- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega,
Mpwapwa
"HAPA kwetu hakuna matukio ya mimba kwa wanafunzi, labda kama wanatoa huko kabla ya kugundulika shuleni," ndivyo anavyodokeza mmoja wa walimu wa Shule ya Msingi Malolo katika wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.
Anaongeza: "Tutawezaje kuwagundua watoto kama wana mimba au la wakati hakuna mwalimu wa kike hapa? Ni vigumu kwa mwalimu wa kiume kumchunguza mtoto wa kike."
Shule hiyo yenye wanafunzi 386 (wavulana 189 na
wasichana 197) haina walimu wa kike kwa
zaidi ya miaka 30, hali inayoleta changamoto kubwa hasa kwa watoto wa kike.
Uchunguzi umebaini kwamba, licha ya changamoto nyingi
zinazoikabili shule hiyo iliyo katika Kata ya Malolo, tatizo la uhaba wa
walimu, hususan wa kike, limekuwa sugu kiasi cha kuleta mazingira magumu kwa
wanafunzi wasichana ambao wameshindwa kupata elimu ya hedhi.
“Kukosekana kwa walimu wa kike ni changamoto kubwa, kwa
sababu wasichana wengi wanapevuka mapema tangu wakiwa darasa la tano, hivyo
wanaposhindwa kupewa elimu ya namna ya kujihifadhi wengi huamua kubaki nyumbani
na kukosa masomo mpaka wanaporejea katika hali ya kawaida,” amedokeza mwalimu mwingine ambaye hakupenda kutajwa kwa kuwa si msemaji.
Mwalimu huyo amesema kwamba, ni vigumu kwa walimu wa kiume
kuzijua changamoto za watoto wa kike, lakini kama wangekuwepo walimu wanawake
ingekuwa rahisi hata kuwapatia elimu ya afya pamoja na suala zima la uhusiano
ili kuepusha mimba za utotoni.
Aidha, amedokeza kwamba, ingawa shule hiyo haina rekodi za
mimba, lakini ni muhimu ikiwa wanafunzi hao wakapatiwa uelewa ili waweze
kujitunza.
“Mwalimu wa kike ndiye anayeweza kuwanasihi kwa kina kwa
sababu ya uzoefu alionao kama mwanamke, anaweza kuwaelimisha hata namna ya
kujitunza wanapokuwa katika hedhi, lakini ni vigumu kwa sisi wanaume kuketi na
watoto wa kike na kuanza kuwaelewesha suala hilo kwa ufasaha,” alisema.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Boniface Massawe, alikiri kwamba
ukosefu wa walimu wa kike ni changamoto kubwa kwa wanafunzi wasichana ambao kwa
mazingira ya vijijini, wengi wao wanapokuwa kwenye hedhi hujihisi kama wagonjwa
na baadhi hutega masomo kwa kuwa hawajui jinsi ya kujihifadhi.
“Tuko walimu saba tu, wote wa kiume, na sijawahi kusikia
kama alikuwepo mwalimu wa kike kwa miaka ya karibuni,” alisema Mwalimu Massawe.
Takwimu zinaonyesha kwamba, Wilaya ya Mpwapwa ina jumla ya
walimu 1,283 ambapo kati yao 670 ni wanaume na 583 wanawake.
Bosco Paulo Mwaluga ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji ambaye pia
anakaimu nafasi ya Ofisa Mtendaji wa Kata ya Malolo, ambaye anabainisha kwamba
kukosekana kwa walimu wa kike kunaleta ugumu wa kutambua hata watoto wanaopata
ujauzito ingawa anasema hakuna kesi zozote za mimba.
“Kesi za mimba hakuna, kwa sababu ni lazima kuwepo na
ushahidi… ingewezekana kuwagundua watoto waliopewa ujauzito kama wangekuwepo
walimu wa kike,” anasema.
Ofisa Mtendaji huyo anasema, tetesi kadhaa zimewahi kuwepo
kuhusu baadhi ya wanafunzi wa kike kuwa na ujauzito, lakini hakuna
iliyothibitishwa.
“Mwaka jana kulikuwa na tetesi kwamba watoto wawili walikuwa
na mimba, lakini baada ya uongozi wa shule kuwapeleka kupima walikutwa hawana,
inawezekana kabisa wazazi ama jamaa zao waliwatoa mimba hizo kwa sababu mpaka
mwanamume uone dalili kwamba huyu ana mimba, maana yake mama wa watoto tayari
watakuwa wamegundua mapema na kuchukua hatua hata za kutoa mimba hizo.
“Ingekuwa rahisi kugundua mapema kama wangekuwepo walimu wa
kike maana wao wanazijua dalili tangu mapema,” anasema Bosco.
Uhaba wa walimu
Shule hiyo ni moja kati ya shule tatu za msingi katika Kata
ya Malolo ambapo nyingine ni Idodoma na Nzugilo, ambazo zote zimekuwa
zikikabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu bila kujali jinsia.
Mwalimu Massawe anasema kwamba, kwa miaka mitatu iliyopita
shule hiyo ilikuwa na walimu wanne baada ya mmoja kwenda kusoma, ambapo mzigo
wa ufundishaji ulikuwa mkubwa na hivyo kukwamisha maendeleo ya kitaaluma.
“Mimi nimefika hapa Januari, lakini kuna walimu wengine
wawili wameongezwa ambapo mmoja ametoka Shule ya Mtejeta iliyoko mjini Mpwapwa
na mwingine amejihamisha mwenyewe kutoka Shule ya Kimagai,” alisema.
Uchunguzi umebaini kwamba, licha ya kuongezeka kwa walimu
hao watatu, bado shule hiyo inahitaji walimu wawili wa ziada kwani kwa sasa
uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi shuleni hapo ni watoto 56 kwa mwalimu mmoja,
tofauti na uwiano wa kitaifa wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45.
Maendeleo ya kitaaluma shuleni hapo yanaonekana pia kuwa
duni, kwani kati ya watoto 54 waliomaliza darasa la saba mwaka 2016, ni 21 tu
ndio waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwaka huu.
Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Malolo, Bosco Mwaluga,
anasema ukosefu wa walimu kwenye shule za msingi za kata hiyo ni changamoto
kubwa ambayo inakwamisha maendeleo ya elimu.
“Hapa Malolo ameletwa Mwalimu Massawe ambaye alikuwa
Nzugilo, Mwalimu Selemani Saidi kutoka Mtejeta na Mwalimu Emmanuel Kagali,
ambaye amejihamisha mwenyewe kutoka Kimagai ili arudi hapa kijijini kwake,”
anasema Bosco.
Shule ya Msingi Idodoma yenye wanafunzi 314 inao walimu
wanne tu kwa mwaka wa nne sasa, ambapo uwiano ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi
79.
Aidha, Shule ya Msingi Nzugilo yenye wanafunzi 507 ina
walimu nane ukiwa ni uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 63.
Nyumba za walimu
“Tuna changamoto kubwa pia ya nyumba za walimu, hapa Malolo
zipo nyumba tatu tu ambazo haziwatoshi walimu saba waliopo, zinahitajika nyumba
nyingine nne,” anasema Mwalimu Massawe.
Hali hiyo, anasema, imewafanya walimu wengine kwenda kupanga
mitaani kwa gharama zao wenyewe, jambo ambalo linawaongezea mzigo na gharama za
maisha.
Anaongeza kwamba, kukosekana kwa nyumba za uhakika ni
kikwazo kingine kinachoweza kukwamisha kuletwa kwa walimu wapya, hasa wa kike,
hivyo kuiomba Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kuhakikisha makazi ya walimu
yanapewa kipeumbele.
Akizungumzia masuala mengine, Mwalimu Massawe alisema
changamoto ya ukosefu wa vitabu vvya kiada na ziada bado ni kubwa, ambapo kwa
sasa kitabu kimoja za ziada kinatumiwa na wanafunzi nane badala ya wanafunzi
watatu kama Sera ya Elimu na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM)
inavyoelekeza.
Suala la afya na usafi nalo ni changamoto kubwa kwa
wanafunzi wa shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1975, ambapo ina matundu nane tu ya
vyoo.
“Ni changamoto kubwa kwa sababu kuna wanafunzi 189 wa kiume
na 197 wa kike, matundu haya hayatoshi kabisa,” alisema Mwalimu Massawe.
Kwa watoto wa kiume, tundu moja linatakiwa kutumiwa na
wanafunzi 25 wakati wasichana 20 wanatakiwa kutumia tundu moja, jambo ambalo
katika shule hiyo halipo kwa kuwa wastani tundu moja linatumiwa na wanafunzi
48.
Comments
Post a Comment