Featured Post

KIWANDA CHA MAJI IMAGE KUONGEZA UZALISHAJI

Geofrey Kikoti, Msimamizi wa Kiwanda cha Maji cha Rocks, akiwaonyesha waandishi baadhi ya mitambo inayotumika katika uzalishaji.

Na Mwandishi Wetu, Iringa
KIWANDA cha Maji cha Rocks kilichoko katika Kijiji cha Iyayi, wilayani Kilolo kinatarajia kuongeza uzalishaji baada ya kuwasili kwa mashine kubwa kuliko ya sasa.

Geoffrey Kikoti, msimamizi mkuu wa kiwanda hicho, alisema kwamba, kwa sasa uzalishaji ni mdogo kutokana na uwezo wa mashine iliyopo.
“Uzalishaji wetu siyo mkubwa kwa sababu mashine iliyopo ni ndogo, lakini tumepata mashine kubwa ambayo itaweza kuzalisha kiwango kikubwa tofauti na sasa,” alisema Kikoti.
Kufungwa kwa mtambo huo mkubwa kutakuwa fursa nzuri kwa wananchi wa maeneo hayo na Kata nzima ya Image, kwani watapatiwa ajira na hivyo kujikwamua na hali ngumu ya uchumi.
Hata hivyo, Kikoti alisema kwamba, changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa ni masoko, ingawa wameanza mkakati wa kutafuta masoko katika mikoa mingine nchini.
Kiwanda hicho kilichoanzishwa miaka mitatu iliyopita na kuanza kazi mwaka 2011, ni cha pili kinachozalisha maji mkoani Iringa baada ya kile cha Tanzathai kinachozalisha Maji Africa, ambacho kilikuwa cha kwanza kuanzishwa nchini tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Kikwazo kingine ni ukosefu wa umeme wa uhakika, kwani wanatumia jenereta ambalo gharama zake ni kubwa zaidi kuliko umeme wa gridi ya Taifa, hali ambayo pia inaathiri uzalishaji.
“Kwa sasa tunazalisha lita 540 tu kwa wiki, lakini tukipata umeme wa uhakika pamoja na kufunga mashine kubwa, tutakuwa na uwezo wa kuzalisha mara tatu au nne zaidi,” alisema.


Comments