Featured Post

HII HAPA NDIYO MIUNDOMBINU MUHIMU YA GESI TANZANIA


Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini Blog
KATIKA kuhakikisha sekta ya mafuta na gesi asilia inafanikiwa, uimarishaji wa miundombinu ni jambo la msingi ambalo serikali ya Tanzania imejizatiti kulitekeleza.
Licha ya kuwepo kwa wawekezaji wengi, lakini miundombinu inapaswa kumilikiwa na serikali yenyewe kama inataka kuwa mshiriki wa moja kwa moja na kusimamia mazao na mapato yatokanayo na rasilimali hizo.

Miongoni mwa miundombinu hiyo ni pamoja na bandari, bomba la gesi, mitambo ya kuchakata gesi asilia, mitambo ya kufua umeme wa gesi, mtambo wa kusindika gesi ya kimiminika, barabara, reli na mambo mengine kadha wa kadha.
MaendeleoVijijini inaangalia baadhi ya miundombinu hiyo na ni kwa namna gani serikali imejitahidi kuimarisha.

Bandari ya Mtwara
Zamani ikijulikana kama ‘Bandari ya Karanga’, bandari hiyo ilijengwa kati ya mwaka 1948 na 1954 ikiwa sehemu ya mradi wa karanga Tanganyika, zao ambalo lilikuwa likilimwa kwa wingi nchini. 
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, uendelezaji wa bandari hiyo uliendana na ujenzi wa reli kutoka Mtwara mpaka Nachingwea kwa ajili ya kusafirisha vifaa kwenda Nachingwea kwenye uzalishaji na kusafirisha bidhaa jamii ya karanga kutoka Nachingwea kwenda bandarini Mtwara. 
Bandari hiyo ilikuwa na uwezo mkubwa wa kuhimili tani nyingi, lakini kuanguka kwa mradi wa karanga kuliathiri uwezo wa bandari hiyo. 
Aidha, miundombinu mibovu katika mikoa ya kusini mwa Tanzania nayo ilidumaza maendeleo na hivyo hata bandari yenyewe ikakosa ufanisi.
Kufuatia kugundulika kwa gesi ndani ya mwambao kusini mwa Tanzania, bandari ya Mtwara imekuwa muhimu sana kwa kampuni za kimataifa za mafuta na gesi ambazo zinaendesha shughuli zao Mtwara kwani zinatumia bandari hiyo katika shughuli zao za uzalishaji hasa kusambaza mahitaji kwa meli zinazochimba gesi baharini.  
Kwa zaidi ya miaka sita iliyopita, bandari ya Mtwara imeongeza asilimia 23.9 ya mizigo kwa mwaka, idadi ya mizigo iliongezeka kutoka tani 204,429 mwaka 2012/2013 mpaka tani 356,000 mwaka 2013/2014.
Takwimu kutoka bandari ya Mtwara zinaonyesha kuwa meli 544 hususan kutoka China, Ulaya, na Kenya ziliwasili bandarini mwaka 2015. 
Mwaka 2013, serikali ya Tanzania ilitangaza kuwekeza Dola za Marekani milioni 214 kwa ajili ya upanuzi na uimarishaji wa bandari ya Mtwara kufikia viwango vya kimataifa.
Hii ni baada ya serikali kuingia mkataba na serikali ya Japan kufanya uchambuzi wa awali. 
Kwa mujibu wa meneja wa bandari, maamuzi hayo yalichukuliwa kutokana na shughuli za uchimbaji gesi asilia zinazoendelea Mtwara na Lindi.
Mradi huo utajumuisha upanuzi na uimarishaji wa miundombinu pamoja na ununuzi wa vifaa kama mashine za kubebea mizigo na matrekta.
Kiasi cha Shs. 2.95 bilioni zilipangwa kutumika kuimarisha miundombinu ya bandari pekee. 
Kwa sasa, bandari ina uwezo wa kupokea tani za mizigo 400,000 kwa mwaka. Uwezo huo utaongezeka na kufikia tani za mizigo milioni 28 kwa mwaka. 
Mamlaka ya Bandari (TPA) imenunua hekta 263 kwa ajili ya upanuzi wa bandari ya Mtwara hali ambayo itaongeza uwezo wa bandari kupokea kwa wakati mmoja meli saba kutoka nne za sasa.
Hekta nyingine 100 zimepatikana kwa ajili ya ujenzi wa bandari huru na nyingine 400 zimeshatafutwa kwa ajili ya shughuli za mafuta na gesi ambapo kampuni mbalimbali zimeshawasilisha maombi ya kutekeleza mradi huo lakini maamuzi bado hayajachukuliwa. 

Bomba la Gesi Mtwara-Dar es Salaam
Mwezi Julai 2012, serikali ya Tanzania ilizindua rasmi ujenzi wa bomba la gesi lenye urefu wa kilometa 532 kutoka Mnazi Bay mpaka Dar es Salaam. Tayari bomba hilo limekamilika na lilizinduliwa Septemba 2015 na Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Mradi huo ulijumuisha ujenzi wa bomba lenye ukubwa kati ya inchi 24-36 kutoka Mnazi Bay mkoani Mtwara, ikiunganishwa Somanga Funga kupitia njia iliyoko sasa kutoka SongoSongo mkoani Lindi, na hatimaye Kinyerezi jijini Dar es Salaam.
Bomba la inchi 24-limejengwa kutoka Mnazi Bay kwenda Somanga ambapo bomba lililopo la inchi 16 kati ya Somanga na Dar es Salaam limepanuliwa kufikia inchi 36 na lina na uwezo wa kusafirisha futi za ujazo milioni 210 za gesi kwa siku, kutoka futi za ujazo za sasa milioni 105.
Bomba la inchi 16 lilililokuwa linatumika awali kutoka SongoSongo mpaka Dar es Salaam, ambalo lilikuwa linamilikiwa na kampuni ya SONGAS Limited Tanzania lilikuwa na changamoto ya kiuwezo pamoja na kuongezeka kwa mahitaji ya gesi na nishati jijini Dar es Salaam. 
Ujenzi wa bomba hilo pia ulijumuisha ujenzi wa mtambo wa kuchakata gesi eneo la Madimba mkoani Mtwara na SongoSongo, Lindi. Mitambo miwili ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi I na Kinyerezi II yenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 150 na 240, mutawalia, inaendeshwa na gesi asilia.
Mwezi Septemba 2012, Wizara ya Fedha kwa niaba ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Exim ya China walitiliana saini makubaliano ya mkopo wa miaka 33 wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.225 kwa riba ya asilimia 2 kwa ajili ya ujenzi wa bomba la gesi linalounganisha eneo la Msimbati na Mnazi Bay mpaka Dar es Salaam.
Kampuni zilizosimamia ujenzi huo ni China Petroleum Technology and Development Corporation (CPTDC) na China Petroleum Pipeline Engineering Corporation (CPPEC). 
Mradi huo una uwezo wa futi za ujazo milioni 350, na uwezekano wa kufikia futi za ujazo milioni 750 za gesi kwa siku.
Sasa hivi, mitambo miwili ya kusindika gesi kule Madimba na Somanga Funga inajengwa na Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) na miradi inategemewa kuanza mwishoni mwa mwaka 2014. 
Baada ya ujenzi kukamilika, bomba hilo litakuwa na uwezo wa kusafirisha gesi ambayo itatumika kuzalisha umeme wa megawati 3,920. Uwezo wa sasa katika mitambo hiyo miwili ni kuzalisha umeme wa megawati 1,509.85.
Mahitaji ya sasa ya umeme nchini Tanzania ni megawati 720 kwa siku. Uzalishaji wa gesi kisiwani Songo Songo ambayo inasafirishwa kwa bomba mpaka Dar es Salaam, inazalisha megawati 320 ya umeme na kusambazwa kwenye viwanda 37.
MaendeleoVijijini inajua kwamba, sehemu ya gesi kutoka SongoSongo inatumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kupikia na uendeshaji wa vyombo vya moto.
Gesi inayozalishwa Mnazi Bay inatumika kuzalisha umeme wa megawati 10 kwa sasa ambao unatumika mkoani Mtwara, japo uwezo wake ni kuzalisha megawati 18.
Ukiachia watumiaji wa majumbani, mradi huo pia utafaidisha watumiaji wakubwa wa umeme vikiwemo viwanda na unategemea kusaidia nchi kukidhi mahitaji yake ya umeme, ambapo kwa sasa matumizi yanaongezeka huku mahitaji ya umeme yakikua kati ya asilimia 10-15 kwa mwaka.

Mitambo ya Gesi Madimba na Songo Songo
Moja ya mitambo ya kuchakata gesi nchini unajengwa eneo la Madimba mkoani Mtwara na kampuni za China Petroleum Engineers, China Chemical Engineering Secondary Construction Corporation na Worley Parson. 
Mtambo mwingine wa gesi ulijengwa kisiwani SongoSongo na unamilikiwa na kampuni ya SONGAS Ltd; kampuni ya ubia kati ya CDC Globeleq, Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO)Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na TDFL.

Songo Songo – Somanga Funga – Dar es Salaam
Mwezi Oktoba mwaka 1995, kampuni za Ocelot Tanzania Inc. na Trans Canada Pipeline Ltd (TCPL Tanzania Inc.) kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania, Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), walianzisha kampuni ya SONGAS Limited.
Kisiwa cha Songo Songo.

SONGAS Limited imeendeleza eneo la gesi la Songo Songo katika wilaya ya Kilwa mkoani Lindi kwa kutengeneza vifaa vya kusindika gesi kwenye Kisiwa cha Songo Songo, na bomba la kusafirisha gesi ya asili hadi Dar es Salaam, ambako inatumika kama akiba inayoendesha jenereta tano za kufua umeme. 
Mitambo miwili ya kusindika gesi kule Songo Songo, yenye uwezo wa futi za ujazo milioni 35 kwa siku inamilikiwa na Serikali ya Tanzania. 
Gesi iliyosindikwa inasafirishwa kupitia bomba la kilometa 25, lenye inchi 12, kutoka Songo Songo hadi Somanga Funga, na kutoka Somanga Funga ilikuwa ikisafirishwa kupitia bomba la kilometa 207, lenye inchi 16, hadi Ubungo Dar es Salaam. 
Ujenzi wa bomba hilo ulianza mwaka 2003 na ulikamilika mwezi Mei 2004. Mgawanyo wa kwanza wa gesi ulifika Dar es Salaam mwezi Julai 2004 na ndio wakati uendeshaji wa kibiashara wa mradi huo ulianza rasmi.

Bomba la Dar-Tanga-Mombasa
Pamoja na nia ya kuongeza biashara, serikali za Kenya na Tanzania zinataka kutengeneza bomba la gesi lenye urefu wa kilometa 530 kutoka Dar es Salaam hadi Tanga na hatimaye Mombasa nchini Kenya.
Bomba hilo litajumuisha vituo vya ugawaji gesi mjini Tanga na Mombasa.
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imeipa kazi kampuni ya COWI kwa ushirikiano na Runji and Partners kufanya upembuzi yakinifu kuhusu ujenzi wa bomba hilo.

Mtambo wa Gesi ya Kimiminika (LNG)
Kampuni za Statoil na BG Group zipo katika mazungumzo ya kuweka mtambo wa njia mbili wa gesi kwa gharama inayokadiriwa kuwa dola za kimarekani bilioni 14.
Shughuli hiyo ya pamoja inakuwa ya kwanza nchini ambako hadi sasa akiba ya gesi yenye futi za ujazo zaidi ya trilioni 50 imegundulika. 
Hata hivyo, ratiba ya utekelezaji wa mradi huo bado haijawekwa wazi ingawa tayari eneo maalum la ujenzi wa mtambo huo limekwishapatikana mkoani Lindi na kinachofanyika sasa ni kufanya tathmini ili kuwalipa fidia wananchi pamoja na kuwatafutia eneo jingine.
Serikali inapendelea mtambo wa kusindika gesi ya kimiminika ujengwe eneo la ufukweni, tofauti na maoni ya wawekezaji ambao walitaka ujengwe mbali na ufukweni katika nchi ya jirani ya Msumbiji. 
Kwa mujibu wa Mark Todd, Meneja wa Mawasiliano ya Nje wa BG Group, BG na Statoil wameshatuma pendekezo la pamoja kuhusu eneo linalofaa kwa mtambo huo na wanasubiri jibu kutoka serikalini. Statoil na BG wanapendelea mtambo wa gesi ya kimiminika ujengwe eneo la Likong’o-Mchinga kusini mwa mji wa Lindi.
Gesi iliyowekwa katika hali ya kimiminika (LNG), ni gesi safi, isiyo na rangi, yenye kimiminika kisicho na sumu, inayotengenezwa kwa kuipoza gesi ya asili kufikia kipima joto cha Fahrenheit 260° (sawa na Sentigredi 163°), ambapo inakuwa kimiminika. Mchakato huu hufanywa ili kurahisisha usafirishaji wa gesi asilia uwe na ufanisi zaidi kwa kutumia maroli au meli.
Gesi ya kimiminika huchukuwa nafasi ndogo hadi mara 615 ya gesi iliyo katika muundo wa hewa. Zaidi ya hayo, gesi ya kimiminika hailipuki katika mazingira yasiyodhibitiwa, kwa hiyo, katika hali isiyotegemewa ya kumwagika kwa gesi ya kimiminika, gesi hiyo inakuwa na uwezekano mdogo wa kutoa mlipuko.
Faida nyingine za gesi ya kimiminika inajumuisha ukweli kwamba mchakato wa kuifanya kimiminika unapunguza oksijeni, carbon dioxide, salfa na maji kutoka kwenye gesi hiyo, inayofanya gesi hiyo kuwa karibu na metheni asilia. Gesi hiyo ikifikishwa mwisho wa safari yake, huifadhiwa katika hali yake ya kimiminika hadi inapotiwa joto tena kurudi katika hali yake ya gesi ya asilia.

Mtambo wa kufua Umeme Mtwara
Mwaka 2013, kampuni ya Symbion Power ya Marekani, Tanesco na General Electric International walikubaliana kutengeneza mtambo wa kufua umeme unaotumia gesi wenye megawati 600 mjini Mtwara ili kutoa umeme kwa mikoa ya kusini mwa Tanzania.
Mwaka huo huo (2013), kampuni ya General Electric International (GE), inayojishughulisha na teknolojia ilijiunga na mradi huo kuharakisha utekelezaji wake. 
Mradi huo unahitaji Dola za Marekani bilioni 1, na utajumuisha ujenzi wa kilometa 650 za njia ya umeme kutoka Mtwara kwenda Songea kwa lengo la kupanua gridi ya taifa kutoka Makambako, mkoani Njombe hadi Songea.
Mtambo huo wa umeme utasambaza megawati 30 kwenye kiwanda cha saruji cha Dangote kilichoko Mtwara na megawati 20 kwenye kiwanda cha kutengeneza mbolea cha Mtwara.
Pamoja na mahitaji hayo, uwanja wa ndege wa Mtwara unahitaji megawati 6 na mgodi wa urani wa Namtumbo mkoani Ruvuma unahitaji megawati 30. 
Mnunuzi mwingine wa umeme kutoka kwenye mtambo huo ni kampuni ya Wentsworth Resources ya Uingereza. 
Pamoja na mahitaji ya ndani ya nchi, Tanesco imepokea maombi ya kusambaza umeme kwenye mikoa ya kaskazini nchini Msumbiji.

Mradi wa Umeme Kinyerezi
Mtambo wa gesi wa Kinyerezi.

Kinyerezi I na Kinyerezi II ni mitambo ya kuzalisha umeme ambayo inaendeshwa kwa kutumia gesi ambayo imejengwa jijini Dar es Salaam.
Mitambo hiyo inapokea gesi asilia kutoka Mtwara kupitia Bomba la Gesi la Mtwara-Dar es Salaam, ambapo kituo cha Kinyerezi I kina uwezo wa kuzalisha megawati 150 za umeme. 
Gharama za mradi wa umeme wa Kinyerezi I ni Dola za Marekani milioni 183. Gharama za ujenzi wa mtambo huo zilitolewa na serikali kupitia Tanesco ambapo mradi wenyewe ulisimamiwa na kampuni ya Jacobsen Electro kutoka Norway. Kituo hicho kilikamilika mwanzoni mwa mwaka 2015 na kilizinduliwa Septemba 2015 na Rais mstaafu Jakaya Kikwete. 
Kituo cha uzalishaji umeme cha Kinyerezi II kiligharamiwa kwa ubia kati ya serikali ya Tanzania na serikali ya Japan huku ukisimamiwa na kampuni ya Japan ya Sumitomo Corporation. Mradi wa Kinyerezi II utazalisha megawati 240, na ulikamilika mwezi Desemba 2015. 
Vituo vya kuzalisha umeme vya Kinyerezi I na II kwa pamoja vitazalisha takriban asilimia 20 ya mahitaji ya umeme nchini, hivyo kuwapatia nafuu wananchi ambao kwa miaka sasa wamekuwa wakipata shida ya upatikanaji wa umeme wa uhakika. 

Kinyerezi III na IV
Mradi wa Kinyerezi III ni ubia kati ya Tanesco na Shanghai Electric Power Company ya China. Kituo hicho kinategemewa kuzalisha megawati 300 za umeme.
Kampuni ya Shanghai Electric Power inamiliki asilimia 60 ya hisa huku Tanesco ikiwa na asilimia 40. Ubia huo ulisainiwa Oktoba 2014, huku uchambuzi yakinifu ukiwa umefanyika mwezi Januari 2014. Uzalishaji wa kwanza wa megawati 180 za umeme ulitarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka 2015 wakati mradi ulipokamilika. 
Kufuatia kukamilika kwa mradi huo, umeme utakaozalishwa utapelekwa kwenye kituo kidogo kinachojengwa eneo la Kinyerezi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kusambazwa kwenye gridi ya taifa. 

Kituo cha Kinyerezi IV kinasimamiwa na kampuni ya Poly Group ya China na kina uwezo wa kuzalisha megawati 450 za umeme. 

Comments