- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
MPANGO WA MATUMIZI
BORA YA ARDHI YA KIJIJI - 6
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini blog
SHERIA ya Ardhi ya Vijiji katika Fungu la 12 na 13 inatoa
taratibu na maagizo ya kisheria kuhusu misingi ya mipango ya matumizi bora ya
ardhi ya vijiji.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, ardhi ya kijiji itagawanywa
katika mafungu matatu; Mosi, ni ardhi inayokaliwa na kutumiwa na watu, familia
au kikundi cha watu kwa mujibu wa Sheria za Kimila.
Pili, ni ardhi ya makazi au matumizi ya jumuiya ambayo
inaweza kutolewa kwa njia ya mgao wa Halmashauri ya Kijiji, na Tatu, ni ardhi
ya pamoja ambayo halmashauri ya Kijiji itapendekeza kwa Mkutano wa Kijiji maeneo
na makusudio ya matumizi ya maeneo hayo.
MaendeleoVijijini
inafahamu kwamba, mapendekezo ya Halmashauri ya Kijiji yanaweza kuwasilishwa
kama mpango wa matumizi bora ya ardhi ya kijiji au sehemu ya kijiji.
Pia, uandaaji wa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ya Kijiji
unapaswa kuzingatia ushiriki wa wanakijiji wote (wadau mbalimbali kwa kujali
jjinsia, rika na kadhalika) na upangaji na utekelezaji wa hatua kwa hatua kama
zilivyoainishwa kwenye Mwongozo wa Ushirikishwaji katika Mpango wa Usimamizi wa
Matumizi Bora ya Ardhi Vijijini.
Umuhimu wa mipango na usimamizi wa matumizi bora ya ardhi ni
kwamba, ardhi ni mali asasi, jukwaa la maisha ya binadamu, na inatumika
kuzalisha mazao, kufugia mifugo, kuhifadhia wanyamapori na misitu, kujenga
nyumba, huduma na kadhalika.
Kwahiyo, Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Kijiji ni utaratibu
wa kutathmini na kupendekeza namna mbalimbali za matumizi ya maliasili au
rasilimali ili kuinua hali ya maisha ya wanakijiji na kuondoa umaskini.
Maliasili muhimu katika ngazi ya kijiji ni udongo, maji,
mwanga wa jua, mimea na kadhalika.
MaendeleoVijijini
inatambua kuwa, matumizi stahili ya maliasili hizo hutegemea zaidi uwezo wa
watu wa kutumia na kusimamia vipaumbele vyao, uchumi wa jamii na uendelevu wa
maliasili hizo.
Kwahiyo basi, mipango ya usimamizi wa matumizi bora ya ardhi
unapaswa kutambulika kama ni utaratibu wa kupanga, kutekeleza na kuhuisha
matumizi ya ardhi.
Utaratibu huo unafaa zaidi iwapo utafanyika kwa njia ya
ushirikishwaji, ikiwa na maana kuwa watumiaji wakubwa wa ardhi ambao ni wanakijiji wanashirikishwa kikamilifu.
Ili kuhakikisha kuwa wanakijiji wanashiriki kikamilifu, ni
muhimu kuzingatia makundi mbalimbali yaliyopo katika kijiji (pamoja na jinsia),
ambayo yana utashi na malengo yanayotofautiana.
Upanuaji wa makazi, maeneo ya kilimo, maeneo ya malisho,
ukataji miti kwa matumizi mbalimbali, mahitaji ya maji na kadhalika vinazidi
kusababisha mzigo au kani kwenye ardhi kwa matumizi mbalimbali.
Uchunguzi wa MaendeleoVijijini
unaonyesha kuwa, hali hiyo inasababisha kuongezeka kwa idadi ya migogoro
miongoni mwa watumiaji wa ardhi, kutokuwa na uhakika wa miliki na matumizi ya
ardhi, maendeleo duni ya soko la ardhi lisilo rasmi, uharibifu wa udongo na
vyanzo vya maji, ufyekaji wa misitu, ongezeko la kuhamahama kwa watu na mifugo,
na kupanuka kwa ukame na tishio la jangwa.
Migogoro inayojulikana sana nchini Tanzania ni kati ya
wakulima na wafugaji, ambapo imeshuhudiwa mamia ya wananchi wakipoteza maisha
kutokana na mapigano baina ya jamii hizo.
Kupanuka kwa kilimo katika ardhi ya malisho kunatokana na
ongezeko la watu na uharibifu wa ardhi na mazingira, hivyo kuwalazimisha
wafugaji kulisha zaidi kupita kiasi katika maeneo yaliyobaki au kuhamisha
mifugo yao kwenye maeneo ambayo awali yalikuwa hayana mifugo au ilikuwa
michache na kusababisha migogoro mipya katika maeneo hayo.
Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya, Rukwa, Iringa, Njombe
na Ruvuma) na mikoa ya Kusini na Mashariki (Pwani, Morogoro, Lindi na Mtwara)
awali haikuwa na mifugo mingi na mingine haikuwa kabisa na mifugo kama ng’ombe,
lakini hivi sasa wafugaji wa jamii za Wasukuma na Wamasai wamevamia na kuweka
makazi kutokana na kufuata malisho.
Matumizi mengine ya ardhi ambayo yamekuwa na migogoro ni
kati ya kilimo na misitu, kilimo na mbuga za wanyama, upanukaji holela wa
makazi katika ardhi ya kilimo, malisho na misitu, hususan upanukaji wa miji.
Kadhalika MaendeleoVijijini
inafahamu kwamba, kuna migogoro ya chinichini kwa mfano kati ya kijiji na
miongoni mwa wanakijiji au wakulima wakubwa (wawekezaji), makundi mbalimbali ya
kijamii na uchumi (jinsia), familia na watu binafsi wanaodai haki ya matumizi
katika maliasili za eneo moja la ardhi.
Uchunguzi unaonyesha kwamba, wakati mwingine kampeni za
kilimo fulani, kampeni za upandaji miti na kadhalika huzidisha migogoro hiyo
kama watu hawakushirikishwa na kukubaliana, mathalan miti ipandwe wapi na kwa
namna gani.
Uzoefu unaonyesha kwamba, migogoro hiyo hukwaza matumizi
endelevu ya ardhi na kudumaza maendeleo vijijini.
Juhudi za serikali na taasisi nyingine kuhamasisha wakulima
wadogo kuwekeza kwenye matumizi endelevu ya ardhi mara nyingi hushindwa kama
migogoro ya ardhi inakuwa haijatatuliwa vizuri na panapokuwa hakuna uhakika wa
miliki ya ardhi.
Kwa kawaida wakulima wako radhi kuwekeza katika ardhi yao
kwa ajili ya kupata pato kubwa na uzalishaji endelevu pale tu wanapokuwa na
uhakika wa kuitumia ardhi hiyo kwa muda mrefu, ili wanufaike na uwekezaji wao.
Kwahiyo, Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ya Kijiji hujaribu
kuweka utaratibu wa matumizi ya rasilimali za ardhi kwa kutatua migogoro,
kuimarisha miliki za ardhi na matumizi yake, kugawa ardhi na kuboresha matumizi
na hifadhi ya ardhi kulingana na mapendekezo na uwezo wa walengwa.
Huo ni mchango mahsusi katika maendeleo vijijini na nyenzo
muhimu katika kuboresha hali ya maisha ya watu, kuondoa umaskini na utunzaji wa
mazingira (maliasili).
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (UN-FAO)
linafasili mipango ya matumizi ya ardhi kama, Utaratibu wa tathmini ya uwezo wa
ardhi na maji, unaojumuisha chaguzi mbadala za matumizi ya ardhi na hali ya
uchumi na jamii, ili kuchagua na kutumia aina bora za matumizi ya ardhi.
Madhumuni yake ni kuchagua na kutekeleza matumizi ya ardhi
ambayo yatatosheleza kwa zaidi, mahitaji ya watu, wakati huo huo yakitunza
maliasili kwa siku za mbele.
Msukumo mkubwa katika kupanga ni haya ya mabadiliko, haja ya
kuwa na usimamizi bora au haja ya kuwa na aina tofauti kabisa ya matumizi ya
ardhi kutokana na mabadiliko ya hali halisi.
Mwelekeo wa ushirikishwaji wa walengwa katika mipango na
usimamizi wa matumizi bora ya ardhi unazingatia, Kwanza kabisa, umuhimu wa
mipango ya matumizi na usimamizi wa ardhi utokane na watumiaje wa ardhi
wenyewe, ambao ndio wanaoathirika moja kwa moja na migogoro na uharibifu wa
ardhi, na amao ndio watanufaika kutokana na usimamizi wa matumizi ya rasilimali
kuboreshwa.
Ni vizuri kuhakikisha wanakijiji wanahusika kikamilifu
katika kuandaa utaratibu, ugawaji ardhi na kutawala upangaji katika hatua zote.
Uwezo wa wenyeji katika kufanya uamuzi unajengwa kupitia
uhamasishaji wa taasisi zilizopo kwenye kijiji.
Ni vyema pia kuzingatia kazi ya kukusanya taarifa na
uchambuzi wake, mambo gani yawe muhimu, na mipango yenyewe kwamba itokane na
wenyeji na hivyo kuweza kunyumbulika na kushirikisha taaluma za sekta
mbalimbali.
Kwa upande wa wataalam, jukumu lao kubwa ni kuasisi,
kushauri na kuwezesha mfumo wa ushirikishwaji katika mipango na usimamizi wa
matumizi bora ya ardhi kuliko kutayarisha mipango yao wenyewe kama
ilivyozoeleka katika mipango msonge (juu-chini).
Wataalam wanapaswa wawe makini kuhakikisha viwango na
ushauri wa kitaalam vinazingatiwa.
Ni muhimu sana wataalam wa sekta kuu za matumizi ya ardhi
kama ilivyoainishwa katika Hatua ya 1 wakati wa kuunda Timu ya PLUM ya Wilaya
wakawezesha kwa pamoja hatua hii ili kupata muafaka wa matumizi ya ardhi ya kijiji
unazozingatia viwango vya utaalam wa sekta zote, hususan kilimo, maliasili,
mifugo na ardhi.
Sekta hizo zikishauri na kufikia uamuzi wa matumizi ya ardhi
ya kijiji bila ushirikiano, na kwa nyakati tofauti, hujikanganya, kuwakanganya
wanakikiji, na kupoteza muda na rasilimali.
Kesho tutaangalia kuhusu
aina ya matumizi ya ardhi kwenye ngazi ya kijiji.
Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com.
Tupigie: +255 656 331974
Comments
Post a Comment