Featured Post

WATALII ZANZIBAR HAWAJAKAUKA LICHA YA MSIMU ULIOPO KUZOELEKA KUWA WACHACHE

Na Jumia Travel Tanzania
Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio lukuki takribani kila sehemu utakayoipendelea. Mji Mkongwe uliopo visiwani Zanzibar ni mojawapo ya maeneo hayo yenye utajiri wa vivutio vya watalii kama vile maisha na vyakula vya wakazi wake, biashara pamoja na majengo ambayo yanayoakisi tamaduni za mataifa tofauti kama vile Waarabu, Waajemi, Wareno, Waafrika na Waingereza ambayo yamekuwepo tangu karne za 18 na 19.

Katika kuhakikisha maeneo hayo yanajulikana miongoni mwa watanzania na wageni wanaotembelea nchini, Jumia Travel wamezindua kampeni ambayo itakuwa ikiangazia maeneo mbalimbali.

Ikiwa imejikita kwenye Mji Mkongwe wa Zanzibar, kampuni hii ambayo inajishughulisha na huduma za hoteli kwa njia ya mtandao ilifanya mahojiano na Meneja Operesheni wa Africa House Hotel, Bw. Justus Kisome na mazungumzo yalikuwa kama ifuatavyo.


JT: Unaizungumziaje hoteli yako?

Justus: Africa House Hotel ni hoteli ya nyota nne inayopatikana kwenye jengo la kihistoria linalomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lililopo katika Mji Mkongwe wa Zanzibar. Hoteli yetu ina vyumba 15 vikiwa na hadhi tofauti kukidhi haja ya wateja mbalimbali wanaotembelea hapa. Miongoni mwa vyumba hivyo 6 vinatazamana na bahari ya Hindi ambavyo huwapatia wageni fursa ya kutazama tukio nadra na kuvutia la kuzama kwa jua. Vyumba 9 vinawapatia wateja mandhari nzuri ya Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao umebarikiwa kuwa na majengo na tamaduni za kale kwa karne kadhaa sasa.

JT: Unadhani ni vitu gani vinaifanya hoteli yako kuwa ya kipekee?

Justus: Naweza kusema kwamba tunajivunia hoteli yetu kuwa ndiyo pekee yenye maktaba katika Mji Mkongwe huu wa Zanzibar ambapo wageni wanayo fursa ya kujisomea masuala mbalimbali. Lakini pia ukiachana na hilo, Africa House Hoteli ndiyo hoteli pekee yenye mgahawa unaopika vyakula vya Kichina katika Mji Mkongwe wa Zanzibar. Mgahawa huu tumeujenga hivi karibuni, hakuna hoteli yoyote hapa yenye huduma kama hii, mgahawa unaendelea vizuri kwani tunapata maombi ya huduma mpaka moja kwa moja kutoka nchini China.



JT: Je unafikiri wateja wako ni wa aina gani? Kutoka ndani au nje ya nchi?
Justus: Naweza kusema kwamba idadi kubwa ya wateja wetu ni mchanganyiko, wengi wakiwa ni kutoka nje ya hapa Mji Mkongwe. Kwa wageni wa hapa nyumbani wengi tunaowapokea hupendekezwa na serikali na kwa wenyeji pia huwaleta au kuwaelekeza wageni wao kuja hapa.

JT: Ni shughuli gani zinazopendelewa kufanywa au kuuliziwa zaidi na wateja pindi wanapotembelea hoteli yako?

Justus: Asilimia kubwa ya wageni tunaowapokea hapa huja kwa madhumuni ya kibiashara au kikazi sio kwa mapumziko. Kwa ujumla, kama zilivyo hoteli nyingi kwenye Mji Mkongwe, hufanya sehemu hii ni kama kituo na kisha kuendelea na safari zao. Hivyo basi, mara nyingi wageni wanaofika hapa hulala kwa siku moja au mbili na kisha kuendelea na safari zao kama vile kwenda sehemu za ufukweni, uwanja wa ndege au bandarini.

JT: Una maoni gani juu ya ukuaji wa utalii wa ndani? Je kuna mabadiliko yoyote uliyoyaona?

Justus: Ukuaji wa utalii wa ndani kwa hapa Mji Mkongwe ni mzuri kwani wageni huongezeka mara kwa mara kadiri siku zinavyokwenda. Ingawa hatupokea wageni wengi wazawa kwenye hoteli yetu lakini kuna idadi kubwa ambao huwaleta wageni wao hapa. Hata kama hawatembelei hapa lakini kuna maeneo mengi ambayo tunawaona watalii wazawa wakitembelea na kwenye mitaa ya Mji Mkongwe.

JT: Unaizungumziaje Zanzibar kama mojawapo ya sehemu inayopendelewa kutembelewa zaidi? Je unadhani umaarufu wake unaongezeka au kupundua kadiri miaka inavyozidi kwenda?

Justus: Zanzibar kama kitovu cha utalii bado ni imara na kinaedelea kukua kadiri siku zinavyozidi kwenda. Wateja ni wengi na wanaendelea kuongezeka. Kwa mfano, kuanzia mwezi wa Julai, Agosti na huu wa Septemba ni vipindi ambavyo huwa tunapokea wageni wachache lakini tofauti na kipindi cha nyuma wateja ni wengi na kuna baadhi ya hoteli zimejaza vyumba na zingine zikiwa zimebakisha vichache! Hii ni ishara na dalili nzuri kwamba hali ni shwari huku Zanzibar ambapo kwa kipindi kama hiki hapo awali hakukuwa na wageni wengi kama sasa.

JT: Unazungumziaje kuhusiana na tozo mbalimbali kwenye sekta ya utalii, ukiachana na 18% za VAT, je zinaathiri biashara yako?

Justus: Kwa upande wangu naweza kusema kwamba Zanzibar haijaathirika na hizo tozo mbalimbali na sidhani kama zimeathiri biashara yetu. Kwa mfano, tozo ambazo zinalipwa ni zilezile na wageni kutoka nje ambao wanakuja nchini kuja kutembelea vivutio mbalimbali zikiwemo kodi na viingilio. Kama kungekuwa na athari basi tungewasikia wageni wakilalamika lakini wanaridhika na kuelewa kuwa ni taratibu ambazo ziko kama sehemu nyingine ukizingatia ni vivutio ndivyo wamekuja kuviangalia na sanasana huwashawishi na wageni wengine kuja kutembelea Zanzibar.

JT: Una maoni gani juu ya shughuli za mitandaoni kwenye kukuza sekta ya utalii nchini Tanzania?

Justus: Ni kweli dunia imebadilika hususani kwenye namna biashara zinavyoendeshwa siku za hivi karibuni. Kama zilivyo sehemu zingine, Zanzibar nayo imeipokea teknolojia ya mtandaoni vizuri kwa sababu idadi kubwa ya wageni tunaowapokea tunawapata kwa njia ya mtandaoni. Na kitu kizuri ni kwamba wanaiamini mitandao hiyo katika kufanya huduma zao na sisi tunajiimarisha kila kukicha kwenye Nyanja hiyo.

JT: Kwa kuongezea, unauzungumziaje ushirikiano baina ya Jumia Travel na hoteli yako? Unadhani ni msaada katika uendeshaji wa biashara yako?
Justus: Mahusiano na ushirikiano wetu na Jumia Travel ni mazuri kwani wanatusaidia kwa kiasi kikubwa kwenye uendeshaji wa shughuli zetu. Jumia Travel inakuja vizuri na inakua kwa sasa kwani mchango wake kwenye uendeshaji wa shughuli zetu ni mkubwa kutokana na wao kuwepo kwenye soko. Ukilinganisha na mwanzo ambapo kulikuwa na changamoto kadhaa kama vile kutokuwepo na mawasiliano ya kutosha pale kunapokuwepo na matatizo. Hivi sasa wanatutembelea na kuwasiliana mara kwa mara kujua tunafanyaje shughuli zetu. Naweza kusema wanastahili pongezi kwa hilo na naamini timu ya sasa iliyopo inafanya kazi vema na inajitambua zaidi.

Comments