- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
MOSCOW, RUSSIA
OFISA wa zamani wa Jeshi la Muungano wa Usovieti ambaye
anasifiwa sana kwa hatua yake ambayo huenda ilizuia vita vya nyuklia kati ya
Marekani na muungano huo wakati wa Vita Baridi amefariki dunia akiwa na miaka
77.
Stanislav Petrov alikuwa kwenye zamu katika kituo cha Urusi
cha kutoa tahadhari kuhusu nyuklia mapema siku moja mwaka 1983 mitambo ya
kompyuta ilipofanya makosa na kutoa tahadhari kwamba kulikuwa na makombora
yaliyokuwa yamerushwa na Marekani kuelekea Urusi.
Alichukua uamuzi wa busara kuamua kwamba tahadhari hiyo
haikuwa sahihi.
Aidha, hakupiga ripoti kwa wakuu wake.
Kitendo hicho chake, ambacho kilifichuliwa baadaye, huenda
kilizuia vita vya nyuklia.
Petrov alifariki dunia akiwa nyumbani kwake Moscow mwezi
Mei, lakini taarifa za kifo chake zimefichuliwa wakati huu.
Katika mahojiano na Idhaa ya Kirusi ya BBC mwaka 2013,
petrov alisema jinsi alivyopokea taarifa zilizopigwa chapa na kompyuta mapema
asubuhi ya 26 Septemba 1983 ambazo zilikuwa zinadokeza kwamba Marekani ilikuwa
imerusha makombora kadha.
"Nilikuwa na data zote [kudokeza kwamba lilikuwa
shambulio la makombora ambalo lilikuwa linaendelea]. Iwapo ningeituma ripoti
hiyo kwa wakubwa wangu, hakuna yeyote ambaye angezitilia shaka," amesema.
"Nilichohitajika kufanya ni kufikia simu; na kupiga
simu ya moja kwa moja kwa makamanda wetu wakuu - lakini sikuweza kusongea
kwenye simu. Nilijihisi kana kwamba nilikuwa nimekalia kikaangio."
Ingawa kwenye mafunzo yake alikuwa ameelezwa wazi kwamba
anafaa kuwasiliana na wakuu wa jeshi la Usovieti mara moja akipokea tahadhari,
Petrov badala yake aliamua kumpigia afisa wa zamu katika makao makuu ya jeshi
na akasema kulikuwa na hitilafu ya kimitambo.
Muungano wa Usovieti na Marekani wote
wawili walikuwa wameelekezeana silaha nyingi za nyuklia wakati wa Vita Baridi
Iwapo angekuwa amekosea, milipuko ya kwanza ya nyuklia
ingetokea dakika chache baadaye.
"Dakika 23 baadaye niligundua kwamba hakukuwa na chochote
kilichokuwa kimetendeka. Iwapo lingekuwa shambulio la kweli, basi kufikia
wakati huo ningekuwa tayari nimefahamu. Niliweza kupumua," anakumbuka.
Uchunguzi uliofanywa baadaye uligundua kwamba setilaiti za
Usovieti zilikuwa zimetambua kimakosa miali ya jua ambayo ilikuwa inaakisi
kutoka kwenye mawingu kuwa makombora yaliyokuwa yamerushwa.
Petrov, waliyestaafu akiwa na cheo cha luteni kanali,
alifariki dunia 19 Mei lakini habari za kifo chake zilifahamika zaidi mwezi
huu, kutokana na simu moja iliyopigwa kibahati.
Mwandaaji wa filamu kutoka Ujerumani, Karl Schumacher,
ambaye alifanya habari kuhusu kitendo cha Petrov kufahamika zaidi kimataifa,
alimpigia simu kumtakia heri siku ya kuzaliwa kwake mnamo tarehe 7 Septemba.
Hata hivyo, alifahamishwa na mwanawe wa pekee wa kiume wa
Petrov, Dmitry Petrov, kwamba alikuwa ameshafariki dunia.
Schumacher alitangaza habari hizo mtandaoni na hapo ndipo
zilipoanza kuenea kwenye vyombo vingine vya habari.
CHANZO: BBC
Comments
Post a Comment