Featured Post

MAGONJWA YA SUNGURA: MATATIZO YA MAGEGO (MOLARS AND PREMOLARS)


Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog

SUNGURA wanasumbuliwa sana na magego ambayo huendelea kukua tu hata kama watakuwa wakubwa na hayakomi kama ilivyo kwa binadamu na wanyama wengine.

Kwa sungura, magego yote (molars and premolar) yameshikamana pamoja na yanaitwa meno ya shavu (cheek teeth).
Meno haya yanaweza kurefuka bila utaratibu maalum, au kama mpangilio wa meno hauko vizuri (malocclusion).
Hili ni tatizo linalowapata sana sungura wa kufugwa hasa wale wa mapambo, na linaweza kutokea wakati wa kuzaliwa kutokana na ugonjwa au kwa sababu nyingine.
Hata hivyo, kurefuka kwa meno ya shavu (magego) hutokea zaidi kwa sungura wenye umri wa kati au wakubwa, wakati sungura wadogo wanaweza kupatwa na na matatizo hayo.
Sungura wa aina ya Dwarf na Lop wako hatarini zaidi kupatwa na tatizo la mpangilio mbovu wa magego.

Dalili na Aina

 * Kushindwa kutafuna chakula
* Kukosa hamu ya kula na kupungua uzito
* Kupendelea kunywa maji kwenye bakuli kuliko kufyonza kwenye chupa
* Kunywa maji mengi kupita kiasi
* Kutokwa na majimaji puani
* Kusaga meno
* Kutokwa na machozi mara kwa mara
* Maumivu

Chanzo

Kurefuka kwa meno ni jambo la kawaida kwa sungura wazee hasa wale wa mapambo – sizungumzii wanaofugwa kwa ajili ya nyama.
Mara nyingi sungura hao hujikuta meno yao yakirefuka sana kuliko wanapokuwa katika umri mdogo.
Hata hivyo, tatizo la kurefuka kwa magego kusiko kwa kawaida kwa sungura ‘wazee’ hutokana na ukosefu wa vyakula vigumu na visivyo na nyuzi nyuzi.
Uwepo wa vyakula vigumu na vyenye nyuzi nyuzi huwafanya sungura watafune na wasage meno yao, hivyo kutokuwa rahisi kwa magego kuendelea kurefuka bila mpangilio.
Kama tatizo hili litatokea kwa sungura wadogo wakati wa kuzaliwa – hasa wa jamii ya Dwarf (Mbilikimo) au Lop, basi hilo ni tatizo la uzazi na haliwezi kuzuilika.

Uchunguzi

Daktari wa mifugo anaweza kuchunguza ili kubaini ukuaji huo wa magego usio wa kawaida.
Uchunguzi wa kikemia wa bacteria kutokana na usaha kwenye meno unashauriwa ufanyike.
Uchunguzi mwingine unaweza kuhusisha vipimo vya CT scan, X-Ray kwenye kichwa na uchunguzi wa mkojo.

Tiba

Tiba inategemea na ukubwa wa tatizo. Upasuaji unaofahamika kitaalam kama (coronal reduction), ambapo magego yanakatwa, ni njia mojawapo muhimu. Dawa za maumivu zinaweza kutolewa kwa sungura.

Maisha na Matunzo

Sungura ni lazima aangaliwe kwa karibu na hakikisha meno yake yanakatwa kila baada ya wiki nne had inane, kama inavyopaswa.
Ni muhimu kuangalia meno ya sungura wako kila wakati kwa kumtumia mtaalamu wa mifugo, na sungura wako anaweza kuwa anahitaji kupunguzwa meno yake kwa kumtumia mtaalamu huyo ili kuyafanya yawe katika urefu unaotakiwa.
Kama sungura wako ataonekana hapendi kula, ana matatizo wakati wa kula, ana uvimbe usoni ambao unaweza kuwa dalili ya matatizo ya meno, au ataonekana anadondosha chakula kingi wakati anakula, mpeleke au mwite ofisa mifugo haraka amwangalie.

Kinga

Ili kuzuia ugonjwa wa meno – mpangilio mbovu na kurefuka kwa magego kusiko kwa kawaida – punguza kiwango cha chakula cha punje (pellets), matunda laini au mboga za majani kwenye mlo wa sungura.
Badala yake, wapatie vyakula vigumu vyenye nyuzi nyuzi kama nyasi kavu (hay) au nyasi mbichi ili kuhakikisha wanatafuna na kusaga meno yao, jambo ambalo huwafanya wawe na magego yenye urefu unaostahili.
Hii pia ni muhimu sana kwa sungura wote, siyo wale wa mapambo tu.
Kwa bahati mbaya, ni vigumu kuwakinga kama tayari wameonyesha dalili za tatizo la magego, ambalo linahitaji tiba.

Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Tupigie: +255 656 331974


Comments