Featured Post

JINSI YA KUSHUGHULIKIA MIPAKA YA ARDHI YA KIJIJI

MPANGO WA MATUMIZI BORA YA ARDHI YA KIJIJI - 3
Ramani ya Kijiji cha Kapunga wilayani Mbarali ni mfano halisi wa michoro inayoonyesha mipaka ya kijiji.

Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini blog
SHERIA ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999 inatoa tafsiri ya ardhi kwamba ni pamoja na udongo juu na chini ya uso wa nchi pamoja na mimea inayoota au kupandwa juu yake, majengo, mawe, milima na kadhalika.
Ardhi hii, kwa mujibu wa sheria hiyo, inaweza kumilikiwa na kundi la watu, mtu binafsi, taasisi na kusimamiwa na mamlaka mbalimbali.

Hata hivyo, maji, madini na petrol havimilikishwi chini ya Sheria hiyo, ndiyo maana mahali ambako utafiti umefanyika na kugundulika kuwa kuna madini au mafuta, serikali imekuwa ikiwahamisha watu na kufanya shughuli hizo yenyewe ama kwa kutafuta wawekezaji.
Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 imeweka Kanuni za Msingi ambazo ni kama zifuatazo:
* Kutambua kwamba ardhi yote ya Tanzania ni mali ya umma na imekabidhiwa kwa Rais kama mdhamini mkuu kwa niaba ya raia wote.
Kwahiyo ardhi yote ya Tanzania ni mali ya raia wote kwa pamoja, lakini mtu binafsi anayo haki ya kukalia na kuitumia ardhi ambayo ni hakimiliki, na hakimiliki kwa mujibu wa Sheria hiyo ni mali.
* Kuhakikisha kwamba haki zote zilizopo katika ardhi na umilikaji wa ardhi kwa muda mrefu unatambuliwa, unafafanuliwa na kulindwa kisheria.
* Kuwezesha ardhi kugawiwa kwa haki na kupatikana kwa raia wote.
* Kudhibiti kiasi cha ardhi ambacho mtu mmoja au kampuni inaweza kumiliki au kutumia.
* Kuhakikisha kwamba ardhi inatumika kwa uzalishaji na kwa matumizi endelevu.
* Kutambua maslahi katika ardhi yana thamani na thamani hiyo inalindwa katika uhamisho wowote wa maslahi ya ardhi.
* Kulipa fidia KAMILI, ya haki na kwa wakati kwa mtu yeyote ambaye Hakimiliki au ukaliaji ardhi wa muda mrefu unaotambuliwa au ukaliaji ardhi wa kimila kwa kutwaliwa na Taifa kwa mujibu wa Sheria hii au chini ya Sheria ya Utwaaji Ardhi.
Wakati wa kufanya uthamini wa ardhi kwa ajili ya fidia mambo yafuatayo lazima yazingatiwe:
-         Thamani ya soko ya mali iliyopo
-         Posho ya usafiri
-         Upotevu wa faida au makazi
-         Gharama aliyotumia kuipata ardhi husika
-         Gharama nyingine yoyote ya kupoteza mtaji wa ardhi
-         Riba ya soko kulipwa kutokana na ucheleweshaji malipo ya fidia.
* Kuweka mfumo madhubuti, rahisi na wazi wa kusimamia kwa ufanisi masuala ya ardhi.
* Kuwezesha wananchi wote washiriki katika uamuzi unaohusiana na miliki au matumizi ya ardhi yao.
* Kuwezesha uendelezaji wa soko la ardhi.
* kuweka kanuni za Sheria za Ardhi zinazomwezesha kila mtu kupata ardhi na kwa utaratibu unaoeleweka kwa raia wote.
* Kuanzisha utaratibu huru, wenye ufanisi na wa haki wa kuhakiki migogoro ya ardhi ili kusikiliza na kutoa uamuzi wa kesi za ardhi bila ucheleweshaji.
* Kuwezesha utoaji wa elimu ya utawala na Sheria za Ardhi kwa kuandaa na kutekeleza program ya uhamasishaji wa umma kwa kutumia aina zote za vyombo vya upashanaji habari.

Aina za Ardhi
Ardhi yote nchini Tanzania ni mali ya umma, chini ya Rais kama mdhamini.
Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999 imeainisha aina kuu tatu za ardhi katika Tanzania kama ifuatavyo:
Mosi, Ardhi ya Kawaida – Hii ni ardhi yote ya umma ambayo siyo ardhi ya hifadhi au ardhi ya kijiji na inajumuisha ardhi ya kijiji ambayo haikaliwi wala kutumika na husimamiwa na Kamishna wa Ardhi.
Pili, Ardhi ya Hifadhi – Hii inajumuisha ardhi iliyotengwa kwa matumizi kama hifadhi za misitu, hifadhi za mbuga za taifa za wanyamapori, maeneo mengine ya hifadhi ya barabara na miji.
Pia ardhi iliyotunzwa kama ardhi ya masaibu na ardhi hii husimamiwa na Afisa Mteule au mamlaka ya hifadhi.
Tatu, Ardhi ya Kijiji – Hii ni ardhi ya umma ambayo mipaka yake imewekwa kwa sheria yoyote au utaratibu wa kiutawala kama ardhi ya kijiji.
Ardhi ndani ya kijiji kilichosajiliwa au kutambulika chini ya Sheria ya Serikali za Mitaa (Tawala za Wilaya) Namba 7 ya mwaka 1982 na Sheria ya Makazi ya Vijiji, Namba 27 ya mwaka 1965 kila moja kwa upande wake ni ardhi ya kijiji.
Pia Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 (1999) inabainisha ardhi kama ardhi ya kijiji, inapokuwa siyo ardhi ya hifadhi, ambayo imekaliwa na wanakijiji husika, kwa muda wote usiopungua miaka 12 kabla ya kuanza kutumika kwa Sheria hii.
Sheria ya Ardhi ya Vijiji (1999) imeweka utaratibu maalum wa kubadili (kuhawilisha) ardhi ya kijiji kuwa ardhi ya hifadhi au ardhi ya kawaida, ili kuwalinda wanakijiji wasinyang’anyawe ardhi yao na watu wan je ya kijiji.
Ardhi hii ya Kijiji husimamiwa na Halmashauri ya Kijiji.
Kimsingi, ardhi yote ya Tanzania inabakia kuwa ardhi ya umma chini ya Rais kama mdhamini kwa niaba ya Watanzania wote.
Rais na mtu yeyote ambaye Rais amekasimu kazi zake kwake kwa mujibu wa sheria, wakati wote mtu huyo atatekeleza majukumu hayo kama mdhamini.
Kwa mantiki hiyo basi, aina hizi tatu za ardhi: Ardhi ya Kawaida, Ardhi ya Hifadhi na Ardhi ya Kijiji; ni kwa ajili ya usimamizi na wasimamizi wakiwa ni wadhamini kwa kukasimiwa mamlaka hayo na Rais.

Uhawilishaji wa Ardhi
Pale ambapo Rais anakusudia kubadilisha (kuhawilisha) eneo lolote la ardhi, kutoka aina moja kwenda nyingine, anaweza kumuagiza Waziri mhusika wa Ardhi kuendelea kufanya hivyo kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi (1999) Fungu la 5-6.
Kuwezekana kwa mabadiliko hayo kunatoa msingi wa mipango ya matumizi ya ardhi ya Taifa, Kanda, Mikoa na Wilaya.
Ngazi hizo ni muhimu ili kuoanisha miundombinu ya msingi kama njia za mawasiliano na huduma za jamii, hifadhi ya vyanzo vikuu vya maji, wanyamapori, malisho, misitu na mabonde ya maji yanayojumuisha vijiji mbalimbali.
Katika mtazamo huo, mipango ya matumizi ya ardhi ya wilaya inapaswa kulenga kuainisha maeneo ya Ardhi ya Kawaida, Ardhi ya Hifadhi na Ardhi ya Vijiji, na inapohitajika, mabadiliko yake.
Ikumbukwe kuwa mabadiliko yoyote yafuate taratibu za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha walengwa, kumshauri Waziri husika na hatimaye Rais atekeleze mabadiliko kulingana na taratibu na sheria za ardhi.

Ardhi ya Kijiji
Kimsingi ardhi ya kijiji ni ardhi ya umma ambayo mipaka yake imewekwa kwa sheria yoyote au utaratibu wa kiutawala.
Hii inamaanisha kwamba, ardhi ya kijiji inaweza kupakana na Ardhi ya Kawaida, Ardhi ya Hifadhi na au Ardhi ya Kijiji kingine.
Wasimamizi wa Ardhi ya Kijiji (Halmashauri ya Kijiji) wana wajibu wa kuwasiliana na Mamlaka za Hifadhi (kama wanapakana) na Halmashauri za Vijiji jirani, ili kutambua na kuweka mipaka ya kijiji inayokubalika kwa pamoja.
Mara nyingi hiyo siyo kazi rahisi kwa sababu baadhi ya migogoro mikubwa ya ardhi ipo katika ngazi ya mipaka ya vijiji.
Kuna migogoro ya mipaka kati ya hifadhi za misitu na vijiji; hifadhi za wanyamapori na vijiji; mashamba binafsi (ardhi ya kwaida0 na aghalabu kati ya kijiji na kijiji.
Kujaribu kuweka au kupima mpaka ambao bado mgogoro wake haujatatuliwa mara nyingi hulipua na kukuza mgogoro wenyewe.
Kwa kutambua hilo, mwongozo wa usimamizi wa matumizi ya ardhi vijijini, kwa kuzingatia Sheria ya Ardhi ya Vijiji, umeweka wazi utaratibu wa kuweka na kupima mipaka ya vijiji.
Utaratibu huo umetumika katika wilaya za mfano, hususan katika vijiji vingi vya wilaya za Kilindi na Handeni mkoani Tanga, na kutoa matunda mazuri.
Kesho tutaangalia uwekaji wa mipaka ya ardhi ya kijiji.

Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com. Tupigie: +255 656 331974


Comments