Featured Post

MIAKA 28 YA KIFO CHA FRANÇOIS LUAMBO MAKIADI


Na Daniel Mbega
MIAKA 28 iliyopita, siku na tarehe kama ya leo (yaani Alhamisi, Oktoba 12, 1989) majira ya saa 1 asubuhi ndipo niliposikia taarifa kupitia BBC kwamba mwanamuziki nguli wa rhumba barani Afrika, Franco, alikuwa amefariki dunia.
Franco alifariki wakati akitibiwa katika hospitali moja jijini Brussels, Ubelgiji, tena alifariki mbele ya dada yake Marie Louise, mkewe Annie baadhi ya wanawe na baadhi ya wanamuziki wa bendi yake.

Zile fununu zilizokuwa zimeenea tangu mwaka 1987 kwamba nguli huyo alikuwa anaumwa sasa zikachukua sura mpya baada ya watu kuanza kuvumisha kwamba huenda maradhi ya Ukimwi ndiyo yaliyokuwa yamekatisha uhai wake.
Hii ilitokana na sababu mbili: kwanza, tangu mwaka 1987 zilipovuma habari hizo kwamba jamaa anaumwa baadaye akaanza kutoonekana mara kwa mara jukwaani. Lakini pili ni baada ya kutoa albam yake – ya mwisho akiwa hai – ya Attention na SIDA (Jihadhari na Ukimwi) mwaka 1987 ambayo kwa hakika hata taasisi za afya za kimataifa, hususan zilizo katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, zinastahili kumuenzi hata leo.
Siyo ajabu kutokea kwa madai hayo, kwa sababu siri ya mgonjwa anaijua mgonjwa mwenyewe na daktari, labda wawili hao waamue kuitoa hadharani. Lakini ni jambo la kawaida hata sasa kwa binadamu kujifanya madaktari – mabingwa wa kupima homa kwa viganja – ambapo wakimuona mtu kakonda kidogo utawasikia wakisema “Yule, aah tayari ana ngwengwe!”
Franco mwenyewe katika kibao cha Attention na SIDA anaimba hivi: “Moto azua malade balobi Sida, moto azua fevre balobi Sida, moto akonda balobi Sida, moto akufa balobi akufi na Sida…” (Mtu akiugua wanasema anaumwa Ukimwi, Mtu akiwa na homa wanasema Ukimwi, mtu akikonda tu wanasema ana Ukimwi, Mtu akifa wanasema amekufa kwa Ukimwi). Upo hapo mjomba!?
Kwa vyovyote vile, dunia ilikuwa imempoteza mwanamuziki ambaye alileta mabadiliko makubwa ya muziki wa Afrika ukakubalika ulimwenguni kote.
Watanzania, hasa wale vijana wa zamani, watamkumbuka kutokana na onyesho kubwa alilolifanya pale kwenye Uwanja wa Taifa (Shamba la Bibi) jijini Dar es Salaam mwaka 1973.
Alipozaliwa Julai 6, 1938 katika Kijiji cha Sona Bata, katika Jimbo la Bas Congo magharibi mwa Congo, si baba yake Joseph Emogo wala mama yake waliojua kama mtoto huyo aliyezaliwa njiti angeweza kuja kuwa mtu mashuhuri sana duniani.
Baba yake alikuwa mfanyakazi wa Shirika la Reli enzi hizo za ukoloni wa Mbelgiji wakati mama yake alikuwa akioka mikate na kuiuza sokoni. Mama yake alimpa jina la Makiadi, lakini alipobatizwa kanisani akapewa jina la Francis (ambalo ndilo Franco).
Wakati akiwa mdogo, wazazi wake wakahamia jijini Kinshasa.
Akiwa na umri wa miaka saba tu, Franco alitengeneza gitaa la kienyeji ambalo alilitumia kupiga na kuwavutia wateja pembeni mwa mama yake wakati akiuza mikate na maandazi.
Kipaji chake kiligunduliwa na mpiga gita mashuhuri wa enzi hizo, Paul Ebengo Dewayon, ambaye alijitolea kumfunza Franco jinsi ya kupiga vyema ala hiyo ambayo baadaye ikamfanya aitwe Sorcerer of Guitar (yaani Mchawi wa Gitaa).
Mwaka 1950, akiwa ndiyo kwanza ametimiza miaka 12, Franco alianza kutengeneza jina wakati akiwa na bendi ya Watam iliyokuwa ikiongozwa na Paul Dewayon. Uwezo wake wa kulikung’uta gitaa ulikonga nyoyo za mashabiki wengi ambao walistaajabia umahiri wake wakati umri ukiwa unamsuta.
Josky Kiambukuta, Madilu Bailu 'System' na Pepe Ndombe Opetum.

Miaka mitatu baadaye Franco alirekodi wimbo wake wa kwanza uliokwenda kwa jina la Bolingo na Ngai na Beatrice (Mpenzi wangu Beatrice). Baada ya kukubalika kuwa mmoja wa wana bendi ya Loningisa Studio, kiongozi wa bendi hiyo Henri Bowane alitoa nadhiri kwamba angeishi na Franco katika maisha yake yote yaliyosalia.
Chini ya Henri Bowane, Franco akawa mpiga gita la solo ambapo alikuwa akipiga staili ya Sebene na akaanza kutunga na kuimba yeye mwenyewe kwa staili za rumba, za Kiafrika na hata za Kilatini.
Mnamo Juni 1956 pamoja na kwamba alikuwa akipewa kazi nyingi katika studio, Franco akaamua kuunda bendi akiwa na Jean Serge Essous na De La Lune ambao pia walikuwa wakiimba pale Loningisa Studio. Bendi hii iliyokuwa ikifadhiliwa na mfanyabiashara Omar Kashama wakaipa jina la OK Jazz ambapo ilikuwa ikipigia katika Baa ya OK iliyokuwa ikimilikiwa na mfanyabiashara huyo.
Hapa ndipo kwenye mkanganyiko kuhusu neno OK. Kiasili lilikuwa ni kifupisho cha Omar Kashama, mfadhili wa bendi, lakini baadaye ikajipambanua na herufi hizo zikimaanisha Orchestra Kinois.
Essous alikuwa na kipaji cha upulizaji wa ala kuanzia clarinet hadi saxophone. Wanamuziki wengine waanzilishi walikuwa mpiga bass Augustin Moniania Roitelet, mpiga drums La Monta LiBerlin na Saturnin Pandy, mpiga gitaa Nicolas Bosuma Bakili Dessoin na mwimbaji Philippe Lando Rossignol pamoja na Vicky Longomba.
Bendi hiyo, ikiwa imesheheni vijana wenye vipaji na usongo wa kufanya vizuri kwenye muziki, ghafla ikaanza kuziteka hisia za mashabiki wa muziki nchini Congo. Ilikuwa wazi kwamba hawa jamaa hawakuwa wamedhamiria kupiga muziki wa kujiburudisha, bali kupata mafanikio zaidi wakipiga rhumba lenye kasi siyo kama lile la Africa Jazz ya Joseph Kabaselle ‘Le Grand Kalle’. Kila siku walipiga muziki kwenye studio iliyokuwa ikimilikiwa na Mgiriki mmoja na mara chache wakawa wanatumbuiza kwenye sherehe kama harusi.
Albam ya kwanza ya bendi hiyo ilikuwa inaitwa On Entre OK on sort KO (Ukiingia sawa, ukitoka unapigwa KO) wimbo ambao ulitungwa na Franco. Baadaye hii ndiyo ikawa kauli mbiu ya bendi. Mwaka  1957, mwimbaji kiongozi Rossignol aliondoka kwa sababu tu ya husuda katika masuala hayo ya sanaa lakini bendi haikupoteza mwelekeo. Nafasi yake ikajazwa na mwimbaji Edo Nganga.

Baadaye mwaka huo, mpiga sax maarufu kutoka Zimbabwe Isaac Musekiwa alijiunga na bendi hiyo. Baadaye akaja kuwa mmoja wa marafiki wa karibu wa Franco. Wakati huo, uongozi wa bendi ulikuwa chini ya Vicky Longomba, Essous na Franco. Mwaka 1958  Franco alifungwa kwa kosa la  ajali ya barabarani.
Mapema katika miaka ya 1960 wakati Vicky na Essous walipoondoka na kujiunga na Africa Jazz, Franco ndiye akawa kiongozi wa OK Jazz moja kwa moja. Africa Jazz wakati huo ndiyo ilikuwa bendi maarufu zaidi Congo ikiwa na wanamuziki wenye vipaji kama Tabu Ley na mpiga gitaa mashuhuri Docteur Nico Kasanda.
Kufuatia kuondoka kwa Vicky na Essous pamoja na wanamuziki wengine kadhaa, Franco akawachukua waimbaji Mulamba Joseph maarufu kama Mujos na Kwamy Munsi pamoja na mpiga gitaa Simaro Masiya Lutumba. Mpiga sax Verkys Kiamuangana Mateta ndiye aliyejaza nafasi ya Essous.
Essous, pamoja na wanamuziki wengine kutoka Congo Brazaville kama De La Lune , Celestine Kouka na Edo Nganga, baadaye wakaanzisha bendi iliyokuja kuwa maarufu enzi hizo, Les Bantous de la Capitale, iliyokuwa na maskani yake Brazzaville. Les Bantous baadaye ikawa taasisi ya taifa nchini Congo-Brazaville. OK Jazz na Les Bantous mara kwa mara walishirikiana na kubadilishana wanamuziki. Miongoni mwa wanamuziki walioimbia bendi zote tangu miaka ya 1980 alikuwa Papa Noel. Wanamuziki wengine walioimbia Les Bantous ni pamoja na Tchico Tchicaya na Pamelo Mounka. Bendi hizo mbili pia zilishirikiana katika albam ya Pont Sur le Congo.
O.K. Jazz wakiwa Brussels, Ubelgiji mwaka 1961.

Mwaka 1962 Franco alifanya ziara yake ya kwanza kabisa nje ya Congo wakati alipozuru Nigeria huku akitoa albam ya Cherie Zozo. Baadaye mwaka huo, Vicky Longomba akarejea pamoja na mwimbaji Lola Checain.
Purukushani za kisiasa katika nchi yake ya Kongo Franco alilazimika kuhamia Ubelgiji kwa ajili ya kurekodi nyimbo zake.
Baada ya nchi kutulia ikiwa chini ya uongozi wa rais Mobutu Seseseko Kuku Ndengebu Wazabanga ambaye alibadilisha jina la Kongo kuwa Zaire, Franco alirudi nchini mwake na akafanya tamasha kambambe la Festival OK Jazz for African Arts lililofanyika Kinshasa mwaka 1966.
OK Jazz iliisaidia sana Serikali ya Mobutu katika mambo ya kisiasa kupitia nyimbo zake zilizokuwa na mafunzo mengi. Franco hakuona soni katika kusifia mazuri wala kuonya mabaya pamoja na kwamba aliwekwa lupango mara nyingi alipokiuka taratibu za nchi. Kwa ujumla alikuwa kipenzi cha Mobutu na maswahiba wakubwa mno.
Ndiyo maana mwaka 1984, wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu nchini Zaire mwaka 1985, Franco akatoa kibao cha kampeni akimnadi Mobutu kisemacho: Candidat na Biso Mobutu (yaani Mobutu ndiye mgombea wetu). Kibao hiki ambacho kinaimbwa kwa muda wa dakika 19 na sekunde 31, kilivuma sana enzi hizo. Hapa nakuletea mashairi yake ambayo nimeyatafsiri mwenyewe kwa Kiswahili.
Katikati ya miaka ya 1960 OK Jazz sasa ilikuwa inaitwa Tout Puisant Orchestra Kinnie Jazz (TPOK Jazz) na ilikuwa na wanamuziki zaidi ya 20. Tout Puisant ikimaanisha ‘Wote Wana Uwezo’, sasa ilikuwa inajivunia wanamuziki wenye vipaji na ikaanza kushindana na Africa Jazz, jukumu ambalo lilikuwa rahisi kufuatia kuondoka kwa Tabu Ley na Docteur Nico na kuunda Africa Fiesta.
Mwishoni mwa miaka ya 1960 Franco alikabiliana na mapinduzi kwenye bendi yake wakati waimbaji Kwamy Munsi na Mujos walipowaongoza wanamuziki tisa kuihama bendi hiyo. Miezi michache baadaye ilikuwa zamu ya Verkys Kiamuangana kuondoka.
Verkys alikuwa mpuliza ala mahiri ambate upulizaji wake wa sax uliendana hasa na upigaji wa gita la solo wa Franco. Pia alikuwa mcheza shoo mzuri na aliongeza ladha kila walipofanya maonyesho. Alipoondoka TPOK Jazz, akaanzisha bendi yake aliyoiita Orchestra Veve, ambayo ilimsumbua sana Franco katika suala la mapato kwenye miaka ya 1970. Veve iliipua albam kadhaa zilizoshika chati ya juu zikiwemo Lukani, Se Kizengi, Nakomitunaka , Zonga Andowe na nyinginezo. Verkys pia alimiliki na kuongoza bendi nyingine mbili: Orch Kiam na Orch Lipua Lipua. Miongoni mwa wanamuziki waliocheza kwenye bendi za Berkys katika miaka ya 1970 ni Kabasele Yampanya maarufu kama Pepe Kalle na Nyboma Mwandido. Verkys aliachana kabisa na muziki katika miaka ya 1980 na kujikita zaidi kwenye biashara.
Haya yalikuwa baadhi ya matukio ya kushtua ambayo Franco alilazimika kukabiliana nayo ili kuivusha bendi yake kwenye mawimbi mazito. Kuziba pengo la Verkys, Franco alimchukua Rondot Kassongo wa Kassongo kutoka Orchestre Negro Success pamoja na mdogo wake mwenyewe Franco, Bavon Marie Marie.pia Franco akamchukua mpiga solo mahiri Mose Fan Fan. Kuwasili kwa Fan Fan kulirejesha uhai katika sekta ya nyuzi. Fan Fan akaleta mipigo mipya ya gitaa kwenye sebene, ambayo ilikuwa myepesi, ya kasi na inayochezeka. Mtindo huu ulifahamika zaidi kama Sebene ya ba Yankees Fan Fan na unasikika zaidi katika nyimbo nyingi zikiwemo Dje Melasi na Mongando.
Mashabiki wa muziki Tanzania wanamkumbuka alipipigia za Orchestra Makassy na Orchestra Matimila.

T.P.OK. Jazz ilikuwa ikifanya maonesho takriban nchi zote za Afrika, ukijumuisha sehemu mbalimbali za Chad na Sudan hata kuweza kutunisha ‘mfuko’ kuwa mnono.
Franco, akamnyakua mtunzi na mwimbaji mahiri DRC, Sam Mangwana kutoka Afrisa International ya Tabu Ley. Sam ambaye baba yake ni raia wa Zimbabwe wakati mama yake alikuwa raia wa Senegal, lakini yeye alizaliwa na kukulia katika jijini Kinshasa.
Sam anaongea kwa ufasaha lugha za Kiingereza, Kifaransa na Kireno. Pamoja na idadi ya Waafrika waliyokuwepo katika bendi hiyo, yaelezwa kwamba ujio wake uliipa nguvu za aina yake na kuwa tishio kwa bendi ya Afrisa alikotoka.
Miaka ya 1970 mwanzoni, Vicky Longomba, aliyekuwa akikaimu nafasi ya urais wa bendi, aliondoka.  Naye mpiga gitaa la solo, Mose Fan Fan aliondoka pia wakajiunga na mwanamuziki Youlou Mabiala kuunda bendi ya Orchestre Somo Somo.
Vicky Longomba alianzisha bendi yake ya Orchestra Lovy ambayo haikupata umaarufu sana. Alikuja Tanzania na kuweka maskani yake.
Franco alipata pigo kubwa mwaka 1970 kwa kufiwa na mdogo wake  Bavon Marie-Marie Tshongo ambaye kifo chake kilitokana na ajali ya gari alipokuwa akiendesha kwa hasira baada ya kukorofishana na kaka yake Franco wakigombea mwanamke ambaye naye alikufa katika ajali hiyo. Lilikuwa pigo kubwa kwa Franco kwa miezi kadhaa aliacha hata kupiga muziki.
Mara baada ya kurejea, akarekodi nyimbo nyingi akiomboleza kifo cha mdogo wake Bavon Marie Marie Tshongo.
Franco, akaanza kuijenga upya bendi, wakati huo rais wa nchi hiyo Joseph Mobutu, alifanya mageuzi ya kutaka majina ya miji na ya Wakongoman kuwa ya asili, hali iliyosababisha jina la  nchi hiyo kubadilika toka Congo-Kinshasa ikawa Zaire. Franco akachukuwa jina la L’Okanga La Ndju Pene Luambo Luanzo Makiadi. Hata rais na akawa Mobutu Sese Seko badala ya Joseph Mobutu.
Wakati huo, mwimbaji Fredy Mayaula Mayoni  alijiunga katika kikosi cha T.P.OK. Jazz  akiwa  na wapiga magita akina Mpundi Decca, Gege Mangaya, Michelino Mavatiku Visi na Dizzy Madjeku.
Watanzania wa miaka hiyo watamkumbuka vyema Mayaula Mayoni kwamba alikuwa ni winga nambari 7 wa klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam, na itakumbukwa kwamba katika pambano moja dhidi ya mahasimu wao, Simba, mwaka 1972, Mayaula ndiye aliyefunga mabao yote mawili katika matokeo ya 2-0 pale Uwanja wa Taifa.
Franco, akamteua Simaro Lutumba, kuwa mkuu wa bendi. Ni wakati huo huo Sam Mangwana alitoka na kibao cha Luka Mobali Moko.
Mwaka 1970 Franco alikuwa ni Rais wa wanamuziki wa Kongo na pia kuajiliwa na kampuni ya kugawa mirabaha ya wanamuziki.
Aliendelea kutajirika kwa kuweza hata kunua ardhi nchini Ufaransa, Ubelgiji na Kongo, na kuwa na nightclub nne kubwa kuliko zote Kinshasa kwa wakati huo na kufanya klabu yake kuwa ndio makao makuu yake. Hapo ilijengwa studio kubwa, ofisi na nyumba za kuishi kadhaa.
Katikati ya miaka ya 1970, Franco alikuwa mmoja wa matajiri wa Congo, akiwa amewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye maeneo yaliyopo katika nchi za Ubelgiji, Ufaransa na Zaire (DRC) alikonunua ardhi kote. Alikuwa akimiliki miradi mikubwa katika Jiji la Kinshasa ikiwemo klabu maarufu za usiku nne, mojawapo iliyokuwa kubwa kuliko zote ikiitwa Un-deux-trois ambako ndiko yalikuwa makao makuu yake. Hapo ilijengwa studio kubwa, ofisi na nyumba za kuishi. T.P.OK. Jazz ilikuwa ikipiga muziki kila mwisho wa wiki kwenye jumba lililojulikana kama Packed.
Franco hakuwa tu mwanamuziki mzuri bali pia aliendesha vizuri sana biashara zake za kurekodi na kampuni alizozianzisha wakati huo. Alikuwa na lebo kama (Surboum OK Jazz, Epanza Makita, Boma Bango and Éditions Populaires).
Katika miaka ya 70 muziki wa Congo ulishika kasi sana Afrika na Franco akiongoza jahazi kwa nyimbo kama Infidelité Mado, na akaendeleza kupiga mitindo mbalimbali kama Bolelo na muziki uliotokana na ngoma za asili toka Kongo zikichanganywa na mapigo kutoka Cuba.
Mwaka 1973 alitoa kibao kingine kilichotikisa Afrika, AZDA. Wimbo huu kwanza ulirekodiwa kama tangazo kwa ajili ya kampuni ya Volkswagen VW. Mahusiano yake na Mobutu yalikuwa na mawimbi mara wakipatana mara wakikosana kutokana na Franco kuwa anatumia nyimbo zake kukosoa serikali ya Mobutu.
Josky Kiambukuta Londa, aliyekuwa mtunzi na mwimbaji mahiri, alijiunga rasmi katika bendi mwaka 1974. Mwanamuziki Youlou Mabiala alirejea tena mwaka huo. Jazz.
Hata hivyo, Sam Mangwana aliondoka na kuwa mwanamuziki wa kujitemegea huko nchini Cote d’IvoireNdombe Opetum akachukuliwa  na T.P.OK. Jazz akitokea Afrisa International ili kuchukua nafasi ya Mangwana. Mwaka 1975, Franco alifyatua wimbo mahiri wa Bomba Bomba Mabe.
Mwaka 1976, mwimbaji Daniel Ya Ntesa maarufu Zitani Dalienst Ya Ntesa na mpiga gitaa Gerry Dialungana, walijiunga na T.P.OK. Jazz. Mayaula Mayoni kwa umahiri wake, mwaka huo akatoka na wimbo wa Cheri Bondowe uliofyatuliwa katika albam iliyojumuisha nyimbo za Alimatou na Bisalela.
Franco Luambo Makiadi, aliingiza mwimbaji wa kike Mpongo Love mwaka 1977. Mpongo, ambaye alikuwa mlemavu, akatokea kuwa mwimbaji maarufu katika bara la Afrika, akitumia uchangamfu wake akiwa jukwaani, sauti na utunzi mzuri na sura jamali. Mpigaji gitaa Papa Noel Nedule, alijiunga baadaye na mwaka huo huo bendi hiyo ikaiwakilisha Congo kwenye sherehe kubwa za Utamaduni wa Kiafrika huko Lagos, Nigeria.
Mwaka 1978, Franco alitoka na nyimbo mbili za Helene na Jacky, ambazo zilielezwa kuwa, zilikuwa ni za kudhalilisha ungozi wa serikali ya nchi yao na kwamba hakuzipitisha katika Kamati ya Kuchunguza Mashairi kama ilivyokuwa kawaida ya wakati ule. Matokeo yake Franco alipatikana na makosa na hatimaye alifungwa jela pamoja na wanamuziki wengine, akiwemo Simaro Lutumba.
Franco aliachiwa huru miezi miwili baadaye kutokana na maandamano mitaani kutaka afunguliwe. Mwaka huo huo, Mayaula Mayoni alifyatua kibao cha Nabali Misere (Nimeoa majanga) na baada ya kipindi akaondoka katika bendi hiyo kwenda kupiga muziki wa kujitegemea.
Kufikia kipindi hiki TPOK Jazz ilikuwa kubwa kiasi iliweza kumeguka kuwa mbili moja ikifanya kazi Afrika wakati nyingine ikiwa inafanya maonyesho Ulaya.
Mwaka 1979, Franco alihamisha eneo la kurekodia kutoka Kinshasa akapeleka Brussels, Ubelgiji akitafuta sehemu yenye zana bora za kurekodia. Mwaka huo huo alifanya ziara ya kutembelea nchi za Afrika ya Kati, huku Kiambukuta Josky akiachia kibao kilichojulikana kama Propretaire.
Katika kipindi cha miaka ya 1980-1989, ndicho kilicholeta mafanikio makubwa katika bendi na ya kiongozi Franco Luambo Makiadi. Alirekodi wastani wa albam nne katika kipindi hicho.
Katika kipindi hicho Franco alitunukiwa hadhi ya Rais wa Umoja wa Wanamuziki Zaire (UMUZA) akiwa pia anaitwa ‘Le Grand Maitre’ (Grand Master). Wakati huo OK Jazz ilikuwa imara kweli kweli kwani safu ya uimbaji ilikuwa na Josky, Madilu, Dalienst ya Ntesa, Ndombe Opetum na Youlou Mabiala. Upande wa magitaa walikuwepo Simaro Masiya Lutumba, Papa Noel, Dizzy Madjeku, Jerry Dialungana na Wuta Mayanda maarufu kama Wuta Mayi. Wapuliza ala walikuwa Matalanza, Isaac Musekiwa, Empopo Loway na Rondot Kassongo. Josky na Dalienst ndio waliokuwa nyota wakubwa wa bendi mbali ya Franco mwanzoni mwa miaka ya 1980. Josky alitoa nyimbo kama Soweto, Nostalgie, Mbanzi ya Kamundele, na Tokabola sentiment (wimbo huu unafahamika sana na mashabiki kama Kizunguzungu). Dalienst alitoa nyimbo kama Tantine, Mouzi na wimbo maarufu wa  Bina na Ngai na respect (cheza name kwa adabu).
Wakati Josky na Ntesa wapo, Madilu alikuwa hatii timu kabisa kwenye safu ya mbele, zaidi alikuwa muitikiaji. Lakini alipata shavu kuanzia mwaka 1983, ambao ulikuwa na mafanikio makubwa kwa Franco na Tabu Ley baada ya kurekodi karibu albam 10 jijini Paris na kufanya ziara kwa mara ya kwanza Marekani. Madilu alishiriki akiwa mwimbaji wa mbele kuanzia kwenye albam ya Chez Fabrice hasa katika wimbo wa Non, ambao ni wa taratibu na wa mazungumzo ambapo Franco na Madilu wanajibizana. Baada ya hapo ndipo akapata chati kwenye nyimbo nyingine zilizofuata na hasa Mamou au Tu Vois?
Mwaka 1982, Sam Mangwana alirejea katika bendi na kwa kipindi kifupi, akashirikiana na Franco, ambapo waliachia kibao kilichopewa jina la Cooperation. Franco pia alishirikiana na aliyekuwa hasimu wake kimuziki Tabu Ley mwaka 1983, wakafyatua albamu nyingi ikiwemo ile ya Ngungi.
Mwaka 1983 Franco na bendi yake ya T.P. OK Jazz walizuru Marekani kwa mara ya kwanza. Mwaka huo wimbo wa Non ulifyatuliwa.
Katikati ya miaka ya 1980, bendi iliendelea kuchanganya mauzo mazuri ya rekodi zao, zikiwemo za Makambo Ezali Borreaux, 12,600 Letters to Franco, Pesa Position, Mario na Boma Ngai na Boma Yo. Katika kipindi hicho, Madilu System akawa mwimbaji mwongozaji katika kikosi hicho.
Haya hapa ni mashairi ya kibao cha 12,600 Letters (kwa Kifaransa inatamkwa Douze Mille Six Cents Lettresyaani Barua Elfu Kumi na Mbili na Mia Sita)! Umeimbwa Kifaransa kwa kuchanganya na Kilingala, lakini nimeyatafsiri mashairi hayo.
Mwaka 1986, watunzi na waimbaji Josky Kiambukuta na Zitani Dalienst Ya Ntesa, walijiona kana kwamba hawapewi muda wa kutosha wa kuonyesha vipaji vyao, hivyo wakaondoka kwenda kuunda bendi yao.
Naye Simaro Lutumba, akatoka na kibao ‘matata’ akiwa nje ya bendi ya T.P. OK. Jazz kikiitwa Maya. Kama ilivyo kawaida ya wanamuziki kuhama hama, mwimbaji Malage de Lugendo, alichukuliwa kuongeza nguvu, pia Kiesse Diambu ya Ntessa aliyetoka bendi ya Afrisa na mwimbaji mwanamke Joliet Detta wakajiunga na T.P.OK. Jazz.
Mwanzoni wa mwaka 1987, Franco aliachia wimbo mrefu wa dakika 15, akaupa jina la Attention Na Sida (Jihadhari na Ukimwi). Pia mwaka huo huo wa 1987, T.P.OK. Jazz ilialikwa kwenye Michezo ya Nne ya Afrika huko Nairobi, Kenya. Ni mwaka huo huo 1987, alitoa albamu ya Les On Dit, ikiwa na nyimbo nane.
Baniel Bambo na Nana Akumu

Franco alitangaza kujiunga katika bendi yake kwa waimbaji wawili wa kike, Nana Akumu na Baniel Bambo. Waimbaji hawa wanasikika vyema wakijibizana na Franco pamoja na kiitikio cha Madilu System katika wimbo maarufu wa Flora, une femme defficile (Flora, mwanamke mgumu).
Lakini mwaka 1988, Kiambukuta Josky na Dalienst wakarejea tena katika bendi.
Kwa sababu zisizofahamika, mwaka 1975 Franco alisilimu na kuitwa Abubakkar Sidikki, lakini jina hilo halikuwahi kufahamika na wengi wala mwenyewe hakuwahi kushiriki katika imani ya Kiislamu. Mwaka 1988 akaamua kurejea katika dini yake ya Ukristo katika dhehebu la Roman Katoliki.
Mwaka 1989, haukuwa mzuri kwa bendi hiyo kutokana na hali ya afya ya kiongozi wao Franco, kuanza kuzorota. Alihamishiwa moja kwa moja katika mji wa Brussels, Ubelgiji kwa matibabu zaidi. Hakuweza kupiga muziki kwa kipindi kirefu, hata kama alijaribu, alimudu kwa dakika 20 tu.
Kutokana na hali hiyo, bendi ikaanza kupoteza mwelekeo, ambapo wanamuziki waliorejea katika bendi hiyo akina Malage de Lugendo, Dizzy na Decca walirejea Kinshasa kuangalia njia nyingine ya kuendesha maisha yao. Malage de Lugendo akajiunga na Zaiko Langa Langa.
Mwaka huo huo, Sam Mangwana alishirikiana na Franco kutoa albam yenye jina la Forever. Albam hiyo ilikuwa imepambwa na picha inayomuonesha Franco akiwa amepungua mwili kwa kiasi kikubwa, zikiwa ni ishara za ugonjwa uliokuwa ukimkabili. Na hiyo ilikuwa ndiyo albam yake ya mwisho.
Franco Lwambo Makiadi, alifariki dunia akiwa katika hospitali moja nchini Ubelgiji, Oktoba 12, 1989 akiwa na miaka 51.
Mwili wake ukarudishwa nchini Congo, huku jeneza lake likiwa limefunikwa bendera ya taifa lake la Congo (Zaire wakati ule). Mwili wake ulipitishwa katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Kinshasa, ukiagwa na maelfu ya wakazi wa jiji hilo na vitongoji vyake, huku ulinzi mkali wa Polisi ukiimarishwa na baadaye serikali ikatangaza siku nne za maombolezo ya kitaifa. Wakati wa siku hizo za maombolezo radio ya taifa hilo ilikuwa ikipiga nyimbo za Franco hadi Oktoba 17, 1989 alipozikwa kwa heshima zote za kitaifa.
Katika uhai wake, alidai kwamba OK Jazz ilitoa zaidi ya albam 150 katika kipindi cha miaka 30.
MWENYEZI MUNGU AMREHEMU. AMENI!


IMETAYARISHWA NA www.maendeleovijijini.blogspot.com. Ukirejea ni lazima eleze chanzo ambacho ni www.maendeleovijijini.blogspot.com.

Comments