- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Vitalu vya gesi katika eneo la Bahari Kuu (Offshore).
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
JUMLA
ya leseni 26 zimetolewa kwa kampuni 18 zinazojishughulisha na utafiti wa mafuta
na gesi asilia katika vitalu mbalimbali nchini Tanzania tangu mwaka 2001 hadi
Julai 2014.
Kumbukumbu
zilizopo zinaonyesha kwamba, leseni 23 kati ya hizo ni za utafiti wakati leseni
tatu ni za uendelezaji.
Aidha,
leseni nyingine 22 bado hazijatolewa katika vitalu kadhaa ambapo mbili (katika
Kitalu 4/1B na 4/1c) ziko chini ya uangalizi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC) na vitalu vinne vimeombwa na kampuni ya Shell ya Uholanzi.
Vitalu
hivyo, ambavyo bado havijajadiliwa ni Kitalu Namba 9, Namba 10, Namba 11, na
Namba 12, ambapo mchakato wa kuyapitia maombi hayo unaelezwa kwamba unafanyika
na kuna uwezekano mkubwa kwa Shell kupatiwa vitalu hivyo kwa sababu inakidhi
vigezo vyote.
Shell,
ambayo sasa ndiyo kampuni kubwa iliyowekeza maeneo makubwa zaidi hasa baada ya
kununua hisa nyingi katika kampuni ya BG ya Uingereza ambayo inamiliki vitalu
vingi, ndiyo ilikuwa kampuni ya kwanza kabisa pamoja na BP ya Uingereza kufanya
utafiti katika Tanganyika mwaka 1952 katika maeneo ya Visiwa vya Pemba, Unguja
na Mafia.
Pengine
baada ya kutanua makucha kwa kuinunua kampuni ya BG kutaifanya Shell kuaminika
zaidi na huenda ikafikiriwa kupewa baadhi ya maeneo iliyoomba.
Vitalu
nane kati ya 22 bado zabuni ziko wazi na vinahusisha Kitalu Namba 5 katika maji
ya kina kirefu, Kitalu cha Bonde la Kisangire, Bonde la Ziwa Eyasi Wembere,
Bonde la Mandawa, Kitalu cha Luwegu, Bonde la Ziwa Rukwa Kaskazini (liliachwa
na kampuni ya Heritage), Kitalu cha Selous, na Kitalu cha Tunduru.
Aidha,
leseni nyingine nane ziko katika mzunguko wa sasa wa zabuni na zinahusisha
maeneo ya Kitalu Namba 4/2A, 4/3A, 4/3B, 4/4A, 4/4B, 4/5A, 4/5B pamoja na
Kitalu cha Kaskazini mwa Ziwa Tanganyika.
Leseni za utafiti
Kumbukumbu
zinaonyesha kwamba, leseni tatu zimetolewa kwa kampuni za BG na Ophir kwa
pamoja katika Vitalu Namba 1, 3 na 4 katika maji ya kina kirefu wakati kampuni
ya Dodsal Resources Limited yenyewe ina leseni ya Kitalu cha Bonde la Ruvu na
tayari imegundua akiba kubwa ya gesi asilia.
Kampuni ya Heritage Oil na Petrodel zina leseni mbili katika Vitalu vya
Latham na Kimbiji, lakini Heritage pia ina leseni nyingine mbili katika Bonde
la Rukwa (Kusini) na Bonde la Kyela.
Ndovu Resources ina leseni mbili za utafiti katika Vitalu vya Mtwara na
Kisiwa cha Nyuni wakati Leseni ya utafiti katika Visiwa vya Pemba na Unguja
imepewa kampuni ya Atrim Resources huku Jacka Resources ikiwa na leseni katika
Bonde la Ruhuhu na Beach Petroleum ikimiliki leseni ya Kusini mwa Ziwa
Tanganyika.
Swala Energy ina leseni mbili za Bonde la Pangani na Kilosa, Dominion
Petroleum ina leseni ya Kitalu Namba 7 katika maji ya kina kirefu, Maurel et
Prom ina leseni za Bigwa wilayani Mkuranga na Mafia, Ophir ina leseni ya East
Pande, Motherland Industries ina leseni ya Bonde la Mto Malagarasi na Mnazi Bay
Kaskazini leseni iko chini ya kampuni ya Hydrotanz.
Kampuni ya Afren na Petrodel zina leseni moja katika Kitalu cha Bonde la
Tanga, Petrobras na Shell kwa pamoja zina leseni ya Vitalu Namba 6 na 8, wakati
Statoil na ExxonMobil kwa pamoja zinamiliki leseni ya Kitalu Namba 2.
Leseni za uendelezaji
Maeneo
yanayozalisha gesi nchini Tanzania ni machache na ilichukuwa miaka mingi kuanza
uzalishaji huo kutokana na matatizo ya miundo mbinu, kukosekana kwa soko la
ndani, na kushindikana kusafirisha gesi nje ya nchi kutokana na akiba ya gesi
kuwa kidogo.
Eneo la uzalishaji
la Songo-Songo, ambalo linasimamiwa na kampuni ya Pan African Energy, kwa sasa
linazalisha gesi asilia yenye akiba ya ujazo futi milioni 110 kwa siku. SongoSongo imekuwa ikizalisha gesi
tangu mwaka 2004. Gesi inayozalishwa SongoSongo inachangia kuzalisha kiasi
kikubwa cha umeme unaotumika kwenye viwanda na kwa wateja wa kawaida katika
jiji la Dar es Salaam.
Eneo la uzalishaji
la Mnazi Bay lilianza uzalishaji wa gesi Januari 2007 kupitia bomba lenye urefu
wa maili 17 kwenda kwenye kituo cha kuzalisha umeme wa megawati 12 kilichopo
Madimba, Mtwara.
Mnazi Bay
inasimamiwa na kampuni ya Maurel et Prom, Wentworth Resources na Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Septemba 12, 2014,
kampuni hizo zilitiliana saini makubaliano ya kuuziana gesi na serikali kwa
lengo la kupeleka futi za ujazo milioni 130 za gesi asilia kwenye bomba jipya
la gesi linalotoka Mnazi Bay kwenda Dar es Salaam. Bomba hilo ambalo linamilikiwa
na serikali, limeanza kutumika mwaka 2015.
Eneo la Kiliwani Kaskazini nalo limeanza uzalishaji
wake wa kwanza tangu Aprili 4, 2016 na Ndovu Resources ndiyo yenye leseni hiyo.
Gesi ya kwanza ilichimbwa katika kisima cha Kiliwani North-1, eneo ambalo liko
jirani na eneo la Songo Songo, ambako gesi itakayopatikana huko itasafirishwa
hadi katika mtambo wa kuchakata gesi wa Songo Songo.
Uzalishaji huo umeanza kwa kuzalisha futi za ujazo
kati ya milioni 25-30 kwa siku katika siku 90-100 za kwanza kabla ya kuanza
uzalishaji mkubwa, ambapo kwa mujibu wa taarifa ya kampuni hiyo, gesi hiyo
itauzwa kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa bei kama
inavyoelekezwa katika Mkataba wa Uuzaji wa Gesi uliosainiwa na pande zote
mbili.
Utoaji wa leseni
Leseni
zote hizo zimetolewa kwa awamu tangu mwaka 2001 ambayo ndiyo ilikuwa awamu ya
kwanza kabisa. Utoaji huo wa leseni
wa kwanza wa utafiti na uzalishaji wa gesi na mafuta ulitangazwa Juni 2000 na
kufungwa tarehe 19 Aprili 2001. Ulifanyika jijini London, Uingereza.
Vitalu sita (6)
vilivyokuwa kwenye kina cha maji kati ya mita 200 na 2,000 ndani ya mwambao
vilinadiwa, lakini ombi moja tu kutoka kampuni ya Petrobras ndilo
lililopokelewa. Hatimaye, kampuni ya Petrobras ilipewa Mkataba wa Kuchangia
Uzalishaji wa kitalu namba 5.
Awamu ya pili ya utoaji wa leseni ilifanyika Houston, Texas, Marekani
ambapo zabuni zilifunguliwa Juni 3, 2001 na kufungwa Julai 5, 2002.
Katika awamu hiyo, vitalu saba (7) vilivyokuwa kwenye kina cha maji kati ya
mita 200 na 2,000 baharini, kikiwemo kimoja kilichokuwa kwenye maji yenye kina
kifupi zaidi kusini mwa Zanzibar, na sita (6) kwenye kina kirefu cha maji
pembeni mwa kisiwa cha Pemba na Unguja vilinadiwa. Eneo hili lilichukua ukubwa
wa kilometa za mraba 114,123.
Maombi mawili yalipokelewa kutoka kampuni ya Shell International na Global
Resources. Kampuni zote ziliomba vitalu namba 9-12. Kamati ya wataalamu kutoka
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na Wizara ya Nishati na
Madini ilibaini ombi la kampuni ya Global Resources kuwa halikidhi masharti kwa
kuwa halikuonesha ushahidi wa uwezo wa kifedha wala uzoefu wa utafutaji wa gesi
na mafuta ndani ya bahari. Shell bado inasubiri uamuzi baada ya kuomba tena
zabuni hiyo ilipoitishwa, na ina nafasi kubwa ya kushinda kwenye vitalu vyote –
namba 9-12.
Ufunguzi wa zabuni katika awamu ya tatu ulitangazwa Mei 2004 na kufungwa
Mei 2005. Ufunguzi ulifanyika
Denver, Colorado, Marekani na ulihusisha eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba
71,103.
Leseni za vitalu saba (7) vilivyokuwa kwenye kina cha maji kati ya mita
200-2,000 zilinadiwa, na vitalu vitatu (3) – kitalu namba 1, 2 na 6 –
vilitolewa. Kitalu namba 1 kilitolewa kwa kampuni ya Ophir Energy, kitalu namba
2 kwa kampuni ya Statoil na kitalu namba 6 kwa kampuni ya Petrobras.
Mwezi Aprili 2006, leseni za vitalu namba 3 na 4 zilitolewa moja kwa moja
kwa kampuni ya Ophir Energy na serikali.
Mwezi Julai 2006, serikali ilitangaza zabuni kwa ajili ya vitalu viwili
vilivyokuwa vimebaki kwa wakati huo na mnamo Januari 19, 2007, leseni ya kitalu
namba 7 ilitolewa kwa kampuni ya Dominion Petroleum na kitalu namba 8 kwa
Petrobras.
Utoaji wa leseni awamu ya nne ulizinduliwa rasmi Oktoba 25, 2013 wakati wa
mkutano na maonyesho ya pili ya sekta ya gesi na mafuta Tanzania.
Zoezi hilo lilipaswa kufanyika Septemba 2012, lakini lilicheleweshwa
kutokana na kusubiriwa kupitishwa kwa Sera ya Taifa ya Gesi Asilia Tanzania.
Awamu hii ilifungwa Mei 15, 2014 na ilihusisha eneo la mwambao Kaskazini
mwa Ziwa Tanganyika na vitalu saba (7) vya baharini kwenye kina cha maji kati
ya mita 2,000 na 3,000.
Vitalu hivyo vinatofautiana ukubwa kutoka kilometa za mraba 2,545 mpaka
zaidi ya 3,600, na vipo mashariki na karibu na maeneo ambayo yameshagundulika
kuwa na gesi.
Vitalu vingine viwili (2) viliachwa kwa ajili ya TPDC, na inatafuta
mshirika kupitia njia ya ushindani ili kuendesha utafiti kwenye vitalu hivyo.
Miongoni mwa vitalu hivyo, vinne viliombwa: Kitalu namba 2A kiliombwa na
kampuni ya Mubadala Petroleum; kitalu namba 3A na China National Offshore Oil
Corporation (CNOOC Ltd), Statoil kwa kushirikiana na ExxonMobil nao walikiomba;
Kitalu namba 3B na Gazprom; na kitalu cha kaskazini mwa Ziwa Tanganyika
kiliombwa na Ras Al Khaimah Gas LLC (Rakgas).
Vitalu vinne (4) vya baharini 4A, 4B, 5A and 5B, havikuombwa.
Kampuni za BG Group na Ophir Energy, ambazo zimekuwa zikiendesha shughuli
zao za utafutaji wa gesi asilia nchini, hazikuwasilisha maombi yao.
Maombi yaliyowasilishwa yanapitiwa na TPDC kuhakikisha kwamba yametimiza
vigezo na masharti yaliyowekwa na serikali. Waombaji watakaofanikiwa watakutana
na TPDC na serikali kujadiliana vipengele vya Mkataba wa Kuchangia Uzalishaji.
Imeandaliwa na www.maendeleovijijini.blogspot.com.
Simu: +255 656 331974
Comments
Post a Comment