- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
JUMA SALIM LAIZER UBAO 'KING MAKUSA': MMASAI WA LONGIDO MTUNZI WA 'ZOGOLO JANGU' ALIYEPIGA SOLO, SAX, KINANDA, TUMBA NA KUIMBA KATIKA SINGLE TRACK MOJA NDANI YA DAKIKA NNE!
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Juma Ubao 'King Makusa' akicharaza gitaa.
Juma Ubao ‘King Makusa’ (alizaliwa mwaka 1950,
Dodoma, Tanzania, akipewa jina la Juma Salim Laizer) ni mwanamuziki mahiri
ambaye mwaka 1976 aliwaacha hoi watangazaji wa Radio Tanzania Dar es Salaam
(RTD) baada ya kuimba na kupiga ala tano tofauti ndani ya dakika nane wakati
akirekodi wimbo mmoja.
Juma Ubao ni mwanamuziki mwenye vipaji vingi ambavyo ni
watu wachache wanaojaliwa kuwa navyo na umahiri wake unakumbukwa kuanzia miaka
ya 1970 hadi 1990 wakati muziki wa dansi ulipokuwa kwenye chati ya juu.
Juma Ubao
anakumbukwa kwa kutoa mchango mkubwa katika kujenga taifa kutokana na
kuhamasisha wananchi kwenda kujiunga katika Vijiji vya Ujamaa, ukimbizaji wa Mwenge,
na Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika kupitia muziki.
Maisha yake ya awali
Jila lake
halisi ni Juma Salim Laizer, aliyezaliwa mkoani Dodoma mwaka 1950 kwa mama
Sheila Sindano na baba yake ni Mmasai Salim Laizer. Tunaweza kusema, Juma Ubao
ni Mmasai wa kwanza kuwa mwanamuziki katika enzi zake ingawa hivi sasa wapo
wasanii wengi wa Kimasai.
“Kabila
langu ni Mmasai ingawa nimezaliwa Dodoma, lakini asili yangu ni Kijiji cha
Mabebu kilichopo Longido, mkoani Arusha,” alipata kusimulia Ubao.
Juma Ubao 'King Makusa' (kushoto) akicharaza gitaa. Kulia na Andy Brown Swebe enzi za uhai wake.
Kutokana
na kawaida ya Wamasai ambao huhama hama na mifugo wakitafuta malishi na maji,
babu wa babu zake alijikuta amefika Kondoa, mkoani Dodoma na mababu zake hao
wakasilimishwa katika Uislamu ingawa baadaye wakaweka maskani yao mjini Dodoma.
Baba yake Salim
Laizer aliyeishia darasa la tano, alikuwa mhasibu katika Shirika la Reli la
Afrika ya Mashariki (EAR) akifanyika kazi katika mji wa Iringa.
Jina la
Ubao alipachikwa na wapenzi na mashabiki wa muziki baada ya kuridhishwa na
upigaji wa ala nyingi kwa wakati mmoja, wakimlinganisha na ubao ambao hutumiwa
katika kufanya kazi nyingi.
Juma Ubao
alipata elimu yake katika shule ya msingi ya Wamissionari ya Consolata mjini
Iringa hadi alipomaliza darasa la nane mwaka 1965.
Alikuwa miongoni mwa
wanafunzi wa shule hiyo waliofaulu mtihani wa darasa la nane, akachaguliwa kwenda
kujiunga katika shule ya Sekondari ya Tosamaganga ya mkoani humo hadi
alipomaliza kidato cha nne mwaka 1969.
Miaka hiyo
wasomi hawakuwa wengi nchini Tanzania, hivyo elimu ilikuwa mithiri ya
‘lulu’. Elimu yake ya kidato cha nne
ilimpatia kazi nzuri mwaka 1970 kwenye kitengo cha Colito Barracks iliyopo
Lugalo jeshini, ambako alikuwa akijifunza muziki katika bendi ya muziki wa
mapipa (brass band).
Hamu ya muziki
ikaanzia hapo na mwaka 1972 alijiunga na bendi ya Polisi Jazz ‘Vangavanga’. Baadaye
alijiunga katika bendi ya King Africa iliyokuwa na wanamuziki mchanganyiko kutoka
Zambia na Wacongo akina Frolie, Monga Stanii na Tomaa ‘Kabotolo’. Bendi hiyo
ilikuwa ikiporomosha muziki wake katika ukumbi wa Mikumi Tours, uliokuwa
ukimilikiwa na mfanyabiashara maarufu Fadhili Batengas, maeneo ya Tazara,
Buguruni.
Mwaka 1973
kulipoanzishwa Vijiji vya Ujamaa nchini Tanzania, Juma Ubao alishiriki
kikamilifu kuhamasisha wananchi kwenda kujiunga katika vijijini hivyo.
“Tulinusurika
kuliwa na Simba tukiwa porini huko Mkongo wilaya ya Rufiji, wakati wa oparasheni
ya Vijiji vya Ujamaa,” alipata kukumbuka Juma Ubao.
Safari
yake katika muziki iliendelea kwa kujiunga katika bendi ya STC Jazz iliyokuwa
ikimilikiwa na Shirika la Umma la State Trade Corporation mwaka 1975.
Baadaye
STC ikabadilishwa kuwa Bodi ya Biashara ya Ndani (Board of Internal Trade) ambapo
bendi hiyo nayo ikabadili jina na kuitwa Biashara Jazz. Juma Ubao alipigia
bendi hiyo hadi mwaka 1982 wakati bendi ilipotoweka katika taswira ya muziki.
Ikumbukwe
kwamba miaka ya 1970 baadhi ya mashirika ya umma yalianzisha vitengo vya michezo
na burudani. Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) lilikuwa na bendi ya UDA
Jazz waliokuwa wakipiga katika mtindo wao wa ‘Bayankata’, Kiwanda cha nguo cha
Urafiki kilikuwa na bendi ya Urafiki Jazz wakitamba na mtindo wa ‘Chakachua’,
Shirika la Bima la Taifa (NIC), nalo lilikuwa na bendi ya Orchestra Bima Lee
wakitamba na mtindo wa ‘Magnet Tingisha’.
Mwaka 1976
akiwa Biashara Jazz ndipo alipopachikwa jina la King Makusa ambapo mwenyewe
alipata kukumbuka tukio hilo akisema:
“Mwaka
1976 tulikwenda studio za Radio Tanzania (RTD), kurekodi nyimbo zetu.
Niliwaacha midomo wazi watayarishaji na watangazaji wa wakati huo akina Khalid
Ponela, John Luanda, Charles Hilary, Frank Kirumbi, Gilbert Boma na fundi
mitambo wao James Mhilu na Crispin
Lugongo, wakinishuhudia nikipiga sehemu
sita katika wimbo mmoja ndani ya dakika nane. Nilitayarisha wimbo, nilipiga
solo, niliimba, nilipapasa kinanda, nilipuliza saxophone, na kutwanga tumba
katika ‘single track’ ndani ya dakika nane…”
Kwa watangazaji
hao, ilikuwa ni kitu kipya ambacho hakikuwahi kufanywa na mwanamuziki mwingine
yeyote. Ndipo hapo walipompachika jina la King Makusanya, likiwa na maana ya
Mfalme Makusanya. Lakini wakashauriana na kufupisha kuwa ‘King Makusa’, jina ambalo
lilivuma na kufunika majina yake mengine ya Salim Laizer.
Enzi zake
wakati akipiga muziki ukumbini, alikuwa anapiga gita na kinanda, kila ala kwa
wakati wake. “Wakati ninaimba gita huliweka ubavuni, saxophone huiweka mgongoni
na kinanda pembeni huku watu wakinishangaa,” alijisifia Juma Ubao.
Mwaka 1987
Juma Ubao aliteuliwa kuwa miongoni mwa wanamuziki 57 waliounda kundi la
Tanzania All Stars waliotoka na wimbo wa Fagio
la Chuma ukiwa ni kauli mbiu ya Rais wa Awamu ya Pili, Alli Hassan Mwinyi,
juu ya uwajibikaji.
Mwaka
1989, Juma Ubao alikuwa muasisi wa bendi ya Six Manyara akiwa na wanamuziki
wakongwe akina Suleiman Mwanyiro, Hassan Bitchuka, Kassim Rashid ‘Kizunga’,
Kasola Rajabu na Manicho Athumani. Wakiwa katika bendi hiyo walifumua vibao vya
Batuli na Salama zikiwa ni tungo za Juma Ubao mwenyewe. Nyimbo nyingine
zilikuwa Maselina, Fatuma Samahani Sana
na Tabu.
Bendi hiyo
ya Six Manyara iliundwa kwa madhumuni ya kutangaza fahari za utalii wa Tanzania
zikiwemo mbuga za wanyama, Mlima Kilimanjaro na vivutio vingine vilivyopo
nchini humo. Bendi hiyo ilisafiri kwenda kutangaza utalii katika nchi za Uganda
na Kenya mwaka 1991. Wakiwa Kenya walirekodi nyimbo nne katika kampuni ya
PolyGram kwenye Long Play. Waliporejea nchini Tanzania wanamziki wake wengine
walirudi katika bendi zao za zamani lakini yeye akaamua kubaki na bendi hiyo
hadi sasa.
Juma
alipumzika mambo ya muziki kwa muda na kuutumia muda huo kwenda kusoma masomo
ya jioni akiwa na lengo la kujiendeleza kielimu, akisomea Uhasibu na Biashara
na akatunukiwa cheti ambacho kilimpa nafasi ya ajira katika Shirika la Ndege
Tanzania (ATC) kama mhasibu katika Klabu ya Jet. Baadaye akahamishiwa Uwanja wa
Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere ambako alipewa kitengo cha kusimamia vyakula
vya kwenye ndege.
Katika
kitengo hicho, Ubao alilipunguzia kwa kiasi kikubwa shirika hilo gharama za
malipo zilizokuwa zikilipwa. Yeye alisimamia ipasavyo vyakula vyote kuandaliwa kutoka
Klabu ya Jet, badala ya kuvinunua katika Hoteli ya Kilimanjaro.
Baadaye ATC
ikaanza kuyumba kiuchumi hali iliyosababisha kupunguza baadhi ya wafanyakazi
wake mwaka 2002, miongoni mwao akiwa Juma Ubao.
Mwaka 2000
Six Manyara ilirekodi nyimbo za Somo
Somo, Leo Leo zilizopigwa katika mahadhi ya mduara. Wimbo wa Zogolo Jangu uliimbwa kwa lugha ya
Kizaramo ikiwa na maana ya ‘Jogoo Langu’. Wimbo wa Sakina ulipigwa katika mtindo wa reggae na nyingine ni Msichana, na Tuluka Chibite ulirekodiwa kwa lugha ya Kigogo ukiwa na maana ya ‘Inuka
Tuondoke’. Wimbo mwingine uliotia fora wakati huo ni Bide, ambao Juma Ubao alitunga na kuimba kwa lugha ya Kipogoro.
Juma Ubao akichangia mada kwenye mojawapo ya majukwaa ya sanaa na muziki, wakati akiwa Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA).
Demokrasia
katika tasnia ya muziki ilifanya kazi yake pale mwaka 2008 Juma Ubao alipochaguliwa
kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA) akichukua nafasi
hiyo baada ya Kassim Mapili aliyekuwa mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho,
kumaliza muda wake.
Juma Ubao
amekwisha pewa nafasi nyingi za uongozi katika tasnia ya muziki nchini Tanzania.
Mwaka 2009, aliteuliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA).
Juma Ubao
aliiomba serikali kuwatambua wanamuziki wa zamani ambao walitoa mchango mkubwa
kupitia tasnia ya muziki wakati wa kutafuta Uhuru, kuijenga nchi pamoja na
kushirki katika harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika.
“Kuthaminiwa
kwa wanamuziki hawa si kwa kuwapa pesa pekee, la hasha, bali ni kuwepo kwa utaratibu japo wa kuweka majina
yao kwa baadhi ya mitaa, shule ama hospitali katika halmashauri za Manispaa
zetu ili yawe kama vielelezo kwa vizazi vijavyo,” alifafanua.
Familia
Juma Ubao
ni baba wa familia ya mke na watoto watano. Anamtaja mkewe Ashanti Mwinjuma
kwamba katika kipindi chote katika muziki, ndiye aliyekuwa akimfariji na kumpa moyo
kila alipokuwa akikwama.
Watoto
wake ni Athumani, ambaye amefuata nyayo zake, yupo nchini Austria, akifanya
mambo ya muziki. Laizer, Ibrahimu, Aboubakar na Salma.
Imeandaliwa
na www.maendeleovijijini.blogspot.com.
+255 656 331974. Ukinakili tafadhali taja chanzo hiki.
Comments
Post a Comment