Featured Post

HIVI NDIVYO MAPATO YA MAFUTA NA GESI ASILIA YATAKAVYOSIMAMIWA TANZANIA


KATIKA kuhakikisha sekta ya mafuta na gesi asilia inawanufaisha Watanzania wa sasa na kizazi kijacho, Serikali imeunda mfuko maalum wa kusimamia mapato ya gesi asilia.
Mfuko huo wa Mapato ya Gesi Asilia (NGRF) ni Mfuko wa Rasilimali (Sovereign Wealth Fund) wa Serikali ya Tanzania ulioanzishwa mwaka 2015.

Kwa kuanzisha mfuko huo, Tanzania imefuata mfano wa nchi zaidi ya 20 ambazo hadi kufikia Agosti 2013 zilizindua aina tofauti za miundo ya mifuko hiyo inayoshughulikia mapato ya fedha yatokanayo na shughuli za uchimbaji.
Nchi kama Norway yenye watu 5,214,900 tu, idadi ambayo ni sawa na wakazi wote wa Dar es Salaam, ilianzisha mfuko wa aina hiyo unaoitwa Government Pension Fund-Global) tangu ilioanza uzalishaji wa mafuta katika miaka ya 1960 kwa lengo la kulinda rasilimali hizo ili zinufaishe kizazi kijacho.
Mpaka sasa, Norway ina akiba ya Dola 900 milioni (takriban Shs. trilioni 1,939) kwenye mfuko huo, ambapo kwa idadi ya watu waliopo nchini humo, ni sawa na kusema kila raia anamiliki kiasi cha Dola 173,077 (Shs. 373,028,000).
Ingawa sheria inaruhusu serikali kuchukua asilimia 4 ya fedha hizo ili kufanya shughuli nyingine za maendeleo, hususan uwekezaji, lakini kutokana na kujimudu kiuchumi, ni mwaka jana tu ndipo Norway ilipanga kuchukua kiasi ili kuwekeza.
Uanzishwaji wa mfuko huo nchini Tanzania ulipendekezwa kwenye Sera ya Taifa ya Gesi Asilia ya Tanzania iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini Tanzania na ikapitishwa na Baraza la Mawaziri mwezi Oktoba 2013. 
Kwa mujibu wa sera, mfuko huo (NRGF) umeundwa kwa lengo la kuhakikisha kuwapo kwa uwazi na uwajibikaji kuhusu ukusanyaji, ugawaji, matumizi na usimamizi wa mapato ya Gesi Asilia
Sera hiyo inasema kwamba, miongozo iliyo wazi itaandaliwa kwa uwazi au kupitia mazungumzo ya kitaifa kwa matumizi makuu ya muda mfupi na ya muda mrefu ya mfuko huo. 
Aidha, sera inasisitiza kwamba usimamizi wa matumizi ya mfuko wa mapato ya gesi asilia lazima uendane na mipango na mikakati ya maendeleo ya taifa. 
Kimsingi, mfuko unatarajiwa kushika dhamana ya mapato yatakayopatikana kutokana na shughuli za gesi kwa ajili ya uwekezaji katika sekta nyingine, pamoja na kutoa fedha katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kuzingatia akiba kwa ajili ya vizazi vijavyo. 
Pamoja na kuanzishwa mfuko huo, kutakuwa na majadiliano ya kila mwaka bungeni kuhusu sehemu ya mapato ya gesi asilia itakayoingizwa kwenye bajeti ya taifa.
Mfuko utasimamiwa na kuendeshwa na Benki Kuu ya Tanzania na utafanyiwa ukaguzi wa kimahesabu na kitengo maalum cha serikali ya Tanzania kilichotegemewa kuanzishwa mwaka 2015 ili kusimamia mapato ya mali asili.
Kama ilivyoelezwa katika makala zilizotangulia, Tanzania imekuwa ikifanya tafiti kuhusu upatikanaji wa gesi kwa zaidi ya miaka 60 sasa ambapo ugunduzi wa kwanza wa gesi asilia ulifanyika katika Kisiwa cha Songo Songo mwaka 1974 ukifuatiwa na ugunduzi mwingine kule Mnazi Bay mwaka 2006. 
Tangu mwaka 2010, kumekuwa na ugunduzi mkubwa wa gesi wa maeneo ya ufukweni na mbali ya fukwe, maendeleo ambayo yaliamsha swali moja la msingi nalo ni jinsi gani serikali itasimamia sekta hiyo ya gesi asilia inayokua kwa kasi nchini.
Suluhisho pekee lilikuwa ni kuandaliwa kwa sera ya taifa kuhusu gesi asilia, ambayo ilipitishwa na Baraza la Mawaziri Oktoba 10, 2013.
Sera hiyo ambayo imeandaliwa kwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12-2015/16), Mpango wa Taifa wa Kukuza na Kupunguza Umasikini (Mkukuta, 2010 - 2015), na sera za sekta mbalimbali, imejikita katika mihimili mitano.
Mihimili hiyo ni, Kuhakikisha serikali na raia wanafaidika kwa kiasi kikubwa kutokana na sekta ya gesi; Kukuza na kuimarisha mfumo wa usimamizi na rasilimali watu katika sekta ya gesi; Kuimarisha Uwazi na Uwajibikaji; Kutengeneza mfumo makini wa udhibiti majanga, kukinga na kulinda afya ya wananchi, usalama na mazingara; na Kuingiza sekta ya gesi katika uchumi mpana kwa lengo la kubadilisha hali ya kijamii na kiuchumi.
Yapo malengo 15 mahsusi yanayoongoza sera hiyo, miongoni mwayo ni; Kuendeleza miundombinu ya kushughulikia gesi asilia, kurahisisha usafirishaji wa gesi kwa kuifanya kimiminika, usafirishaji wa gesi, uhifadhi na usambazaji; kuhakikisha mapato yatokanayo na gesi asilia yanasimamiwa kwa uwazi, kuimarisha ufanisi, kuimarisha uhusiano kati ya sekta ya gesi na sekta nyingine za kiuchumi, kuhakikisha kuwa serikali na wananchi wana utaalamu wa kutosha kushiriki kwa ufanisi katika mlolongo wa thamani kwenye sekta ya gesi asilia, kuimarisha, kuthibiti na kutathmini uwazi na uwajibikaji katika shughuli za gesi asilia; na kusimamia kwa ufanisi matarajio ya wananchi kuhusu faida itokanayo na shughuli hiyo.
Ingawa sekta ya gesi asilia inahusisha awamu tatu ambazo ni Utafiti na Uzalishaji; Usafirishaji na Uhifadhi; na Usafishaji wa gesi, sera hiyo imejikita katika Usafirishaji, na Usafishaji wa gesi huku eneo la Utafiti na Uzalishaji litasimamiwa na sera nyingine tofauti.
Hatu hiyo, kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya gesi, inaonekana kuiweka nchi katika upande wa hasara kwani kujumuisha shughuli za utafiti na uzalishaji katika sera kungeliwezesha Taifa na wananchi kushiriki na kufaidika na gesi asilia tangu hatua ya awali kwani utafiti na uzalishaji ndiyo hatua ya mwanzo kabisa.
Serikali imekwishasema kwamba, haina mpango wa kuchukua fedha zote ambazo zimetokana na sekta ya gesi na kuziweka Hazina kama ilivyokuwa katika sekta ya madini.
Mapato yatokanayo na gesi asilia yatawekwa kwenye mfuko maalumu na ni jukumu la Watanzania kuamua kipaumbele cha matumizi ya mapato hayo, utaratibu ambao utarahisisha wananchi kuhusisha moja kwa moja maendeleo yao na ya nchi na gesi asilia. 
Ili kuhakikisha usimamizi mzuri na wenye ufanisi katika sekta ya gesi asilia, sera imependekeza kuongeza nguvu kwenye mfumo wa kifedha, kisheria na kiudhibiti. 
Hali hiyo ndiyo iliyofanya itungwe Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Gesi Asilia ya mwaka 2015, lakini pia sheria nyingine maalum zikatunga ama kurekebishwa, ikiwemo Sheria na Kanuni za Gesi Asilia, Sheria ya Kodi ya Mapato (Cap. 332) na Sheria ya Ewura (Cap. 414).
Sera inatambua umuhimu wa wahusika wakuu katika kusimamia, kudhibiti, na kutathmini sekta ya gesi nchini ili kuleta matokeo chanya kwenye sekta hiyo.
Sera inataja Serikali Kuu, Mamlaka ya Serikali za Mitaa, TPDC, Mamlaka ya Udhibiti, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Sekta Binafsi, Taasisi za Elimu na Utafiti, Vyombo vya Habari, Taasisi za Kijamii na Jamii, kama taasisi za msingi katika usimamizi wa sekta hiyo.
Pamoja na uwepo wa rasilimali nyingi za asili, kuongezeka kwa ugunduzi wa gesi na mafuta pamoja na kuongezeka kwa uwekezaji kwenye sekta hiyo, ukuaji mdogo wa uchumi na kuongezeka kwa umaskini imekuwa ndiyo taswira ya nchi za Afrika ambazo zimejaaliwa kuwa na rasilimali za asili.
Ili kuhakikisha kwamba mapato yatokanayo na mafuta, gesi na madini yanawanufaisha wananchi na kuepukana na kinachojulikana kama ‘laana ya rasilimali za asili’ (resource curse), jitihada za kutungwa kwa sera ya kuwawezesha na kuwashirikisha wazawa kwenye nchi mbalimbali zenye rasilimali hizo zimeshika kasi.
Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zenye rasilimali hizo, imepisha sera ya kuwawezesha wazawa kwenye sekta ya gesi na mafuta ya mwaka 2014.
Kuna maelezo mengi kuhusu dhana ya Uwezeshaji na Ushirikishaji Wazawa, lakini Sera ya Uwezeshaji na Ushirikishaji Wazawa ya Tanzania inayohusu Mafuta na Gesi ya mwaka 2014, ina tafsiri ‘Uwezeshaji na Ushirikishaji’ kama “faida inayopatikana ndani ya nchi kwenye shughuli za mafuta na gesi kupitia ushiriki na uendelezaji wa wazawa (Watanzania) na biashara zao kupitia ajira, teknolojia, bidhaa, huduma, mitaji na kukuza uwezo wa kitafiti kwenye sekta. ”
Aidha, Sera inaongeza kwamba ushiriki wa biashara za Watanzania unaweza kutekelezwa kupitia: Uendelezaji wa wataalamu, ajira na mafunzo kwa Watanzania, uwekezaji katika usambazaji wa huduma na bidhaa kwa lengo la kushawishi kampuni zinazoendesha shughuli zao kwenye sekta ya mafuta na gesi nchini kufanya manunuzi yao nchini.
Kwa ujumla, katika sekta ya mafuta na gesi, uwezeshaji na ushirikishaji wazawa ni jitihada ya serikali kuhakikisha kwamba bidhaa na huduma nyingi zinazohitajika kwenye mnyororo wa uzalishaji zinapatikani kwenye nchi husika ambako shughuli ya uchimbaji inafanyika, na si nje ya nchi.
Sera ya Uwezeshaji na Ushirikishaji Wazawa ya mwaka 2014 inalenga maeneo makuu matatu ambayo ndiyo msingi wa kufanikisha uwezeshaji na ushirikishaji wa Watanzania kwenye sekta ya mafuta na gesi.
Maeneo hayo ni Kuandaa mikakati ya utekelezaji wa uwezeshaji na ushirikishaji wazawa kwa nia ya kuzalisha wafanyakazi wa kutosha wenye ujuzi na maarifa; Kuandaa mikakati mahsusi ya kukuza usambazaji wa teknolojia na maarifa kutoka nje ya nchi, pamoja na kuwekeza kwenye eneo la utafiti na uendelezaji kwenye sekta ya mafuta na gesi; na Kuweka mfumo ambao utawawezesha watanzania na biashara zao kutumia kikamilifu fursa kusimamia, kusambaza bidhaa, huduma na utaalamu wao kwenye sekta ya mafuta na gesi.
Ili kutimiza hayo, pamoja na mambo mengine, sera hiyo inatarajia taasisi za serikali na kampuni za gesi na mafuta kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha uwepo wa kutosha wa Watanzania wenye ujuzi na utaalamu ambao ni muhimu katika kutekeleza na kutimiza malengo ya sekta ya mafuta na gesi.
Kwa mujibu wa sera hiyo, kuna maeneo makuu matano (5) ya kusimamiwa kwenye sekta ya mafuta na gesi nchini, ambayo ni, Kukuza uwezo wa Watanzania na uhamishaji wa teknolojia kutoka nje; Ushiriki wa Watanzania na kampuni za Kitanzania; Manunuzi na matumizi ya bidhaa na huduma za Tanzania; Uzalishaji wa bidhaa ndani ya nchi; na Manufaa ya kiuchumi na kijamii yatokanayo na sekta ya mafuta na gesi.
Lengo kuu la sera hiyo ni kutoa miongozo kufanikisha ushiriki wa hali ya juu kwenye uwezeshaji na ushirikishaji wa Watanzania katika maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi ili kuhakikisha Watanzania wanafaidika vema kutokana na uwekezaji kwenye mafuta na gesi.
Malengo hayo mahsusi ni Kuimarisha biashara za Watanzania ili ziweze kushindana kwa kuwawezesha wafanyabiashara wazawa kuweza kukidhi mahitaji ya sekta ya mafuta na gesi; Kutafuta teknolojia kutoka nje ya nchi kwa lengo la kuongeza tija katika usimamizi wa sekta ya mafuta na gesi; Kuwezesha taasisi za elimu nchini kutoa mafunzo sahihi kwa ajili ya sekta ya mafuta na gesi.
Malengo mengine ni Kuhakikisha Watanzania – wenye ujuzi na wasio na ujuzi – wanashiriki kikamilifu kwenye shughuli zote za sekta ya mafuta na gesi; Kuongeza thamani kwenye bidhaa za mafuta na gesi na kutengeneza ajira kupitia kampuni za wazawa kwenye sekta ya mafuta na gesi; Kuhakikisha kampuni za gesi na mafuta zinafanya manunuzi ya bidhaa na huduma za Tanzania kwa mujibu wa masharti ya leseni zao; na Kuimarisha masuala ya kijinsia kwenye sekta ya mafuta na gesi na kushughulikia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi na UKIMWI pamoja na magonjwa mengine ya kuambukizana.
Chini ya Sheria ya Petroli (Utafiti na Uzalishaji) Tanzania ya 1980, maombi ya utafiti au uendelezaji wa rasilimali sharti yajumuishe mapendekezo kuhusu mafunzo na ajira kwa Watanzania. 
Hata hivyo, Sera ya Nishati Tanzania ya 2003 pia inaelezea masuala yanayohusu uwezeshaji wa ushirikishaji wa Watanzania kwenye sekta ya gesi na mafuta, n msisitizo mkubwa umewekwa kufanikisha uwezeshaji na ushirikishaji.
Ukiondoa sheria na sera tajwa hapo juu, mwongozo wa Makubaliano ya Kuchangia Uzalishaji pia umeainisha kwenye ibara ya 20 na 21 umuhimu wa uwezeshaji na ushirikishaji wa Watanzania, na unapitiwa mara kwa mara kuhakikisha unaendana na maendeleo ya kisekta.
Mwongozo huo wa 2013 una maelekezo ya namna ya kuwawezesha na kuwashirikisha wazawa.
Kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya 1980, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, kwa niaba ya Wizara, ndilo lenye wajibu wa kusimamia utekelezaji wa vipengele vinavyohusu uwezeshaji na ushirikishaji wa Watanzania vilivyoko kwenye mwongozo wa Makubaliano ya Kuchangia Uzalishaji.
Waziri wa Nishati na Madini, kwa mujibu wa sera na sheria husika, anatakiwa kushauriana na taasisi za serikali zinazohusika na sekta ya mafuta na gesi ili kupendekeza namna bora ya kushawishi kampuni za kigeni kuendeleza uwezo wa kiteknolojia na ujuzi wa Watanzania na kampuni za Kitanzania kuanzisha viwanda na vitengo vya uzalishaji. 
Sera hiyo pia inapendekeza uanzishwaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Petroli na Kamati huru ambayo itasimamia utekelezaji wa sera hiyo.
Sera imeanzisha kamati ya kitaifa ambayo imepewa wajibu wa kuratibu na kusimamia utekelezaji kamili wa sera hiyo ambapo kazi ya kamati hiyo ni “kusimamia, kuratibu, na kufuatilia utekelezaji wa sera kwa kushirikiana na taasisi na wasimamizi mbalimbali wa sekta; itapitia, kuchambua na kupitisha kwa ajili ya utekelezaji mipango ya kuwezesha na kushirikisha watanzania (ikiwemo ya biashara, mitaji, manunuzi, uagizaji wa bidhaa/mahitaji nje, ajira na mkakati wa kuwawezesha watanzania kushika nafasi za uongozi kwenye kampuni za mafuta na gesi, na kukuza uwezo wa watanzania), kupitia ripoti zinazowasilishwa na waendeshaji pamoja na kushirikiana na sekta binafsi kuwawezesha watanzania kutumia fursa zilizopo kikamilifu.”
Kamati inapaswa kuwa chini ya uenyekiti wa Wizara ya Nishati na Madini, na itakuwa na wajumbe kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Biashara na Viwanda, Mwanasheria Mkuu, Wizara ya Fedha, Wizara ya Kazi na Ajira, Ofisi ya Raisi – Kitengo cha Sera, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mamlaka ya Manunuzi Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Wizara ya Mambo ya Ndani – Uhamiaji, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), na Wawakilishi wawili kutoka asasi za kiraia.
Kimsingi, uafiti na uzalishaji wa mafuta ghafi nchini Tanzania unasimamimiwa na Sheria ya Petroli (Utafiti na Uzalishaji) ya mwaka 1980 (Fungu 328 R.E. 2002), ambayo inatumika Tanzania Bara na Visiwani. 
Sheria hiyo ilitungwa kufuatia ugunduzi wa gesi katika kisiwa cha Songo Songo miaka ya 1970, wakati huo Tanzania ilikuwa imefanya ugunduzi kidogo wa gesi ukilinganisha na futi za ujazo trilioni 57 za sasa.
Sheria imeweka mambo makuu kama masuala ya utawala yanayohusiana na utoaji wa leseni za utafiti, uwezo wa usimamizi kwa wizara, haki na wajibu wa wanaopewa leseni.
Kwa upande mwingine, inaeleza haki za watu wanaoathirika au kupata usumbufu katika michakato ya utafiti na uendelezaji na pia jinsi ya kutatua migogoro na kubainisha gharama zinazohusiana na utafiti na uendelezaji.
Sheria hiyo inaunda Ofisi ya Kamishna anayeshughulikia masuala ya Petroli, ambaye anateuliwa na Rais. 
Hata hivyo, kamshina amepewa mamlaka ya kisheria kuchagua mtu yeyote kuwa ofisa aliyepewa mamlaka ya kumsaidia katika utekelezaji wa sheria hiyo. 
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), japo halitajwi moja kwa moja katika sheria hiyo, lina malengo ambayo yanahusika moja kwa moja na utekelezaji wake wakati ambapo Ofisi ya Kamishna inayohusika na masuala ya Petroli na TPDC kwa pamoja zinatekeleza majukumu ya Wizara ya Nishati na Madini.
Sheria inaeleza kwamba hakuna anayeruhusiwa kuendesha utafiti au uendelezaji wa shughuli za petroli bila ya kuwa na leseni ambazo chini ya sheria hiyo zinatolewa kwa watu binafsi ambao ni raia wa Tanzania, au kampuni zilizosajiliwa nchini Tanzania chini ya Sheria ya Makampuni au sheria nyingine yoyote isiyokuwa hiyo ya kampuni. 
Maelekezo yanayopatikana katika leseni za utafiti na uendelezaji yanajumuisha tarehe ya kutolewa, eneo la utafiti, utekelelezaji na masharti, na Sheria pia inazungumzia utaratibu wa kurejesha, kuhamisha, kusitisha na kusimamisha leseni.
Sheria imeweka wazi utaratibu wa kutatua migogoro ambapo Kamishna amepewa uwezo wa kutoa uamuzi kuhusu migogoro inayotokea au inayohusiana na watu wanaoendesha shughuli za utafiti na uendelezaji.
Wenye kutoridhika na uamuzi au maelezo yatolewayo na Kamishna, wamepewa nafasi ya kukata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania ndani ya siku 60 baada ya uamuzi wa kamishna kutolewa.
Sheria imempatia Waziri uwezo wa kutunga kanuni na taratibu ili kurahisisha utekelezaji wa sheria hiyo, lakini ni kanuni na taratibu chache zilizotungwa, hali ambayo ni changamoto.
Kwa kuwa sheria hiyo ilitungwa wakati ambao ugunduzi wa gesi ulikuwa mdogo sana kulinganisha na akiba kubwa iliyopo sasa, kuna ulazima wa kuwa na sheria itakayosimamia sekta ya gesi ili kuweka miongozo inayoeleweka katika sekta hiyo ambayo itashughulikia masuala muhimu yanayoibuka kutokana na kukua kwa sekta husika.



Comments