- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
MPANGO WA MATUMIZI
BORA YA ARDHI YA KIJIJI - 4
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini blog
BAADA ya kukamilisha hatua ya 2 ya PLUM itajitokeza bayana
kama mipaka ya kijiji inatambulika na au ilikwishapimwa.
Timu ya PLUM ya Wilaya inaweza kurahisisha kazi hiyo kwa
kuhakiki kupitia Ofisi ya Ardhi ya Wilaya na kuweka orodha ya vijiji katika
makundi yafuatayo:
Mosi, vijiji ambavyo vimekwishapimwa (vina ramani ya mipaka)
na havina migogoro ya mipaka. Vijiji hivyo moja kwa moja viandaliwe Cheti cha
Ardhi ya Kijiji.
Pili, vijiji ambavyo mipaka yake inatambulika (lakini
havijapimwa) na havina migogoro ya mipaka. Vijiji hivyo vinaweza kuandaliwa
ramani ya mipaka kwa njia rahisi ya chombo cha upimaji (GPS) na kuandaliwa
Cheti cha Ardhi ya Kijiji.
Tatu, vijiji ambavyo mipaka yake ilikwishapimwa, lakini kwa
sasa vina migogoro ya mipaka, kama vimegawanywa. Migogoro ya mipaka itatuliwe
kwanza na kubaini mipaka inayokubalika kwa pande husika.
Nne, vijiji ambavyo havijapimwa na vina migogoro ya mipaka,
ambapo migogoro hiyo haina budi kutatuliwa kwanza na kubaini mipaka
inayokubalika kwa pande zote husika.
Jukumu la awali na la msingi ili Halmashauri ya Kijiji
isimamie ardhi ya kijiji kwa mujibu wa sheria, ni kutambua mipaka ya kijiji na
kupata Cheti cha Ardhi ya Kijiji.
Katika kufanya hilo, Halmashauri ya Kijiji husika haina budi
kuwasiliana na mamlaka za ardhi inayopakana na kijiji kama vile Mamlaka ya
Hifadhi, na Halmashauri za Vijiji jirani, ili wakubaliane mpaka wa ardhi yao.
Halmashauri ya Kijiji aghalabu itakasimu shughuli hiyo kwa
kamati, kama vile Kamati ya kusimamia Matumizi ya Ardhi au Mazingira.
Kukubaliana kuhusu
mipaka
Mamlaka na halmashauri za Vijiji jirani huombwa na
Halmashauri ya Kijiji kinachohakiki mipaka yake kuwakilishwa na walau watu
wawili katika kujadili na kukubaliana uwandani (kwenye maeneo husika) kuhusu
mipaka yao.
Hawa wawe watu ambao wanaheshimika na wanaelewa vizuri
kuhusu mipaka ya vijiji husika.
Ni muhimu pia wawepo wapima wataalam (aghalabu kutoka
wilayani) kama washauri ili kuwezesha zoezi hilo kutekelezwa kwa ufanisi.
Timu ya majadiliano ya mipaka itembelee maeneo, kufanya
majadiliano na makubaliano kuhusu mahali halisi pa kila kona, ambapo kila kona
huwekewa alama ya muda kwa shimo au kigingi.
Makubaliano huwekwa kwenye kumbukumbu kama miniti au
muhtasari, kuonyesha maelezo ya mahali penye kona au alama, ikiwa na majina na
sahihi za wajjumbe wa timu nzima.
Baadaye wawasilishe makubaliano hayo katika Halmashauri za
Vijiji husika, ambazo ndizo zenye mamlaka ya kuweka mikataba ya makubaliano.
Ili kudhibiti ukiukaji wa makubaliano yaliyokwishafikiwa,
Wilaya za handeni na Kilindi zilibuni na kutumia Hati ya Makubaliano ya Mipaka
ya Vijiji ambayo ni mfano mzuri na inaweza kutumika mahali popote vijijini.
Utatuzi wa migogoro ya
mipaka ya vijiji
Fungu la 7 (2) la Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya mwaka
1999 kinatoa utaratibu wa kutatua migogoro ya mipaka ya kijiji na vijiji au
mamlaka nyingine.
Halmashauri ya Kijiji inapaswa kufanya kila juhudi kufikia
makubaliano ya mpaka na majirani zake ikiwemo kuhusisha na kupata ushauri wa
Halmashauri ya Wilaya husika.
Wilaya inaweza kutumia timu ya PLUM ya wilaya kama mshauri
wa utatuzi wa migogoro ya mipaka ya vijiji.
Watendaji wa wilaya wanaofanya kazi kama washauri au
wasuluhishi wa migogoro ya mipaka ya vijiji ni muhimu wakaelewa na kutumia
mbinu za usuluhishi ili kuepuka upendeleo, uonevu, upuuzaji, na kutokuzingatia
sheria, hivyo kufikia tu kwa muda au kukuza mgogoro badala ya kusaidia kutatua.
Ili kusaidia kutatua migogoro ya muda mrefu ya mipaka ya
vijiji katika wilaya za Handeni na Kilindi, Tume ya Taifa ya Matumizi Bora ya
Ardhi (NLUPC) iliendesha semina ya Mbinu za Usuluhishi wa Utatuzi wa Migogoro
ya Mipaka kwa timu ya wilaya ya ushauri na usuluhishi.
Endapo juhudi za Halmashauri za Wilaya zitashindwa kufikia
makubaliano au kutatua mgogoro, Sheria ya Ardhi ya Vijiji (1999) imeweka
utaratibu wa kutatua migogoro ya mipaka ya vijiji kama ifuatavyo:
* Waziri wa Ardhi atateua mtu kuwa msuluhishi kati ya Kijiji
na Kijiji au mtu au chombo ambacho kimeshindwa kuafikiana kuhusu mpaka, ili
kusuluhisha na kushawishi kufikia makubaliano.
* Kama msuluhishi atashindwa atashauri Waziri kuteua
mchunguzi ambaye atafanya uchunguzi kwa maelekezo na utaratibu ulioainishwa
katika hati ya uteuzi.
* Wakati uchunguzi unaendelea ni makosa kwa Mhusika yeyote
(Kijiji, mtu, chombo) kuchukua hatua zinazoweza kuathiri matokeo ya mgogoro.
* Waziri atayakubali mapendekezo yaliyotokana na uchunguzi
na kuwa utatuzi wa mgogoro wa mpaka labda kama ana sababu nzito zinazohusiana
na maslahi ya umma.
* Uamuzi wa Waziri kutokana na ushauri wa Mchunguzi ndio
uamuzi wa mwisho wa mgogoro wa mpaka kati ya kijiji na majirani zake.
Makubaliano ya matumizi
ya ardhi
Ikiwa itakuwa vigumu kukubaliana mipaka, au wakati utatuzi
unasubiri mkondo wa Sheria, makubaliano ya matumizi ya ardhi kwa pamoja
yanaweza kutumika kama sehemu ya njia ya kutatua mgogoro na kuendelea na
majadiliano.
Njia hii hutumika katika kurekebisha mgogoro uwe wa manufaa
na usilete ugomvi.
Katika hali ya namna hiyo, Mamlaka na Halmashauri za Vijiji
wanaweza, kwa mfano, kuafikiana na kurasimisha matumizi ya rasilimali za ardhi
katika eneo la vijiji husika chini ya masharti maalum kama vile sehemu ya
malisho ya pamoja, sehemu ya kilimo cha umwagiliaji wa pamoja, au sehemu ya
hifadhi ya msitu wa pamoja.
Mpango wa pamoja wa vijiji wa matumizi bora ya ardhi unaweza
kusaidia kutatua au kuepusha mgogoro kati ya vijiji viwili au zaidi vilivyo
jirani, na hivyo kuboresha usimamizi wa eneo linalochangiwa lenye mgogoro.
Haja hii inatokea wakati maliasili ya ardhi iliyopo katika
kijiji kimoja inakuwa pia ya muhimu kwa watumiaji wanaoishi katika kijiji au
vijiji vingine vya jirani zaidi, au maeneo mengine, wakazi wa vijiji jirani
wanategemeana katika makubaliano ya usimamizi wa matumizi ya ardhi.
Mifano mingine ni mabonde madogo, ardhi ya malisho, vyanzo
vya maji, sehemu maalum za jadi ambazo huchangiwa na vijiji zaidi ya kimoja.
Sheria ya Ardhi ya Vijiji (1999) katika Fungu la 11 inatoa
utaratibu wa kufikia makubaliano ya matumizi ya ardhi ya pamoja, ambao
umenukuliwa katika Miongozo ya PLUM.
Kuweka alama kwenye
mipaka
Ni dhahiri kwamba, jambo la mipaka ni muhimu sana kwa kuwa
linatoa fursa kwa kila Kijiji kupata Cheti cha Ardhi ya Kijiji na kupewa
mamlaka ya kutawala ardhi ya kijiji, ikijumuisha kuwa na mamlaka ya kupanga na
kugawa rasilimali kama vile ardhi ya mashamba, ardhi ya malisho, misitu, maji, barabara na
kadhalika.
Makubaliano ya mipaka yakifikiwa wapimaji wa ardhi na
wajumbe wa kamati ya ardhi (kwa niaba ya Halmashauri ya Kijiji), ikibidi na
baadhi ya wajumbe wa timu ya majadiliano, hubadilisha alama za muda (mahimo au
vigingi) katika kona za mipaka na kuweka alama za kudumu za mipaka kama vile
mawe ya upimaji (beacons).
Baada ya kona za mipaka ya kijiji kuwekwa katika eneo kwa
alama za kudumu, upimaji wa kitaalam unaweza kufanyika na kijiji kutayarishiwa
ramani ya mipaka ya kijiji inayoonyesha vile vile mipaka ya majirani zake.
Vijiji vilivyowekewa alama za mipaka vinahesabiwa kama
vimepimwa.
Upimaji wa mipaka hauna budi kuhusisha wataalam wa upimaji
ardhi na vyombo vya upimaji kama alama za rejea, darubini na kadhalika.
Upimaji huo hatimaye huwezesha kuchora ramani ya mipaka ya
kijiji kwa usahihi wa ukubwa wa maeneo.
Kesho tutaangalia kuhusu
Cheti cha Ardhi ya Kijiji pamoja na Usajili wa Vijiji.
Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com.
Tupigie: +255 656 331974
Comments
Post a Comment