Featured Post

HAYA NDIYO MAENEO YENYE UTAJIRI WA MAFUTA NA GESI NCHINI TANZANIA


TANZANIA ina futi za ujazo trilioni 57 za gesi ambayo tayari imethibitishwa baada ya tafiti nyingi na ugunduzi kufanyika.
Karibu futi za ujazo trilioni 47 kati ya hizo ni za gesi iliyogunduliwa katika mwambao na katikati ya bahari mbali na ufukweni, ususan Kusini mwa Tanzania, ambapo pamoja na kuwepo kwa vitalu takriban 12 katika maji ya kina kirefu, lakini gesi kwa sasa inazalishwa Songo Songo, Mnazi Bay na Msimbati-1 pamoja na Kiliwani Kaskazini (KN-1).
Eneo la Songo Songo lilonapatikana karibu na Kisiwa cha Songo Songo mkoani Lindi, lina ukubwa wa kilometa za mraba 170, na futi za ujazo bilioni 879 za gesi, ambapo linaendeshwa na kampuni ya Orca Exploration chini ya Makubaliano ya Kuchangia Uzalishaji (PSA) iliyoingia na TPDC na ni ndio mradi wa kwanza wa uzalishaji gesi Tanzania.
Mkoani Mtwara, jumla ya futi za ujazo bilioni 667 za gesi zimegundulika mpaka sasa katika eneo la Mnazi Bay, ambapo eneo hilo liligunduliwa na kampuni ya ENI mwaka 1981, baada ya kampuni hiyo kuchimba kisima.
Kampuni ya Wentworth Resources ilikuja kugundua eneo la Msimbati-1 mwaka 2005 ambapo visima vinne viko tayari kwa uzalishaji na gesi ya kwanza ilitegemewa kuanza kutumika mwaka 2015. Kwa sasa, eneo hilo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 756 linasimamiwa na kampuni ya Maurel et Prom. 
Kwa upande mwingine, kampuni ya Ndovu Resources (Aminex), inasimamia eneo la Kiliwani-Kaskazini lenye futi za ujazo bilioni 45 za gesi. Eneo hili tayari limeanza uzalishaji na lilikuwa linasubiri kukamilika kwa ujenzi wa bomba.
Utafiti katika mwambao wa Bahari ya Hindi unaonyesha kwamba, vitalu vinne kati ya 8 ambavyo vinaendeshwa ndani ya mwambao kwa sasa vilipatikana katika mzunguko wa mwisho wa zabuni ulioishia mwezi Mei 2014 ambapo waombaji walikuwa kampuni ya Urusi ya Gazprom na ya China ya CNOOC Ltd. 
Kampuni ya BG Group imekuwa ikiendesha Kitalu Namba 1, Kitalu Namba 3 na Kitalu Namba 4 tangu mwaka 2010 na imefanikiwa kufanya ugunduzi wa gesi kwenye maeneo hayo. 
Mwaka 2013, kampuni ya Pavilion Energy ilichukua asilimia 20 ya hisa kwenye vitalu namba 1, 3 na 4 na mwishoni mwa mwaka 2014 kampuni ya BG Group ilijitoa katika umiliki wa kitalu namba 3. Mshirika wake anaendelea na utafiti. 
Kampuni ya Ophir Energy, ikiwa na asilimia 20 ya hisa, ilinunua kampuni ya Dominion Petroleum mwezi Februari 2012 na kupata asilimia 80 ya hisa katika kitalu namba 7. Kampuni hiyo haijafanikiwa kugundua gesi kwenye kitalu hicho. 
Petrobras nayo kwa upande wake iliingia mkataba na TPDC kwenye Kitalu namba 5 mwaka 2004, na mwaka 2011 iliuza hisa zake kwa kampuni ya Shell Deepwater Tanzania BV, ambayo ilipata umiliki wa asilimia 50 wa kitalu hicho. Kisima cha Zeta-1 kilichimbwa mwaka huo huo na hakukuwa na mafanikio. 
Aidha, mnamo mwaka 2006, kampuni ya Petrobas ilisaini makubaliano na TPDC kwa ajili ya Kitalu Namba 6, kilichopo kwenye Bonde la Mafia na ilipofika mwaka 2013, Statoil ikanunua asilimia 12 kwenye kitalu hicho kutoka kampuni ya Petrobas.
Tangu mwaka 2007, Statoil imekuwa ikisimamia kitalu namba 2 chenye ukubwa wa kilometa za mraba 5,500. Statoil kwa kushirikiana na ExxonMobil, imefanya ugunduzi sita wa uwepo wa gesi katika kitalu hicho. Gunduzi nne zilifanyika kipindi cha 2012/13, na mbili mwaka 2014.

Utafiti wa nje ya mwambao
Shughuli za utafiti nje ya mwambao nchini Tanzania zinaendeshwa katika eneo ambalo linaunda sehemu ya au linapakana na Mkondo wa Bonde la Ufa la Afrika Mashariki (EARS). Tayari mapipa bilioni 2 ya mafuta yamegunduliwa katika eneo la Bonde la Ziwa Albert nchini Uganda na kiasi kingine kimegundulika nchini Kenya.
Tangu Novemba 2011, kampuni ya Heritage Oil imekuwa ikifanya utafiti kwenye eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 8,745 kusini mwa Bonde la Ziwa Rukwa na Januari 2012 ikaongeza kilometa za mraba 1,934 kwenye leseni ya Bonde la Kyela mkoani Mbeya. Maeneo yote yana mfanano wa kijiologia wa haidrokaboni iliyoko Bonde la Ziwa Albert nchini Uganda.
Leseni ya kampuni ya Swala Energy, eneo la Kilosa-Kilombero lenye ukubwa wa kilometa za mraba 17,675, na leseni ya utafiti Pangani yenye eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 17,156 lililoko kwenye eneo la mpasuko wa Pangani (Pangani Rift) ni sehemu ya EARS.
Kwa sasa, kampuni ya Jacka Resources inasubiri uidhinishaji wa wizara ili kuanza utafiti wa eneo la kilometa za mraba 8,400 kwenye Bonde la Ruhuhu ambalo linapakana na Bonde la Ziwa Nyassa kwa upande wa magharibi, ikiwa ni sehemu pia ya EARS.
Ziwa Tanganyika liko magharibi mwa EARS. Mwaka 2010, kampuni ya Beach Energy na TPDC zilitiliana saini kwa ajili ya kitalu cha kusini mwa Ziwa Tanganyika.
Takwimu zilizopo tangu miaka ya 1980 zinaonyesha uwepo wa rasilimali mafuta ndani ya ziwa hilo.  
Kampuni ya Ras-Al-Kaimah iliwasilisha maombi kwa ajili ya kitalu namba 9 kilichopo kaskazini mwa Ziwa Tanganyika chenye ukubwa wa kilometa za mraba 9,670.2 katika mzunguko wa mwisho wa utoaji leseni. 
Leseni za utafiti eneo la nje ya mwambao bado ziko wazi, kama eneo la leseni la Ziwa Eyasi ambalo kampuni ya Ufaransa ya Total ilionesha nia mwaka 2014. 
Kisima cha Ntorya-1 kilichochimbwa na kampuni ya Ndovu (Aminex) ambayo inasimamia leseni ya Ruvuma yenye ukubwa wa kilometa za mraba 3,447 imefanikiwa kugundua futi za ujazo trilioni 1.9 za gesi. Ikiwa imekusudia kutafiti uwezekano wa haidrokaboni kwenye bonde la Ruvuma, uchimbaji wa kisima cha Likonde-1 haukuwa na mafanikio.

Kitalu Namba 1
Kitalu Namba 1 kipo eneo la Bonde la Mafia ndani ya mwambao kutoka Ruvuma na Delta ya Rufiji kwenye mpaka na Msumbiji, kwenye kina cha maji kutoka meta 100 mpaka 3,000.
Kitalu hiki kinamilikiwa na kampuni ya BG Group ya Uingereza kwa asilimia 60, huku kampuni ya Ophir Energy na Pavillion Energy kila moja ikiwa na asilimia 20. Jumla ya ugunduzi sita wa gesi umeshafanyika kwenye kitalu hiki tangu mwaka 2010 ndani ya kilometa 100 eneo la mwambao na kwenye kina cha maji kati ya mita 900 mpaka 1,600.
Kati ya visima 6 vilivyochimbwa mpaka sasa (Chaza, Jodari, Jodari Kaskazini, Mkizi, Mzia, na Taachui), ni viwili tu ndivyo vimebainishwa kuwa na ugunduzi mkubwa wa gesi ambavyo ni Mzia yenye futi za ujazo trilioni 4.7, na Jodari yenye futi za ujazo trilioni 4. 
Mwishoni mwa raundi ya tatu ya utoaji leseni, Kitalu Namba 1 kilikabidhiwa kwa kampuni ya Ophir Energy lakini ilipofika Mei 2010, Ophir Energy iliuza asilimia 60 ya hisa zake kwenye kitalu hicho kwa BG Group. 
Ilipofika Aprili 2011, Ophir Energy na BG zilitangaza ugunduzi wao wa kwanza kwenye kitalu hicho, ambao ulifanyika kwenye kisima cha Chaza-1. Kisima hicho kiko umbali wa kilometa 18 kutoka eneo la pwani na meta 952 kwenye kina cha maji baharini. Kisima hicho kina akiba kubwa ya gesi.
Mnamo Machi 2012, mafanikio yaliyopatikana kwenye kisima cha Jodari-1 kwenye kitalu hicho, ambapo idadi ya futi za ujazo trilioni 3.4 ziligundulika na ilipofika Mei 2012, kampuni hizo zikatangaza ugunduzi wa gesi katika kisima cha Mzia-1 ambapo futi za ujazo zilizokadiriwa kuwa trilioni 3.5 ziligunduliwa. Kisima hicho kinapatikana kilometa 45 kutoka pwani ya Tanzania na kilometa 45 kaskazini mwa mpaka wa bahari na Msumbiji.
Septemba 2012, ilitangazwa kwamba utafiti zaidi umeongeza ugunduzi katika kisima cha Mzia kufikia futi za ujazo trilioni 6 na ilipofika Februari 2013, wamiliki wa kitalu hicho walitangaza mpango wa uhakiki kwenye kisima cha Mzia-2 na hadi kufikia Mei 2013 walitangaza kuongezeka kwa gesi iliyogundulika kutoka futi za ujazo 3.5 hadi kufikia futi za ujazo trilioni 4.5.
Mnamo Machi 2013, BG na Ophir Energy walitangaza kufanikiwa kwa jaribio kwenye kisima cha Jodari-1 ambalo lilikuwa la kwanza kufanyika ndani ya kina kirefu cha maji baharini nchini, ambalo lilithibitisha uwepo wa gesi asilia kwenye eneo la Jodari.
Julai 2013, ugunduzi katika kisima cha Mkizi-1 ulitangazwa. Kisima hicho kipo meta 1,301 ndani ya kina cha maji kati ya kisima cha Mzia na Jodari, ambapo futi za ujazo trilioni 0.6 ziligundulika.
Aidha, Novemba 2013, Ophir na BG walitangaza mafanikio mengine kwenye eneo la Mzia katika kisima cha Mzia-3 ambacho kilichimbwa kilometa 6 kaskazini mwa kisima cha Mzia-1. Kisima hiki kimebainika kuwa na gesi asilia kama ilivyo kwa visima vya Mzia-1 na Mzia-2. Tathmini ya awali ya matokeo ya Mzia-3, yanaonesha kuongezeka kwa futi za ujazo trilioni 0.7 na kufikia jumla ya futi za ujazo trilioni 5.3 kwa eneo la Mzia.
Mwaka huo, kampuni ya GAIL kutoka India na Pavillion Energy walitangaza nia ya kununua hisa kwenye vitalu namba 1, 3 na 4 na ilipofika Desemba, Pavillion Energy iliingia makubaliano na Ophir Energy kununua hisa za asilimia 20 kwenye vitalu namba 1, 3 na 4 kwa Dola za Marekani bilioni 1.288.
Mnano Juni 2014, Ophir na BG walitangaza ugunduzi kwenye kisima cha Taachui-1 kwenye kitalu namba 1. Kisima cha Taachui-1 kinapatikana karibu na mpaka wa magharibi wa kitalu namba 1 na kilichimbwa kwa kina cha meta 4,215. Makadirio ya ugunduzi ni futi za ujazo trilioni 1.0.

Kitalu Namba 2
Kampuni ya Statoil ya Norway ndiyo inamiliki leseni ya uchimbaji ya kitalu namba 2 ambapo ina asilimia 65 ya hisa huku ExxonMobil Exploration and Production Tanzania Limited ikimiliki asilimia 35 zilizobaki.
Kitalu hicho kinapatikana kwenye Bonde la Mafia ndani ya mwambao kutoka Delta ya Ruvuma na Rufiji kwenye Mkoa wa Mtwara. Kitalu kina eneo la kilometa za mraba 11,099 na kina cha maji cha meta 3,000. Idadi ya akiba ya gesi asilia iliyogunduliwa kwenye kitalu hicho inakadiriwa kuwa futi za ujazo trilioni 21.
Kitalu hicho kilitolewa kwa Statoil mwishoni mwa awamu ya tatu ya utoaji wa leseni mwaka 2005 na ilipofika Aprili 18, 2007, Statoil ilitia saini Mkataba wa Kuchangia Uzalishaji na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC). 
Mwezi Machi 2010, Statoil na ExxonMobil zilitangaza utiaji saini wa kuhamisha asilimia 35 ya hisa za kampuni ya Statoil kwenye kitalu namba 2 kwenda kwa kampuni ya ExxonMobil.
Mnamo Februari 2012, kampuni hizo zilitangaza ugunduzi mkubwa wa gesi asilia katika kisima cha Zafarani, ambao umetoa mpaka futi za ujazo trilioni 5. Ilipofika Juni 2012, kampuni hizo zilitangaza ugunduzi mkubwa wa pili kwenye kitalu hicho ambao ulifanyika kwenye kisima cha Lavani, ambapo makadirio ya mwanzo yalionesha uwepo wa akiba ya gesi asilia futi za ujazo trilioni 3. Kisima cha Lavani kinapatikana kilometa 16 kusini mwa kisima cha Zafarani.
Aidha, mnamo Desemba 2012, kampuni hizo zilitangaza ugunduzi wa tatu kwenye eneo la kitalu, ambao ulifanyika kwenye kisima cha Lavani-2 ambacho kipo takriban kilometa 5 kusini-mashariki mwa kisima cha Lavani-1 na kilometa 20 kusini mwa kisima cha Zafarani-1.
Mnamo Machi 2013, ugunduzi wa futi za ujazo kati ya trilioni 4-6 wa gesi asilia katika kisima cha Tangawizi-1 ulitangazwa. Ugunduzi huo ulifanya idadi ya akiba ya gesi asilia katika kitalu namba 2 kuwa kati ya futi za ujazo trilioni 15-17.
Ilipofika Desemba 2013, Statoil na ExxonMobil walitangaza ugunduzi wa ziada ya futi za ujazo trilioni 2-3 kwenye kisima cha Mronge-1, ambao ulifanya idadi ya akiba ya gesi asilia kwenye kitalu namba 2 kuwa kati ya futi za ujazo trilioni 17-20. 
Aidha, Juni 2014, ugunduzi wa ziada wa futi za ujazo trilioni 2-3 za gesi asilia ambao ulifanyika kwenye kisima cha Piri-1 ulitangazwa, na kufanya jumla ya akiba ya gesi asilia kwenye kitalu kufikia futi za ujazo 20. Mwezi Oktoba 2014, wamiliki wa kitalu walitangaza ugunduzi wa saba kwenye kitalu namba 2 wa kiasi cha futi za ujazo trilioni 1.2 ulifanyika kwenye kisima cha Giligiliani-1, na kufanya jumla ya akiba ya gesi asilia kwenye kitalu kufikia futi za ujazo trilioni 21.

Kitalu Namba 3
Kitalu hiki kinapatikana kwenye Bonde la Mafia ndani ya mwambao kutoka Delta ya Ruvuma na Rufiji kwenye kina cha maji kati ya meta 100 na 3,000.
Kampuni ya Ophir Energy inamiliki kitalu hicho kwa asilimia 80, huku kampuni ya Pavillion Energy ikiwa na asilimia 20.
Mpaka sasa, ni kisima kimoja tu ndicho kimeshachimbwa kwenye kitalu hiki – kisima chenye jina la Papa-1, ambako gesi asilia iligundulika mwaka 2012.
Ophir Energy ilikabidhiwa kitalu hicho na Serikali ya Tanzania mnamo Aprili 2006, lakini mwezi Mei 2010 BG Group ikanunua asilimia 60 ya hisa kutoka kampuni ya Ophir Energy.
Mwezi Agosti 2012, Ophir na BG zilitangaza kwamba kisima cha Papa-1 kiligundulika kuwa na akiba ya gesi asilia na uchunguzi wa awali ulionyesha uwepo wa akiba ya gesi asilia futi za ujazo trilioni 0.5 – 2.0.
Hata hivyo, Oktoba 2014, BG Group ilijiondoa kwenye umiliki wa kitalu namba 3 kwa sababu hakukuwa na matumaini yoyote ya ugunduzi. Kufuatia uamuzi huo wa BG Group, kampuni ya Ophir Energy iliomba serikalini kuchukuwa asilimia 60 za BG kwenye kitalu hiki, na hivyo kufanya idadi ya umiliki wake kufikia asilimia 80.

Kitalu Namba 4
Kitalu namba 4 kinapatikana kwenye Bonde la Mafia ndani ya mwambao kwenye Delta ya Ruvuma na Rufiji ndani ya kina cha maji chenye urefu wa meta 100 mpaka 3,000.
Kitalu hicho kinamilikiwa na BG Group kwa asilimia 60, huku Ophir Energy na Pavillion Energy zote zikiwa na asilimia 20 kila moja. Mpaka sasa, kumefanyika ugunduzi kwenye kisima cha Pweza na Chewa mwaka 2010, na kisima cha Ngisi mwaka 2013.
Mnamo Aprili 2006, kitalu namba 4 kilitolewa na serikali moja kwa moja kwa kampuni ya Ophir Energy lakini Mei 2010 Ophir Energy ikahamisha hisa zake zenye thamani ya asilimia 60 kwa kampuni ya BG Group. 
Oktoba 2010, Ophir Energy na BG Group zilitangaza ugunduzi wa kwanza kwenye kitalu hicho ambao ulifanyika kwenye kisima cha Pweza-1 ambacho kinapatikana kilometa 85 kutoka mwambao kwenye kina cha maji urefu wa meta 1,400.
Mnamo Desemba 2010, ugunduzi wa pili ulifanyika na kutangazwa ambao ulifanywa kwenye kisima cha Chewa-1 kinachopatikana kilometa 80 kutoka mwambao kwenye kina cha maji chenye urefu wa meta 1,315.
Aidha, Julai 2013, kampuni hizo zilitangaza mafanikio chanya kwenye kisima cha Ngisi, na kufanya uwepo wa akiba ya gesi asilia kwenye eneo la visima vya Chewa-Pweza-Ngisi kuwa futi za ujazo trilioni 4.5. Kisima cha Ngisi-1 kilichimbwa kilometa 5 kaskazini mashariki ya kisima cha Chewa-1.
Mwezi Agosti 2014, mafanikio ya majaribio kwenye kisima cha Pweza-2 yalitangazwa. Kisima hicho kilichimbwa kilometa 2 kusini mwa kisima cha Pweza-1 na ugunduzi huo ulifanya akiba ya gesi asilia kwenye eneo la visima vya Pweza kuwa futi za ujazo trilioni 1.7. 
Mwezi Oktoba 2014, BG na Ophir ilitangaza mafanikio ya majaribio kwenye kisima cha Pweza-3 ambacho kilichimbwa kilometa 2 kaskazini ya kisima cha asili cha Pweza. 

Kitalu Namba 5
Kitalu namba tano kinapatikana Bahari ya Hindi kwenye kina cha maji kati ya meta 600 na 3,000 na kinasimamiwa na Petrobras ya Brazil pamoja na Shell ya Uholanzi.  
Kitalu hicho ni miongoni mwa vitalu vya awali vilivyoko ndani ya bahari vilivyotolewa kwa kampuni za kimataifa za gesi na mafuta.
Mwaka 2001, kitalu hicho kilikabidhiwa kwa kampuni ya Petrobras mwishoni mwa awamu ya kwanza ya utoaji leseni lakini ilipofika mwishoni mwa mwaka 2011, Petrobas iliuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Shell
Mwezi Agosti 2011, Petrobas na Shell zilianza kuchimba kisima cha Zeta-1, lakini kisima hicho kilichochimbwa na meli ya Ocean Rig Poseidon hakikufanikiwa na hatimaye kuachwa mwaka mmoja baadaye (2012) na kusababisha hasara ya Dola za Marekani milioni 200 kwa kampuni ya Shell. Mwaka 2012, kisima cha pili kilichimbwa lakini hakuna matokeo yoyote yaliyotangazwa kwenye kitalu hicho.

Kitalu Namba 6
Kitalu namba 6 kina eneo la kilometa za mraba 5,549 kinachopatikana kwenye Bonde la Mafia ndani ya mwambao wa Tanzania kwenye kina cha maji chenye urefu wa meta 1,800 na kinapatikana takriban kilometa 170 kaskazini mwa kitalu namba 2, ambako Statoil imefanikiwa kugundua gesi kwa wingi. 
Kitalu hicho kinaendeshwa na kampuni ya Petrobras Tanzania Ltd ambayo inamiliki asilimia 38, huku kampuni ya Shell Deepwater Tanzania B.V. ikiwa na asilimia 50 na Statoil asilimia 12 ya hisa. 
Awali kitalu hicho kilitolewa kwa kampuni ya Petrobras wakati wa awamu ya tatu mwaka 2005.
Mwaka 2011, kampuni ya Petrobras iliingia katika makubaliano ya kuuza hisa zake asilimia 50 kwa kampuni ya Shell na mnamo Mei 2013, Petrobras ilikubali kuuza asilimia 12 ya hisa zake kwa Statoil. Hakuna ugunduzi wowote wa gesi uliopatikana mpaka sasa.

Kitalu Namba 7
Kitalu hicho kinapatikana kaskazini mwa vitalu namba 1, 2, 3 na 4 ambavyo vimegundulika kuwa na gesi asilia kwa wingi.
Kitalu hicho kilitolewa kwa kampuni iliyo chini ya kampuni ya Ophir Energy ya Dominion Petroleum mwezi Januari 2007 ambayo inakimiliki kwa asilimia 80. 
Mnamo Novemba 2013, Dominion ilianza uchimbaji wa kisima cha kwanza kwenye kitalu hicho ambacho kinaitwa Mlinzi Mbali-1 na kinapatikana takriban kilometa 210 mashariki mwa jiji la Dar es Salaam kwenye kina cha maji takriban meta 2,600.
Kisima hicho kilichimbwa na meli ya Deepsea Metro I. Uchunguzi wa awali kabla ya uchimbaji ulionyesha kwamba kisima hicho kilikuwa na dalili za uwepo wa gesi asilia.
Januari 2014, kampuni ya Ophir ilitangaza kwamba uchimbaji ulikuwa umekamilika na kwamba hakukuwa na dalili za uwepo wa gesi asilia na mnamo Novemba 2014, Ophir ilitangaza kwamba kisima cha pili kilichochimbwa kwenye kitalu hicho hakikuwa na dalili za uwepo wa gesi asilia pia. 
Kwa ujumla, jitihada bado zinaendelea kufanywa na kampuni mbalimbali zilizowekeza kutafa utafiti katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania na matumaini ya kuwepo kwa akiba nyingi ni makubwa.



Comments