- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Unknown
on
- Get link
- X
- Other Apps
Yanga
Bwanga (kushoto). Picha kwa hisani ya zenjdar.co.uk
Na Daniel Mbega
NAMKUMBUKA
mtangazaji nguli wa kipindi cha michezo cha Radio Tanzania Dar es Salaam (RTC wakati huo - sasa TBC Taifa), marehemu Abdul Masoud, katika siku ambayo
Yanga ilimsajili kiungo mshambuliaji machachari Yanga Fadhil Bwanga kutoka kwa
'Wagosi wa Kaya' Coastal Union mwaka 1976 kama sikosei. Nilikuwa mdogo sana
wakati huo, lakini ndiyo kwanza nilikuwa ninapenda michezo hasa tukiwa
tunajikusanya nyumbani kwa Balozi wa Nyumba Kumi, jirani yetu tu pua-na-mdomo, aliyekuwa na redio ya
'Mkulima' kila siku saa mbili kasorobo.
Siikumbuki vizuri siku hiyo, lakini ninachokikumbuka ni utangulizi wa
habari kuu ya siku hiyo ambapo Abdul Masoud alisema: "Haya tena, mambo
kangaja huenda yakaja... Leo katika Uwanja wa Mkwakwani Coastal Union yaifunga
Yanga... Lakini Yanga Fadhil Bwanga ajiunga na Yanga!"
Naam, yalikuwa ni maneno mazito hasa ikizingatiwa ushabiki wa mpira wakati
huo ulivyokuwa juu tofauti na sasa ambapo utandawazi umewafanya wengi wanashabikie
timu za Ulaya wanazoziona kwenye luninga.
Vijana waliokuwa katika hirimu ya kaka zangu walikuwa na ubishani mkubwa na huo ndio uliotufanya hata sisi watoto kupenda michezo, hasa mpira. Wakati huo ndiyo burudani pekee ambayo tuliweza kuisikiliza kwenye redio ukiacha vipindi vya muziki wa Chaguo la Msikilizaji na vinginevyo.
Haikushangaza hata mara moja kukuta watoto tukigeuza maboga kuwa mpira, na wakati mwingine 'msambi' ambao ulitengenezwa na matambara. Ndiyo mipira iliyokuwa ikitumiwa na kaka zetu, magozi tuliyasikia tu redio.
Siku hiyo Yanga ilikuwa imefungwa na Coastal Union katika mchezo mkali wa
kirafiki kwenye Uwanja wa Mkwakwani. Mwaka huo Coastal Union haikufika fainali
ya Ligi ya Taifa (sasa Ligi Kuu) baada ya kutolewa kwenye hatua ya Kanda.
Lakini kikosi chake kilikuwa imara mno. Ikumbukwe pia kwamba, Abdul Masoud
wakati huo ndiye alikuwa Katibu Mwenezi wa Yanga baada ya kuchaguliwa katika
uchaguzi uliosimamiwa na serikali kufuatia mgogoro mkubwa uliokuwa umeikumba
klabu hiyo na kuwafukuza wachezaji 20, ambao baadaye ndio waliounda Pan
Africans, akiwemo Rais wa sasa wa TFF, Leodgar Tenga,Gibson
Sembuli, Sunday Manara, Boi Idd 'Wickens', Ally Yusuf, na wengineo.
Pamoja na kuwa
na wachezaji chipukizi, lakini Yanga ilishindwa kufua dafu mbele ya Wagosi wa
Kaya.
Baada ya
mchezo huo Yanga wakamtorosha Yanga Fadhil Bwanga na kwenda 'kumhifadhi' kwa
ndugu zake Pangani ili Coastal wasiushtukie mchezo huo. Coastal walipopata
fununu waliweka mtego barabarani na kukagua kila gari iliyopita. Ilivumishwa
kwamba Yanga Bwanga alisafirishwa na lori la mkaa, lakini (watanisahihisha
wakongwe) inaelezwa kwamba baada ya kupumzika siku kadhaa Pangani, alipitia
Bagamoyo na kuingia Dar. Hiyo ndiyo hadithi yake, naamini wakongwe wanaweza
kunisahihisha katika hili.
Hata hivyo, hapa nazungumzia tukio lililofanywa na Yanga Bwanga katika
mechi baina ya Yanga na Simba mwaka 1977 ambapo alivunja pambano hilo.
Siku hiyo ya Jumapili Novemba 27, 1977 kwa mara nyingine Simba iliifunga
tena Yanga kwa mabao 2-1 katika pambano ambalo lilivunjika dakika 12 kabla ya
wakati wake kutokana na mchezaji Yanga Bwanga wa Yanga kukataa kutoka nje baada
ya kuamuliwa na mwamuzi kufanya hivyo.
Bwanga, kwa makusudi kabisa, alimpiga daluga Nicodemus Njohole wa Simba
kifuani ikiwa ni kulipiza kisasi kwa mchezaji huyo ambaye alikuwa amemtegea
wakati wakiwania mpira. Bwanga alikuwa ameonywa mara ya kwanza kwa kadi ya
njano katika dakika ya 16 alipomfanyia rafu Nicodemus tena na hivyo baada ya
rafu mbaya kwa mara ya pili ikalazimika atolewe nje.
Lakini mchezaji huyo hakushtuka kwa amri hiyo badala yake akaendelea
kurukaruka uwanjani akifanya mazoezi mepesi. Mwamuzi Stephen Lutayangirwa baada
ya kusubiri kwa dakika 10 alipuliza kipenga cha kumaliza mchezo.
Mchezo wenyewe ulikuwa wa kwanza wa kuwania Kombe la Jitegemee, ambapo
uliharibiwa kabisa kutokana na uchezaji mbaya wa wachezaji wa timu zote ambao
walikuwa wakitembezeana madaruga na kuonyeshana ubabe wa dhahiri.
Kulikuwa na vipindi vichache sana vyenye msisimko na mara nyingi kulikuwa
na rafu na mchezo wa hasira. Mwamuzi naye alistahili lawama kwa kufanya mchezo
kuharibika zaidi. Hakuwa mkali inavyopasa kila wachezaji walipokuwa wakifanya
makosa uwanjani.
Ukali pekee aliouonyesha wenye busara ni alipomtoa nje ya uwanja Daudi
Salum 'Bruce Lee' wa Simba na Ayubu Shaaban wa Yanga walipokingiana ngumi.
Kabla ya hapo alikuwa amewaonyesha kadi za njano Omar Mahadh na Daudi Salum wa
Simba, na Yanga Bwanga wa Yanga.
Mameneja wa timu hizo Mohammed Viran wa yanga na Abdulrahman Khamis
Muchacho wa Simba ndio walioonyesha urafiki baada ya kuvunjika kwa mchezo huo
kwani walitoka nje wakiwa wameshikana mikono huku wapenzi wa timu hizo mbili
wakilaumiana kwa mchezo mbovu wa timu zao.
Simba iliwazidi kimchezo wapinzani wao katika dakika za mwanzo hadi
walipojipatia bao lao la kwanza katika dakika ya 18. Mpira uliotoka kwa
Abdallah Kibadeni aliyeupeleka mbele ulimkuta Jumanne Hassan Masimenti ambaye
naye alitoa pasi ya kichwa kwa George Kulagwa ambaye aliachia mkwaju mkali
ambao kipa wa Yanga Isega Isindani alishindwa kuukumbatia. Rahim Lumelezi
aliyekuwa karibu akauwahi na kuutumbukiza wavuni.
Kuanzia hapo hadi mapumziko mchezo ulipooza sana ingawa Yanga ilikuwa
ikicheza kwa ufundi zaidi ambao ungewaletea goli la kusawazisha kunako dakika
ya 22 kwa kiki ya nguvu iliyopigwa na Karabi Mrisho lakini ikapaa juu ya goli.
Yanga iliwaingiza
Ramadhan Mwinda na Danny Mwalusamba badala ya Karabi Mrisho na Burhani Hemed
kipindi cha pili kilipoanza, lakini mabadiliko hayo hayakuleta tofauti sana.
Katika mojawapo ya
hatari langoni mwa Simba, Filbert Rubibira aliunawa mpira na mwamuzi akaamuru
penalty ipigwe. Wachezaji wa Yanga walitegeana kupiga mpaka Charles Mwanga
alipojitolea lakini alipopiga mpira ukaota mbawa kwa kupaa juu ya goli.
Simba ilijiongezea bao la pili dakika ya 54. Bao hilo lilianzia na mpira wa
kona iliyochongwa na Abdallah Kibadeni na kusababisha kizaazaa langoni, Nico
Njohole akatokea na kufunga kirahisi.
Bao pekee la Yanga lilifungwa na Ezekiel Grayson dakika ya 64. Mohammed
Kajole ndiye aliyesababisha bao hilo baada ya kuuachia mpira ambao angeweza
kuokoa akidhani kipa wake Omar Mahadh atauwahi. Ezekiel akatokea na bila taabu
akafumua mkwaju uliotinga wavuni.
Yanga ikaanza kucheza vizuri kuanzia hapo hadi mchezo ulipovunjika, lakini
juhudi zao hazikuzaa matunda.
Yanga: Isega Isindani, Charles
Mwanga, Fadhil/Boniface Makomole, Selemani Jongo, Hashim Kambi, Sam Kampambe,
Burhani Hemed/Danny Mwalusamba, Ezekiel Grayson, Karabi Mrisho/Ramadhan Mwinda,
Yanga Bwanga, Ayoub Shaaban.
Simba: Omar Mahadh, Daudi
Salum, Mohammed Kajole, Aloo Mwitu, Filbert Rubibira, Athumani Juma, Rahim
Lumelezi, Nico Njohole, Jumanne Hassan, Kibadeni, George Kulagwa.
NB: Makala haya ni
kutoka kwenye miswada ya vitabu vya 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA YANGA' na ‘UBINGWA
WA SOKA TANZANIA’ vya mwandishi Daniel Mbega, ambavyo viko katika hatua za
mwisho kuchapishwa. Ukirejea ni lazima eleze chanzo ambacho ni www.maendeleovijijini.blogspot.com.
Comments
Post a Comment