Featured Post

NAWA MIKONO KWA SABUNI ILI UOKOE MAISHA


Na Elikunda Materu
USAFI ni jambo muhimu sana katika dira ya afya ya jamii ya kupunguza maambukizi na athari za maradhi.
Kupungua kwa haraka kwa vifo vinavyotokana na magonjwa ya kuambukiza kulikoonekana katika nchi tajiri mnamo karne iliyopita kusingeweza kufikiwa bila uboreshaji wa hali ya juu wa afya ya jamii.

Kupanda kwa viwango vya maisha kuliwawezesha  watu kujali zaidi usafi pale ambapo maji safi yaliwafikia majumbani mwao, na bei ya sabuni ilipokuwa nafuu kiasi kwamba  ilikuwa rahisi kuweka sabuni katika kila sinki.
Lakini juhudi za pamoja baina ya harakati za afya ya jamii na sekta binafsi zimewezesha mambo kama vile usafi wa mikono, makazi, na katika maisha kuwa ni sehemu ya maisha ya jamii.
Kwa kutambua umuhimu wa kunawa mikono kwa maji na sabuni, ndipo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na wadau wengine nchini, huratibu maadhimisho ya “Siku ya Kunawa Mikono Duniani” ambayo kilele chake huwa tarehe 15 Oktoba, kila mwaka.
Siku hii Kwa hapa nchini, maadhimisho haya yalianza kufanyika mwaka 2008, lengo la maadhimisho hayo ni kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kunawa mikono kwa maji na sabuni ili kujikinga na magonjwa ya kuambukiza
Nchini Tanzania takwimu za mwaka 2010 zinaonyesha watoto zaidi ya laki moja wenye umri wa chini ya miaka mitano waliambukizwa ugonjwa wa kuhara ambapo kati ya hao 440 walifariki dunia.
Vifo hivi visingetokea endapo jamii ingezingatia tabia za usafi kwani tafiti zinaonesha kuwa unawaji wa mikono kwa maji na sabuni hupunguza kwa asilimia 42 - 50 magonjwa ya kuhara na asilimia 30 kwa magonjwa ya mfumo wa hewa.
Umuhimu wa siku hii unatokana na ukweli kuwa mikono iliyochafuliwa huchangia kwa kiasi kikubwa kuenea kwa magonjwa kama kuhara, kipindupindu, minyoo, magonjwa ya macho na ngozi pamoja na magonjwa mengine yanayoshambulia mfumo wa hewa kama vile mafua na homa ya mapafu (pneumonia).
Kwa bahati mbaya, katika nchi maskini hadithi hizi hazijaleta tofauti ya maisha. Hadi kufikia mwishoni mwa karne ya 20, watu bilioni mbili bado hawakuwa na uwezo wa kupata maji safi kadiri inavyotakiwa, na watu bilioni moja hawakuwa na  maji safi ya kunywa yanayotosheleza mahitaji yao.
Jitihada za kuhamasisha kwa ufanisi hali ya usafi zimekuwa za polepole sana na mara nyingi bila mafanikio.
Ingawa maendeleo ya viwanda yamerahisisha upatikanaji wa sabuni majumbani, bado hayajafanikiwa kuhamasisha hali ya usafi au mwamko wa watu kuhusu unawaji mikono kwa sabuni kwa kiwango cha juu ili kwenda sambamba na matokeo ya maendeleo hayo.
Vyanzo vikuu viwili vya vifo vya watoto katika nchi zinazoendelea kwa sasa ni magonjwa ya kuhara na maambukizi ya mfumo wa upumuaji. Kitendo kidogo cha kunawa mikono kwa sabuni kinaweza kuondoa takribani nusu ya hatari ya kuambukizwa magonjwa ya kuhara na takribani theluthi ya maambukizi ya mfumo wa upumuaji.
Hali hii inakifanya kitendo cha kunawa mikono kuwa chaguo bora zaidi la kuzuia maambukizi ya magonjwa kuliko chanjo au kinga nyingine yoyote.
Ikiwa nchi zinazoendelea zinataka kufikia malengo yao ya maendeleo ya milenia ifikapo mwaka 2015 ya kupunguza vifo vya watoto, ajenda hii iliyosahaulika katika karne ya 20 haina budi kutiliwa maanani. Haitoshi tu maji safi na salama kupatikana kote, bali pia tabia ya kunawa mikono kwa sabuni lazima iwe kwa watu wote.
Kunawa mikono ni njia madhubuti zaidi ya kuzuia au kujikinga dhidi ya magonjwa ya kuhara.
Ushahidi unaonesha kwamba unawaji mikono ulioboreshwa unaweza kuwa na matokeo makubwa kwa afya ya jamii katika nchi yoyote, na unaweza kwa kiasi kikubwa, kupunguza vyanzo vikuu viwili vya vifo vya watoto kwa magonjwa ya kuhara na maambukizi ya mfumo wa upumuaji.
Kwa sababu kitendo cha kunawa mikono kwa sabuni kinaweza kuzuia ueneaji wa vijidudu visababishavyo magonjwa, kinaweza kuwa kinga madhubuti zaidi kuliko kinga nyingine yoyote au tabia nyingine yoyote ya usafi.
Unawaji wa mikono kwa maji na sabuni ni njia rahisi na yenye uwezo mkubwa wa kuzuia magonjwa niliyo yataja hapo awali.
Takwimu za unawaji wa mikono kwa hapa Tanzania zinaonesha kuwa asilimia 20 ya watu hunawa mikono kabla ya kuandaa chakula na kwamba asilimia 13 pekee ya vyoo ndivyo vyenye vifaa vya kunawia mikono.
Idadi hii ni ndogo na ni ishara kuwa unawaji wa mikono hususani baada ya kutoka chooni bado upo chini.
Hali hii inaonekana katika maeneo mengi yenye vyoo vya kulipia na katika makazi ya watu kumeshindikana kuzingatia uwekaji wa vifaa hivi kama maji yakutosha na sabuni, hivyo kuhatarisha maisha ikiwamo kuzuka kwa magonjwa ya mlipuko kwa wakati fulani wowote kama jamii haitachukua tahadhari.
Iwapo kutakuwa na uhamasishaji mkubwa, tabia ya kunawa mikono kwa sabuni inaweza kuchukuliwa kuwa ni kinga ya kujipatia mwenyewe.
Takriban kila kaya duniani, bila kujali hadhi yake kiuchumi, huwa na sabuni.
Hata hivyo, unawaji mikono kwa sabuni katika nyakati muhimu, kwa kiasi kikubwa, haufanyiki kabisa au haufanyiki ipasavyo.
Ili kufikia malengo ya maendeleo ya milenia ya kupunguza vifo vya watoto yafikiwe, mienendo ya kunawa mikono haina budi kuboreshwa sanjari na upatikanaji wa maji safi na salama.

 Imetayarishwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Simu: +255 656 331974.

Comments