- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Kabeya Chibangu Badu, maarufu zaidi tu kama Kabeya Badu (alizaliwa Januari
22, 1945 Likasi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) alikuwa mwanamuziki wa Congo
aliyezamia nchini Tanzania ambako ndiko alikopata umaarufu zaidi kuliko nchi
yake ya asili.
Na akiwa Tanzania, ambako pia aliwahi kumuoa mwanamuziki wa Nuru Mhina 'Baby White', ndiko alikojenga maisha yake na familia kwa ujumla.
Maisha yake ya awali
Elimu ya msingi
aliipata katika shule ya Ecole Officialle Laique de Kolwezi katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (wakati huo ikiitwa Congo Leopoldville) na kuhitimu mwaka
1959.
Kabeya alianza tangu
akiwa mdogo na alipopata umri wa kwenda kanisani, akajiunga katika kwaya akiwa
anaimba nyimbo za Injili.
Ni huko kanisani ndiko
alikojifunza jinsi ya kutengeneza ‘melody’ na baadaye mwaka 1963, akiwa anajiamini
kwamba anaweza kufanya muziki, alikwenda kujiunga na bendi ya muziki wa dansi
ya Ricco Jazz, iliyokuwa katika Wilaya ya Kolwezi.
Akiwa Kolwezi, mbali
ya kufanya muziki, Kabeya alijiunga na chuo cha ufundi ambako alichukua ufundi seremala
na uashi.
“Tangu nikiwa mdogo,
nilipenda sana nyimbo na uimbaji wa Tabu Ley Rochereau na Joseph Kabaselle ‘Le
Grand Kalle’, nikatamani siku moja nifikie hadhi yao,” aliwahi kukaririwa
akisema enzi ya uhai wake katika mojawapo ya mahojiano yake na wanahabari.
Familiya yake
ilijitahidi kumpa moyo ili aweze kufanya vizuri katika muziki, hivyo ilimshauri
Kabeya kujifunza lugha ya Kifaransa ambayo inazungumzwa nchini mwao.
Kabeya alikubaliana
na ushauri huo na aliingia katika chuo kilichokuwa kikimilikiwa na dhehebu la Protestant
huko Kananga. Kiu ya Kabeya ilipozwa wakati alipopokea cheti baada ya kufuzu
somo hilo la Kifaransa.
Harakati za Kabeya Badu
za kutafuta maisha zilimfikisha kufanya kazi katika gazeti moja la Reality Congolese la mjini Kananga, akiwa
kwenye kitengo cha usambazaji mwaka 1967.
“Baada ya miaka
miwili kupita, mmiliki wa gazeti hilo alikamatwa baada ya gazeti hilo kuandika
habari zilizomuudhi rais wa wakati huo Mobutu Sese Seko, hatma yake gazeti
likafungiwa, tukakosa kazi,” alipata kueleza.
Lakini huo haukuwa
mwisho wa maisha, kwani mwaka huo huo Kabeya alianza rasmi safari yake ya
muziki ambapo alijiunga na bendi ya Lupe Jazz kabla ya kuhama na kujiunga na
bendi nyingine ya Amide Success.
Hakuishia hapo, kwani
aliondoka tena na kujiunga na bendi ya Santa Fee kabla ya kuelekea katika bendi
ya Lupina Nationale, ambako alikutana na Kasongo Mpinda ‘Clayton’ huko Kananga.
Utulivu katika bendi
kwake haukuwepo kabisa. Aliondoka tena kwenda kujiunga katika bendi ya Lupe Revolution,
iliyokuwa ya vijana kama yeye.
Jina na sifa za
uimbaji wake zikazagaa ndipo alipochukuliwa na Omer Baba Gaston Ilunga wa
Ilunga katika bendi yake ya Baba Nationale mwezi Septemba 1968.
Mwaka 1970, Kabeya
alishawishika kwenda kutafuta ajira mjini Kinshasa. Alibahatika kupata ajira
katika bendi ambayo baadaye akagundua kwamba ilimpa ahadi za uongo za maslahi,
naye akaachana nayo.
Kati ya mwaka 1971 na
1972 Kabeya alipiga muziki katika bendi ya Festival du Zaire katika jiji la Kinshasa.
Kabeya alirudi Likasi
mwaka huo huo wa 1972 na kujiunga na bendi ya Safari Nkoi baada ya kuitwa na
mwanamuziki Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’. Katika bendi hiyo pia aliwakuta
wanamuziki wengine magwiji Freddie Ndala Kasheba na Baziano Bwetii. Yeye na
King Kiki walikuwa wamesoma darasa moja katika shule ya msingi ya shule ya
Ecole Officialle Laique de Kolwezi, ambako walihitimu mwaka 1959.
“Tangu tukiwa vijana
tulikuwa tukielewana sana na Kiki, ndiyo sababu nimekuwa naye sambamba tukienda
sehemu mbalimbali pamoja au yeye ananiita,” Kabeya alisema enzi ya uhai wake
alipohojiana na mwandishi mkongwe wa burudani Rashid Mtagaluka.
Hata wakati walipokuwa
Kolwezi wakipiga muziki katika bendi ya Safari Nkoi, walipanga nyumba moja na
walichangia bajeti ya chakula kwa pamoja kila mwisho wa mwezi.
Mwaka 1973 uongozi wa
Safari Nkoi ulianza kuwafanyia ‘mtimanyongo’ wanamuziki wake akiwemo King Kiki ambaye
hata hivyo aligundua mapema hali hiyo, akamshawishi Kabeya kuondoka na kwenda
kuanzisha bendi yao.
Lakini kabla
hawajaazisha bendi yao, akajitokeza tajiri mmoja aliyejulikana kwa jina la Paradiso,
akimtaka Kiki kwenda Lubumbashi kuanzisha bendi yake. Kiki hakumwacha Kabeya,
mwaka 1974 wakaenda Lubumbashi kuunda bendi ya tajiri huyo ya Buka Buka Mabele,
lakini ukiritimba wa tajiri huyo ukasababisha bendi hiyo kufa baada ya miezi
sita tu.
Baada ya kufa kwa
bendi hiyo, mwishoni mwa mwaka 1974 Kiki aliamua kwenda Kinshasa lakini kabla
hajaondoka, aliwashawishi Kabeya na wanamuziki wenzake warejee Safari Nkoi. Walikubali
ushauri huo nao wakarejea na kupokelewa na uongozi wa Safari Nkoi kwa mara
nyingine tena. Kwa kipindi hicho akiwa Safari Nkoi, Kabeya akawa na mawasiliano
ya karibu na Kiki akimshawishi kurudi Safari Nkoi kwa vile hali ya utulivu
katika bendi ilikuwa imeimarika.
King Kiki alirejea
Lubumbashi mwaka 1976, akitokea Kinshasa pasipo kumafamamisha mtu yeyote.
Walikuwa wanapiga
muziki katika ukumbi mmoja wa Rele Night Club
mjini Lubumbashi, ghafla Kiki akapanda jukwaani na kushika ‘mic’ akaanza
kuimba. Wote wakashikwa na butwaa wakimuona kama ‘shetani’ aliyetua kimiujiza
jukwaani.
Mwaka 1977 Kiki alifuatwa
na Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’ aliyetokea Marquis du Zaire iliyokuwa nchini
Tanzania. Kiki alimuuliza Mzee Paul kama wanamuziki waliokuwepo Marquis du Zaire
walikuwa wanakidhi viwango. Mzee Paul alijibu kwa wasiwasi na kupendekeza bora
kuchukua wanamuziki wengine huko Congo. Kiki alipendekeza wanamuziki wa
kuondoka naye kwenda Tanzania akiwemo Kanku Kelly Kashama (mpuliza saxophone), Mutombo
Lufungula Sozy ‘Adios’, Ilunga Banza ‘Mchafu’ (gitaa la bass) ambao wote
walikuwa Safari Nkoi. Wakiwa safarini kwenda Tanzania walipitia mji wa Kamina
ambako walimpata mnenguaji mwanadada Ngalula Tshiandanda aliyekuwa akinengua katika bendi ya Sakayonsa
ya mjini humo.
Kabeya Badu alikuwa
akiwasiliana na King Kiki na akamuahidi kwamba atajitahidi naye aende Tanzania.
Ahadi ya Kiki kwa Kabeya
ilitimia baada ya kufika Marquis du Zaire. Safu ya uimbaji ikaonekana kupwaya.
Alipendekeza kuongezwa kwa wanamuziki zaidi ili kuimarisha bendi hiyo. Chibangu
Katayi ‘Mzee Paul’ kwa mara nyingine tena akatumwa kwenda Congo kuwaleta
wanamuziki waliopendekezwa na Kiki ambao ni watunzi na waimbaji Kabeya Badu na
Kalala Mbwembwe, Monga Kiyombo aliyekuwa akipiga gitaa la rhythm na saxophone,
Ngoyi Mubenga (tarumbeta), na Khatibu Iteyi Iteyi (saxophone).
Mara tu baada ya
kutua Marquis, Kabeya alitunga na kuimba nyimbo nyingi, baadhi yake ni ‘Ndoa ya Kwangu na Mama Kazi’, ‘Pondamali’, ambazo zilirekodiwa na ‘Kibwe Mutombo’, ‘Muntanda
Muli’, ‘Lwembe’ na ‘Maneno’,
ambazo hazikuwahi kurekodiwa.
Kabeya Badu alidumu na
Marquis du Zaire kwa miaka miwili baadaye mwaka 1980, alichoropoka na kwenda
akijunga na King Kiki katika bendi ya Orchestra Safari Sound (OSS) iliyokuwa ikimilikiwa
na mfanyabiashara maarufu Hugo Kisima.
Akiwa na OSS, Kabeya
alitunga na kuimba nyimbo za ‘Nani Atashika
Jembe’ na ‘Pole Ndugu’. Wimbo wa ‘Yuyu’ alioutunga ulipigwa na kurekodiwa
katika kipindi cha Klabu Raha Leo Show kilichokuwa kikirushwa na Radio Tanzania
Dar es Salaam (RTD).
Kabeya Badu alikuwa
akihitajika sana katika bendi hizo mbili pinzani wakati huo za Marquis na OSS.
Hivyo, akawa mithiri ya ‘muigizaji’ kwa kuhamahama. Alirejea tena Marquis kwa
kipindi kifupi kisha mwaka 1986 akatakiwa kurejea kwa mara nyingine tena katika
bendi ya Orchestra Safari Sound, wakati huo bendi ilikuwa chini ya uongozi wa Ndala
Kasheba na haichukua muda mrefu akatoka na wimbo uliowapagaisha wapenzi wa OSS wa
‘Ziada’. Wimbo huo aliuimba peke yake
kwa hisia kali akimlilia Ziada, na ukamuongezea sifa kubwa miongoni mwa
waimbaji wa muziki wa dansi nchini Tanzania.
Nyimbo nyingine
zilikuwa za ‘Kuruthumu’, ‘Simba Wala Watu
Wamevamia Mji’, ‘Mama Mwita’, ‘Kayanda’ na nyingine nyingi.
Kabeya Badu alimwelezea
King Kiki kuwa ndiye aliyekuwa anaujua umuhimu wake: “Kiki ndiye aliyekuwa
akijua umuhimu wangu katika muziki toka mwanzo hadi akanipachika jina la ‘Changa
cha Mkonyoyo’ ikiwa na maana ya ‘Siri iliyofichika’”. Hiyo ilikuwa baada ya
Kabeya kutunga wimbo wa ‘Changa cha Mkonyoyo’ uliokuwa na ujumbe mzito lakini haukuwahi
kurekodiwa.
Aliondoka OSS na
kwenda kujiunga kwa mara nyingine tena na Marquis du Zaire mwaka 1988, lakini hakadumu
akachukuliwa na kwenda kujiunga na bendi ya Tancut Almasi iliyokuwa na makazi
yake mjini Iringa.
Mwaka 1990 akaamua
kurudi kwao Likasi katika Jimbo la Katanga nchini Congo DR. Lakini mwishoni mwa
mwaka 1998 alirejea Tanzania na mwaka 1999 akapewa kazi ya kuanzisha bendi ya Magoma
Moto Sound ya jijini Dar es Salaam. Bendi hiyo haikudumu sana, hivyo mwaka 2001
akajiunga na bendi ya La Capitale ‘Wazee Sugu’ iliyokuwa inaongozwa na King
Kiki.
Mauti
Kabeya Badu alikuwa
mwimbaji mahiri katika bendi ya La Capitale aliyewaacha wapenzi na mashabiki wa
muziki wa dansi nchini Tanzania wakiwa bado wanamhitaji.
Aliaga dunia Machi 6,
2013 akiwa katika Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa
kwa maradhi ya figo, akiwa amefikisha umri wa miaka 68.
Msiba wa Kabeya
uliwatia simanzi na majonzi makubwa waombolezaji waliofika katika Hospitali ya Muhimbili
kuuaga mwili wake na katika mazishi yaliyofanyika katika Makaburi ya Kinondoni Machi
7, 2013. Watu walibubujikwa na machozi mara walipoona mwili wake ukishushwa
kaburini.
Tangu alipoanza
safari yake katika muziki, Kabeya Badu kamwe hakuwa mtu mwenye soni. Alikuwa
tayari kuiacha bendi na kwenda nyingine wakati wowote ule, ili mradi maslahi
yawe mazuri kwa sababu muziki kwake ndiyo ilikuwa ajira.
Wakati mauti
yanamfika, Kabeya Chibangu Badu aliacha mjane na watoto nane, kati yao watano
ni wa kike.
Wasifu
Jina: Kabeya Chibangu Badu
Kuzaliwa: Januari 22, 1945
Mahali: Likasi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Bendi alizopitia: Ricco Jazz, Lupe Jazz, Amide Success, Santa Fee, Lupina Nationale, Lupe Revolution, Baba Nationale, Festival du Zaire, Orchestra Safari Nkoi, Buka Buka Mabele, Marquis du Zaire, Orchestra Safari Sound, Tancut Almasi, Magoma Moto Sound,
Nyimbo alizotunga: ‘Ndoa ya Kwangu na Mama Kazi’, ‘Pondamali’, ‘Kibwe Mutombo’, ‘Muntanda Muli’, ‘Lwembe’ na ‘Maneno’ (Marquis); ‘Nani Atashika Jembe’, ‘Pole Ndugu’, ‘Yuyu’, ‘Ziada’, ‘Kuruthumu’, ‘Simba Wala Watu Wamevamia Mji’, ‘Mama Mwita’, ‘Kayanda’, ‘Changa cha Mkonyoyo’ (OSS).
Comments
Post a Comment