburri. Alizaliwa mwaka 1955.
         
2005-06 Makamu wa Rais, ALICE NZOMUKUNDA, Burundi
Kama Naibu Mkuu wa Nchi na Serikali, Nzumukunda alikuwa akishughulikia Masuala ya Uchumi na jamii.
Aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Bunge la Taifa (Transitional National Assembly) kati ya mwaka 2004-05 na Msemaji wa Chama cha Wanawake nchini Burundi (RAFEBU - Ralliement des associations des Femmes Burundaises) na Umoja wa Wanawake (League of the Women) wa chama cha CNDD-FDD.

2015 – mpaka sasa. Makamu wa Rais SAMIA SULUHU HASSAN, Tanzania
Dkt. John Magufuli akiwa na Samia Suluhu Hassan baada ya kumpendekeza kuwa mgombea mwenza wake Julai 12, 2015 mjini Dodoma.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, akila kiapo cha uaminifu kushika wadhifa huo.

Bi Samia Suluhu alizaliwa Januari 27, 1960 visiwani Zanzibar. Alisomea shule za msingi za Chawaka (Unguja), Ziwani (Pemba) na Mahonda (Unguja) na kati ya 1966 na 1972 na kisha akasomea masomo ya upili Ngambo, Unguja (1973-1975) na Lumumba, Unguja (1976).
Alisomea kozi mbalimbali hadi akafikia kupata shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire nchini Marekani.
Kazi
Aliajiriwa kama mchapishaji katika serikali ya Zanzibar mwaka 1977 na akapanda ngazi hadi kuwa afisa wa mipango serikalini kati ya 1987 na 1988.
Alihudumu pia kama meneja wa mradi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) Zanzibar kati ya 1985 na 1997, na pia kama meneja mkurugenzi wa Mwamvuli wa NGO 1998 hadi 1999.
Bi Samia anasema kuwa njia yake ya ufanisi haijakuwa rahisi kama inavyodhaniwa.
''Safari yangu katika siasa imekuwa njia ndefu na yenye tija.''
Kimsingi ufanisi wangu katika siasa za Tanzania umetokana na uweledi na umakini katika kila jambo ninalolifanya.''
''Sio rahisi kuwajibikia familia yako wakati huohuo ukiendelea na maisha ya siasa elimu na majukumu mengine ya kikazi," anasema Bi Samia.
Familia
Aliolewa mwaka wa 1978, kwa Bw Hafidh Ameir, ambaye wakati huo alikuwa afisa wa Kilimo .
Walijaliwa watoto wanne.
Mmoja kati ya wanawe Wanu Hafidh Ameir (1982), ni mwakilishi maalum katika bunge la Zanzibar

Siasa
Alijiunga na siasa mwaka wa 2000.
Wakati huo alijiunga na bunge la wawakilishi la Zanzibar kama mjumbe maalum.
Haikuchukua muda mrefu nyota yake ikaanza kung'aa na akateuliwa kuwa waziri na rais Amani Karume, akipewa wadhifa wa Waziri wa Leba, Jinsia na Watoto.
Alitumikia taifa hadi mwaka wa 2005 alipochaguliwa tena na kuteuliwa upya kama waziri, wakati huu akipewa wizara ya Utalii, Biashara na Uwekezaji katika serikali ya visiwani.
Mwaka wa 2010 alichaguliwa kuwa mwakilishi wa jimbo la Makunduchi.
Punde tu akateuliwa na rais Jakaya Kikwete kuwa waziri wa maswala ya muungano katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akihudumu chini ya Makamu wa Rais Mohamed Gharib Bilal.
Machi mwaka 2014, aliwania na kuchaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa Bunge maalum la Katiba nmjini Dodoma. Bi Hassan alichaguliwa kwa kura 390 sawa na asilimia 74.6 na kumshinda mpinzani wake Amina Abdalla Amour ambaye alipata kura 126 sawa na 24%.
Julai mwaka 2015, Dkt John Magufuli alimteua kuwa mgombea mwenza.
Wale wanaomjua Bi Hassan wanasema kuwa ni mchache wa maneno.

Comments