Featured Post

NSSF ARUSHA KUWASHTAKI WAAJIRI 126 KWA KOSA LA KUTOWASILISHA MICHANGO YA WAAJIRIWA INAYOFIKIA SHILINGI BILIONI


 Meneja kiongozi wa NSSF mkoa wa Arusha katikati  Dr. Frank Maduga akizungumza na waandishi wa habari juu ya kuwapeleka waajiri 126 mahakamani kwa kosa la kutowasilisha michango ya waajiriwa inayofikia kiasi cha shilingi bilioni moja nukta tano kwa kipindi cha miezi sita sasa.  


NA ANDREA NGOBOLE, PMT
Jumla ya Kampuni 126 zinazodaiwa kiasi cha shilingi bilioni moja pointi tano zinatarajiwa kufikishwa mahakamani wiki ijayo na shirika la Taifa la hifadhi ya jamii NSSF mkoani Arusha kwa kosa la kutowasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa kipindi cha miezi sita iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mapema jana meneja kiongozi wa NSSF mkoani Arusha Dr. Frank Maduga amesema kuwa makampuni hayo yamegawanyika kati ya waajiri wakubwa 14 wanaolipia kiasi cha shilingi milioni 50  na kuendelea, wajiri wa kati 69 wanaolipia milioni 5 hadi 49.9 na wale waajiri wadogo 53 wanaolipia kiasi cha shilingi elfu ishirini hadi milioni  4.9 kwa mwezi ambapo jumla ya michango yao inafikia Zaidi ya bilioni moja nukta tano mpaka sasa.

“Waajiri wakubwa wote wamekwisha pelekewa onyo la Mwisho na sasa taratibu za kimahakama zinaendelea hivyo kuanzia jumatatu ya tarehe 2 october 2017 mtawajua ni waajiri gani wameshindwa kutekeleza wajibu wao na kwa kiasi gani wanadaiwa kila mmoja wao” alisema dokta Maduga

Amesema kuwa Mashitaka yatakayokuwa yakiwakabali waajiri hao ni kutowasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati na kwa muda unaozidi miezi sita, kitendo hicho kimekuwa na madhara makubwa kwa wafanyakazi na wategemezi wao kwa kukosa huduma za matibabu , fao la uzazi na pia kuna baadhi ya wanachama taarifa zao za kumbukumbu hazioneshi fedha yoyote katika muda ule ambao michango haijawasilishwa na kusababisha taharuki na msongo wa mawazo kwa wafanyakazi husika.

Mwanachama ana haki ya kulipwa michango yake yote akiacha kazi au kampuni ikifa na kuacha kuendesha biashara hulazimika kulipa fedha zote za michango ya wanachama na wao kama taasisi inayosimamia haki za waajiriwa huhakikisha malipo yote yanalipwa na kutolea mfano kampuni za snowcrest na mukidoma zilizositisha shughuli zake na kutangaza kufilisika  walihakikisha kuwa kila mfanyakazi anapata mafao yake bila wasiwasi wowote.

Amesisitiza kuwa mwanachama akishaacha kazi atasubiri kwa kipindi cha miezi sita ndiyo aweze kupewa fao la kustaafu na kipindi hiki huwekwa ili kumpa nafasi mwanachama kuweza kutafuta kazi na ama kuajiriwa na kampuni nyingine na changamoto inayowakabili ni kuwa baadhi ya wanachama hufoji barua za kuacha kazi ili waweze kupewa mafao yao huku bado wanafantya kazi jambo ambalo halikubaliki kwa mwanachama kulipwa fao lake huku anafanya kazi.

Naye Straton Simon Afisa msimamizi wa fao la matibabu NSSF kanda ya kaskazini inayowakilisha mikoa ya ARUSHA,KILIMANJARO, TANGA na MANYARA amesema kuwa fao la matibabu hutolewa bure na mfuko huo kwa kila mwanachama anayekuwa amewekewa michango yake kwa miezi mitatu  na kuendelea na fao hili halihusiani na kukatwa akiba yako siku utakayostafu kazi au kampuni yako kusimama kufanya kazi hivyo amewataka wanachama wasiwe waoga kutumia fao hili kwani lina faida kwa mwanachama na wategemezi wake wane ambao ni mke au mume na watoto wane.

Amesema kwa Arusha pekee NSSF ina mkataba wa matibabu kwa wanchama wake na hospitali 34 zinazotibu wanachama wote wa hiari na wale waajiriwa ambao mpaka sasa wanafikia 18,400  na kwa kanda nzima ya kaskazini wanafikia wanachama 34000 wanaopata fao hilo la matibabu na kuwasihi wanachama wengine wote wahakikishe wanajaza fomu na kuchagua moja ya hospital ambayo ungependa kutibiwa kati ya hizo hospitali 34 ili wanufaike na fao hilo muhimu kwa maisha ya mwanachama.

Comments