- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
“KILA raia wa
Norway, hata yule ambaye hajazaliwa, ana uhakika wa akiba ya Kroner takriban
600,000 wakati hapa Tanzania pekee, kila mmoja anadaiwa zaidi
ya Shs. 700,000 kutokana na Deni la Taifa,” ndivyo anavyosema Profesa Patrick
Lumumba, Mkuu wa Shule ya Sheria ya Kenya.
Profesa Lumumba anasema kwamba,
uchumi imara wa Norway unaotokana na usimamizi madhubuti wa mafuta na gesi,
ukichangiwa na idadi ndogo ya watu ambao asilimia kubwa ni wazalishaji,
umeifanya nchi hiyo kuwa mfano duniani katika ukuzaji wa uchumi.
Profesa Lumumba alisema uchumi wa
nchi nyingi zinazoendelea hasa barani Afrika ambazo zina rasilimali mbalimbali
unashindwa kukua kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo uongozi mbovu, rushwa,
uzembe pamoja na idadi kubwa ya watu.
Hali hiyo, alisema inazifanya nchi
hizo kuwa na mzigo mkubwa wa kuhudumia watu wake na kushindwa kutoa huduma bora
kama elimu, afya na nyinginezo, hivyo kulazimika kukopa ili kuziba pengo
lililopo.
“Norway ina watu milioni 5.2 tu,
idadi ambayo ni sawa na wakazi wote wa Dar es Salaam, lakini uchumi wake ni
mkubwa, wameweza kulinda rasilimali zao na kudhibiti kasi ya kuzaliana ili kuwa
na nguvu imara inayopata huduma zote muhimu.
“Kwa mujibu wa sharia inayosimamia Mfuko Maalum wa mapato ya rasilimali hizo (Government
Pension Fund-Global), serikali imeruhusiwa kuchukua asilimia 4 ya
fedha hizo ili kufanya shughuli nyingine za maendeleo, hususan uwekezaji,
lakini kutokana na kujimudu kiuchumi, ni mwaka jana tu ndipo ilipanga kuchukua
kiasi ili kuwekeza,” alisema Profesa Lumumba.
Kulingana na takwimu zilizopo, Tanzania
inaelemewa na mzigo wa deni la Shs. 35.01 trilioni huku
ikijikongoja kukuza uchumi wake, wakati nchi ndogo ya Norway ina akiba ya Dola
900 bilioni katika Mfuko huo Maalum, ambazo ni takriban Shs. trilioni
1,939.
Hali hiyo inawafanya raia 5,214,900
wa Norway, nchi inayotegemea uchumi mkubwa wa mafuta, kuwa na akiba ya wastani
wa Dola 173,077 (Shs. 373,028,000) kila mmoja, fedha ambazo zimeanza kuwekwa
kwenye mfuko huo kwa zaidi ya miaka mingi, lengo likiwa kuwekeza kwa vizazi
vijavyo utajiri huo unaotokana na mafuta.
Norway inaamini kwamba, ipo siku
mafuta yatakwisha, hivyo wanapaswa kuweka akiba ya fedha kwa vizazi vijavyo ili
navyo vije vinufaike kwamba nchi yao iliwahi kuwa na rasilimali za mafuta
badala ya kusoma kwenye vitabu kama historia bila kuona manufaa yoyote.
Kutokana na deni linaloikabili
Tanzania, wachambuzi wa masuala ya uchumi na wanasiasa wamekuwa wakisema
kwamba, kwa Watanzania milioni 45 waliopo sasa, maana yake kila mmoja
anadaiwa Shs. 778,000, huku utafiti na takwimu ukionyesha kiwango
cha umaskini vijijini kimepungua kwa asilimia 6.1 katika kipindi cha miaka
mitano iliyopita.
Dk. Joel Silas wa Idara ya Uchumi ya
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema kwamba, uwiano wa uchumi na idadi ya watu
ni muhimu kuzingatiwa, kwani ndio unaoweza kupima maendeleo ya mtu mmoja mmoja
na taifa kwa ujumla.
Mtaalamu huyo wa uchumi anasema,
baadhi ya nchi zimepiga hatua kiuchumi kutokana na idadi ya watu na rasilimali
zilizopo, na kusisitiza kwamba uzazi wa mpango ndiyo njia pekee inayoweza
kufanikisha jitihada za mataifa yanayoendelea kujikwamua kiuchumi.
“Huwezi kuzungumzia maendeleo bila
kutazama idadi ya watu, hata nyumbani, chakula kinapikwa kulingana na watu
waliopo, wakati mwingine katika hali ya umaskini, inalazimu watu waliopo, hata
kama watakuwa wengi, wagawane chakula hicho hata kikiwa kidogo – ndiyo hali
inayozikabili nchi zinazoendelea ambazo zinashindwa kukidhi mahitaji ya watu
wake na kulazimika kukopa,” anasema.
Ingawa Tanzania inajivunia
kugunduliwa kwa uchumi mpya wa gesi na mafuta, lakini hauwezi kusaidia ikiwa
kasi ya ongezeko la watu haitapungua, huku idadi kubwa wakiwa tegemezi.
Wakati Tanzania yenye ukubwa wa
kilometa za mraba 947,303 na idadi ya watu milioni 45, ni watu milioni 25.59 tu
wanaofanya kazi na kuzalisha, ikizidiwa kwa mbali na Norway ambayo kati ya watu
milioni 5.2, karibu watu milioni 3 (sawa na asilimia 69) wenye umri kati ya
miaka 15-74 wanafanya kazi.
Aidha, Pato la Taifa la Tanzania
(GDP) nalo liko chini (Dola 48.06 bilioni) huku kipato cha mwananchi mmoja
mmoja kikiwa Dola 768, wakati GDP ya Norway ni Dola 363.290 bilioni na kipato
cha mwananchi mmoja ni Dola 69,712 kwa mwaka.
Ongezeko la idadi ya watu duniani,
ambalo linachangiwa na mambo mengi, yakiwemo ukosefu elimu na huduma za uzazi
wa mpango, linatajwa kuwa janga linalokwamisha hata Malengo
Endelevu ya Dunia.
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia,
idadi ya watu duniani inaongezeka kwa watu 200,000 kila siku
huku asilimia kubwa ikiwa ni katika nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.
Katika kipindi cha miaka 20 kati yam
waka 1980 na 2000 idadi ya watu duniani iliongezeka kutoka bilioni 4.4 hadi
watu bilioni 6, huku asilimia 85 ya ongezeko hilo ikitokea katika nchi maskini
na zinazoendelea.
Kupungua kwa idadi ya vifo
vinavyotokana na uzazi katika miongo kadhaa, kumesaidia kuongeza idadi ya watu
lakini kumekuwa changamoto kubwa katika uchumi wa mataifa mbalimbali kutokana
na kusababisha uhaba wa ajira pamoja na huduma nyingine muhimu za
kijamii.
Mahitaji muhimu kama chakula, huduma
za afya, elimu, makazi, ardhi, ajira na nishati yanakumbwa na changamoto kubwa
kwenye mataifa yanayoendelea ambayo uchumi wake unajikongoja.
Mnamo Septemba 25, 2015, nchi zote
wanachama wa Umoja wa Mataifa ziliridhia malengo 17 kwa nia ya kutokomeza
umaskini, kulinda sayari dunia, kudumisha ustawi kwa wote ikiwa ni sehemu ya
agenda ya maendeleo endelevu ambapo kila lengo limepangiwa kukamilika katika
kipindi cha miaka 15 ijayo.
Ili kuyafikia malengo hayo, serikali,
sekta binafsi, taasisi za kijamii na jamii kwa ujumla inapaswa kushiriki
kikamilifu katika njia zote ambazo zinaweza kuleta tija, lakini suala la uzazi
wa mpango likipaswa kupewa kipaumbele.
1. Kutokomeza kabisa umaskini wa
namna zote
2. Kutokomeza njaa, kuhifadhi chakula
na kuboresha lishe pamoja na kuhimiza kilimo endelevu
3. Kuhakikisha maisha bora na
kudumisha ustawi wa wote katika kila umri
4. Kuhakikisha ushirikishwaji na
upatikanaji wa elimu bora pamoja na kudumisha fursa za kujifunzia kwa
wote
5. Kufikia usawa wa jinsia na
kuwawezesha wanawake na wasichana
6. Kuhakikisha upatikanaji na
usimamizi endelevu wa maji na mazingira
7. Kuhakikisha upatikanaji wa nishati
ya gharama nafuu, ya uhakika, endelevu na ya kisasa kwa wote
8. Kudumisha ukuaji endelevu wa
uchumi wenye ushirikishwaji, na ajira za kudumu na zenye tija kwa watu
wote
9. Kujenga miundombinu bora,
kudumisha ushirkishwaji wa maendeleo endelevu ya viwanda na kuchochea
ubunifu
10. Kupunguza matabaka ndani na
miongoni mwa nchi zote
11. Kuyafanya majiji na makazi ya
watu kuwa ya ushirikishwaji, salama, bora na endelevu
12. Kuhakikisha uwiano sawa wa
uzalishaji na matumizi
13. Kuchukua hatua za dharura
kupambana na mabadiliko wa mazingira na athari zake
14. Kutunza na kusimamia matumizi
endelevu ya bahari na rasilimali za majini kwa maendeleo endelevu
15. Kulinda, kuhuisha na kudumisha
matumizi endelevu ya vyanzo vya maji, usimamizi endelevu wa misitu, kukabiliana
na hatari ya jangwa, na kukomesha na kutunza ardhi ili kuokoa viumbe hai
16. Kudumisha Amani na kushirikisha
jamii kwa maendeleo endelevu, kudumisha upatikanaji wa haki kwa wote na kujenga
taasisi imara na zinazowajibika katika ngazi zote
17. Kuimarisha njia
za utekelezaji na kutoa kipaumbele cha Ushirikiano wa Dunia kwa Maendeleo
Endelevu
Comments
Post a Comment