Featured Post

KANDA BONGO MAN ALIVYOFIKIA UFALME WA MUZIKI AFRIKA

Kanda Bongo
Kanda Bongo Man akiwa na mwandishi wa makala haya Hemed Kimwanga, wakati huo akiwa mhariri wa burudani wa gazeti kongwe la Mfanyakazi.

Na Hemed Kimwanga
KUNA binadamu watano hapa duniani ambao hulka, weledi na umahiri wao katika sanaa havitapatikana au kufanywa na yeyote yule labda ipite miaka 200 kuanzia sasa.
Hata hivyo, silika, weledi na umahiri wa binadamu hao umetofautika kuanzia ule wa soka, masumbwi, karate, kung-fu hadi muziki.

Katika muziki dunia haitapata mtu mwenye mvuto na mwenye hisia kali kama Micahel Jackson maarufu ‘The Wacko Jacko’ wa Marekani ambaye alitamalaki katika muziki aina ya ‘Pop’ kiasi cha kuwa mchawi na mfalme wake.
Mwingine ni Nesta Robert Marley maarufu kama ‘Bob Marley’ wa Jamaica ambaye alitamalaki pia kwenye muziki aina ya ‘Reggae’ ukiwa na nasaba na pilikapilika za ukombozi wa fikra na nadhari kiasi cha kumfanya binadamu ajitambue.
Bila shaka hakuna atakayekataa kwamba Bruce Lee wa Hong Kong ambaye alitoroka nchini mwake kwenda Marekani ambako alifichua siri ya unyago wa Wachina katika sanaa ya ‘Kung-fu’ iliyotumika kujihami wakati wa vita ni binadamu mwingine ambaye hatatokea kwenye karne hii labda ipite miaka 200.
Kanda Bongo Man akifanya vitu vyake.
Bruce, katika karate na mateke alikuwa mwepesi kama mwanga wa umeme, mwili wake ulijikunja namna alivyotaka. Alijua kuuchezea na kuuweka sawia hata kujilinganisha na Paka katika kunyata na kusaka adui bila miguu au viatu kusikika huku macho yake yakiona hata kwa kupitia kisogoni.
Wataalamu wa filamu wanasema kuwa Bruce Lee alifanya kazi kwa mikono na mwili wake kwa asilimia 95 ya picha nzima bila kutegemea ‘uongo wa computer au teknolojia’; yaani ‘screen play’ ambayo yeye aliitumia kwa asilimia tano tu kwenye picha zake. Ujasiri huu ulimpa umaarufu mkubwa na nd’o kiini cha maelezo haya.
Hawa watatu hatunao tena katika dunia hii. Lakini kuna wengine wawili ambao bado tunao na ni vyema tukaomba kwa Mola tuendele kuwa nao hadi siku itakapofika ya historia kujirudia.
Mmoja wa watu hao wawili ni Edson Arantes do Nascimento maarufu kama ‘Pele’ wa Brazil. Huyu, historia iliyokwishaandikwa kufikia leo hii, inasema kuwa hajawahi kuishi binadamu mwenye uwezo wa kucheza soka au kandanda kama yeye.
Uchezaji wake, hapan’shaka ulizingirwa na maajabu, ujuzi, silika, weledi na umakini hata kufananishwa na uchawi.
Wazungu ambao wanaaminika kuwa nd’o walioendelea kuliko binadamu wengine hapa duniani, wanakubali kuwa Pele ni mchawi wa soka.
Wamewahi kumuita kwa majina mengi yanayoshabihisha ‘uchawi’ kama vile ‘maestro’, ‘legendary’, ‘wizardy’, ‘uncompromising’, ‘ace’ na sema mengine utakayo.
Kwa hakika na bila ubishi wowote, majina yote hayo yanaashiria kuwa Pele hakuwa mtu wa kawaida katika soka.
Wa mwisho lakini si wa kubeza katika dawati hilo ni Cussius Clay maarufu kama Muhammad Ali wa Marekani. Huyu alikuwa mwana-masumbwi ambaye pengine naye hatatokea katika dunia hii mpaka ipite miaka 200.
Hili alilisema mwenyewe mwaka 1973 wakati alipohojiwa na waandishi wa habari wa kimataifa akiwa katika matayarisho ya kupambana na George Foreman jijini Kinshasa, DRC mwaka uliokuwa ukifutia.
Alisema, “You will never get somebody like me for another 200 years”.
Alikuwa na maana ya kusema kwamba dunia haitampata mtu wa kufu yake mpaka baada ya miaka 200.
Hapa barani Afrika, yuko mwanamuziki ambaye alailitetemesha bara hili nadunia nzima kwa muziki wake wa “Kwasa Kwasa” kiasi cha kupendwa kama chumvi mbogani au sukari kwenye chai.
Hata hivyo, Kanda Bongo Man anasema kitendo cha kufukuzwa kwake nchini Kenya kwa saa nne kilimsaidia kujenga jina lake duniani. Kwani mwaka mmoja baadaye aliweza kupata mwaliko mnono wa kuja Bongo kwa ziara ya mwezi mmoja.
Ziara ya kwanza mwaka 1992, alialikwa na aliyekuwa mfanyabiashara maarufu kwa wakati huo, Rogers Malila wakati ziara ya pili alialikwa mwaka huo huo na Paul Lyimo, mmiliki wa iliyokuwa hoteli maarufu ya Bushtrekkers ya jijini Dar.
Lyimo kwa sasa anamiliki hoteli ya ‘La Prima’ ikimaanisha kwa lugha ya Kitaliano, ‘Nambari Wani’, pia ya Dar.
Wakati nchini Kenya alipata msukosuko mkubwa uliosababishwa na mke wa Rais, hapa Bongo alikaribia kumponza Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi kiasi cha kukiona kiti chake kuwa cha moto.
Kwani ujio wake hapa Bongo kwa mara ya pili ulikutana na mgomo mkubwa wa manesi na madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Wafanyakazi hao walikuwa wakiandamana kushinikiza nyongeza ya mishahara na mazingira mzuri ya kazi.
Akiwa anatokea Dodoma kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, mzee Mwinyi alikwenda moja kwa moja Uwanja wa Uhuru (wakati huo Uwanja wa Taifa) baada ya kutua kwa ndege kwenye Uwanja wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Huko uwanja wa Taifa ndiko Kanda Bongo Man alikuwa atumbuize maelfu ya mashabiki wake na wa mtindo wake wa ‘Kwasakwasa’ akiwa ameruithi ufalme wa mtindo kutoka kwa muasisi wake Kabaselle Ya Mpanya maarufu “Pepe Kalle”.
Kimpangilio, kuliwekwa bendi mbili za kutumbuiza kabla ya mfalme huyo wa ‘Kwasakwasa’ kupanda jukwaani kufanya vitu vyake.
Bendi ya kwanza kuburudisha watu ilikuwa ‘Tatu Nane’ ambayo nd’o kwanza ilikuwa imejitokeza machoni mwa Wabongo.
Sipati kukwambia; kwani pamoja na Bendi hii kupiga muziki uliosheheni ngoma za hapa Bongo, ilikuwa maajabu makubwa katika siku huyo.
Kwani kama ambavyo siku zote Wabongo huwa hawapendi vya kwao, wasanii hawa wa bendi ya Tatu Nane walizomewa na hata kupigiwa makelele ya kufukuzwa jukwaani.
 ‘Ondokeni …ondokeni’, ndivyo mashabiki waliofurika uwanjani hapo walivyokuwa wakiwananga vijana hao wa Tatu Nane.
Ndipo baadaye alipopanda jukwaani Dakta Remmy Ongara maarufu ‘Dakta Remmy’ na bendi yake ya Super Matimila ambaye naye alichukua muda mrefu kupiga wimbo wake wa “Siku ya Kifo” ambao katika enzi zile nd’o ulikuwa maarufu.
Kutokana na kuurefusha wimbo huo, mzee Mwinyi aliomba aondoke uwanjani kwa udhuru wa kurejea Ikulu kupumzika ili baadaye aweze kukutana na manesi na madaktari waliokuwa wamegoma.
Alisema alifanya hivyo ili kupata muafaka na hivyo kuokoa maisha ya wagonjwa ambao wengine walikuwa tayari wamekufa kwa kukosa huduma.
 “Nakutakieni kila kheri na uhondo mkubwa wa mwanamuziki mahiri, Kanda Bongo Man”, alisema Rais mstaafu Mwinyi kuwaambia mashabiki waliofurika uwanjani huku akishuka kuelekea kwenye gari lililokuwa limemleta pale uwanjani.
Lakini kama ilivyo kwa Sungura kuwa na akili za ziada, Kanda Bongo Man ambaye kwa wakati wote huo alikuwa amehifadhiwa kwenye hema mbali kidogo na jukwaa kuu la wageni wa heshima, alitoka mbio na kukimbia kwa kasi hadi mbele ya ‘Rais’ Mwinyi. Akafanikiwa kuagana naye kwa kupeana mikono huku picha kedekede zikipigwa.
Kumbe jitihada hizo za kupiga picha na Rais zilikuwa kwa ajili ya kumbukumbu zake na pia kujitangaza duniani kuwa yeye Kanda Bongo Masn ni “Man” kwelikweli.
Ndipo kimbembe kilipojitokeza kesho yake na wiki nzima iliyofutia kwenye magazeti. Kwani baadhi ya magazeti yalimlaumu mzee Mwinyi kuwa alikuwa hakujali vifo vya wagonjwa hospitalini na badala yake alijali zaidi burudani ya Mkongomani huyo na hasa wimbo wake maarufu wa wakati huo “Isambe Monie”.
Kwa miaka mitano kuanzia mwaka 1990, wimbo wa “Isambe Monie” ulikuwa pendwa kwa kiwango kikubwa sawa na chumvi mbogani, sukari chaini, sharubati kwa burudani ya koo, tende swaumuni na sema utakacho ndugu yangu.
Hebu tujikumbushe beti za wimbo huo, “Isambe eeh, yoka ngai mawa. Isambe iyoo ooh oohoo X2. Muana mama eehh, Yoka ngai mawa, Isambe iyoo ooh oohooo. Libala bankoko, eleki ngoi elengi, Isambe iyoo ooh oohoo mama ah”.
Maneno machache lakini yenye maana kamili iliyokamilika na kukubalika kimaadili. Katika wimbo huu, Kanda Bongo Man anamlilia Isambe kwa kumwambia kuwa asimtese kwa mapenzi. Kwamba afungashe mapenzi ya mababu ambao walipendana kwa dhati pale walipofunga ndoa.Ilikuwa haifunguki mpaka kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu pale alipomchukua mmoja wao.
Anamwambia kuwa hiyo, ilitokana na mila na desturi za mababu zetu za kuoa ukoo uliokuwa unakubalika kijadi, kimila, kiheshima, kikazi na usiokuwa na maradhi ya kuambukizana na yale yaliyoshindikana kama ukoma, mbaranga au kifafa.
Kwamba ilikuwa wanaolewa wanadada wasafi wenye adabu na sifa ya upole, ukarimu na utuhekima basi. Kwamba hao nd’o walikuwa na nafasi ya ndoa na wala haikuwa vinginevyo kama ilivyo leo hii ambapo watu wanaokotana usiku na kesho mchana  ndoa zinafungwa.
Ndoa za sasa si ndoa bali ni ndoano na mauzauza matupu. Yaani ghafla mtu anaweza kuibuka na kufunga ndoa na mwanamke asiyemjua ukoo wake, familia yake wala tabia na urari wa ukoo wao.
Kwa yeye kakutana naye baa au kilabu cha kangara leo, kesho anatangaza ndoa na kuoa si jambo la ajabu. Matokeo yake hakuna tena heshima ya ndoa bali kinachobakia ni ndoano.
Mtu hawezi kutofautisha mume ni yupi na mke ni yupi. Kelele, mipayuko na ngumi mkononi mtindo mmoja kiasi cha watu kutotofautisha wawili hao iwaou ni mke na mume kweli au ni mtu na hawara au malaya wake wa mtaani.
Basi, magazeti yaliandika makala kadhaa za kumbeza mzee Mwinyi. Katuni kedekede za kumkejeli mzee huyo zikachorwa. Iliyokuwa kabambe zaidi ni ile iliyomuonesha muuguzi mmoja akifuma vitambaa wakati akiwa kazini lakini jirani na kitanda cha mgonjwa.
Alioneshwa namna alivyokuwa akifuma vitambaa hivyo huku Yule mgonjwa akiwa anapiga kelele kwa maumivu makali, “Yalaa, nesi nakufaa, yalaa; nisaidie”.
Nesi naye akawa akijibu, “Ngoja kwanza Isambe iishe”.
Kanda Bongo Man (kushoto) akiwa na promota aliyemleta nchini kwa mara ya kwanza mwaka 1992, Paul Lyimo.
Makala na katuni hizo ziliashiria kuwa ‘Rais’ Mwinyi hakujali maslahi ya manesi na madaktari. Kwamba alikwenda kumsikiliza Kanda Bongo Man uwanjani badala ya kusilikiza madai yao. Kwani wao nd’o wafanyakazi muhimu waliokuwa wamebeba maisha ya wagonjwa mikononi mwao.
Hawakuona hata ukweli kuwa, ‘Rais’ Mwinyi hakuona hata namna Kanda Bongo Man alivyokuwa akinengua pale uwanjanai juu ya jukwaa nadhifu alilotengenezewa. 
Lakini kiukweli ni kuwa kejeli ile haikuachwa ipite tu kama ‘waa la mvua’. Alikukwako mwandishi mmoja wa burudani akiwa maarufu kama chumvi kwa wakati huo.
Huyu alipambanua ukweli ulivyokuwa kwenye makala zake na kufikia kuzalisha neno ‘uchwara’ ambalo kwa leo ni maarufu.
Basi, hizo nd’o ‘enzi zile’ za Kanda Bongo Man. Alipeleka mtafaruku kila alipokwenda. Nchini Zimbabwe watu walikanyagana kiasi cha kumzalisha kwa kumbana mwanamke mja mzito aliyejitosa uwanja wa michezo amuone tu mwanamuziki huyo akinengua akiwa na “Abakosi” zake; yaani suti zake kabambe.
Huko Paris, Ufaransa Kanda Bongo Man alikuwa kipenzi cha watoto na kinamama kama Michael Jackson. Ujerumani alikuwa maarufu kama Elvis Presley, mkwewe Michael Jackson.
Katika Congo zote mbili; yaani Brazzavile na Kinshasa alikuwa mtamu kama asali. Uganda nd’o kwao alikoanzia maisha kwa kushona nguo kiasi cha kujishonea staili za nguo zilizoteka hisia za watu.
Kanda Bongo Man alitua Uganda mwishoni mwa miaka ya themanini akikimbia vita na shida za Congo DRC. Lakini alipofika Kampala akaanza kupiga muziki katika bendi ndogo ndogo za jijini humo. Alikuwa akiujua muziki vizuri.
Kwani akiwa kwao Zaire alipiga na kuimba kwenye bendi moja na mapacha maarufu wa ‘Zaire’, kina Soki Vangu na Soki Dyanzenza wa Bella Bella.
Kanda Bongo Man anasema kuwa kila akiwakumbuka rafiki zake hao moyo wake humuuma. Lakini hubaki akiwaombea kwa Mwenyezi Mungu awaweke mahala pema peponi.
Anafahamisha kuwa walikuwa asusa wa mwanzo kabisa wa gonjwa hatari la UKIMWI walilolipata kutokana na umamtashau na utanashati wao katika kuimba na kuvaa.
Kwani, kama yeye, mapacha hao nao walikuwa wakipiganiwa na wanawake popote pale walipotumbuiza. Hakika ni kosa la marehemu; kwani hawakutumia kondomu.
Kwa kuwakumbuka na kuwapa heshima kubwa, Kanda Bongo Man, katika albamu yake ya ‘Isambe Monie’ amewatungia wimbo aliouita ‘Freres Soki’; akiwa na maana “Rafiki zangu kina-Soki”.
Lakini hebu tujiulize, ‘Kanda Bongo Man aliyapataje mafanikio haya?’.
 Mwenyewe anasema, “Siwezi kusema eti ni ujanja wangu, akili yangu au uchawi, bali ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu tu”.
Anasema anamuamini Mungu kupita maelezo na kwamba kwa alivyomsaidia na kumtoa katika ufukara wa kutupa hana cha kumlipa isipokuwa shukrani tu na bidii za kumuomba na kumtafuta kwa nyimbo na mapambio kokote aliko.
“Kila albamu yangu lazima iwe na wimbo mmoja wa kumtukuza Mungu”, anasema Kanda Bongo Man katika mahojiano na mwandishi huyu wakati akiwa katika matembezi ya kawaida jijini Dar.“Nina albamu tano na nyimbo tano za kumshukuru Mungu”.
Kanda Bongo Man anasema kuwa aliingia katika imani ya Mwenyezi Mungu siku moja alipokutana na mtu mmoja jijini Paris, Ufaransa alikokuwa akiishi kama chokoraa ingawa alikuwa na kipaji chake cha kuimba.
“Mwanzoni sikuwa najihusisha na imani za Mungu”, anaendelea, “kwani nilikuwa nakufuru kwa kusema kuwa hakuna Mungu na kuwa watu hufanikiwa kwa maarifa na ujanja wao wenyewe”.
Lakini siku hiyo alipokutana na mtu huyo, alijaribu kumuomba msaada wa fedha za chakula akimlalamikia kuwa alikuwa akiishi maisha magumu mno.
 “Nitakupa pesa ya chakula”, anamnukuu mtu huyo akimwambia. “Lakini twende kwanza tukamsifu Mungu Kanisani, kisha umuombe akupe bahati na upendo kwa watu ili ufanikiwe”.
Kanda Bongo Man anasema kuwa alimfuata mtu yule kwa kikembe kwa sababu tu hakuwa na chochote mfukoni. Walipofika huko Kanisani, mtu huyo alimtambulisha kwa waumini wenzake. Waumini wale walimsihi Kanda Bongo Man amuamini Mungu na kwamba kwa maombi ya dhati angemnyanyua katika dunia.
“Hakuna zaidi ya uwezo na nguvu za Mungu”, anawanukuu waumini wale wakimuambia. “Atakutoa kutoka sakafuni hadi juu ya dunia”.
Anasema ndipo alipoanza kumuomba Mungu kwa dhati amsaidie katika kazi zake za mikono yake na moyo wake.
“Kwa kweli namshukuru sana Mwenyezi Mungu amenisikiliza na kunikubalia maombi yangu”, anayakinisha Kanda Bongo Man. “Leo hii mimi naishi maisha ya kheri. Cha kumlipa sina bali kumtungia wimbo mmoja katika kila albamu ninayotoa”.
Hakika utakubali kuwa nyimbo zake zote za kmsifia Mungu ni nzuri. Nyimbo hizo mara nyingi zimekuwa zikipendwa kwa kiwango kikubwa.
Wimbo kama ‘Yesu Kristo’ kwenye albamu yake ya ‘Isambe Monie’ umekuwa ukitumika kwenye mikusanyiko mingi ya maombi iwe ya raha au ya huzuni. Mwenyewe anasema kila akiusikia wimbo huo, hutoa chozi la shukrani kwa Mwenyezi Mungu.
Kanda Bongo Man ambaye kwa sasa anaishi jiji la Manchester, Uingereza amekwishapiga muziki wake na kuteka mashabiki karibu dunia nzima.
Lakini mwenyewe anasema hawezi kuisahau siku alipofanya shoo yake kubwa katika uhai wake anayoiita “The show of my life”; yaani “Onesho la maisha yangu” mwezi Agosti 1992.
Anasema shoo hiyo aliifanya kwenye ukumbi wa ‘Tanzania Room’ wa hoteli ya Kilimanjaro, jijini Dar maarufu leo hii kama ‘Hyatt Kempiski’.
Kwanini anaiita shoo ya maisha yake? Kanda Bongo Man anajibu, “Licha ya kutozwa bei kubwa kuliko shoo yangu nyingine yoyote niliyowahi kuifanya duniani kote, lakini ukumbi ulifurika hadi watu wengine wakabakia kuchungulia madirishani na kwenye korido (kumbi ndogo)”.
Kwa taarifa yako, ndugu msomaji, shoo hiyo ilitozwa shilingi 250,000 kwa mtu mmoja. Hebu angalia fedha hizo katika mwaka huo wa 1992! Jinsi pesa ilivyokuwa na thamani kwenye miaka hiyo. Kima cha chini cha mshahara wakati huo kilikuwa Shs. 5,000 tu! Kwahiyo kiingilio hicho kilikuwa kama mishahara ya kima cha chini ya miezi 50.
Basi, mapedeshee wa ukweli wa wakati huo na sio kama hawa wa leo, nd’o walioingia kwenye shoo hiyo. Walijazana kwenye ukumbi wa ‘Tanzania Room’ kucheza ‘Isambe Monie” iliyorudiwa kwa zaidi ya mara hamsini kwa maombi ya mashabiki waliokuwa wamezinguka isivyo kawaida.
Kwa kweli ukizichakachua fedha hizo kwa thamani ya sasa dhidi ya dolari ya Kimarekani, hapan’shaka zinafikia milioni 38 na ushei.
Fikiria basi onesho la bei hiyo iwapo litakuwako leo hii. Je, watakaoingia ukumbini watakuwa kina nani?. Bila shaka, Rais Jakaya Mrisho Kikwete na watu wenye haiba na hadhi yake nd’o utawakuta kwenye shoo hiyo.
Hakya Mungu tena.Wengine watakuwa Waandishi wa Habari kwakadi maalum na zaidi zaidi wasanii wa filamu lakini kwa kujikweza ili waonekane wanazo.
Ndivyo basi ilivyokuwa siku hiyo. Hakukuwa na ‘bora liende’ wala ‘wapiga debe’. Wao walikuwa na shoo zao za kwenye viwanja vya michezo. Waliokuwemo humo walikuwa watu wa matawi ya juu.
Kwa wale ambao wanakumbuka enzi ya Kanda Bongo Man huo nd’o ukweli wenyewe. Kwamba kwa kupendwa alikuwa sawa na ‘Michael Jackson’ wa Afrika.
Aliimba kwa sauti ya kuita, kumbembeleza, kutongoza, kuchombeza na kuhanikiza. Akacheza kwa  kulishambulia jukwaa. Akapiga saluti akiwa anadansi.
Usiseme pale alipozunguuka kwa kasi ya ajabu jukwaani akitoa madoido yake murua yaliyorandana na mavazi yake ya bekosi na suti ya ukweli.
Ndipo alipopendeza na kuwashika watu zaidi hasa alipoonesha mbwembwe zake na ule mwanya wake wa hamu uliowaroga wengi hasa kinamama. Lakini kama alivyosema yeye, ‘Wala hawakunipata’.
Basi, utanashati wake huo, hasa alipokuwa jukwaani nd’o uliwafanya watu mpaka leo waseme kuwa, ijapokuwa Michael Jackson ni mfalme wa Pop, yeye Kanda Bongo Man ni mfalme wa mtindo wa ‘Kwasakwasa’ uliomfanya apate hadhi ya ‘U-Michael Jackson’ wa Afrika na kuufikia ufame wa muziki barani Afrika.
Wallah tena bila udaku wala umbeya ni kwamba utanashati na ushambuliaji wake wa jukwaa, ndio uliowafanya wanamauziki wetu wa hapa nyumbani kuzinduka na kujua kuwa muziki ni zaidi ya kusimama jukwaani na kuimba. Ni kwamba unahitaji kujituma kikwelikweli.
Naam; msomaji wangu tafuta siku moja umtembelee pale jiji la Machester nchini Uingereza. Utamkuta akiwa na famlia yake yenye watoto watatu wanaokwenda shule za ukweli katika jiji hilo la maraha yote ya burudani ikiwemo soka ya kukata na shoka.
Kama utaona soo kumfuata nyumbani kwake, basi pitia kwenye Kituo chake cha mafuta cha Strowk kilichoko katikatinya jiji hilo la Manchester.
Alamsik bin nuuur.


Simu 0718-885870 na 0786-846719

Comments