- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega,
MaendeleoVijijini Blog
TANZANIA inaweza kupata asilimia kati ya 60
hadi 80 ya mauzo ya gesi asilia mara tu gesi hiyo itakapouzwa katika soko la
kimataifa bila kusubiri wawekezaji warudishe gharama zao zote, imefahamika.
Uchunguzi unaonyesha kwamba, kulingana na
mkataba wa Makubaliano ya Kuchangia Uzalishaji (Production
Sharing Agreement – PSA), Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya ndani – Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), inamiliki
asilimia 40 ya hisa kwenye miradi hiyo ya gesi, lakini wakati gesi hiyo
itakapoanza kuuzwa wawekezaji wanaweza kupata kati ya asilimia 20 hadi 40 tu.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, katika mfumo huo, kampuni za mafuta zinapewa haki ya
kurudisha gharama za uwekezaji na matumizi mengine na zinapata mapato ya mwaka
yajulikanayo kama – “gharama za mafuta” (Oil Costs).
Baada ya kutoa gharama za uwekezaji na
matumizi mengine, kiasi kinachobaki kijulikanacho kama – “faida ya mafuta” (oil
interest) – kinagawanywa kwa kufuata mgawanyo wa asilimia uliokubalika katika
mkataba.
Edward Kateka, Mwanasheria wa kampuni ya Statoil kutoka Norway iliyowekeza katika
Kitalu Namba 2 kwenye Bahari Kuu, aliwaeleza waandishi wa habari mwishoni mwa
wiki wakati wa warsha ya siku moja kwamba, uchimbaji wa gesi utakuwa na manufaa
zaidi kwa Tanzania ambayo itaanza kuchukua mapato makubwa hata kabla ya
wawekezaji kurudisha gharama zao, tofauti na ilivyo kwenye sekta ya madini.
“Wawekezaji tuna asilimia 60 kwenye mradi
na serikali kupitia kampuni ya ndani (TPDC) ina asilimia 40, lakini mara tu
gesi itakapoanza kuuzwa sisi tutapata asilimia kati ya 20 na 40 wakati asilimia
kubwa itachukuliwa na serikali yenyewe,” alisema Kateka.
Aliongeza kwamba, tayari Statoil na mshirika
wake ExxonMobil
wamekwisha wekeza kiasi cha Dola za Marekani bilioni 2 kwenye mradi huo ambapo
jumla ya futi za ujazo trilioni 22 zimegundulika katika visima vya Zafarani,
Piri, Tangawizi, Giligilani, Mronge, Mdalasini na Lavani.
Ili kufanikisha uzalishaji huo wa gesi,
Kateka alisema, upo umuhimu mkubwa wa kujengwa kwa mtambo wa kusindika gesi ya
kimiminika (LNG) ambao utasaidia kuisindika na kuisafirisha katika soko la nje.
Hata hivyo, MaendeleoVijijini
inatambua kwamba, chini ya mkataba wa Makubaliano ya Kuchangia Uzalishaji (PSA),
mkandarasi (mwekezaji) hawi na umiliki wa moja kwa moja wa mafuta au gesi
iliyoko ardhi, bali umiliki wa rasilimali hizo unakuwa kwa dola.
Katika hali hiyo mkataba huo wa PSA, ambao
uaonekana kuwa na tija zaidi kwa rasilimali za nchi husika, unaandikwa kwa
mkandarasi kuweza kuchimba mafuta ya serikali kwa niaba ya serikali.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, makubaliano
ya kuchangia uzalishaji yalianza kutumika Indonesia mwaka 1966, wakati serikali
ilipoamua kuhodhi umiliki wa mafuta ardhini, na hivyo kampuni ya kimataifa
ilikuwa na haki ya kufanya utafiti wa mafuta lakini ikapata haki ya kumiliki na
kuyauza (au kiasi fulani cha mafuta hayo) mara yanapochimbwa.
Kule Indonesia, kwa mujibu wa taasisi ya Revenue Watch, sasa National Resources Governance
Institute (NRGI), mtindo wa
kutoa leseni ya maridhiano uliondolewa kwa kuchukuliwa kama ni sera ya kibeberu
na ya wakati wa ukoloni na mfumo wa makubaliano ya kuchangia uzalishaji
ulianzishwa katika muktadha wa harakati za “utaifa katika rasilimali” miongoni
mwa nchi zizalishazo mafuta duniani kote.
Tangu wakati huo, makubaliano ya kuchangia
uzalishaji yameenea duniani na sasa ni mfumo wa kawaida wa kufanya biashara,
hususan katika maeneo ya Asia ya Kati na Caucasus.
Faida na hasara zake
Katika mfumo huu, gharama zote na tahadhari
za uendeshaji zinakuwa juu ya kampuni ya kimataifa ya mafuta katika mpangilio
wa makubaliano ya kuchangia gharama, na serikali mwenyeji inakuwa na faida ya
ziada kwamba inakuwa na faida yoyote itakayopatikana bila ya kufanya uwekezaji,
isipokuwa ikikubali kufanya hivyo.
Mtambo wa kusindika gesi.
Mtaji mkubwa wa serikali ni eneo pamoja na
rasilimali zilizomo chini yake, lakini pia hapa inaruhusiwa kupeleka wataalamu
wake kuwa miongoni mwa watumishi na inaweza kufuatilia kwa karibu uzalishaji na
masoko yalivyo kuliko ilivyo kwenye Mkataba wa Maridhiano.
Hasara ya makubaliano ya kuchangia
uzalishaji kwa serikali mwenyeji ni kwamba, kampuni inaweka gharama kubwa za
ziada kwa makubaliano ya kitaalam, na serikali lazima ipate wataalam wa
kiufundi, kimazingira, kifedha, kibiashara na kisheria.
Hii inawezekana zaidi katika baadhi ya nchi
zenye utajiri wa mafuta zaidi kuliko nyingine, kwa sababu serikali inatakiwa
kuandaa mazingira ya kuwasomesha wataalam wake ambao watakuwemo kwenye utendaji.
Aina za Mikataba
ya Mafuta na Gesi
Kabla ya Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi
ya Zanzibar, wakati utafiti wa kwanza wa mafuta na gesi ulipofanyika kati ya
mwaka 1952 na 1964, aina ya mikataba iliyotumika baina ya taifa chini ya
Serikali ya Kikoloni ya Waingereza na kampuni zilizofanya utafiti ilikuwa ya Maridhiano
(Concessional Agreements).
Kwa hiyo hata
kampuni za Shirika la Petroli la Uingereza (British Petroleum - BP) na
Shell ya Uholanzi zilipopewa sehemu ya kufanya tafiti na uchimbaji katika
ukanda wa pwani pamoja na visiwa vya Mafia, Pemba na Zanzibar (Unguja),
zilitumia mikataba hiyo.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, mikataba ya aina hiyo haiwezi kuinufaisha nchi mwenyeji
na yenye rasilimali zake, kwa sababu mkandarasi anamiliki mafuta yote yaliyoko
ardhini na kulipa kiasi kidogo kwa serikali.
Kwa bahati nzuri, katika awamu hiyo ya
kwanza mafuta hayakupatikana na kampuni hizo ziliondoka nchini wakati huo,
vinginevyo kama zingalikuwa zimepata mafuta na gesi enzi hizo, leo hii Tanzania
ingekuwa inalia kwa kukosa mapato ya kutosha.
Hata hivyo, katika uhalisia, mikataba mingi
ni zao la mchanganyiko wa vipengele vilivyomo ndani ya kila moja ya mikataba hiyo.
Mikataba yote ya mafuta na gesi ni lazima
izingatie masuala makuu mawili, kwa mujibu wa taasisi iitwayo Revenue Watch
Institute: jinsi faida, ambayo mara nyingi huitwa “kodi za pango”, inavyogawanywa
kati ya serikali na kampuni zinazohusika, na jinsi gharama zinavyopaswa
kushughulikiwa.
Mkataba wa Maridhiano
Mkataba wa Maridhiano
(Concessional Agreement) ni utaratibu wa zamani kabisa wa mikataba ya
mafuta, ukiwa umeanzishwa mara ya kwanza wakati wa mfumuko wa mafuta nchini Marekani
miaka ya 1800.
Kwa mujibu wa National Resource Governance
Institute, wakati mfumo wa maridhiano ulipoanzishwa duniani kote, uliegemea
upande mmoja zaidi wa kampuni kuliko nchi zenye rasilimali leo hii ambazo
wakati huo zilikuwa tegemezi, makoloni, au nchi zilizowekwa chini ya udhamini
wa dola nyingine au tawala nyingine.
MaendeleoVijijini inatambua kwamba, Mikataba ya Maridhiano
inafuata mfumo wa umiliki wa ardhi wa Marekani, ambapo mmiliki wa ardhi
anamiliki rasilimali zote zilizomo ardhini katika eneo analomiliki na
kinadharia rasilimali zote zilizomo juu yake.
Maridhiano yanatoa sehemu ya ardhi, na
rasilimali zilizo chini ya ardhi zikijumuishwa, kwa kampuni, ili kama kampuni
itagundua mafuta kwenye kipande cha ardhi, inamiliki mafuta hayo.
Katika mikataba ya maridhiano mkandarasi pia
ana haki zilizotengwa kuchunguza na kutafuta mafuta katika eneo hilo.
Wakati faida kwa kampuni inakuja moja kwa
moja katika muundo wa umiliki wa mafuta au gesi iliyopatikana, serikali
iliyotoa maridhiano inafaidika katika mfumo wa kodi na malipo mengine ya
uzalishaji katika mafuta na gesi iliyozalishwa.
Kampuni hushindana kwa kupandishiana dau,
pamoja na kutiliana saini bonasi, kwa ajili ya leseni ya haki hizi.
Aina hii ya makubaliano ni ya kawaida
duniani kote na inatumika Kuwait, Sudan, Angola na Ecuador, miongoni mwa nchi
nyingine.
Faida na hasara zake
Kwa serikali, MaendeleoVijijini
inajua kuwa, mikataba ya maridhiano ina faida ya moja kwa moja zaidi kuliko
makubaliano ya aina nyingine, na kiwango cha msaada wa kifani na kitaaluma
unaotakiwa si wa hali ya juu kama inavyohitajika kujadili na kufikia
makubaliano kwenye mkataba wa ubia au makubaliano ya kuchangia uzalishaji.
Serikali inakuwa haina haja hata ya
kutafuta wataalam ama kuwasomesha wataalam wake, kwa sababu kampuni inayowekeza
ndiyo yenye jukumu la kuwatafuta wataalam hao mahali kokote.
Kampuni husika pia ndiyo inayotoa mtaji
pamoja na zana nyingine zinazotakiwa, hivyo serikali haina haja ya kuingia
gharama yoyote.
Pia serikali mwenyeji inapata malipo
yanayotolewa na mkandarasi bila ya kujali kwamba mafuta yamepatikana au
uzalishaji wa kibiashara unafanyika.
Tahadhari zote za kifedha za uendelezaji,
ikiwa ni pamoja na gharama za uchunguzi (utafiti) zinachukuliwa na mkandarasi.
Hasara kuu kwa serikali ni kwamba, kampuni
inayoingia katika uzabuni wa mkataba ina kawaida ya kuchukua tahadhari katika
zabuni zao.
Kama mafuta na gesi hayakuhakikishwa
kunakuwa hakuna uhakika kwamba gharama za kampuni zitalipwa, kwa hiyo serikali
inaweza ikakosa kiasi kikubwa cha kipato kilichotarajiwa.
Wakati mwingine inakuwa vigumu kufuatilia
na kujua kiundani hasa uzalishaji uliofanyika na kampuni inaweza kudanganya kwa
sababu serikali haina wataalam wabobezi kwenye eneo hilo ambao wanaweza
kusaidia ufuatiliaji.
Mikataba ya
Huduma
Mkataba wa Huduma (Service Agreement) hautoi
haki ya kumiliki mafuta ardhini.
Tofauti na makubaliano ya kuchangia
uzalishaji, katika mkataba wa huduma kampuni ya kimataifa haipati kabisa umiliki,
au haki ya kumiliki mafuta yazalishwayo.
Katika hali hii kampuni inalipwa malipo kwa
huduma yake katika kuchimba mafuta ya serikali.
Hii inawezekana kwa nchi zenye utajiri wa
kutosha, ambazo zinaweza kuilipa kampuni fedha hata kabla mafuta ama gesi
haijapatikana.
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, ni vigumu kwa nchi zinazoendelea zenye rasilimali kama
Tanzania, ambazo hata bajeti zake zimekuwa zikishindwa kufikiwa kila mwaka,
huku wananchi wakitegemea utajiri mara wanapoambiwa kwamba kumegunduliwa mafuta
ama gesi nchini mwao bila kutathmini gharama zilizopo.
Mikataba ya Ubia
Uchunguzi wa MaendeleoVijijini
unaonyesha kwamba, mpangilio mwingine, ambao mara nyingine huchukuliwa kama ni
aina ya nne ya mipangilio ya kimkataba, ni ubia (Joint Venture), ambao
unahusisha dola kupitia kampuni ya taifa ya mafuta, kuingia ubia na kampuni au
kikundi cha kampuni za mafuta.
Ubia wenyewe katika hali hii unapewa haki ya kutafiti, kuendeleza, kuzalisha na kuuza mafuta.
Ubia wenyewe katika hali hii unapewa haki ya kutafiti, kuendeleza, kuzalisha na kuuza mafuta.
Kwa sababu hakuna mfumo wa ubia
uliokubalika kwa pamoja, mikataba ya ubia haitumiki sana kama mikataba ya
msingi kati ya kampuni ya mafuta na serikali mwenyeji.
Ubia unazitaka serikali wenyeji na kampuni
kufanya shughuli kwa pamoja, na hivyo kama wawili hao wakishindwa kufanya kazi
pamoja, makubaliano yanaweza kuwa na usumbufu na mizozo hutokea mara kwa mara.
Faida na hasara zake
Kwa serikali, faida pekee ya ubia ni kwamba
haiwi peke yake katika kutoa uamuzi kuhusu masuala ya mafuta na gesi, na
inaweza kutegemea wataalamu na sehemu ya ubia wa kampuni kubwa ya kimataifa.
Moja ya hasara kubwa ya mikataba ya ubia ni
kwamba, inahitaji majadiliano marefu zaidi na inahitaji ushauri mkubwa zaidi wa
kisheria na kitaalamu kwa sababu miundo yake inakuwa na utata sana.
Zaidi ya hayo, gharama pia lazima
zichangiwe na pande zote mbili, ikimaanisha kwamba serikali mwenyeji ni
mshiriki wa moja kwa moja na mwenye kuwajibika katika uchimbaji wa rasilimali,
na uwajibikaji pia unakuja na suala la kuhusika na masuala mengine, ikiwa ni
pamoja na suala la uharibifu wa mazingira.
Mikataba
inayotumika Tanzania
Kama ilivyoelezwa awali, kabla ya Uhuru,
mkataba uliotumika ulikuwa wa Maridhiano.
Hata hivyo, katika awamu ya pili ya utafiti
wa mafuta nchini iliyokuwa na matukio muhimu mawili - kwanza kuanzishwa kwa
kampuni inayomilikiwa na serikali, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), mnamo
1969, na pili ugunduzi mkubwa wa gesi katika eneo la Songo Songo, ndipo
yalitokea mabadiliko.
Baada ya kuanzishwa kwa TPDC, mkataba wa
kwanza wa Kuchangia Uzalishaji (PSA) ulisainiwa kati ya TPDC na AGIP (Aziende Generale Italiana
Petroli - kampuni ya mafuta ya Italia) kwenye eneo ambalo lilikuwa chini ya
usimamizi wa kampuni za BP na Shell katika Awamu ya Kwanza.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, mnamo mwaka
1973, AGIP aliingia ubia na kampuni ya AMOCO na kuchimba visima vitano, vitatu
ufukweni na viwili mbali na ufukwe. Maandiko mengine yanaonyesha kwamba jumla
ya visiwa sita vilichimbwa na AGIP na AMOCO huku vitatu vikiwa ufukweni na vitatu
mbali na ufukwe.
Uchimbaji huu ulisababisha ugunduzi mkubwa
kule Songo Songo mwaka 1974. Ugunduzi huo ulithibitishwa na TPDC katika
programu yake ya visima vitatu iliyotekelezwa kuanzia mwaka 1975 hadi 1979.
Kuanzia 1978, TPDC ikaingia katika utafiti
kwenye maeneo ya ufukweni na mbali na ufukwe.
Utafiti wa ufukweni ulijumuisha maeneo ya
Ruvu, Kimbiji/Bigwa, Pemba, Mafia na Ruvuma, wakati ule wa mbali na ufukwe
ulijumuisha Songo Songo, Pemba na Zanzibar.
Sheria ya Mikataba Sura ya 345 (kama
ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002) ndiyo inayosimamia mikataba nchini.
Mkataba (ambao kwa mtazamo mwingine wa
kisheria unajulikana kama makubaliano) unatekelezwa kwa kufuata sheria,
ukitanguliwa na pendekezo la mkataba (ofa), makubaliano na mwisho ahadi ya
utekelezaji.
Kwa mfumo wa sheria ya Jumuiya ya Madola,
mkataba una vipengele vifuatavyo: Uhalali wa kisheria, uwepo wa pande
zinazoingia mkataba, utoaji wa ofa na kukubali kutekeleza ofa iliyotolewa,
uzingatiaji wa sheria na wajibu wa pamoja miongoni mwa pande mbili au zaidi
zinazoingia mkataba.
Sheria hii inatoa mwongozo wa jumla, athari
za kisheria kwa aina zote za mikataba inayoingiwa Tanzania.
TPDC imepewa mamlaka ya kisheria kuingia mkataba, kumiliki hisa, kutoa leseni
na kuendesha shughuli za mafuta na gesi nchini kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri
ya Tanzania.
Mikataba inayoingiwa kwenye sekta ya mafuta
na gesi ni makubaliano kwa mujibu wa Kifungu Namba 14 cha Sheria ya Petroli
(Utafiti na Uzalishaji) ya mwaka 1980. Makubaliano hayo yanasimamiwa na Kifungu
Namba 42 cha sheria hiyo hiyo ambacho vipengele vyake vinasimamia masharti ya
leseni ya uendelezaji katika sekta ya mafuta na gesi.
Tangu TPDC ilipoanzishwa, mikataba ambayo
imekuwa ikiingiwa na wakandarasi ni ya Kuchangia Uzalishaji (PSA).
Makubaliano hayo
kwenye sekta ya mafuta na gesi uliandaliwa
na TPDC kama mwongozo wa makubaliano ya kimkataba kwa ajili ya utafiti na
uendelezaji wa sekta ya mafuta na gesi nchini.
Kwa hakika, ni mwongozo wa namna hii
unaosimamia makubaliano/mikataba kwenye sekta ya mafuta na gesi kwenye nchi
nyingi zinazoendelea.
Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com.
Simu: +255 656 331974.
Comments
Post a Comment