Featured Post

SUNGURA KUTOKWA DAMU PUANI (EPISTAXIS)


Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog

TATIZO la sungura kutokwa na damu puani kitaalam linaitwa Epistaxis na inawezekana baada ya wafugaji wa sungura wamewahi kukumbana nalo na hawakujua ni nini.

Kutokwa na damu puani kwa sungura hutokea kutokana na mojawapo kati ya sababu tatu zisizo za kawaida: tatizo la kuganda kwa damu, uvimbe mkubwa, au ugonjwa wa kiungo (organ disease).
Matatizo yanayosababishwa na kutokwa damu puani yanaweza kutofautiana kuanzia yale madogo kama kupiga chafya hadi yale ya hatari kama upungufu wa damu (anemia) kutokana na kupoteza damu nyingi, au njia ya upumuaji, na kushindwa kufanya kazi kwa njia ya mfumo wa damu.
Mfumo wa mmeng’enyo nao unaweza kuathiriwa pia kama sungura anameza kiwango kikubwa cha damu.

Dalili

* Kutokwa na damu puani
* Kupiga chafya, kutokwa na majimaji, kuonekana kwa damu kwenye miguu ya mbele
* Kutokwa na machozi mara kwa mara
* Kutokwa na mate mara kwa mara
* Kupoteza hamu ya kula
* Damu katika mkojo, kinyesi, au katika maeneo mengine ya mwili kama tatizo la kutokwa damu (hemorrhage) lipo
* Kinyesi cheusi (kutokana na damu kuchanganyika na chakula) hasa kama alimeza damu.

Chanzo

Sungura wako hatarini kupatwa na tatizo la epistaxis kama watakuwa na mfumo daifu wa kinga ya mwili au kama wanaishi katika mazingira yasiyo safi na salama.
Sababu kubwa za tatizo hili ni pamoja na:
* Maambukizi ya bacteria au kuvu (fungal)
* Tatizo la mzizi wa jino (tooth root abscess)
* kuingiza kitu kigeni ndani ya pua — hususan kipande cha majani (kama nyasi au hata mbegu)
* Jeraha la jino — hasa kutokana na kutafuna nyaya za umeme
* Jipu kubwa au uvimbe kwenye eneo la ndani la pua
* Tatizo la kuganda kwa damu — yaweza kusababishwa na madhara ya kemikali za aina ya anticoagulant.

Uchunguzi

Ofisa mifugo atafanya uchunguzi wa jumla kwa sungura wako, akichunguza pia historia ya dalili hizo pamoja na matukio ambayo yanaweza kusababisha hali hiyo.
Kunaweza kukawa na sababu nyingi kwa hali hiyo, hivyo ofisa mifugo anaweza kutumia mbinu tofauti za uchunguzi kujua tatizo ni nini hasa.
Mchakato huu unaongozwa na uchunguzi wa kina zaidi wa matatizo yanayotokeza hadharani, bila kuzingatia kwanza sababu zilizozoeleka hadi tatizo halisi litakapogundulika na kama linaweza kutibika kwa usahihi.
Uchunguzi wa jumla wa damu utafanyika, ikiwemo uchunguzi wa kikemia wa damu pamoja na kuangalia kiasi cha damu.
Uchambuzi wa damu unaweza kuonyesha upungufu wa chembe chembe za damu pamoja na anemia.
Kiwango cha mzunguko wa damu kitaangaliwa kuona kama damu hiyo ina kawaida ya kuganda hali ambayo inaweza kuleteleza kukoma kwa kuvuja kwa damu.
Matatizo ya kuganda kwa  damu yanaweza kusababisha kuvuja kwa damu na tatizo sugu la kutokwa damu (hemorrhage).
Uchunguzi wa kimaabara utahusisha X-ray kwenye fuvu la kichwa na mifupa ya taya kuangalia uvimbe, ukuaji au majeraha, na X-ray ya kifua kuangalia mfumo wa upumuaji kuona kama kuna uwezekano wa uvimbe kusambaa (kama kuna dalili za kansa).
Inategemea na nini kilichoonekana, kipimo cha Computed Tomography (CT-Scan) na kile cha Magnetic Resonance Imaging (MRI) vinaweza pia kutumika kwa sungura wako.
Kama majipu au uvimbe utaonekana, ofisa mifugo anaweza kufanya kipimo cha biopsy kwa kuangalia tishu ya nyama za pua, au kuchukua sampuli ya ute wa mifupa (bone marrow). Sampuli za damu na majimaji zinaweza kuchukuliwa kuangalia kama kuna maambukizi ya bacteria na kuvu (fungus).

Tiba 

Ofisa mifugo atahitaji kutibu dalili kwanza; hii inamaanisha kuzuia kuvuja kwa damu kabla ya afya ya sungura wako haijawa mbaya zaidi.
Dawa zitatolewa kuzuia kuvuja kwa damu na kusaidia mzunguko mzuri wa damu.
Kama kutakuwa na jeraha, dawa za aina ya antibiotics zinaweza kutumika. Vinginevyo, tiba itategemea na uchunguzi wa mwisho.

Maisha na Utunzaji

Ufuatiliaji wa utunzaji wa sungura wako utahusisha uchunguzi wa mara ya pili wa mzunguko wa damu na muda wake ili kuzuia kujirudia kwa tatizo.
Ukiwa nyumbani, utahitaji kuwachanguza sungura wako kama wana dalili zozote za magonjwa, na uyatengeneze mazingira wanayoishi sungura wako kuwa salama zaidi wasije wakaumia, ili kuzuia kuvuja damu.
Kama sungura wako watagundulika wana tatizo katika mfumo wa mzunguko wa damu, unatikiwa uwe mwangalifu wasije wakaumia na kupata majeraha, hata kama ni madogo.
Japokuwa siyo mara nyingi sana, lakini sungura wanaweza kupata ugonjwa wa upungufu wa damu (anemia) na kuzimia kama tatizo hili la epistaxis halitatibiwa kwa usahihi.

Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Tupigie: +255 656 331974



Comments