- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini blog
SUNGURA ni
mmoja wa wanyama wanaozaana kwa kasi kubwa. Sifa hii imekuwa chagizo katika
mukhtadha mzima wa kuhamasisha ufugaji wa sungura kibiashara kwa sababu mkulima
anaweza kuwa na kundi kubwa la sungura katika kipindi kifupi.
Lakini kwa
dhima hii, ndipo wametokea baadhi ya watu wa kati – madalali ambao baadhi yao
wamesajili makampuni kabisa kisheria – wanaowahamasisha wakulima kwa kuwapigia
hesabu za kwenye makaratasi kwamba watakuwa mamilionea ndani ya kipindi kifupi
bila kuzingatia uhalisia wenyewe.
Watu hawa,
ambao asilimia 99 ni wale ambao hawajawahi kufuga wala kuona adha na changamoto
za mifugo, wamefikia hatua ya kuwasainisha wakulima mikataba ya kinyonyaji kwa
madai kwamba wao wanajua wapi masoko yalipo wakati ukweli biashara wanayoifanya
ni ile ya ‘mkulima kwa mkulima’, yaani wanaangalia nani wamemsainisha mkataba
na kama anao sungura wa mbegu wanakwenda kuchukua na kumuuzia mwingine.
Soko la
namna hiyo tunaweza kulifanya sisi wenyewe wakulima kama tutaunda umoja wetu
madhubuti badala ya kutegemea madalali ambao wanatunisha vitambi maofisini bila
kujua adha iliyopo katika ufugaji wenyewe.
Nimewahi
kuzungumza huko nyuma kuhusu suala la uzalishaji wa sungura, kwamba ni wanyama
wanaozaa kwa kasi. Sungura wa jamii nyingi kipindi cha uzazi hudumu kwa miezi
tisa kwa mwaka, kuanzia Februari hadi Oktoba.
Sehemu
nyingine kama Australia na New Zealand, kipindi cha uzazi huwa kati ya Julai na
Januari.
Sungura
jike anafikia uwezo wa kuzaa anapokuwa na miezi sita wakati dume anakuwa
amekomaa anapofikisha miezi saba.
Kipindi
cha mahaba kwa sungura jike na dume huwa ni kifupi sana, ni kati ya sekunde 30
hadi 40 tu hivi. Unapotaka kupandisha, ni vyema kumchukua sungura jike na kumpeleka
katika kizimba cha dume na siyo kinyume chake.
Tabia zao
za mahaba zinahusisha kulambana, kunusana na hapo dume atamfuata jike. Kukojoa
nayo ni moja ya tabia za mahaba kwa sungura.
Mimba
hutungwa takriban saa kumi baada ya tendo la unyumba na baada ya hapo sungura
jike huanza kujitengenezea kiota au shimo na kukinakshi kiota hicho kwa manyoya
yake kutoka katika baadhi ya sehemu zake za mwili, hususan tumboni na eneo
lenye matiti. Hii husaidia pia chuchu kuonekana ili iwe rahisi kwa watoto wake
kuziona chuchu hizo watakapozaliwa, kwa vile watoto wa sungura huzaliwa vipofu
na hawana manyoya.
Macho ya
watoto wa sungura hufunguka siku 11 baada ya kuzaliwa na huanza kula wenyewe
wanapofikisha siku 14. Watoto hao huwa hawana manyoya lakini ngozi yao hulindwa
na aina fulani ya manyoya ya kitoto ambayo huanza kuota siku chache baada ya
kuzaliwa.
Manyoya
magumu huota baada ya wiki tano au sita na akifikisha umri wa miezi sita na
nane manyoya hayo nayo hutoka na kurithiwa na manyoya mengine ambayo huishi
nayo hadi mwisho wa uhai wake.
Sungura
kwa kawaida anabeba mimba kwa siku 35 ingawa wengine wanaweza kuzaa kati ya
siku ya 32 au 33 baada ya kubeba mimba.
Kwa
kawaida, sungura jike aliyeshika mimba hujulikana kwa mwenendo wake, huwa
mtulivu, na hula chakula kidogo.
Sungura
anazaa watoto kati ya wanne na 15 kutegemeana na umri na afya yake na maumbile
ya watoto hutegemea pia umbile la mama. Sungura wenye umbile kubwa huzaa watoto
wakubwa na wenye afya.
Kwa kwaida
sungura hunyonyesha kwa siku 30 ingawa sungura huacha kuwahudumia
(kuwanyonyesha) watoto wake wanapofikisha umri wa wiki nne na tano. Kwa kuwa
maziwa yake yana virutubisho vingi, sungura hunyonyesha watoto wake mara chache
sana, takriban mara moja au mbili tu kwa siku.
Kwa kuwa
ni mnyama ambaye hupata joto kila wakati, hata wakati ananyonyesha, sungura
anaweza kupata ujauzito wakati wowote kama usipokuwa makini na afya yake na
watoto wake.
Hiyo maana
yake ni kwamba, ndani ya mwaka mmoja tangu anapoanza kuzaa, sungura anaweza
kuwa na watoto, wajukuu na vitukuu takriban 800.
Kama
unafuga sungura kibiashara na kwa tija – ingawa wana uwezo wa kuzaa hadi mara
nane kwa mwaka – watengee muda ili wazae mara tano tu kwa mwaka. Hii maana yake
kama atazaa wastani wa watoto nane kwa mara moja, kwa mwaka atazaa watoto 40.
Idadi ya watoto
watakaokua itategemea mama yao ni mzuri kiasi gani katika unyonyeshaji na ubora
wa afya yake pamoja na jitihada zako katika kuwatunza.
Sungura jike ambaye hawezi kufikia kiwango hicho cha uzazi lazima
aondolewe. Kama sungura hazai, basi anakutia hasara kwa sababu anatumia
chakula bila faida.
Wastani wa uzito unaotakiwa ni kati ya kilogramu 2 hadi 2.5 wakati
sungura anapofikisha umri wa wiki nane hadi 10.
Muda huo hutegemea pia na matunzo yako unayompatia, aina ya
sungura, mazingira, na kiwango cha protini unachomchanganyia kwenye lishe yake.
Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com.
Tupigie: +255 656 331974
Comments
Post a Comment