Featured Post

HOMA YA BONDE LA UFA NI UGONJWA TISHIO KWA WANYAMA NA BINADAMU

Mbwa aliyekufa kutokana na ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa.

 

UGONJWA wa Homa ya Bonde la Ufa (Rift Valley Fever) kupitia vyombo vya habari na kupitia Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE) umeripotiwa kulipuka mara kwa mara katika eneo la Afrika Mashariki hasa katika nchi jirani ya Kenya.

Ugonjwa huu, kama jina lake linavyoonyesha hutokea kwenye nchi zilizopitiwa na Bonde la Ufa na Tanzania ni mojawapo ya nchi hizo.
Ugonjwa hutokea baada ya mvua nyingi na mafuriko yanayofuatia kuwepo kwa ukame wa muda mrefu.
Uchunguzi wa remote sensing uliofanywa na Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) unaonyesha kuwa maeneo yaliyo na hatari zaidi ya kuambukizwa na ugonjwa ni pamoja na Kenya, Kusini mwa Somalia, Kusini na Kusini Mashariki mwa Ethiopia, Kusini mwa Sudan na Kaskazini mwa Tanzania.

HISTORIA YA UGONJWA
Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa (Rift Valley Fever) katika nchi ya Kenya umefahamika kwa zaidi ya miaka 60 iliyopita.
Ugonjwa unaofanana na Homa ya Bonde la Ufa ulionekana mara ya kwanza nchini Kenya mwaka 1913.
Tangu wakati huo matukio makubwa ya ugonjwa yameonekana katika nchi nyingi za Bara la Afrika ikiwa ni pamoja na Misri, Sudan, Somalia, Kenya, Msumbiji, Nigeria, Senegal, Tanzania, Uganda, Zambia, Zimbabwe, Namibia na Afrika ya Kusini.
Nchi ya Misri ilikumbwa na ugonjwa huu mwaka 1977 na 1978 ambapo watu wapatao 18,000 waliugua na 598 walikufa.
Nchi ambazo taarifa zilitolewa za matukio ya ugonjwa huu nje ya Bara la Afrika ni pamoja na Yemen na Saudi Arabia.
Kwa hapa Tanzania ugonjwa huu ulionekana mwaka 1979 na 1998 katika mikoa ya Mara, Arusha na Kilimanjaro ambapo ng’ombe, Mbuzi, kondoo na ngamia waliathirika.

CHANZO
Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa (Rift Valley Fever) unasababishwa na virusi viitwavyo Phlebovirus na ambavyo kitaalam vimewekwa katika familia ya Bunyaviridae.
Virusi hivi huweza kuishi kwenye mayai ya mbu aina ya aedes, ambayo yana tabia ya kuishi kwenye vumbi kwa muda mrefu na kuanguliwa wakati wa mafuriko.
Baada ya kuanguliwa mbu hawa husambaza ugonjwa kwenye mifugo na kwa watu wakati wanapofyonza damu.
Mbu aina nyingine kama vile Culex, Mansonia, Anopheles, na Eretmapodites wanaweza kusambaza virusi vya ugonjwa kati ya wanyama na wanyama na kati ya wanyama na binadamu.
Lakini zaidi ya kupata ugonjwa moja kwa moja toka kwenye mbu binadamu wanaweza kupata ugonjwa kupitia kugusa damu au majimaji ya aina nyingine ya wanyama wakati wa kuchinja, kuzalisha wanyama wagonjwa, kushika vitoto vya mbuzi au kondoo vilivyokufa.
Aidha, binadamu wanaweza kupata ugonjwa kutokana na kula vyakula visivyopikwa vizuri vitokanavyo na wanyama wagonjwa au wenye virusi.

DALILI ZA UGONJWA
Dalili kwa mifugo
Ugonjwa huu huwapata ng’ombe, mbogo, kondoo, Mbuzi, ngamia na binadamu. Ugonjwa huonekana zaidi kwenye maeneo ya watu wenye mifugo mingi.
Dalili za kwanza katika wanyama ni kutupa mimba kwa wingi hususan katika kondoo na ngamia na vifo vingi vya ghafla kwa karibu asilimia 90 ya mbuzi na kondoo wachanga.
Kwenye mbuzi na kondoo wakubwa dalili za ugonjwa ni pamoja na kutapika, kutokwa makamasi yenye damu na kuharisha, rangi ya njano kwenye ngozi ya ndani inayofunika macho, midomo na sehemu za uzazi na vifo katika asilimia 10 hadi 20 ya wanyama hawa. Ng’ombe hawaugui sana kama ilivyo kwa mbuzi na kondoo.

Dalili kwa binadamu
Dalili za ugonjwa kwa binadamu ni pamoja na kuumwa kichwa, kuumia macho wakati yanapoangalia mwanga mkali, mafua, homa kali, tumbo kuuma, kutapika na wakati mwingine kutapika damu.
Virusi huchukua muda wa siku mbili hadi sita tangu kuingia mwilini hadi kuanza kuonyesha dalili na ugonjwa unaweza kusumbua kwa muda wa siku tatu hadi saba au zaidi.
Vifo kwa binadamu vinaweza kutokea baada ya virusi vya ugonjwa huu kushambulia ubongo na viungo vingine vya mwili ambapo husababisha kuvuja damu.

KINGA NA NAMNA YA KUUEPUKA
Kama ilivyokwishaelezwa Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa unasababishwa na virusi na unaenezwa na mbu.
Kwa hiyo njia mojawapo ya kuzuia mifugo isipate ugonjwa ni kuiogesha au kuinyunyizia dawa aina ya pyrethroids ambazo ni pamoja na Flumethrin, Deltamethrin na Alphacypermethrin.
Dawa hizi tayari ziko nchini na zinatumika kuogeshea mifugo ili kuikinga isishambuliwe na kupe au mbung’o na zinaweza kutumika pia ili mifugo isishambuliwe na mbu.
Njia ya kuzuia binadamu wasipate ugojwa huu ni kutumia vyandarua. Pia wananchi wanaweza kuepuka ugonjwa huu kwa kupika vizuri vyakula vitokanavyo na mifugo.
Wizara inashauri wananchi wachukue tahadhari hizi hata kama ugonjwa haujaonekana popote nchini kwa sababu kinga ni bora kuliko tiba.

Comments