- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
MPANGO WA MATUMIZI
BORA YA ARDHI YA KIJIJI - 1
Wananchi wa jamii ya Kimasai wakiangalia mchoro wa ardhi wa upangaji wa ardhi ya kijiji chao.
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini blog
SUALA la matumizi bora ya ardhi limekuwa na changamoto kubwa
vijijini ambapo ardhi imekuwa chanzo cha migogoro mingi kwa jamii mbalimbali.
MaendeleVijijini
inatambua kwamba, migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji imesababisha
vifo vya mamia kwa maelfu ya Watanzania na bado kuna kila dalili za migogoro
hiyo kuibuka katika mahali pengi nchini.
Lakini pia kumekuwa na migogoro ya ardhi baina ya wanavijiji
na wawekezaji ambao wamehodhi maeneo makubwa ya ardhi baada ya kuuziwa na
Serikali Kuu kupitia mashirika au Kituo cha Taifa cha Uwekezaji.
Ukiachana na hilo, wanavijiji wenyewe nao wamekuwa wakiuza
ardhi yao kwa watu binafsi kwa nia ya kupata fedha huku serikali za vijiji nazo
zikituhumiwa kuuza akiba ya ardhi ya kijiji, hali ambayo imefanya vijiji vingi
leo hii kukosa hata ardhi kwa ajili ya huduma za jamii kama ujenzi wa shule,
zahanati au hata makaburi.
MaendeleoVijijini
imeshuhudia vijiji vingi katika Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa vikiwa havina
ardhi, jambo ambalo ni la hatari hasa kutokana na ongezeko la idadi ya watu.
Hivi sasa wakati Serikali imekwishaweka utaratibu wa utoaji
wa hati miliki za kimila za ardhi kwa kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali
na Biashara Tanzania (MKURABITA), ndipo wananchi wengi wanazinduka na kuona
kwamba kumbe wanaweza kuyarasimisha mashamba yao na kupata hati miliki ambazo
wanaweza kuzitumia hata kukopa mitaji katika taasisi za fedha.
Katika kutekeleza malengo ya MKURABITA, Serikali kupitia
Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi (NLUPC) ilitoa mwongozo wa
utekelezaji kwa kuanza kupima ardhi za vijiji kwa kuzingatia Sheria Namba 5 ya
Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999, lengo likiwa kutekeleza misingi ya Sera ya Taifa
ya Ardhi ya mwaka 1995.
Sera ya Taifa ya Ardhi inaelekeza, pamoja na mambo mengine,
kwamba upangaji wa matumizi ya ardhi ufanyike kwa mfumo wa ushirikishwaji kwa
kuwahusisha walengwa.
Utaratibu huu unapotumika maana yake unaondoa kwa kiasi
kikubwa uwepo wa migogoro ya ardhi na kudumisha amani pamoja na kuweka mikakati
madhubuti na lengo ya maendeleo kwa pamoja.
MaendeleoVijijini
inafahamu kwamba, katika kufanikisha zoezi hilo, NLUPC huandaa Miongozo ya
Ushirikishwaji Katika Mipango na Usimamizi wa Matumizi Bora ya Ardhi Vijijini
(Participatory Land Use Management – PLUM) kuanzia ngazi ya Wilaya na hatimaye
katika ngazi ya kijiji huwa kuna kamati ya VLUM.
Miongozo hiyo inabainisha hatua kuu sita katika mchakato wa
upangaji na utekelezaji ambapo hatua hizo zinapitia mchakato mzima wa
maandalizi, upangaji, utawala na usimamizi wa ardhi, tathmini, ufuatiliaji,
uimarishaji na urejeaji mipango.
Kwa kufuata mchakato huo, wilaya na vijiji vilivyokwishaanza
utekelezaji wa PLUM kila wakati vinatakiwa view katika nafasi ya kujitathmini
na kuelewa vyema vimo katika hatua gani ya PLUM kwa kufuata Mpango Kazi wa
Jamii (Community Action Plan – CAP) waliojiwekea, ambao kimsingi huandaliwa
katika Hatua ya Pili ya PLUM.
MaendeleoVijijini
inatambua kwamba, hatua hizo sita zilizoainishwa katika Mwongozo wa PLUM
zinahusisha pia utawala na usimamizi wa ardhi kwa kuzingatia sheria za ardhi.
Hatua ya Kwanza ni maandalizi wilayani ambapo inahusisha
uhamasishaji, kuunda timu ya PLUM ya Wilaya, na kuweka Mpango wa Utekelezaji wa
PLUM wa Wilaya.
Hatua ya Pili ni kufanya tathmini ya Matumizi ya Ardhi
Vijijini – PRA ambayo inahusisha uhamasishaji wa taasisi za kijiji na kuweka
mpango kazi wa jamii – CAP.
Hatua ya Tatu inahusu Mipaka ya Ardhi ya Kijiji ambayo
inahusisha kubaini, kuweka na kupima mipaka ya ardhi ya kijiji, utatuzi wa
migogoro ya mipaka, msjala ya ardhi ya wilaya, pamoja na utoaji wa Cheti cha
Ardhi ya Kijiji.
Hatua ya Nne inahusu upangaji wa matumizi bora ya ardhi ya
kijiji na mikakati ya usimamizi na utekelezaji wake, ambapo inahusisha
ushirikishwaji katika mipango na usimamizi, kuainisha hatua stahili za
usimamizi (Land Management Measures), na Sheria Ndogo za Usimamizi wa Matumizi
Bora ya Ardhi.
Hatua ya Tano inahusu Utawala wa Ardhi ya Kijiji, ambayo
inahusisha masjala ya ardhi ya kijiji, utoaji, usajili na usimamizi wa
Hatimiliki za Kimila, na utatuzi wa migogoro ya miliki.
Hatua ya Sita inahusu Utekelezaji wa Hatua Stahili za
usimamizi wa Ardhi na Uimarishaji, ambapo inahusisha mafundi sanifu wa kijiji,
uendelezaji hatua stahili, uimarishaji, tathmini, ufuatiliaji na urejeaji
mipango.
Uundaji wa Timu ya
PLUM ya Wilaya
Uzoefu wa MaendeleoVijijini
unaonyesha kwamba, Timu ya PLUM ya Wilaya huundwa na Halmashauri ya Wilaya
husika, ikihusisha wajumbe 4 – 6 kutoka sekta kuu zinazohusika na matumizi ya
ardhi ikiwemo Kilimo, Mifugo, Maliasili, Ardhhi na Maendeleo ya Jamii.
Kwa kawaida, mtaalam anayehusika na mipango ya matumizi ya
ardhi wilayani ndiye huwa mratibu wa timu hiyo.
Majukumu ya timu ya PLUM ni kuratibu na kuwezesha uandaaji,
utekelezaji na usimamizi wa mipango ya matumizi ya ardhi wilayani.
Katika kutekeleza hayo, hapana budi timu hiyo kuandaa mpango
wa jumla wa utekelezaji, unaoonyesha jinsi gani wilaya inakusudia kuviwezesha
vijiji vyake vyote kuandaa na kutekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi.
MaendeleoVijijini
inatambua kwamba, kwa kufuata vigezo vilivyoainishwa, hupendekeza kuteua baadhi
ya vijiji kuwa vya kuanzia (vya mfano) ambavyo vitawezeshwa katika kipindi cha
muda mfupi (miaka 2-3), vijiji vitakavyoongezeka katika muda wa kati (miaka
3-5), na muda mrefu (miaka 5 na kuendelea) kama inanvyoshauriwa kwenye miongozo
ya PLUM.
Vilevile, timu hiyo huandaa Mpango Kazi (Action Plan) na
kuhakikisha rasilimali zinazohitajika kwa utekelezaji kama vile fedha, nguvu
kazi na vitendea kazi vinapatikana kwa wakati.
Kwa uzoefu uliopo, ni muhimu timu hiyo izingatie uhusishaji
wa sekta zote husika (sectoral integration) katika upangaji na utekelezaji,
ikiwemo miradi na taasisi zisizo za kiserikali (CBOs na NGOs) zinazohusika na
matumizi ya ardhi na rasilimali zake.
Aghalabu, Tume ya Taifa ya Matumizi Bora ya Ardhi (NLUPC)
huwezesha warsha iliyoandaliwa na wilaya husika ili kuhakikisha wilaya
inajiandaa vyema kutekeleza PLUM katika vijiji vyake.
MaendeleoVijijini
inafahamu kwamba, vijijini ambavyo vina mipango ya atumizi bora ya ardhi
iliyoandaliwa kwa ushirikishwaji ikihusisha sekta kuu za matumizi ya ardhi,
vina nafasi kubwa ya kutekeleza kwa ufanisi miradi ya kisekta kama vile PADEP
(Kilimo), WMA na CBFM (Maliasili), na utoaji na usajili wa Hatimiliki za Kimila
(Ardhi).
Uzoefu unaonyesha kwamba, baadhi ya miradi hiyo inataka
kufikia hatua ya kumilikisha ardhi kwa wanavijiji katika maeneo wanayofanyia
kazi.
Kwa mfano, Mradi wa Usimamizi wa Maeneo ya Wanyamapori
(Wildlife Management Areas – WMA) ulishughulikia Vyeti vya Ardhi ya Vijiji na
Hatimiliki za Kimila katika wilaya za Serengeti, Meatu, Iringa Vijijini na
Kilolo.
Mradi wa Maji na Mazingira Vijijini (RWSSP) mkoani Simiyu
ulishughulikia utoaji wa Vyeti vya Ardhi ya Vijiji na Hatimiliki za Kimila kwa
maeneo ya vyanzo vya maji katika Wilaya ya Bariadi, wakati huo ikiwa ndani ya
Mkoa wa Shinyanga.
Aidha, Mradi wa Usimamizi wa Misitu kwa Kushirikisha Jamii
(Community-Based Forest Management – CBFM) ulifanikisha utoaji wa hatimiliki za
Kimila za maeneo ya misitu ya jamii katika wilaya za Liwale mkoani Lindi, na
Iringa Vijijini na Kilolo mkoani Iringa.
Kwa ujumla, MaendeleoVijijini
inaamini kwamba, hatimiliki za ardhi zikitolewa kwa kuzingatia matumizi ya
sekta moja moja zinaweza kukwamisha maendeleo na kuleta migogoro ya matumizi ya
ardhi wakati itakapofikia kukosa ardhi kwa matumizi mengine kwa vile sehemu
kubwa ya ardhi itakuwa imemilikishwa kwa matumizi ya sekta fulani iliyowahi
kuwa na mradi kijijini.
Mfano mzuri ni Kijiji cha Kiwere katika Wilaya ya Iringa
Vijijini, ambapo kupitia mradi wa CBFM (Maliasili) mwaka 2005 kilitenga hekta
4,904 kama msitu wa hifadhi na hekta 1,500 kama msitu wa matumizi mbalimbali
yakiwemo kuni, mijengo, mbao na kadhalika wakati kijiji kizima kina eneo la
hekta 6,859.
Hiyo inamaanisha kwamba eneo lililotengwa kwa ajili yam situ
ni asilimia 93 ya eneo lote la kijiji.
Kwa kuwa hawakutenga maeneo ya kutosha kwa shughuli
nyingine, sasa wanautumia msitu huo kwa shughuli za kilimo na mifugo.
Katika hali kama hiyo, inabidi kusitisha utoaji wa hati
miliki mpaka kijiji kinapokuwa kimeandaa mpango wa matumizi ya ardhi
unaozingatia matumizi ya sekta zote kuu.
Kesho tutaangalia
namna wananchi wanavyoshirikishwa katika tathmini ya ardhi ya vijiji.
Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com.
Tupigie: +255 656 331974
Comments
Post a Comment