- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Unknown
on
- Get link
- X
- Other Apps
Mwandishi wa makala hii, Daniel Mbega (kushoto) akiwa na King Kester Emeneya katika iliyokuwa Hotel Embassy mwaka 2000.
Na Daniel Mbega
NAYAKUMBUKA maneno yake tukiwa
katika Hotel 77 jijini Arusha, siku ya Ijumaa, Novemba 24, 2000, akiniambia kwa
Kilingala: “Mdogo wangu Danny, nimemaliza fedha zote na sina cha kukupa kwa
sababu nilikuja Tanzania kurekodi video ya albamu na nimeshakamilisha, sasa
nataka niondoke na wewe twende Paris, halafu utatafuta chuo usome, ukimaliza
utachagua mwenyewe urudi Tanzania ama utafute kazi huko!”
Namzungumzia mwanamuziki nyota wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Jean Baptiste Emeneya Mubiala Kwamambu ambaye
alifahamika zaidi kama King Kester Emeneya, kiongozi wa bendi ya Victoria
Eleyson.
Urafiki wetu ulivuka mipaka na kuwa
udugu, ambapo kila wakati hakuniita ‘Mwandishi’, bali hata alipokuwa hanioni
alipenda kuuliza: “Petit na ngai Danny eza wapi?” Akimaanisha “Mdogo wangu Danny
yuko wapi?”
Siyo kwa sababu ya kuwa naye bega
kwa bega kwenye kazi zake akiwa hapa nchini, ambako alikuja mara mbili, lakini
pia alisema wazi kwamba nilifanana mno na mdogo wake wa damu.
Hakuwa na mzaha aliponiambia kuhusu
suala la kwenda naye Paris, maana pale pale akamwita meneja wake, Guy
Kimvula, na kumwelekeza kwamba afanye booking Nairobi, Kenya pamoja na jina
langu, maana ndiko walikokuwa wanaondokea kurudi Paris, ingawa ilikuwa lazima
warudi kwanza Dar es Salaam ilikokuwa mizigo yao na ndiko wangechukua ndege
kuelekea Nairobi kabla ya kwenda Ufaransa.
“Una passport!” akaniuliza tena kwa
Kilingala, nikamwambia: “Ninayo lakini iko nyumbani Dar es Salaam.”
“Hakuna shida, tunaondoka leo
kwenda Dar es Salaam, keshokutwa itabidi twende Nairobi na mipango mingine yote
tutakamilisha huko. Lakini tukifika Paris mimi nitakuacha pale nakwenda New
York, Marekani nina shoo huko, nitarejea baada ya wiki mbili,” akaniambia.
Alikuja mara ya kwanza mwezi Julai
2000, kimya kimya, halafu naweza kusema ni mimi mwandishi peke yangu niligundua
ujio wake kwa sababu hakupenda yeyote ajue. Nikafanya naye mahojiano pale
Embassy Hotel – wakati huo ikiwa juu zaidi, na tangu hapo tukajenga urafiki
uliokuwa kama udugu. Pengine ni kutokana na kuifahamu vyema historia yake na
maswali niliyokuwa nikimuuliza, kwani mambo mengine, hasa yaliyomuumiza katika
maisha yake ya muziki, ni wazi hakupenda kuyakumbuka na hakujua kama kulikuwa
na mtu nchini Tanzania ambaye alikuwa anayafahamu.
Alifahamu kwamba watu walikuwa
wanajua kuwa yeye alikuwa mmoja wa wanamuziki waliounda kundi la Les 7 Patrons
de Langa Langa Stars (Wakali Saba wa Langa Langa Stars), lakini swali kwamba
ilikuwaje yeye alifumu na kundi hilo kwa wiki mbili tu mara baada ya
kuanzishwa, kamwe hakulitegemea.
Wakati ulipotokea mgogoro wa
uongozi na mapinduzi ambayo hayakufanikiwa ndani ya Viva la Musica mwaka 1981 huku
yeye akiwa kipenzi cha Papa Wemba katika safu ya uimbaji na Koffi Olomide akiwa
kinara wa utungaji, Emeneya aliondoka pamoja na Esperant Djenga Ka, Djuna
Djanana na Dindo Yogo kwenda kuungana na Evoloko Jocker, Djo Mali na Bozi
Boziana (watatu hao kutoka Zaiko Langa Langa) na kuanzisha kundi hilo la 7
Patrons Langa Langa Stars.
Hata hivyo, yeye alidumu kwa wiki
mbili tu, halafu akarejea Viva La Musica kabla hajaondoka kwa mara nyingine Desemba
24, 1984 na kuanzisha bendi yake ya Victoria Eleyson.
“Wewe umejuaje?” aliniuliza wakati
huo. “Najua ulikuwa mdogo wakati huo!”
Nilimwambia kwamba, mimi nilikuwa
mfuatiliaji mkubwa wa muziki wa Congo na zaidi nilikuwa shabiki namba moja wa
nyimbo zake, kuanzia ‘Nzinzi’ na hata
alipotoa albamu yake ya Polo Kina mwaka
1992 na mtindo wake wa Kidekune.
Naam. Namkumbuka kwa namna
alivyoishi hata na wanamuziki wake kama familia moja, siyo mwajiri na
mwajiriwa. Alikuwa kama baba kwa wanamuziki wake, wengine wakimfanya kama babu
kutokana na kumtania.
Ungemuona wala usingejua kama ni
mzungumzaji. Ndiyo, hakuwa mzungumzaji sana, bali mtu wa vitendo, lakini
alipoamua kupiga stori, hasa kama ‘mnaiva’, basi ungependa. Siku zote alikuwa
mtu wa mipango.
Wakati tunazungumza hapo 77 Hotel
Arusha, tayari alikuwa amekamilisha kurekodi video ya albamu yake ya Longue
Histoire (Hadithi Ndefu) iliyokuwa na Volume I na II ambayo ilirekodiwa na Calbass'
Productions ya Paris, ambapo niliongozana naye kwenda Bagamoyo, Zanzibar na
maeneo mengine ya Dar es Salaam kabla ya kwenda Moshi na Arusha.
Volume I ilikuwa na nyimbo za But Na Filet, Maousso, Washington, Lilas, Noni,
Cigarette, Beatrice, Mimo na Mobeti
Mbonda, wakati Volume II ilikuwa na nyimbo za Mademoiselle, Kimpiabi Bala, Didier Okito, Mamie, Mvula Mitano, Fololo,
Basali Nteke, Pierroccini, Yo Ba Mbongo.
Ni wakati huo alipokuwa ameibuka na
rap mbili mpya za Chakou Libondasi na
Kiwanzenza kupitia kwa marapa wake Eric
Masudi na Guy Moller.
Ni rap ambayo Ally Choki akiwa African Stars 'Twanga Pepeta' aliamua kuichukua na kuweka maneno ya Kiswahili anaposema: "Tunatesa, Twanga Pepeta, hatutaki shari!" wakati Guy Moller alikuwa anasema: "Kiwanzenza, kiliba yaye eee kalika libonge!"
Ukiitazama DVD ya albamu hiyo
utaona kwamba hata mwanadada aliyeigiza kwenye wimbo wa ‘Mousso’ ni Mtanzania,
na wanamuziki wake walivalia mavazi ya Kimasai na kadhalika.
Picha iliyochukuliwa katika clip ya wimbo wa Mousso ambapo wanaonekana rapper Guy Moller, King Kester, Binti wa Kibongo na mwenye rasta na koti jeusi ni Zoe Bella, kaka wa Christian Bella.
Wakati tuko Arusha, siku hiyo
asubuhi ilikuwa twende Mirerani kwa ‘Wazungu wa Mawe’ ambao walitaka kwenda
kutumbuizwa, lakini alipiga hesabu na kuona kwamba ratiba yake ingembana, hasa
kutokana na ziara ya New York na alikuwa pia aende Japan baada ya kutoka
Marekani.
Nimepata kusafiri na wanamuziki
wengi nyota wa kimataifa, lakini kusafiri na kundi la Victoria Eleyson kulikuwa
tofauti sana. Wanamuziki wote walikuwa kama ndugu, tulizungumza na kucheka bila
wasiwasi kwa sababu lugha ya Kilingala haikuwa kikwazo kwangu. Hili nalo
liliwafanya wanamuziki wote wasiamini hata nilipowaambia kwamba mimi ni
Mtanzania.
Zoe Bella, kaka yake Chritian Bella,
yeye mpaka anaondoka ananimbia: “Wewe mutu ya Kisangani, siyo Mutanzania!”
Alikuja na wanamuziki wake wengi
ambao alikuwa amedumu nao kwa muda mrefu ingawa wengine walikwishaondoka. Lakini
miongoni mwa aliokuja nao, ukiacha mwimbaji Zoe Bella, Erick Masudi na Guy
Moller, ni mpiga kinanda Djudjo Chet Music, waimbaji Anthony Sampayo, Sweet
Elesse, Denison Lutula, Spino Nola, Dikando Bols, Guejo Star Gelena, wapiga
magitaa Auguy Lutula, Willy Ebondaki, Ade Lokela na Zozo Malaba, pamoja na
mpiga bass Yves Tshum Tshum, mpiga konga Signora Depatra Uomo na mpiga drums Baby
Mbonda.
Mara kadhaa alipokuja Kinshasa,
alikuwa akiniagiza niende kumtembelea.
Lakini, kama alivyosema Joseph
Kabasele Yampanya ‘Pepe Kalle’, “Liwa ya Moyibi”, yaani “Kifo ni mwizi!” Hakika
kifo si kitu kizuri kabisa hapa duniani japokuwa kila nafsi lazima ionje mauti.
Kama kilivyofanya kwa Pascal Emmanuel
Sinayomi maarufu kama Tabu Ley Rochereau ndivyo kilivyofanya kwa Emeneya, mwanamuziki
mkongwe, msomi na mahiri, pale kilipomchukua akiwa kitandani jijini Paris, Ufaransa
Alhamisi ya Machi 26, 2014.
Jeneza lililokuwa na mwili wa King Kester Emeneya wakati wa kuagwa jjijini Kinshasa.
Mwanamuziki huyo aliiacha dunia
ikiwa na amali zake nyingi ambazo zitakumbukwa milele na wapenda muziki tangu
wa rhumba hadi ule wa kimataifa wenye mahadhi ya kizazi kipya (funky).
Nakumbuka nilipofanya naye
mahojiano mwaka 2000, alitamka wazi kwamba wanamuziki wengi wa Congo alimtukana
sana mwaka 1987 wakati alipoibuka na wimbo wa ‘Nzinzi’.
Maneno ya kwenye wimbo huo hayakuwa
na nongwa, tatizo ni midundo hasa baada ya kuingiza vyombo vingi vya ‘kutengeneza’
vya kielektroniki badala ya kupiga vyombo mubashara kama ilivyokuwa ada kwa
muziki wa Congo.
Lakini wimbo huo wa Nzinzi
uliotengenezwa na studio kubwa ya Sonny Disc, ambao wakongwe walimtukana,
ukaibuka wimbo bora wa Congo kwa karibu miaka miwili mfululizo huku ukishika
pia chati za juu duniani.
Wimbo huo unaelezea mwanamume
ambaye ameoa, lakini hataki kumpendezesha mkewe na badala yake anawanyatia wake
za watu ambao wamependezeshwa na waume zao akiwamwagia fedha kede kede. Mwanamume huyu anafananishwa na Nzi (Nzinzi) na anaambiwa
kwa nini usitumie fedha hizo kumpendezesha mkeo?
Nimeuweka hapa kwa maneno ya
Kilingala:
1)
Mwasi ya bato elengi mingi na ko lula ye
Yayo
moko po nini obongisaka ye te
Moninga
abongisi elengi mingi nako lula ye
Ya
yo moko po nini o vivaka ye te
(Bongisa
mwasi nayo Nzinzi eh eh)
Ebele
ya mbongo oh yo oko zuaka papa
Kaka
ba kwiti na basi oyo ba hina mabala oh
2)
(Bongisa mwasi nayo oh Nzinzi eh eh)
Ne
la laisse pas tomber
Elle
est si fragile
(Bongisa
mwasi nayo oh Nzinzi eh eh)
Ebele
ya mbongo oh yo oko zuaka papa
Kaka
depense na basi oyo ba hina mabala oh
3)
(Bongisa mwasi nayo oh Nzinzi eh eh)
Ne
la laisse pas tomber
Elle
est si fragile
Oh
Nzinzi eh eh eh
Mobali
mabe oh, Nzinzi eh eh eh
Yo
mobali mabe oh
4)
Oh Nzinzi eh eh eh
Yo
type kolo, Nzinzi eh eh eh
Yo
type Kolo
Oh
Nzinzi eh eh eh
Kitoko
ya pampa oh, Nzinzi eh eh eh
Tala
ndenge o nzulusi nga
Oh
Nzinzi eh eh eh
Ba
fiere ya pamba oh, Nzinzi eh eh eh
Yo
mobali mabe eh
5)
Mbanda a lati jaune oh
Nga
na lata rose oh yoh oh oh
Mbanda
a lati vert oh nga na lata blue oh yoh oh oh
Mbanda
a kumbi Benz oh
Nga
na kumba Rolls oh, yoh oh oh
Mbanda
na Ferrari
Nga
na Lamborghini, yoh oh oh
Mbanda
a kumbi BMV oh
Nga
na kumba nini, yoh oh oh
Mbanda
a lati rose oh
Motema
nanga mpasi eh, yoh oh oh
6)
Oh Nzinzi eh eh eh
Mobali
mabe oh Nzinzi eh eh eh
Yo
mobali mabe oh
Oh
Toko eh eh eh
Yo
type kolo oh Toko eh eh eh
Yo
mobali mabe eh
7)
Oh Christino eh
Yo
type kolo oh Christino eh
Tala
ndenge o nzulusi nga
Oh
Nzinzi eh eh eh
Mobali
mabe oh Nzinzi eh eh eh
Yo
mobali mabe oh
Alikotokea…
Jean Baptiste Emeneya Mubiala
Kwamambu alizaliwa Novemba 23, 1956 huko Kikwit katika Jamhuri ya Kiemokrasia
ya Congo. Alikulia katika mazingira ya kidini na wakati nilipozungumza naye,
alisema kwamba alitamani sana awe Padre kabla ya kubadilisha uamuzi na kusomea
elimu dunia, ambapo alihitimu shahada ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha
Lubumbashi mwa 1977.
Alianza kujihusisha na muziki tangu
akiwa chuo kikuu na mwaka 1977 alijiunga na Viva la Musica akitokea Isifi
Lokole na kibao chake cha kwanza ndani ya Viva la Musica cha Milena kilichowaacha hoi-bin-taaban
mashabiki wa muziki ndani na nje ya DRC.
Kama kawaida ya wanamuziki
kuhitilafiana, mwaka 1982 ulikuwa mbaya kwa Papa Wemba kwani kulitaka kufanyika
mapinduzi ya uongozi ndani ya bendi hiyo lakini yalishindikana.
Uasi huo ulisababisha wanamuziki
kadhaa mahiri wa bendi hiyo kujitenga na kila mmoja kuanzisha kundi lake
lililojipambanua kuwa ni mpinzani mkubwa wa bendi ya Viva la Musica.
Wanamuziki hao ni pamoja na Dindo
Yogo aliyejiunga na Zaico, Djuna Djanana, Debaba Star na Pepe Bi Polie
walioanzisha bendi yao ya Chocky Star, Kisangani Esperent aliyeanzisha Langa
Langa Star na Koffi Olomide aliyeamua kuwa mwanamuziki huru hadi alipoanzisha
bendi yake ya Qarte Laten.
Katika vuguvugu hilo, Emeneya
alianzisha bendi yake ya Victoria Eleyson ambapo miaka mitano baadaye alitoka
na wimbo kabambe wa “Nzinzi”
aliouimba akiwa na kundi maarufu la Kassav la Visiwa vya Carrebean.
Wachungizi wa masuala ya muziki
wanasema kuwa Emeneya mpaka anarudi kwa Mungu Baba hakuweza kupiga kibao
kilichoichengua dunia kama hicho.
Ukweli huo unatokana na jinsi
ulivyoimbwa kiufundi kwa kurekodi na Studio ya kimataifa ya Sony Disc ambayo
iliingiza madoido na vimbwanga kabambe na kuufanya uwe wa kimataifa zaidi.
Wimbo wa “Nzinzi” ulimpatia Emeneya
mkataba wa miaka saba kufanya kazi nje ya DRC na kumfanya apae kimuziki na
kupendwa na mashabiki wa kila rika wa dunia.
Ukichanganya na utanashati wake wa
uvaaji nguo murua, Emeneya alikuwa mpenzi wa vijana wa iliyokuwa Zaire na
kumfanya awe “pedeshee” wa kukata na shoka.
Pamoja na kuizunguuka dunia, lakini
Emeneya hakukosa kufika Tanzania ambako alitumbuiza kwenye ukumbi maarufu wa wakati
huo wa Silent Inn jijini Dar akiwa pamoja na akina Dodoo La Zeula Bouche na
bendi yao ya MK Sound.
Wakati huo ndio alikuwa juu ya
dunia na mtindo wake wa “Kide Kune”
ambao ulisheheni vimbwanga vya uchezaji na upigaji Drums kwa umahiri na
kuwachanganya mashabiki wasikae vitini wakati akipiga nyimbo zake.
Emeneya alikuwa mwanamuziki pekee
wa DRC ambaye alifanya onyesho lililoingiza watu zaidi ya 80,000 kwenye ukumbi
wa Studio Manue Engebi jijini Kinshasa aliporejea akitokea duniani baada ya
mkataba wake alioingia na Sony Disc kumalizika mwaka 1984.
Kadhalika mwaka 2002 mwanamuziki
huyo alifanya onesho kabambe kwenye ukumbi wa Zenith jijini Paris Ufaransa,
ukumbi ambao ulizinduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1973 na Tabu Ley na kuujaza
kimakwelini.
Akiwa mzaliwa wa jimbo la Ikwiti
huko Lubumbhashi, Emeneya alijikuta bila kutegemea akiwa tajiri wa kutupa kwa
wimbo wake wa “Nzinzi”.
Kwani, pamoja na nyimbo zake kadhaa
kati ya 1000 alizopiga katika uhai wake, wimbo huo ulimtofautisha na wanamuziki
wengine wengi wa bara la Afrika.
Wachunguzi wa masuala ya muziki
wanasema kuwa wimbo huo ulimfanya awe nje zaidi ya nchi yake na hivyo kufanya
baadhi ya watu ndani ya DRC kutomfahamu zaidi ya kumuona kwenye mitandao kama
Yu-Tube, TV na magazeti.
Sifa kubwa ya Emenea ni uwezo wake
wa kila mwaka kuipua kibao kinachotingisha anga la muziki wa dunia kama kile
cha “Okosi Ngai Mfumu” ambacho kilimfanya awe mwanamuziki bora wa Zaire mwaka
1983.
Akafunga kazi mwaka 1992 na wimbo
wake wa “Polo kina mfundo” ambao ulikisindikizwa na kuhanikizwa na mirindimo
mikali ya mtindo wake mpya uliomuongezea umaarufu wa “Kide kune”.
Hata hivyo, Emeneya alitengeneza
“bifu” la sheria yake kati yake na Wenge Musica mwaka 1994 kiasi cha kuwa
maadui kama Paka na chui.
Kisa kilitokana na kile
kilichodaiwa na wanamuziki wa Wenge Musica kuwa Emeneya alikuwa amewatukana
pale walipokutana kwenye jukwaa moja jijini Kinshasa.
Katika mchuano huo uliohudhuriwa na
watu wengi na hasa vijana watanashati kutokana na bendi zote mbili kuwa na
utitiri wa vijana, Emeneya alipiga wimbo maarufu wa bendi ya Wenge Musica wa “Kala yi Boinge” (Kama Ndege Boieng) kwa
umahiri uliotopea.
Alipomaliza kutumbuiza wimbo huo
akawataka Wenge Musica nao wapige wimbo wake wa “Nzinzi” ambapo vijana hao machachari walishindwa.
Ndipo alipowaambia, “Nyinyi kumbe
ujanja wa bure lakini hamjui muziki. Mimi ndio baba lao kwenu. Nimepiga wimbo
wenu pasipo mazoezi hata kidogo. Nyinyi bado makinda kwangu”.
Maneno hayo yaliwauma vijana wa Wenge
Musica ambao waliapa kuwa wasingeshirikiana tena na Emeneya katika mambo yoyote
yale.
Hata hivyo, mpiga solo wao
mashuhuri, Allan Makaba, alikuja baadaye kufanya “kolabo” na Emeneya, kitendo
ambacho kilisababisha asakamwe na wenzake.
Inaelezwa kuwa kitendo hicho cha
kusakamwa ndiyo sababu kubwa ya Makaba “mchawi wa solo” kujitoa Wenge Musica na
kuwa “Mwanamuziki wa Studio” (Recording Artist).
Mambo hayo ndugu zanguni. Basi
ndiyo hivyo; Emeneya, aliyezaliwa Novemba 23 mwaka 1956 alitutoka kwa
ugonjwa wa moyo na shinikizo la damu ambavyo baadhi ya watu wake wa karibu
wanasema maradhi hayo yalisababishwa na mshtuko wa kifo cha Pascal Onema
maarufu “Tabu Ley” mwishoni mwa mwaka 2013.
Inaelezwa kuwa kifo hicho
kilimmaliza nguvu kwa huzuni iliyotopea na hivyo kumfanya akate tamaa ya maisha.
Yote kwa yote dunia haitasimama
bali itaendelea kuwako huku mashabiki wa muziki wakimhani kwa masikitiko
makubwa mwanamuziki huyu mtanashati “King Kester Emeneya”.
Baadhi ya nyimbo alizoziimba na
mwaka katika mabano ni pamoja na Milena
(1977), Teint de Bronze (1978), Ndako ya Ndele (1979), Musheni (1979), Kayole (1979), Fleur d'ete
(1978), Ngonda (1979), Dikando (1980), La Runda (1980), Ata Nkale
(1979), Dembela (1981), Naya (1982), Ngabelo (1982), Okosi ngai
mfumu (1983), Surmenage (1984), Kimpiatu (1985), Willo mondo (1985), Wabelo
(1986), Manhattan (1986), Deux Temps (1987) na Nzinzi (1987).
Nyingine ni Mokusa (1990), Dikando Remix
(1991), Polo Kina (1992), Every Body (1993), Live in Japan (1991), Every
Body (Remix) (1995), Pas de contact
(1995), Succès Fous (1997), Mboka Mboka (1998), Never Again Plus jamais (1999), Longue
Histoire (Volume 1 & 2) (2000), Live
au Zénith de Paris (2001), Live à
l'Olympia (Bruno COQUATRIX) de Paris (2002), Rendre à César ... ... ce qui est à César (2002), Nouvel ordre (2002) na Le Jour Le Plus Long (2007).
Katika miaka mingine yote hadi
anakufa, Emeneya amekuwa akialikwa na kufanya maonesho kadhaa dunia nzima huku
wengi wakidhani alikuwa amestaafu muziki.
Comments
Post a Comment