Featured Post

POLISI WAREJEA NA MEDALI MICHEZO YA MAJESHI

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akipokea kombe la ushindi wa tatu kutoka kwa Inspekta Hashim Abdallah wakati wa mapokezi ya wanamichezo wa Polisi waliokuwa wakishiriki Michezo ya Majeshi ya Polisi kwa nchi za Afrika Mashariki (EAPCCO Games) nchini Uganda. (Picha na Jeshi la Polisi)
 

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akimpongeza Mwanariadha wa Polisi PC Basili John baada ya kushinda medali ya Dhahabu katika Michezo ya Majeshi ya Polisi kwa nchi za Afrika Mashariki (EAPCCO Games) nchini Uganda hivi karibuni ambapo Polisi Tanzania ilishika nafasi ya Tatu kati ya nchi saba zilizoshiriki michezo hiyo. (Picha na Jeshi la Polisi)

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akimpongeza Mwanamichezo wa Polisi Koplo Gaston Komba baada ya kushinda medali ya shaba kwa upande wa Tae Kwon Do katika Michezo ya Majeshi ya Polisi kwa nchi za Afrika Mashariki (EAPCCO Games) nchini Uganda hivi karibuni ambapo Polisi Tanzania ilishika nafasi ya Tatu kati ya nchi saba zilizoshiriki michezo hiyo. (Picha na Jeshi la Polisi)

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro na Viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja na Wanamichezo wa Polisi walioshiriki katika michezo ya Majeshi ya Polisi kwa nchi za Afrika Mashariki (EAPCCO Games) nchini Uganda hivi karibuni ambapo Polisi Tanzania ilishika nafasi ya Tatu kati ya nchi saba zilizoshiriki michezo hiyo.(Picha na Jeshi la Polisi)

Na Jeshi la Polisi
Wanamichezo wa Polisi walioshiriki michezo ya Majeshi ya Polisi kwa nchi za Afrika Mashariki (EAPCCO Games) Kampala Uganda wamerejea nchini ambapo wamefanikiwa kujinyakujilia jumla ya medali 6, 1 ya dhahabu, 2 za fedha na 3 za Shaba na hivyo kuibuka mshindi wa tatu kwa ujumla katika michezo hiyo iliyoshirikisha majeshi ya Polisi kutoka nchi saba.

Wanamichezo hao wamepokelewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro ambapo alisema Jeshi hilo litaendelea kushiriki michezo mbalimbali ili kujenga afya na ukakamavu kwa Askari pamoja na kuboresha mahusiano ya utendaji kazi katika kubadilishana uzoefu na kuiletea sifa nchi.
IGP Sirro alisema wanamichezo hao wamefanya kazi kubwa ambapo pamoja na uchache wao wameonyesha kuwa wako vizuri katika michezo jambo ambalo ni hazina kubwa kwa Jeshi la Polisi Tanzania.
Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Jamii Mussa Ali Mussa alisema michezo hiyo imeliletea sifa taifa la Tanzania na Jeshi la Polisi kwa ujumla hivyo kuna haja ya kuhakikisha kuwa wanamichezo hao wanakaa kambini muda mrefu pindi itakapojitokeza michezo mingine ili waweze kufanya vizuri zaidi.
Naye mshindi wa medali ya Dhahabu katika riadha mita 800 PC Basil John amesema Michezo hiyo ilikuwa na ushindani mkubwa lakini walijitahidi kupambana ili kuhakikisha wanarejea na medali licha ya kuwa  wachache katika michezo hiyo ya majeshi ya Polisi.
Michezo hiyo ilifanyika Agosti 25 mpaka 30 mwaka huu ambapo nchi zilizoshiriki ni pamoja na mwenyeji Uganda, Tanzania, Kenya, Rwanda, Sudan, Burundi pamoja na Sudani Kusini ambapo Uganda ilichukua ushindi wa kwanza, Kenya wa pili na watatu Tanzania.

Comments