Featured Post

MAGONJWA YA SUNGURA: HOMA YA MAPAFU (PNEUMONIA)


Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog

SUNGURA wanaweza kupata magonjwa haraka kupitia mfumo wa upumuaji kutokana na Homa ya Mapafu (pneumonia), ingawa wanaweza wasipate mafua.

Maambukizi na mizio kwenye njia ya juu ya upumuaji ni matatizo ya kawaida kwa sungura, na daima utayagundua kutokana na kukoroma, mapigo ya moyo kwenda kasi na wakati mwingine kutokwa na majimaji kwenye macho na pua.
Kama sungura wako wanasumbuliwa na matatizo ya pumzi, wanapumua haraka au kutoa sauti au wanatoa majimaji hiyo inaashiria ni tatizo, wasiliana na ofisa ugani haraka.
Kwa kifupi, haya ndiyo matatizo matano sugu ambayo yanawasumbua sungura, lakini ni matatizo ambayo hayagunduliki haraka wakati yanapoanza.
Wafugaji wote wa sungura wanapaswa kujifunza kwa makini kuhusu maradhi ya msingi na matatizo yanayowakabili sungura, kujua dalili zake na namna ya kukabiliana nayo.
Kwa kawaida, Homa ya Mapafu hutokea wakati sungura wanapokuwa na uvimbe kwenye mapafu (severe inflammation) ambao husababisha mfumo mzima wa upumuaji kushindwa kufanya kazi barabara.
Uvimbe huu unaweza kuwa umetokana na maambukizi ya bacteria, kuvu, virusi au vijidudu vingine, au kwa sababu sungura amevuta kupitia pumzi kitu kingine na kimeingia kwenye mapafu.
Changamoto za kimazingira, kama kuwepo na moshi mwingi au harufu ya kemikali, uwezo mdogo wa kumeza, na ugonjwa wa meno unaweza kusababisha homa ya mapafu.

Dalili

Baadhi ya dalilia katika aina zote nne za homa ya mapafu ni pamoja na:
* Kukosa hamu ya kula (Anorexia)
* Kupungua uzito
* Uchovu na kukosa nguvu (Lethargy)
* Homa kali
* Kupiga chafya
* Kutokwa mate mengi
* Kutopenda kufanya mazoezi
* Kutokwa na majimaji puani
* Kutokwa na majimaji machoni
* Kutokwa na usaha puani
* Kutopumua vizuri
* Kukohoa siyo sana kwa sungura.
Homa ya mapafu inayosababishwa na bacteria hutokea wakati bacteria hao wanapoingia katika njia ya chini ya upumuaji (lower respiratory tract), mara nyingi kutokana na kuvuta au kukabwa, lakini vijidudu hivyo vinaweza kuingia kwenye mwili kupitia katika mkondo wa damu.
Kwahiyo anaweza kupata madhara kwenye koromeo, kuvimba, damu kushindwa kupita, kufa kwa tishu, kutunga usaha, na hata mapafu kushindwa kufanya kazi.
Kama mnyama ana kinga dhaifu ya mwili, basi hata bacteria wale ambao mara nyingi huwa wako mdomoni, kooni na mapafuni wanaweza kuwa na madhara.
Kutokana na hayo yote, kutakuwa na oksijeni kidogo sana kwenye damu.
Maambukizi yanayosababishwa na kuvu (fungus) mara nyingi hutokea wakati sungura anapovuta viiniyoga (spores), vikaingia kwenye mapafu (na wakati mwingine mkondo wa damu).
Hii huchochea mfumo wa kinga wa sungura kutuma chembe nyeupe za damu kupambana na vijidudu vivamizi.
Lakini kwa bahati mbaya, chembe hizo hutakwa na kumeza na vijidudu, na kutoa kemikali ya cytokine ambayo inaharibu usambazaji wa oksijeni kwenye mapafu.
Maambukizi ya virusi hutokea kwa njia hiyo hiyo pia, isipokuwa tu ni virusi ndio wanaoingia kwenye mapafu na kuzalisha kemikali ya cytokine.
Hata hivyo, virusi pia wanafanya sungura wawe hatarini kupata maambukizi ya bacteria; kwa maana hiyo, homa ya mapafu inayosababishwa na bacteria inaweza kufanana na homa ya mapafu inayosababishwa na virusi.
Homa ya mapafu inayosababishwa na vijidudu (parasitic pneumonia), kwa upande mwingine, hutokea wakati vijidudu vinapoingia kwenye ngozi au vinapovutwa kwa pumzi, na kusababisha uharibifu wa vijitundu vya seli kwenye mapafu na kufanya sungura asipate hewa ya oksijeni.

Uchunguzi

 * Usikimbilie kuchunguza matatizo ya upumuaji na moyo
* Chunguza mkojo
* Chunguza damu kwa vipimo maalum ili kubaini vijidudu vya maambukizi (kama, bacteria, kuvu, virusi)
* Piga X-ray kiffuani kuangalia kama kuna usaha au uvimbe
* Chunguza kuhusu seli kutokana na majimaji yanayotoka puani na kooni.

Tiba

Kama unahisi sungura wako wana homa ya mapafu wapeleke kwa ofisa mifugo haraka, kwa sababu kutotibiwa mapema kwa tatizo hilo kunaweza kusababisha vifo.
Kama sungura anakosa hamu ya kula, ana homa kali, anapungua uzito, au ana uchovu na kukosa nguvu, lazima awekwe chini ya uangalizi.
Daktari wa mifugo anaweza kutoa tiba ya dawa za aina ya antimicrobial, antiviral, antifungal, au antibiotics, kutegemeana na vijidudu gani vilivyomo na dawa gani zinazofaa kupambana na maambukizi husika.
Kama kifua ama mapafu yamebana, inabidi kuingia oksijeni kwa kutumia nebulization kuzibua njia kwa sungura wako.

Maisha na Matunzo

Kama sungura atakuwa na matatizo hayo na umeanza tiba, hakikisha anapata muda mwingi wa kupumzika lakini wakati huo huo hakikisha sungura anakula na kupata dawa stahiki.
Mbali ya kumpa chakula chake cha punje (pellets), pia mpatie kiasi cha kutosha cha majani mabichi kama kabichi, spinachi na karoti kama nyongeza kwenye mlo wake. Vyakula hivi vinakuwa na majimaji mengi ambayo ndani yake yana oksijeni, hivyo kumsaidia kupata hewa ya oksijeni.
Kama sungura anagoma kula kabisa, basi mpatie uji wa mapande kwa kutumia bomba la sindano.
Daktari wako wa mifugo anaweza kukushauri vyema njia za kufuata kumlisha sungura wako, na chakula gani kinachofaa kwa mazingira maalum.
Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Tupigie: +255 656 331974


Comments