Featured Post

HIZI NDIZO MAMLAKA ZINAZOSIMAMIA SEKTA YA MAFUTA NA GESI TANZANIA


KATIKA kuhakikisha usimamizi madhubuti wa sekta ya mafuta na gesi asilia nchini Tanzania, zipo mamlaka kadhaa za umma ambazo zina majukumu na wajibu mbalimbali kulingana na miundo yake.
Mamlaka tano muhimu zinazosimamia sekta hiyo kuanzia ngazi ya juu ya utafiti hadi ngazi ya chini ya matumizi pamoja na masoko na usimamizi wa mapato ni hizi zifuatazo: 

Wizara ya Nishati na Madini
Wizara hii ndiyo msimamizi mkubwa wa masuala yote yahusuyo nishati na madini na ina dhamana kubwa ya kuhakikisha inainda rasilimali za taifa kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Ilianzishwa chini ya Kifungu cha Sheria Nambari 226 kinachoelezea dhima za Wizara, katika Notisi ya Serikali Nambari 494 ya mwaka 2010, ambayo ilianza kutumika Novemba 24, 2010.
Kabla ya kuanzishwa kwa Wizara ya Nishati na Madini, masuala ya nishati na madini nchini yaliendeshwa na Wizara ya Viwanda na Biashara (1960-1961), Wizara ya Viwanda, Madini na Nishati (1964-1966), Wizara ya Maji, Nishati na Madini (1978-1981), Wizara ya Madini (1981-1984), Wizara ya Nishati na Madini (1986-1990) na Wizara ya Maji, Nishati na Madini (1991-1996).
Kwa mujibu wa Tovuti ya Wizara, wizara inaongozwa na mkakati wa “kupanga sera, stratejia, na sheria kwa uendelevu wa nishati na madini, kuwezesha ukuaji na maendeleo ya kiuchumi,” na dira ya kuwa “taasisi yenye ufanisi katika kuchangia kwa kasi kubwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia maendeleo ya kudumu na matumizi ya nishati na madini Tanzania ifikapo mwaka 2025.”
Wizara hiyo ina dhima kubwa ya kuratibu na kuweka sera zinazofaa, sheria, kanuni na kutoa usimamizi ili kuhakikisha maendeleo ya kudumu katika sekta ya nishati na madini.
Pamoja na majukumu hayo, lakini wizara ina jukumu la kusimamia taasisi mbalimbali zilizo chini yake kama vile; Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Shirika la Madini la Taifa (Stamico), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Chuo cha Madini (MRI).
Wizara inaongozwa na mpango mkakati wa miaka mitano 2011/12 – 2015/16 ambao unamalizika mwaka huu.
Mpango huo unafafanua maeneo matano ya kimkakati ambayo ni Kuinua, kuendeleza na kusimamia sekta ya nishati ili kukuza faida na kuhakikisha upatikanaji wa nishati; Kuinua na kuharakisha upatikanaji wa nishati ya kisasa katika maeneo ya vijijini; Kuinua, kuendeleza na kusimamia sekta ya madini ili kukuza faida; Kuboresha ukusanyaji wa kipato kitokanacho na sekta ya madini na nishati; na vilevile, Kuboresha usimamiaji wa rasilimali watu na fedha.
Muundo wa wizara hii unaonyesha kwamba imegawanywa katika vitengo vikubwa viwili, kitengo kinachoshughulikia Nishati na kitengo kinachoshughulikia Madini.
Kitengo cha Nishati kinaongozwa na Kamishna na kina sehemu tano ikiwa ni pamoja na sehemu zinazoshughulikia Mafuta ghafi, Umeme, Nishati Mpya na yenye kuhuishwa, Maendeleo ya Nishati, na Matumizi ya Gesi.
Kitengo cha Madini kinaongozwa na Kamishna na kina sehemu sita ambazo ni Ukaguzi wa Madini, Uchimbaji Mdogomdogo, Leseni na Usimamizi wa Umiliki wa Madini, Uchumi na Uuzaji wa Madini, Udhibiti wa Vilipukaji, Usafishaji na Uongezaji Thamani ya Madini.

Benki Kuu ya Tanzania
Benki Kuu ndicho chombo kilichopewa majukumu mbalimbali muhimu ya usimamizi wa fedha nchini ambapo miongoni mwa majukumu hayo ni kuhakikisha uwepo wa akiba ya fedha za kigeni kwa lengo la kusaidia kuimarisha uchumi, na akiba hiyo kutumika wakati wa mkwamo wa kiuchumi nchini.
Pia ndicho chombo kinachopaswa kuchochea ukuaji wa soko la fedha nchini, kulinda na kuendeleza taasisi za kifedha zinazosimamiwa vema, na kuhakikisha uwiano imara kati ya fedha ya Tanzania na pesa za kigeni.
Chombo hiki kilianzishwa rasmi Desemba 1965, baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha sheria ya kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambayo ilizinduliwa na Raisi Julius Nyerere mwezi Juni 1966.
Baada ya kupitishwa kwa Azimio la Arusha mwaka 1967, Benki Kuu ilipewa kazi ya kusimamia matumizi ya fedha za kigeni.
Mwaka 1978, Sheria ya Benki Kuu ilifanyiwa marekebisho kutokana na kudorora kwa uchumi nchini, na kuipatia mamlaka ya kusimamia taasisi za fedha. Kwa sasa, BoT imejikita katika kusimamia mfumuko wa bei na kuimarisha bei, mamlaka ambayo yameainishwa kwenye Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 1995 na pia Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006.
Ushiriki wa Benki kuu ya Tanzania (BoT) kwenye sekta ya mafuta na gesi umebainishwa kwenye sera mbili ambazo ni Sera ya Taifa ya Gesi Asilia Tanzania (2013) na Sera ya Uwezeshaji na Ushirikishaji Wazawa Tanzania (2014).
Katika Sera ya Gesi Asilia, wajibu wa BoT kwenye sekta ya mafuta na gesi ni “kuandaa taratibu za kifedha kwa lengo la kuzuia mfumuko wa bei unaoweza kusababishwa na gesi asilia”.
Sera hii imeainisha majukumu makuu matatu ambayo BoT inapaswa kuyatimiza ambayo ni Kuhakikisha kwamba shughuli za gesi hazisababishi athari mbaya kwenye sera ya udhibiti wa fedha na uchumi mpana wa nchi; Kushauri serikali kuhusu athari za sekta ya gesi asilia kwenye uchumi wa nchi; na Kusimamia Mfuko wa Mapato wa Gesi Asilia Tanzania ambao umeanzishwa na sera hii.
Sera ya Uwezeshaji na Ushirikishaji Wazawa Tanzania imeitambua BoT kama moja ya taasisi muhimu katika utekelezaji wa sera hiyo.
Kwa mujibu wa sera hiyo, BoT ina wajibu wa kutekeleza usimamizi wa kifedha na uwezeshaji wazawa kwenye sekta ya gesi asilia nchini.
Aidha, Sera hiyo inabainisha kwamba, BoT itaaandaa mfumo mzuri wa kifedha ambao utaleta uimara kwa muda kutokana na kwamba sekta ya mafuta na gesi inaweza kuchochea mfumuko wa bei nchini kama utaratibu mzuri haujaandaliwa, hivyo kuleta athari inayofahamika kitaalam kama ‘Dutch Disease’. BoT pia inawajibika kutoa na kufuatilia matumizi yaliyoombwa na kupitisha matumizi kwa ajili ya uwezeshaji wazawa nchini.
Muungano wa Washirika wa Maendeleo Tanzania (DPG - Tanzania) wanapendekeza kwamba usimamizi wa Mfuko wa Mapato wa Gesi Asilia lazima ufanyike kwa kuzingatia uwazi na uwajibikaji, ikiwemo namna gani fedha hizo zitatumika kusaidia wananchi.
Taasisi ya NRGI— na kituo cha ‘Vale Columbia Centre on Sustainable International Investment (VCC)’ wamebainisha katika uchambuzi wao wa mifuko ya namna hiyo kwamba msimamizi (kwa maana ya BoT), lazima azingatie sheria na kanuni katika usimamizi wa mfuko huo na mali zake.
Wanashauri kwamba wajibu wa kusimamia mfuko huo lazima uwekwe wazi kwa kutambua ni nani mwenye mamlaka ya mwisho juu ya usimamizi wa mfuko na majukumu yake, wajibu wa msimamizi wa mfuko na wajibu wa idara mbalimbali zilizoko chini ya msimamizi wa mfuko huo – kwa maana hiyo mamlaka zilizo chini ya BoT.
Taasisi ya NRGI inapendekeza kuwepo kwa kikomo cha kiwango cha fedha ambacho msimamizi wa mfuko anaweza kuwekeza kwenye vitega uchumi mbalimbali kama ujenzi na miundo mbinu.
Katika eneo la uwekezaji, uwekezaji nje ya nchi unashauriwa ili mfuko ubaki kuwa ni sehemu ya kuweka akiba tu, na faida itokanayo na uwekezaji utakaofanyika ndiyo itumike.
Aidha, inapendekezwa kwamba taasisi huru zikiwemo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), zipewe mamlaka kamili ya kusimamia mfuko huo.
Muundo wa Utawala wa BoT unaongozwa na Bodi ya Wakurugenzi ambacho ni chombo chenye mamlaka ya juu ya uamuzi na kinawajibika kuweka mwelekeo wa kisera, kupitisha bajeti na kadhalika.
Bodi hiyo inaundwa na Gavana ambaye ndiye mwenyekiti, naibu gavana watatu, mwakilishi wa Wizara ya Fedha, Katibu Mkuu Hazina Zanzibar, wajumbe wanne, na katibu wa bodi. Gavana ana mamlaka ya kuamua ni nani kati ya manaibu hao watatu awe makamu mwenyekiti.

Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura)
Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) ni mamlaka inayojitegemea iliyoanzishwa Februari 2006 chini ya Sheria ya Udhibiti wa Nishati na Maji, (Sura ya 414) na inasimamia udhibiti wa kiteknolojia na kiuchumi katika sekta nne ambazo ni Umeme, Gesi Asilia, Mafuta ghafi na Maji.
Kwa mujibu wa tovuti ya Ewura, mamlaka hiyo inaongozwa na dira ya kudhibiti huduma za nishati na maji kwa uwazi, ubora na ufanisi kwa lengo la kukuza uwekezaji na kuboresha ustawi wa kijamii na kiuchumi kwa jamii ya Watanzania, huku ikilenga kuwa mdhibiti wa hadhi ya kimataifa katika huduma ya nishati na maji.
Majukumu yake makuu ni pamoja na utoaji wa leseni, kupitia gharama za bidhaa, kusimamia utendaji na viwango vya ubora, usalama, afya na mazingira.
Mamlaka pia inatarajiwa kuweka viwango vya bidhaa na huduma zinazotolewa, kudhibiti gharama na tozo, kuunda kanuni na taratibu za kusimamia utendaji wa sekta husika.
Katika kutimiza wajibu wake, mamlaka inajitahidi kuhakikisha kwamba, inakuza ushindani bora na ufanisi wa kiuchumi; inalinda maslahi ya watumiaji (walaji); inalinda maslahi ya kifedha ya wasambazaji wenye ufanisi; inahakikisha upatikanaji wa huduma kwa watumiaji wote ikiwa ni pamoja na watumiaji wenye kipato cha chini, wa vijijini na wasiojiweza; inalinda na kuhifadhi mazingira; na inakuza uelewa na ufahamu wa jamii kwa sekta zote nne.
Ewura inaongozwa na mpango mkakati wa miaka minne ambao miongoni mwa malengo yake ni: Kuwa chanzo cha habari na rejea kwa wadau wote ili waweze kufahamu, na kujihusisha katika michakato ya utoaji wa huduma wenye ufanisi; Kuweka mfumo wa kimkakati unaokubalika wa matokeo na malengo ya msingi, kusimamia mipango na utekelezaji wa shughuli na huduma ambazo Ewura inataraji kuzitoa ndani ya kipindi cha utekelezaji; na Kuhakikisha kila kinachopangwa kinatekelezeka.
Mamlaka hiyo inaendeshwa na Mkurugenzi Mkuu ambaye anasimamia uendeshaji wa kila siku. Mkurungezi Mkuu anasaidiwa na wakuu wa idara na vitengo.
Ewura ina vitengo saba ikiwemo: Umeme, Mafuta Ghafi, Gesi Asilia, Maji na mfumo wa Maji Taka, Huduma za Kisheria, Uthibiti wa Uchumi na Ushirikishwaji Jamii.
Kama mamlaka nyingine za serikali, Ewura ina Bodi ya Wakurungezi ambayo mwenyekiti wake anateuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ewura inadhibiti shughuli za gesi ya asili zinazojumuisha usindikaji, usafirishaji, uhifadhi na usambazaji. Miundombinu ya gesi asilia kama mitambo ya kusindika gesi, mabomba ya upitishaji na usambazaji, pia vinadhibitiwa na mamlaka ambayo inaendesha uchunguzi kwenye maeneo husika ambako shughuli hizo zinaendeshwa.
Mamlaka ina mpango wa kuanzisha viwango na alama ya kudhibiti gesi asilia. Kwa sasa, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) halina viwango mahsusi vya gesi asilia, udhaifu ambao unaruhusu kampuni kutumia viwango tofauti nchini.
Hata hivyo, kwa vile Ewura ilishiriki katika utungaji wa Sera ya Taifa ya Gesi Asilia Tanzania ya mwaka 2013, itakuwa rahisi kuanzisha viwango vya udhibiti kwa sekta hiyo kwa sababu sera sasa inatumika.
Hata hivyo, ziko changamoto kadhaa ambazo zinaikumba mamlaka hiyo kama ifuatavyo:
Mfumo wa Sheria: Changamoto ambazo EWURA ilikutana nazo wakati wa utekelezaji wa mpango mkakati wa pili (2008-11) ni pamoja na kutokuwepo kwa sera ya gesi ya asili (iliyopitishwa 2013), na sheria ya mafuta na gesi pamoja na mwongozo mkuu wa sekta ambazo bado ziko katika ngazi ya wizara).
Miundombinu: Usindikaji gesi usiotosheleza, ukosefu wa miundombinu ya kupitisha gesi, na mahitaji makubwa ya nishati ya gesi yanakwaza utumiaji wa gesi asilia. Bomba jipya linalojengwa kutoka Mnazi Bay kuja Dar es Salaam linategemewa kupunguza msukumo wa matumizi ya nishati hii.
Usalama: Kwa mujibu wa EWURA, kuna changamoto kadhaa za kiusalama katika udhibiti wa sekta hii. Hii ni pamoja na kuvamiwa kwa maeneo yanapopita mabomba ya gesi, na uendeshaji wa biashara pembezoni mwa maeneo yanapopita mabomba na kadhalika.

Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco)
Tanesco ni shirika la kiserikali lililo chini ya usimamizi wa Wizara ya Nishati na Madini ambalo linafanya kazi tatu kuu: Uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme kwa watumiaji Tanzania Bara na pia linauza umeme huo Zanzibar.
Historia ya shirika hilo inaanzia wakati wa ukoloni. Kampuni ya kwanza ya umeme ilianzishwa na wakoloni wa Kijerumani mwaka 1908, ambayo ilikuwa inahudumia reli na mji wa Dar es Salaam ambako wakoloni wengi walikuwa wanaishi.
Wakati Tanganyika ilipochukuliwa na Waingereza mwaka 1920, Idara ya Serikali ya Umeme iliundwa kuchukua nafasi ya ile iliyokuwa ya Wajerumani. Mwaka 1931, serikali ilikabidhi shughuli za uzalishaji wa umeme kwa kampuni binafsi. Miongoni mwa kampuni hizo ilikuwa Tanesco iliyoanzishwa Novemba 26, Novemba 1931, kipindi hicho ikijulikana kama “Tanganyika Electric Supply Company Ltd. (Tanesco).”
Kati ya mwaka 1964 na 1975, serikali ya Tanzania ilinunua hisa zote za kampuni ya Tanesco na kuibadilisha kuwa shirika la serikali. Mpaka Juni 17, 2010, Shirika lilikuwa na wafanyakazi wapatao 5,645, huku wanaume wakiwa 4,516 na wanawake 1,129.
Katika uzalishaji wa umeme, Tanesco inategemea umeme wa maji na mvuke. Mwaka 2012, umeme uliozalishwa kwa maji ulichangia asilimia 57 ya umeme wote uliozalishwa huku gesi na mvuke vikichangia asilimia iliyobaki.
Mwaka 2012, idadi ya umeme uliozalishwa ulikuwa kilowati 5,759,756,313, huku Tanesco ikizalisha kilowati 3,110,436,062, na akiba ya kilowati 2,649,320,551 ikizalishwa na wazalishaji huru wa umeme na kutoka nchi jirani za Uganda na Zambia.
Tanesco inasimamia mabwawa saba ya uzalishaji wa nishati ya umeme ambayo ni: Kidatu (inazalisha 204MW); Kihansi (inazalisha 180MW); Mtera (inazalisha 80MW); Pangani (inazalisha 68MW); Hale (inazalisha 21MW); Nyumba ya Mungu (inazalisha 8MW) na Uwemba (inazalisha 0.82MW).
Tanesco pia inamiliki na kusimamia mtambo wa uzalishaji wa nishati ya umeme unaotumia gesi ulioko Dar es Salaam: Ubungo I (unazalisha 100 MW), Ubungo II (unazalisha 105 MW) na Tegeta (unazalisha 45MW) pamoja na mtambo mpya wa Kinyerezi. Mtwara na Lindi pia kuna mitambo inayotumia gesi kuzalisha umeme ambako kwa pamoja Mtwara/Lindi unazalisha 18MW, na Somanga Fungu 7.5MW.
Kwa upande wa usafirishaji, mfumo wa usambazaji wa umeme una vituo vidogo 43 ambavyo vinaunganishwa na laini za kusafirisha umeme. Laini hizo zina vipimo vifuatavyo: Kilometa 2,732.36 za mfumo wa kilovoti 220, kilometa 1,556.5 za kilovoti 132, na kilometa 580 za kilovoti 66, na kufanya jumla yake kuwa kilometa 4,868.86 hadi kufikia Mei 2014. Idadi ya umeme unaoingizwa kwenye gridi ya taifa ni megawati 1,396.24 ukizalishwa kutoka kwenye mabwawa ya maji, mvuke, gesi na mafuta.
Katika usambazaji, Tanesco inasambaza umeme moja kwa moja kwa mteja. Inakadiriwa kwamba zaidi ya asilimia 80 ya mapato ya shirika yanatokana na watumiaji wakubwa wa umeme 1,700 ambao ni asilimia 0.24 ya wateja wote wa shirika nchi nzima. Wateja wakubwa ni wale ambao wanatumia zaidi ya kilowati 7,500 kwa mwezi.
Huduma za shirika zinawafikia wananchi wachache tu. Kwa mujibu wa takwimu kutoka Benki ya Dunia (2011), ni asilimia 15 tu ya wananchi ndio wanapata huduma ya umeme nchini huku maeneo mengi ya vijijini yakiwa giza.
Hata hivyo, mnamo Juni 2014, serikali iliridhia mabadiliko kwenye sekta ya nishati ambayo, pamoja na mambo mengine, yanapendekeza kuligawa shirika na kuanzisha kampuni huru tofauti tatu: Tanesco itabaki na jukumu la usambazaji wa umeme pekee, huku kampuni mpya zitakazoanzishwa zitakuwa na jukumu la uzalishaji na usafirishaji umeme.
Lengo kuu la mabadiliko hayo ni kuongeza ushindani, kuvutia wawekezaji binafsi kwenye sekta ya nishati na kuhakikisha uwepo wa uhakika wa nishati ya umeme nchini.
Serikali imepanga kutumia Dola za Marekani bilioni 1.15 ndani ya miaka 11 ijayo ya utekelezaji wa mabadiliko ya sekta ya nishati.
Kampuni mpya ya uzalishaji umeme itamilikiwa na serikali na itaorodheshwa kwenye soko la hisa la Dar es Salaam (DSE), huku serikali ikiwa na angalau asilimia 51 ya hisa zote.
Wazalishaji wengine wa umeme watashindana kuuza umeme moja kwa moja kwa wasambazaji, na watumiaji wa umeme.
Kampuni za usafirishaji wa umeme zitamilikiwa na serikali na zitasaidia usambazaji wa umeme kutoka kwa wazalishaji kwenda kwa wasambazaji ambao ni kampuni zinazojitegemea. Kampuni hizo ambazo zitakuwa za umma au binafsi, zitauza umeme kwa wateja kwenye maeneo zinakoendesha shughuli zao.
Chini ya mpango huo, uzalishaji wa umeme unatarajiwa kuongezeka kutoka megawati 1,583 za sasa mpaka megawati 10,000 mnamo mwaka 2025, na uunganishaji umeme utaongezeka kwa angalau asilimia 50 huku ufikaji wa umeme kwenye maeneo mbalimbali utakuwa kwa angalau asilimia 75 kwa mwaka 2025.
Tanzania inakuwa nchi ya tatu Afrika Mashariki kuvunja shirika la umeme na kuunda kampuni mbalimbali zenye majukumu tofauti. Mwaka 2009, Kenya ilifanya mabadiliko hayo na kuvutia wawekezaji binafsi. Mabadiliko hayo yalisababisha upatikanaji wa nishati ya umeme kuongezeka.
Mwaka 2015, serikali iliunda kikosi kazi kufuatilia utekelezaji wa mpango huo na kufanya tathmini ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji unaofanywa na Tanesco, hata hivyo, ni muhimu sana kwa serikali kulipa kwanza madeni ya Tanesco ili kurahisisha mafanikio ya mabadiliko yanayopendekezwa.

Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 8 ya mwaka 2005 kama taasisi inayojitegemea chini ya Wizara ya Nishati na Madini.
Kazi kubwa ya REA ni kukuza na kuchochea upatikanaji wa huduma ya nishati ya kisasa kwenye maeneo ya vijijini Tanzania Bara. REA ilianza kazi Oktoba 2007.
Watanzania wengi waishio vijijini hawana nishati ya umeme, hivyo lengo la REA ni kukuza na kusaidia maendeleo ya nishati vijijini kwa kushirikiana na sekta binafsi, taasisi zisizo za kiserikali, taasisi za kijamii, na taasisi za serikali.
Kazi kuu za REA ni: Kukuza, kuchochea, kusaidia na kuimarisha upatikanaji wa nishati ya kisasa kwa ajili ya matumizi ya uzalishaji vijijini kwa lengo la kuchochea maendeleo vijijini; Kukuza uzalishaji na matumizi ya nishati na kubainisha miradi ya nishati na shughuli mbalimbali vijijini; Kufadhili miradi ya nishati vijijini kupitia Mfuko wa Nishati Vijijini; Kuandaa na kupitia taratibu za maombi, miongozo, vigezo vya uchaguzi, viwango na masharti ya utoaji ruzuku; Kujenga uwezo na kutoa msaada wa kitaalamu kwa waendelezaji wa miradi ya nishati na jamii za vijijini; na Kusaidia utayarishaji wa maombi kwa ajili ya miradi ya umeme vijijini.
REA na Mfuko wa Nishati Vijijini vinasimamiwa na Bodi ya Nishati Vijijini ambayo inaundwa na wawakilishi kutoka Wizara ya Fedha; Wizara ya Nishati na Madini; Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Sekta Binafsi; Jumuiya ya Benki Tanzania; Asasi za Kiraia; wadau wa maendeleo na watumiaji wa nishati.
REA inaongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, ambaye ndiye mtendaji mkuu wa taasisi na Mfuko wa Nishati Vijijini huku ikiwa inaundwa na kurugenzi kuu mbili; moja inahusika na masuala ya fedha na utawala na nyingine masuala ya kiufundi.

Wizara ya Fedha Tanzania
Wizara ya Fedha inasimamia mapato yote, matumizi na kugharamia kifedha uendeshaji wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wizara hiyo inatoa ushauri kwa serikali kuhusu masuala mapana ya kifedha kwa lengo la kukuza uchumi na kuimarisha maisha kwa jamii.
Benki kuu ya Tanzania (BoT) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni miongoni mwa taasisi ambazo zinafanya kazi chini ya Wizara ya Fedha. TRA ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 11 ya mwaka 1995, na kuanza kazi rasmi mwaka 1996. Inasimamiwa na sheria na inawajibika kusimamia kodi za serikali kuu. TRA ni wakala unaojitegemea chini ya wizara.
Majukumu ya Wizara ya Fedha ni kuandaa na kuwasilisha bajeti ya taifa kwenye Bunge la Bajeti kila mwaka. Bajeti inayoandaliwa ni mwongozo ambao unaainisha mapato, matumizi, namna ya kugharamia shughuli za serikali kwa mwaka husika. Kwa ujumla, matumizi mbalimbali ya taasisi za serikali yanaamuliwa na wizara hii.
Wizara hiyo pia ina jukumu la ukusanyaji wa mapato kwani baadhi ya kodi na ushuru zinakusanywa na Wizara ya Fedha yenyewe. Wizara na taasisi nyingine za serikali kama Wizara ya Nishati na Madini Tanzania nazo zinakusanya kodi kama ilivyo kodi ya mrahaba kutoka kampuni za gesi na madini pamoja na ada za uandaaji wa ramani za kijiologia.
Wizara ya Fedha inaandaa na kusimamia sera na sheria za mapato zinazowasilishwa bungeni. Wajibu mwingine wa wizara hiyo ni kuandaa sera na sheria ya kodi, na kusimamia ukopaji wa serikali kwenye masoko ya fedha, kuandaa udhibiti wa sera kwa sekta ya kifedha nchini kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania pamoja na kuiwakilisha Tanzania kwenye taasisi za kifedha za kimataifa.
Katika bajeti ya mwaka 2012/2013, serikali iliweka mkazo kwenye uwekezaji wa miundombinu ya nishati, hususan ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Pia, sera mbalimbali ziliandaliwa kwa lengo la kukuza pato la taifa na kukabiliana na gharama kubwa za maisha kupitia uendelezaji wa uzalishaji nishati mbadala kwa kutumia gesi asilia na kutoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye vifaa mbalimbali vinavyotumika kuhifadhi, kusafirisha na kusambaza gesi.
Kwa niaba ya wizara ya fedha, TRA ilitangaza kwamba msamaha wa kodi kwa kampuni za kimataifa zinazojihusisha na utafiti wa gesi asilia na mafuta ulikuwa Dola za Marekani milioni 58.82, sawa na Shs. bilioni 100, ambapo miradi iliyotekelezwa na kampuni zinazomilikiwa na serikali zilipata msamaha wa kodi wa jumla ya Dola za Marekani milioni 86.47, sawa na Shs. bilioni 147.
Wizara ya fedha, kama mdau wa sekta ya mafuta na gesi, itahusika katika uanzishwaji wa mfuko wa taifa katika kipindi ambacho Tanzania inafikiria kuongeza mapato yake kwa Dola za Marekani bilioni 3 kwa mwaka kutokana na ugunduzi wa zaidi ya futi za ujazo trilioni 57 za gesi asilia.
Mfuko wa Mapato wa Gesi Asilia Tanzania umeanzishwa kwa sheria maalumu. Lengo ni kuhakikisha kwamba sheria iliyoanzishwa inajenga mihimili imara ya kitaasisi na utawala wa mfuko husika.
Kwa hiyo, sheria iliyopitishwa mwaka 2015 imeweka wazi muundo na mfumo wa kisheria ambao mfuko huo utachukua, ikiwemo kuweka wazi ushiriki wa taasisi mbalimbali kama vile Benki Kuu ya Tanzania, Wizara ya Fedha na mamlaka yoyote ya ukaguzi wa fedha katika usimamizi wake.
Wizara inafuatilia matumizi ya bajeti kwa mwaka wa fedha na ukiukwaji wa matumizi yaliyopangwa yanaainishwa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu Hesabu za Serikali ambaye anaandaa ripoti ya ukiukwaji huo baada ya mwaka wa fedha kuisha.
Kwenye sekta ya mafuta na gesi, wajibu wa ufuatiliaji huo uko chini ya Wizara ya Nishati na Madini Tanzania, lakini wizara ya fedha, kama mdau, ni sehemu ya mfumo wa uratibu ambao unalenga kuimarisha uwazi na matumizi sahihi ya mapato yatokanayo na sekta hii.

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
TPDC inamilikiwa kikamilifu na serikali chini ya Wizara ya Nishati na Madini. Shirika hilo lilianzishwa chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma Namba 17 ya mwaka 1969 ya Sheria za Tanzania (ilioondolewa na kubadilishwa na Kifungu Namba 257 cha Sheria ya Mashirika ya Umma cha mwaka 2002 cha Sheria za Tanzania), na kupitia Notisi ya Serikali Namba 140 ya Mei 30, 1969. Shirika hilo lilianza shughuli rasmi mwaka 1973.
Kufuatia kuanzishwa kwake, shughuli kuu ya shirika hili ilikuwa kusimamia shughuli za kampuni ya Mafuta ya AGIP - Azienda Generale Italiana Petroli kutoka Italia, ambayo ilikuwa ni kampuni pekee yenye ridhaa ya kuendesha shughuli za mafuta wakati huo.
Baada ya kugunduliwa eneo la Gesi kule Songo Songo, na kufuatia AGIP kuacha shuguli zake, TPDC ikachukua dhima ya kuthibitisha eneo hilo la gesi pamoja na kulifanyia tathmini.
TPDC inaongozwa na mikakati ya “kushiriki na kujiingiza katika utafiti, maendeleo, uzalishaji na ugawaji wa mafuta na gesi na huduma zinazohusiana na hayo; kuweka mazingira mazuri ya biashara, kulinda mgawanyo wa taifa wa mazao ya mafuta ghafi; na wakati huo huo kuendeleza ubora na kiwango cha usalama kwa kulinda watu, mali na mazingira”.
Shirika lishiriki moja kwa moja kwenye utafutaji, uendelezaji, uzalishaji, na usambazaji wa mafuta na gesi na huduma zitokanazo, na kuweka mazingira mazuri kwa biashara, kulinda upatikanaji wa bidhaa za mafuta, na kwa wakati huo huo, kuandaa viwango vyenye ubora ili kulinda watu, mali na mazingira.
Malengo ya Shirika kama yalivyoainishwa katika Mpango wa Uanzishwaji wake wa mwaka 1969, ni pamoja na: Utafiti na uzalishaji wa mafuta ghafi; Kujishughulisha na vifaa vya usambazaji na uhifadhi; Kupata haki za utafiti na uzalishaji; Mkataba, kumiliki hisa au kushiriki katika mikataba ya ridhaa ya mafuta na gesi, haki za uendeshaji shughuli, na leseni; Kusimamia vitengo vyote vya kisheria vilivyowekwa kwa ajili ya shirika; na Kuweka msingi imara wa shughuli katika kazi za mafuta na gesi.
Shughuli za shirika zinajumuisha utafiti, uzalishaji, usafirishaji, usafishaji wa mafuta ghafi, utafutaji masoko, na usambazaji wa bidhaa za mafuta ghafi. Shughuli hizi zaweza kufanywa kwa kujitegemea au kwa ushirikiano na kampuni ya kigeni kupitia Makubaliano ya Kuchangia Uzalishaji (PSAs).
TPDC ina dhima kadhaa, ambazo ni pamoja na; Kukuza maendeleo na uzalishaji wa sekta ya mafuta; Kuendeleza shughuli za uchunguzi, uzalishaji, usafishaji, uhifadhi, utoaji na usambazaji wa mafuta ghafi; Kujihusisha na shughuli za utafutaji petrol (utafiti, utoboaji, majaribio, tathmini, uchimbaji, uzalishaji, usanifishaji, kuhifadhi, usafirishaji, na kadhalika; Kupata, kwa makubaliano, na kushika dhamana katika shughuli yoyote inayohusisha utafiti na uchunguzi kwenye sekta husika; Kusimamia kisheria masuala ya kitengo chochote kinachomilikiwa au kilichokabidhiwa kwa shirika; Kukuza na kusimamia utafiti wa mafuta na gesi; Kuendeleza na kuzalisha mafuta na gesi; Kusimamia utafiti na uendelezaji wa mafuta na gesi; Kusimamia utafutaji na takwimu za mafuta na kesi; na Kutafuta masoko na kuuza gesi asilia chini ya mpango wa Makubaliano ya Kuchangia Uzalishaji.
Shirika lina hisa kwenye kampuni za mafuta kama BP Tanzania Limited, TAZAMA Pipeline Limited, Mafuta House Investment Co. Limited, na hii ni kwa niaba ya Serikali (Msajili wa Hazina).
Shirika pia linasimamia uendeshaji na kumiliki hisa katika miradi ya kuzalisha umeme wa gesi wa Songo Songo na ule wa maendeleo ya gesi wa Mnazi Bay. Kwa vile shirika linamilikiwa na Serikali, hisa zote zinashikiliwa na Msajili wa Hazina.
Kuna changamoto kadhaa zinazolikabili Shirika. Wanasiasa na maofisa wa ngazi za juu serikalini hawafahamu umuhimu wa shirika kufanya kazi kama shirika la kibiashara la taifa la mafuta linalojitegemea.
Shirika halina uwezo wa kisheria kuanzisha, kuhifadhi na kudhibiti vyanzo vyake vya fedha. Pia, jukumu pacha la shirika ni changamoto kwani linafanya kazi ya usimamizi wa sekta ya mafuta na gesi na wakati huo huo linajihusisha kikamilifu kwenye biashara ya mafuta na gesi.
Serikali imeshauriwa kutazama upya muundo wa shirika kwa kulifanya kuwa msimamizi huru wa sekta ya gesi na mafuta, bila kuhusika kwenye biashara ya sekta hizi. Hii itahakikisha uwepo wa utawala bora katika sekta husika kwa kukwepa mgongano wa kimaslahi.


Comments